-
Kuishi Muda Mrefu Ukiwa na Afya BoraAmkeni!—1999 | Julai 22
-
-
Mazoea ya kufanya mazoezi ya akili. Ule msemo “Uutumie au uupoteze” yaonekana kuwa unatumika si tu kwa misuli bali pia kwa akili. Ijapokuwa kuzeeka huandamana na usahaulifu fulani, uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Marekani Inayochunguza Kuzeeka unaonyesha kwamba ubongo wa mtu aliyezeeka huwa na uwezo wa kutosha kukabiliana na matokeo ya kuzeeka. Kwa hiyo, profesa wa elimu ya neva Dakt. Antonio R. Damasio akata kauli hivi: “Watu wazee wanaweza kuendelea kuwa na uwezo bora sana wa kiakili.” Ni nini kinachofanya ubongo wa watu waliozeeka uendelee kuwa na uwezo mzuri?
Ubongo una chembe za ubongo au nyuroni zipatazo bilioni 100, na chembe hizo zina trilioni nyingi za miunganisho. Miunganisho hii hutenda kama nyaya za umeme ikiwezesha nyuroni “kuwasiliana” na nyingine ili kutokeza kumbukumbu miongoni mwa mambo mengine. Ubongo uzeekapo, nyuroni hufa. (Ona sanduku “Kuchunguza Upya Chembe za Ubongo.”) Lakini, ubongo wa watu wazee bado unaweza kutenda vyema bila nyuroni zilizokufa. Wakati wowote nyuroni ifapo, nyuroni zinazoizunguka hufanyiza miunganisho mipya kati yake na nyuroni nyingine na hivyo hutimiza kazi ya nyuroni iliyokufa. Kwa njia hiyo, ubongo hubadili utendaji fulani kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa hiyo, watu wengi wazee hutimiza mambo yanayohitaji kufikiri sawa na vijana, lakini huenda wakatumia sehemu tofauti za ubongo kufanya hivyo. Katika mambo fulani, ubongo wa mtu mzee hutenda kama mchezaji wa tenisi mwenye umri mkubwa ambaye hutumia ustadi kwa sababu ya kupungua kwa wepesi wake jambo ambalo huenda wachezaji vijana hawana. Lakini, licha ya kutumia mbinu tofauti na za wachezaji vijana, yule mchezaji mzee bado hupata pointi.
Watu wazee wanaweza kufanya nini ili kudumisha uwezo wao? Baada ya kuchunguza zaidi ya watu 1,000 wenye umri wa kati ya miaka 70 na 80, mtafiti wa hali ya kuzeeka Dakt. Marilyn Albert alipata kwamba mazoezi ya akili ni mojawapo ya mambo yanayoamua watu wazee watakaodumisha uwezo mkubwa wa kufikiri. (Ona sanduku “Kudumisha Uwezo wa Kufikiri.”) Mazoezi ya akili hudumisha utendaji wa ‘miunganisho’ ya ubongo. Kwa upande mwingine, watafiti husema kwamba kudhoofika kwa akili huanza “watu wanapostaafu, wanapoamua kulegea, na wanaposema haiwalazimu kuhangaishwa na matukio ya ulimwengu.”—Inside the Brain.
-
-
Kuishi Muda Mrefu Ukiwa na Afya BoraAmkeni!—1999 | Julai 22
-
-
KUDUMISHA UWEZO WA KUFIKIRI
Uchunguzi wa kisayansi uliohusisha maelfu ya watu wazee ulionyesha mambo kadhaa yanayosaidia kudumisha uwezo wao wa kufikiri. Yanatia ndani “kusoma sana, kusafiri, kujishughulisha sana na mambo ya kijamii, elimu, kujiunga na klabu, na vyama vya kitaaluma.” “Fanya mambo mbalimbali mengi iwezekanavyo.” “Endelea na kazi yako. Usistaafu.” “Zima televisheni.” “Jifunze kozi fulani.” Yaaminika kwamba mbali na kuboresha hali ya mtu utendaji huo hutokeza pia sinapsi mpya kwenye ubongo.
[Picha]
Mazoezi ya akili husaidia kudumisha uwezo wa kufikiri
-