-
Maajabu ya Hekima ya KisilikaAmkeni!—2007 | Julai
-
-
Maajabu ya Hekima ya Kisilika
“Kuhama [kwa ndege] ni kati ya mambo ya asili yenye kustaajabisha zaidi.”—COLLINS ATLAS OF BIRD MIGRATION.
DESEMBA 9, 1967 (9/12/1967) rubani mmoja aliona ndege 30 aina ya bata-maji wakiruka mita 8,200 juu ya usawa wa bahari kuelekea Ireland. Kwa nini walikuwa wakiruka juu hivyo ambako hali ya joto ni Selsiasi 40 chini ya sufuri? Zaidi ya kuepuka dhoruba za barafu zilizokuwa katika maeneo ya chini, ndege hao walikuwa wakibebwa kwa upepo uliowasaidia waruke kwa mwendo wa kilomita 200 kwa saa. Inakadiriwa kwamba ndege hao walisafiri umbali wa kilomita 1,300 kutoka Iceland hadi Ireland kwa muda wa saa saba tu.
Ndege ambaye huhamia maeneo ya mbali zaidi ni membe wa aktiki ambaye hutaga kwenye Mzingo wa Aktiki na wakati wa majira ya baridi kali, yeye huhamia maeneo ya Antaktiki. Kwa mwaka mmoja, ndege huyo mdogo husafiri kati ya kilomita 40,000 na 50,000, umbali unaolingana na kuizunguka dunia!
Korongo weupe huzaliana Ulaya Kaskazini na kusafiri kuelekea Afrika Kusini wakati wa majira ya baridi kali, hiyo ikiwa safari ya kilomita 24,000. Maelfu ya ndege hao hupitia Israel wakati wa majira ya kupukutika kwa majani na majira ya kuchipua, wakati uliojulikana katika nyakati za Biblia.—Yeremia 8:7.
Ni nani aliyewapa uwezo huo wa kisilika? Miaka 3,500 hivi iliyopita, Mungu alimwuliza hivi mwanamume mwadilifu Ayubu: “Je, ni kwa sababu ya uelewaji wako kwamba kipanga hupaa juu, kwamba yeye hunyoosha mabawa yake kuuelekea upepo wa kusini? Au, je, ni kwa agizo lako kwamba tai huruka kuelekea juu na kwamba hujenga kiota chake huko juu?” Alipojibu, Ayubu alimsifu Mungu kwa uwezo wa ajabu wa ndege na wanyama wengine.—Ayubu 39:26, 27; 42:2.
Uwezo Unaozidi Silika
Wanadamu, ambao waliumbwa kwa njia ya kustaajabisha na Mungu, hawaongozwi hasa na silika. Badala yake, sisi ni viumbe wenye uwezo wa kujiamulia mambo kwani tuna dhamiri na uwezo wa kuwapenda watu. (Mwanzo 1:27; 1 Yohana 4:8) Kwa sababu ya kuwa na zawadi hizo zote, tunaweza kufanya maamuzi ya haki na yanayotegemea maadili ambayo nyakati nyingine huonyesha upendo mwingi na kujidhabihu.
Bila shaka, mtazamo na tabia ya mtu hutegemea hasa kanuni za maadili na za kiroho ambazo alifundishwa au hakufundishwa alipokuwa mchanga. Kwa sababu hiyo, watu wanaweza kuwa na maoni yanayotofautiana kuhusu lililo sawa na lililo kosa, kuhusu linalofaa na lisilofaa. Tofauti hizo zinaweza kutokeza kutoelewana, kutovumiliana na hata kuchukiana, hasa ikiwa mambo kama utamaduni, uzalendo, na dini yanahusika.
Ulimwengu ungekuwa bora zaidi ikiwa familia yote ya wanadamu ingefuata viwango vilevile ambavyo vinapatana na maadili na kanuni za Biblia, kama tu sote tunavyofuata sheria zilezile za kiasili zinazoongoza ulimwengu wote! Lakini je, kuna mtu yeyote aliye na uwezo na ujuzi wa kuweka viwango vya kufuatwa ulimwenguni pote? Ikiwa yupo, je, atafanya hivyo? Je, tayari amefanya hivyo? Maswali hayo yatajibiwa katika makala inayofuata.
-
-
Mwongozo Bora Kuliko SilikaAmkeni!—2007 | Julai
-
-
Mwongozo Bora Kuliko Silika
“Ikiwa kila mtu ataruhusiwa kujichagulia maadili yake, bila kuwa na kanuni za kuamua ikiwa maadili hayo ni sawa, basi lazima sheria itatumiwa kuhakikisha kwamba kuna tabia nzuri.” —DAKT. DANIEL CALLAHAN.
TUNAWEZA kuona ukweli wa maneno ya Callahan kwani watu wanazidi kupuuza kanuni za maadili hivi kwamba katika sehemu nyingi ulimwenguni, serikali zimelazimika kuweka sheria nyingi ili kuzuia uhalifu. Katika mkutano wa kwanza kabisa wa Kongamano la Akina Mama wa Nigeria, rais wa Nigeria alieleza mahangaiko yake kuhusu wakati ujao wa taifa hilo. Hakuwa akifikiria siasa au umaskini, bali “tatizo zito zaidi,” yaani, “kumomonyoka kwa . . . maadili ya msingi katika familia, kazini, katika jamii na hata katika taifa zima.”
Uchunguzi uliofanyiwa akina mama 1,736 nchini Uingereza ulionyesha kwamba “familia zinazorota kwa sababu ya kuporomoka kwa maadili na kuongezeka kwa familia zenye mzazi mmoja.” Vilevile, maadili yanaporomoka kwa kasi nchini China. Gazeti Time linaripoti kwamba watu wanaanza kufanya ngono mapema zaidi maishani na wana wapenzi wengi kuliko zamani. “Haya ni maisha yangu, nami naweza kufanya chochote ninachotaka,” akasema msichana mmoja Mchina ambaye alijivunia kuwa na zaidi ya wapenzi 100.
Kuporomoka kwa maadili kumewaathiri pia wenye mamlaka. “Watu hawawaoni viongozi wao kuwa mifano ya kuigwa kiadili,” akasema Javed Akbar katika gazeti la Kanada Toronto Star. Aliongezea kusema kwamba wanasiasa, wasimamizi wa mashirika, na pia viongozi wa kidini “wanaonekana kuwa hawana maadili mazuri.”
Kwa Nini Maadili Yameporomoka?
Mambo kadhaa yamechangia hali hiyo. Jambo moja ni roho ya kuasi kanuni ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu. Kwa mfano, uchunguzi uliofanywa Kusini mwa Marekani ulionyesha kwamba wanafunzi wengi wa chuo kikuu waliamini “mtu anapaswa kujiamulia mwenyewe tofauti kati ya mema na mabaya.”
Mwandishi wa mambo ya kisiasa Zbigniew Brzezinski alitaja sababu nyingine. Aliandika kwamba watu leo “hukazia kutosheleza tamaa zao, na kwamba anasa ndilo jambo linaloamua jinsi tabia za watu zitakavyokuwa.” Uhuru na uwezo wa kufanya maamuzi yanayopatana na maadili, ubinafsi, na kujitosheleza tu kunaweza kukuvutia, lakini je, kunasaidia uwe na furaha ya kweli, uradhi, na uhusiano mzuri zaidi pamoja na wengine?
“Hekima huonyeshwa kuwa yenye uadilifu kwa matendo yake,” akasema Yesu. (Mathayo 11:19) Je, kuporomoka kwa maadili kumewafanya watu wawe na furaha na uradhi zaidi? Fikiria matokeo kadhaa: kiwango cha kutowaamini wengine kimeongezeka, hakuna usalama, uhusiano unavunjika, watoto wanakua bila baba au mama, magonjwa ya kuambukiza yanayopitishwa kingono, mimba zisizotakiwa, uraibu wa dawa za kulevya, na jeuri. Mambo haya hayaonyeshi uradhi na kufanikiwa badala yake ni huzuni na kushindwa.—Wagalatia 6:7, 8.
Baada ya kuona matatizo kama hayo katika siku zake, nabii wa Mungu, Yeremia, alisema hivi: “Ninajua vema, Ee Yehova, kwamba njia ya mtu wa udongo haimo katika uwezo wake. Mwanadamu anayetembea hana uwezo wa kuongoza hatua yake.” (Yeremia 10:23) Ndiyo, Mungu hakutuumba tujiongoze, yaani, tujiamulie mema na mabaya. Kinachoonekana kuwa kizuri kwetu kinaweza kudhuru. Methali 14:12 inasema: “Kuna njia ambayo imenyooka mbele ya mwanadamu, lakini njia za kifo ndizo mwisho wake baadaye.”
-