-
Uvutano wa MagazetiAmkeni!—2005 | Oktoba 22
-
-
Uvutano wa Magazeti
Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilipokomesha utawala wa kiukoo huko Ujerumani, serikali ya demokrasi ya kijamii ilianza kutawala huko Berlin. Baadaye, Wakomunisti walijaribu kupindua serikali hiyo mpya. Serikali hiyo na Wakomunisti walihisi kwamba kudhibiti vyombo vya habari kungekuwa sawa na kudhibiti watu na maoni yao pia. Hivyo kukatokea mapambano makali ya kudhibiti vyombo vya habari.
KWA karne chache zilizopita, magazeti yameathiri utamaduni, siasa, yamechangia fungu muhimu katika biashara, na kuathiri maisha ya kila siku ya mamilioni ya watu. Yanaathirije maisha yako?
Yaonekana kwamba mnamo 1605, gazeti la kwanza barani Ulaya lilichapishwa nchini Ujerumani. Katika sehemu fulani leo, karibu watu 3 kati ya 4 walio na umri wa zaidi ya miaka 14 husoma gazeti kila siku. Ingawa katika nchi fulani zinazositawi wakazi 1,000 hupata nakala zinazopungua 20 za gazeti la kila siku, Norway ina zaidi ya nakala 600 kwa kila wakazi 1,000. Kwa ujumla, ulimwenguni pote, magazeti yapatayo 38,000 huchapishwa.
Kila mahali, magazeti hujulisha umma habari muhimu. Lakini yanatimiza mengi zaidi. Magazeti hutoa habari ambazo huathiri maoni ya wasomaji wengi. Dieter Offenhäusser, wa Tume ya Ujerumani ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) anadai kwamba, “kusoma gazeti kila siku” huathiri “mitazamo, mwenendo, na hata maadili yetu ya msingi.”
Wanahistoria wasema kwamba magazeti yamechochea, yakaunga mkono, na kutetea vita. Wanatoa mfano wa vita vya 1870 hadi 1871 kati ya Ufaransa na Prussia, vita vya 1898 kati ya Amerika na Hispania, na Vita vya Vietnam vya 1955 hadi 1975. Wafanyabiashara, wanasayansi, watumbuizaji mashuhuri, na wanasiasa wengi wameangamia kwa sababu ya kashfa iliyochapishwa katika magazeti. Katika kashfa ya Watergate inayojulikana sana ya miaka ya katikati ya 1970, waandishi wa habari wanaofichua ufisadi wa serikali na mashirika ya umma walifunua mambo ambayo yalimlazimisha rais wa Marekani, Richard M. Nixon kujiuzulu. Naam, magazeti yana uwezo mkubwa wa kuathiri maoni ya watu kwa njia nzuri au mbaya.
Lakini magazeti yalianzaje? Habari tunazosoma katika magazeti yetu ni zenye kutegemeka kadiri gani? Tunapaswa kujihadhari na mambo gani ili tunufaike nayo?
[Picha katika ukurasa wa 3]
Wapiganaji wajificha nyuma ya magazeti huko Berlin baada ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu
-
-
Kutosheleza Uhitaji wa HabariAmkeni!—2005 | Oktoba 22
-
-
Kutosheleza Uhitaji wa Habari
“WAATHENE wote na wageni waliokuwa wakikaa huko kwa muda hawakuwa wakitumia wakati wao wa starehe wakifanya chochote ila kuambiana jambo au kusikiliza jambo jipya,” akaripoti Luka, mwandishi wa Biblia, miaka 2,000 hivi iliyopita. (Matendo 17:21) Karne moja mapema, serikali ya Roma ilipotambua hamu ya watu ya kupata habari, ilianza kubandika Acta Diurna, yaani, matangazo ya kila siku, mahali ambapo watu wengi wangeweza kuyaona.
Kufikia karne ya saba, Wachina walikuwa wakichapisha gazeti la kwanza lililoitwa, Dibao (Pao). Huko Ulaya, ambapo watu wengi bado walikuwa hawajui kusoma na kuandika, watu waliokuwa wakisafiri na kusimulia hadithi walieneza habari kuhusu vita, misiba, uhalifu, na mambo mengine. Baadaye, habari kuhusu mambo hayo iliandikwa na picha kuchorwa kwa mikono kwenye vipande vya mbao ambavyo viliuzwa kwenye masoko na maonyesho.
Hatimaye, kampuni za kibiashara ziliboresha barua zao rasmi kwa kutia ndani habari muhimu. Mwishowe, habari hizo zilichapishwa kwenye ukurasa wa ziada ulioitwa nova (habari), ambao ungeweza kusambazwa.
Mwanzo wa Magazeti
Mwanzoni mwa karne ya 17, magazeti mawili ya Ujerumani yalianza kuchapishwa kwa ukawaida. Lile lililoitwa Relation (kusimulia habari), la huko Strasbourg, lilichapishwa mara ya kwanza mnamo 1605; nalo Avisa Relation oder Zeitung (habari zenye mashauri), la huko Wolfenbüttel, lilianza kuchapishwa mwaka wa 1609. Gazeti la kwanza la kila siku huko Ulaya liliitwa Einkommende Zeitungen (Habari Motomoto), nalo lilichapishwa huko Leipzig, Ujerumani, mwaka wa 1650.
Gazeti hilo la kwanza la kila siku huko Leipzig lilikuwa na kurasa nne zenye ukubwa wa kutoshea mfukoni. Kurasa hizo zilikuwa na habari ambazo hazikuwa na mpangilio wowote. Nakala mojamoja za gazeti hilo hazikuwa ghali, lakini andikisho la mwaka mzima lingeweza kugharimu mshahara wa mwezi moja wa mfanyakazi aliyelipwa vizuri. Hata hivyo, uhitaji wa magazeti uliongezeka haraka. Kufikia mwaka wa 1700, Ujerumani peke yake ilikuwa na magazeti ya kawaida 50 hadi 60 ambayo yalisomwa na mamia ya maelfu ya watu.
Mwanzoni, vyanzo vya habari vilikuwa barua, magazeti mengine, wakuu wa posta waliopokea habari kupitia barua na kuinakili, au uvumi uliosikiwa tu na waleta-habari katika sehemu za umma. Hata hivyo, kwa sababu ya kutokea kwa makampuni mengi ya magazeti, wachapishaji walijitahidi kuongeza kiasi cha habari na kuiboresha. Waliajiri wahariri wao wa kwanza stadi. Na kwa kuwa wachapishaji wengi hawangeweza kugharimia mfumo mkubwa wa kupata habari na waandishi wa habari, hamu ya kupata habari ilifanya mashirika ya habari yaanzishwe ili kukusanya na kueneza habari kwa wachapishaji waliojiandikisha.
Uvumbuzi Muhimu
Biashara ya magazeti haingekuwapo bila uvumbuzi muhimu, hasa ule wa Johannes Gutenberg wa mashini iliyochapa herufi mojamoja. Uvumbuzi zaidi ulirahisisha na kupunguza gharama za uchapishaji wa magazeti. Kwa mfano, katika miaka ya 1860, matbaa pana zinazozunguka zilifanya iwezekane kuchapisha habari kwa mfululizo kwenye makaratasi yaliyovingirishwa badala ya kuchapa kurasa mojamoja. Muda mfupi baadaye, mashini ya Linotype ilitumiwa kupanga herufi za chapa za chuma katika kurasa ili kuchapishwa. Kisha, katika sehemu ya mwisho ya karne ya 20, kupanga kurasa kwa kutumia kompyuta kulichukua mahali pa kazi iliyogharimu sana na iliyofanywa kwa mkono.
Wakati huohuo, habari zilisambazwa haraka sana wakati telegramu ilipoanza kutumiwa katika miaka ya 1840, taipureta katika miaka ya 1870, na simu karibu wakati huohuo. Hivi karibuni zaidi, wakati ambapo kuna mamilioni ya watu, magazeti hutumia kompyuta, barua-pepe, na faksi. Maripota hufika mahali penye tukio fulani haraka zaidi kwa gari-moshi, gari, na ndege. Magazeti mengi zaidi husambazwa kupitia njia ya usafiri wa haraka.
Ni Habari Gani Huripotiwa Magazetini?
Katika sehemu nyingi, si tatizo kupata habari za kutosha katika ulimwengu huu unaozidi kuwa mdogo. Kulingana na wahariri wa gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung, “Tatizo ni kuchagua habari kutoka vyanzo vingi sana visivyo na kikomo.” Mashirika ya habari huletea magazeti ya Ujerumani hadithi na habari 2,000 hivi kila siku. Maripota, waleta-habari, habari za televisheni, na vyanzo vingine huwaletea wahariri wa magazeti habari chungu nzima.
Thuluthi mbili ya habari huwa matangazo, yaani, taarifa kwa waandishi wa habari na ripoti kuhusu matukio yaliyopangwa kama vile tamasha, michezo, na mikutano. Wahariri wanapaswa kujua mahitaji ya wasomaji wao ili kuandaa habari ambazo watu wanahitaji kujua kama vile matokeo ya mavuno, siku za kukumbukwa, na maadhimisho.
Watu hupenda sana kurasa zenye habari za michezo, safu za vichekesho, katuni kuhusu siasa, na tahariri. Habari kuu, ripoti kutoka nchi za kigeni, na mahojiano na watu mashuhuri na wataalamu wa masuala hususa zinaweza kuwa zenye kuelimisha na kuburudisha.
Magazeti Yanakumbwa na Matatizo
Gazeti Die Zeit liliripoti hivi mwaka wa 2002: “Biashara ya magazeti huko Ujerumani inakabili matatizo makubwa zaidi ya kifedha katika historia yake.” Na Shirika la Habari la Uswisi liliripoti kwamba katika mwaka wa 2004 idadi ya magazeti yaliyosambazwa ilikuwa chini sana, kwani hiyo ilikuwa idadi ndogo zaidi ambayo shirika hilo limesambaza katika miaka kumi. Kwa nini uhitaji wa magazeti umepungua?
Sababu moja ni kuzorota kwa uchumi ulimwenguni pote, na hivyo kupunguza matangazo ya biashara ambayo yalichangia thuluthi mbili ya mapato ya magazeti mengi. Kati ya mwaka wa 2000 na 2004, gazeti la Marekani, Wall Street Journal lilipoteza asilimia 43 ya mapato yake ya matangazo ya biashara. Je, mapato yanayotokana na matangazo hayo yataongezeka uchumi ukiboreka? Matangazo mengi madogo kuhusu mashamba na nyumba, kazi, na magari sasa hutangazwa kwenye Intaneti. Leo magazeti hushindana na vyombo vingine vya habari kama vile redio, televisheni, na Intaneti.
Kwa upande mwingine, bado kuna uhitaji mkubwa wa habari. Axel Zerdick, profesa wa masuala ya kiuchumi ya vyombo vya habari aliliambia hivi gazeti moja la Frankfurt, Ujerumani: “Tatizo hilo si baya sana kama waandishi wengi wa habari wanavyodhani.” Mhariri mkuu wa gazeti moja la kila siku la Ujerumani alikubaliana na maoni hayo aliposema: ‘Gazeti tunalochapisha bado linatia fora.’
Hata kama magazeti yana habari nyingi sana na yana uwezo wa kuathiri maoni ya watu, bado swali ni: Je, unaweza kutegemea habari yanayotoa? Unawezaje kunufaika na yale unayosoma magazetini?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
WAANDISHI WA HABARI WANA KAZI NGUMU
Huenda mtu akatamani kazi ya uandishi wa habari. Mtu mmoja ambaye amekuwa mwandishi wa habari kwa muda mrefu huko Ufaransa alisema: “Mwandishi wa habari anaweza kujitukuza anapoona jina lake kwenye gazeti.” Hata hivyo, anaweza kupata mfadhaiko kwa sababu ya kazi hiyo. Kwa mfano, hadithi ambayo mtu alitaka kuchapisha inaweza kuripotiwa na mwandishi wa gazeti lingine, mahojiano yakataliwe, na anaweza kungojea kwa muda mrefu tukio fulani kisha likose kutokea.
Mwandishi fulani wa magazeti huko Poland alitaja tatizo lingine. “Hatujui ni lini tutakuwa kazini na ni lini tutakuwa tukipumzika. Nyakati nyingine wakati wetu wa faragha huingiliwa, na huenda kazi ikavuruga maisha yetu ya familia.” Na aliyekuwa mwandishi wa habari katika ule uliokuwa Muungano wa Sovieti alitaja jambo ambalo labda hufadhaisha hata zaidi: “Nilifanya kazi kwa bidii, lakini mwishowe habari hiyo haikuchapishwa.”
Mwandishi wa habari za michezo wa gazeti linalosomwa na watu wengi zaidi nchini Uholanzi alisema hivi: “Mara nyingi mimi huambiwa kwamba sijui chochote. Wasomaji fulani hukasirika au kufadhaika, na kwa kuwa nyakati nyingine michezo hufanya hisia za watu kupanda, wengine hata wametisha kuniua.” Hivyo basi, ni nini huwachochea waandishi wa habari kuendelea na kazi yao?
Bila shaka, kwa wengine ni mshahara wanaopata. Lakini si wote. Mwandishi wa habari anayeandika makala katika gazeti fulani nchini Ufaransa alisema kwamba yeye hufurahia sana kuandika. Mwandishi mmoja wa habari huko Mexico alisema: “Angalau sisi hufaulu kutoa habari ambazo watu wanahitaji kujua.” Na huko Japani, mhariri mkuu wa gazeti la kila siku la pili kusomwa na watu wengi zaidi ulimwenguni alisema: “Mimi hufurahi ninapohisi kwamba nimewasaidia watu na haki inapotekelezwa.”
Bila shaka, si waandishi wa habari pekee wanaohusika katika uchapishaji wa magazeti. Ikitegemea ukubwa na mpangilio wa kampuni ya uchapishaji, huenda kukawa na wahariri, wasomaji wa nakala za masahihisho, wale wanaothibitisha ukweli wa habari zinazotolewa, wahifadhi-nyaraka, na wengine wengi wasiotajwa ambao hufanya kazi kwa bidii ili uweze kupata gazeti.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Gazeti la zamani la Ujerumani na magazeti ya kisasa
[Hisani]
Early German newspaper: Bibliothek für Kunst - und Antiquitäten-Sammler, Vol. 21, Flugblatt und Zeitung, 1922
-
-
Jinsi ya Kunufaika na MagazetiAmkeni!—2005 | Oktoba 22
-
-
Jinsi ya Kunufaika na Magazeti
“Mtu asiyesoma gazeti ni mpumbavu, na yule anayeamini mambo anayosoma kwa sababu tu yako katika gazeti ni mpumbavu hata zaidi.”—August von Schlözer, mwanahistoria na mwandishi wa habari Mjerumani aliyeishi mwishoni mwa karne ya 18.
KATIKA uchunguzi mmoja, maelfu ya watu huko Uingereza na Ufaransa waliulizwa walitumaini shirika gani zaidi kati ya mashirika 13. Vyombo vya habari vilivuta mkia, hata baada ya siasa na makampuni makubwa. Nchini Marekani, bado wasomaji wengi huamini magazeti ya kwao. Lakini uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew unaonyesha kwamba idadi ya watu wanaoamini magazeti imepungua.
Mara nyingi kuna sababu nzuri ya kushuku mambo yaliyoandikwa hasa ikiwa yanahusu masilahi ya nchi ambako gazeti hilo huchapishwa. Inakuwaje basi? Mara nyingi ukweli hupuuzwa. Kama vile mwanasiasa Mwingereza, Arthur Ponsonby, wa karne ya 20 alivyosema wakati mmoja: “Vita vinapotangazwa, Ukweli ndio huathiriwa kwanza.”
Hata wakati vita havijatangazwa, ni jambo la hekima kushuku kwa kadiri fulani habari unayosoma. “Mtu asiye na uzoefu huamini kila neno,” inasema methali moja ya Biblia, “lakini mtu mwerevu huzifikiria hatua zake.” (Methali 14:15) Ukiwa mwangalifu kwa kiasi fulani, magazeti yanaweza kutosheleza tamaa yako ya habari unazohitaji.
Umuhimu wa Habari
Vyombo vya habari ni muhimu leo kwa sababu vinatusaidia tujue mambo yanayotendeka ulimwenguni. Na ni muhimu kujua habari hizo. Kwa nini? Kwa sababu mambo mengi yanayotukia leo yalitabiriwa na nabii mkubwa zaidi aliyepata kuishi, Yesu Kristo. Alipoulizwa kuhusu mwisho wa mfumo huu wa mambo, alisema kwamba wakati wa mwisho kungekuwa na vita, ongezeko la uasi-sheria, upungufu wa chakula, tauni, matetemeko ya nchi, na matukio mengine yanayohusiana na hayo.—Mathayo 24:3-14; Luka 21:7-11.
Pia Biblia inasema: “Katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” Unabii huo unaongezea kusema kwamba katika ‘siku hizi za mwisho,’ watu watakuwa “wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda pesa,” na “wasiotii wazazi.” Watakuwa “wasio na upendo wa asili” na “wasiojizuia, wakali, wasiopenda wema, wasaliti, wenye vichwa vigumu, wenye kujivuna kwa kiburi, wanaopenda raha badala ya kumpenda Mungu.”—2 Timotheo 3:1-5.
Bila shaka unaona unabii huo wa Biblia ukitimizwa mahali unapoishi. Na kwa kweli matukio ya ulimwenguni pote ambayo yanaripotiwa katika magazeti huthibitisha usahihi wa unabii wa Biblia. Je, hiyo inamaanisha kwamba tunaweza kuamini mambo yote tunayosoma katika magazeti? La, hata watu ambao wamejitoa kufanya kazi ya kuandika magazeti wanasema kwamba tunahitaji kuwa waangalifu.
Elewa Matatizo Yanayohusika
Kila mtu, hata watu walio stadi na wanyoofu zaidi, hukosea. Ariel Hart aliandika hivi katika gazeti Columbia Journalism Review: “Katika miaka mitatu ambayo nimefanya kazi ya kujiajiri ya kuthibitisha ukweli wa habari zinazotolewa sijawahi kupata habari ambayo haikuwa na makosa, iwe ilikuwa ya kurasa tano au mafungu mawili.” Anataja mifano ya makosa aliyopata kama vile “mwaka usio sahihi; habari za zamani; makosa ya herufi; habari iliyosambazwa sana ambayo ilitokana na vyanzo visivyotegemeka.”
Lazima waandishi wa habari wakabiliane na vyanzo vya habari visivyotegemeka. Nyakati nyingine, mizaha hutumwa kwenye vyumba vya habari. Mnamo 1999, mfanya-mizaha mmoja aliweka kwenye Intaneti hadithi fulani ya uwongo kuhusu “bustani ya burudani kwenye makaburi,” na kuthibitisha habari hiyo kwa kutaja kituo chenye kuvutia cha kampuni ambayo ingejenga bustani hiyo na nambari ya simu ambayo mdanganyi huyo alitumia kwa ajili ya mahojiano akidai kuwa ni msemaji wa kampuni hiyo. Huduma za satelaiti za shirika la habari la Associated Press hazikugundua mzaha huo, na magazeti mengi ya kila siku huko Marekani yalichapisha habari hiyo. Inasemekana kwamba siri ya kufanikiwa kwa mizaha hiyo ni “kutunga hadithi yenye kusisimua iliyo na picha nyingi za ajabu-ajabu lakini zenye kuaminika.”
Hata waandishi wa habari wenye nia nzuri sikuzote hawaelewi hadithi kwa usahihi. “Kwa kawaida, waandishi wa habari hufanya kazi haraka-haraka,” anasema mwandishi mmoja huko Poland. “Magazeti yanashindana. Kila moja linataka liwe la kwanza kuchapisha habari. Kwa sababu hiyo, ingawa wengi wetu tungependa kuandika makala iliyofanyiwa utafiti mzuri, hatuwezi.”
Mkazo wa Kufuata Mapendezi ya Watu
Kichapo Freedom of the Press 2003—A Global Survey of Media Independence kiliorodhesha nchi 115 kati ya 193 kuwa hazina uhuru au zina uhuru wa kiasi tu. Hata hivyo, hata katika nchi zenye uhuru wa kusambaza habari, vyombo vya habari vinaweza kutumiwa vibaya kwa hila.
Nyakati nyingine, waandishi fulani wa habari hunyimwa habari muhimu, huku wale ambao huwapendeza wanasiasa huruhusiwa kuwahoji na hata kuandamana nao wanaposafiri. Pia mapato yanayotokana na matangazo ya biashara yanaweza kuathiri kuripotiwa kwa habari. Mwandishi mmoja wa habari huko Poland alisema: “Kampuni inayodhamini matangazo fulani katika magazeti inaweza kutisha kuondoa matangazo hayo ikiwa mhariri atachapisha habari mbaya kuihusu.” Na mhariri mmoja wa gazeti fulani huko Japani, ambaye husahihisha habari kabla haijachapishwa alionya hivi: “Kumbuka kwamba si rahisi hata kidogo kuripoti habari zisizopendelea upande wowote.”
Basi huenda ukauliza, ‘ikiwa waandishi stadi wa habari hukabili matatizo kama hayo ili kutokeza habari zinazoaminika, msomaji atajuaje habari anazopaswa kuamini?’
Maoni Yaliyosawazika Yanahitajika
Bila shaka, utambuzi unahitajiwa. Mzee wa ukoo Ayubu aliuliza hivi: “Je, sikio halipimi maneno kama kaakaa linavyoonja chakula?” (Ayubu 12:11) Msomaji anahitaji kuchunguza habari kwa uangalifu ili kuona kama ni ya kweli. Kwa hekima, yeye huipima na kuchagua habari ya kweli. Katika karne ya kwanza, mwanafunzi mmoja wa Yesu Kristo aliwasifu wale waliomsikiliza mtume Paulo lakini wakachunguza vyanzo vya habari ya Paulo ili kuthibitisha ukweli wa mafundisho yake.—Matendo 17:11; 1 Wathesalonike 5:21.
Vivyo hivyo, huenda msomaji wa gazeti akajiuliza maswali haya: Mwandishi wa habari ana uzoefu gani? Yeye huchukia mambo gani? Je, habari aliyoandika inataja mambo hakika ambayo watu wanaweza kuthibitisha? Je, kuna mtu yeyote ambaye angependa kupotosha ukweli wa habari hii? Kwa hekima, huenda msomaji akachunguza vyanzo mbalimbali ili kuthibitisha usahihi wa habari hiyo. Anaweza pia kuzungumza na wengine kuhusu mambo anayosoma. Methali moja ya Biblia inasema: “Anayetembea na watu wenye hekima atakuwa na hekima.”—Methali 13:20.
Wakati huohuo tusitazamie magazeti yaseme mambo kwa usahihi kabisa. Kama tulivyoona, kuna mambo mbalimbali ambayo huzuia magazeti yasiandike habari zisizopendelea upande wowote. Hata hivyo, bado yanaweza kukusaidia kujua mambo yanayotendeka ulimwenguni. Ni muhimu kujua mambo hayo kwa kuwa Yesu alipokuwa akizungumza kuhusu nyakati tunamoishi, alihimiza hivi: “Endeleeni kukesha.” (Marko 13:33) Magazeti yanaweza kukusaidia kukesha hata ingawa hayataji mambo kwa usahihi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]
VYOMBO VYA HABARI VINAPOONYESHA UBAGUZI
Mara nyingi, habari zenye kupotosha hutokana na ripoti zilizotayarishwa haraka-haraka au habari zisizo sahihi. Hata hivyo, habari hizo zilizotolewa kwa nia nzuri zinaweza kueneza upesi uwongo mbaya. Kwa upande mwingine, nyakati nyingine habari zenye kupotosha hutolewa kimakusudi, kama ilivyotukia katika Ujerumani ya Nazi wakati uwongo ulipoenezwa kuhusu watu wa jamii na dini fulani.
Fikiria matokeo ya kampeni ambayo haikufaulu iliyofanywa hivi karibuni ya kuwaharibia sifa Mashahidi wa Yehova katika kesi ya kupigania haki za binadamu huko Moscow, Urusi. “Wasichana watatu walipojiua huko Moscow,” gazeti The Globe and Mail la Toronto, Kanada, liliripoti kwamba “mara moja vyombo vya habari vya Urusi vilidokeza kwamba walikuwa wafuasi shupavu wa Mashahidi wa Yehova.”
Habari hizo zilichapishwa Februari 9, 1999, siku ambayo mahakama iliendeleza kesi iliyokusudiwa kuwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova jijini Moscow. Geoffrey York, ripota kwenye Kituo cha gazeti The Globe and Mail huko Moscow aliripoti hivi: “Baadaye polisi walikiri kwamba wasichana hao hawakuwa na uhusiano wowote na madhehebu hayo. Lakini kufikia wakati huo, tayari kituo kimoja cha televisheni huko Moscow kilikuwa kimeanzisha mashambulizi mapya dhidi ya madhehebu hayo, kikiwaambia watazamaji kwamba Mashahidi wa Yehova walishirikiana na Adolf Hitler katika Ujerumani ya Nazi licha ya uthibitisho wa kihistoria kwamba maelfu ya wafuasi wao waliuawa katika kambi za kifo za Nazi.”
Matokeo yalikuwa kwamba watu wengi wasiojua ukweli au wenye kuhofu waliwaona Mashahidi wa Yehova kuwa ama madhehebu ya kujiua au washirika wa Nazi!
[Picha katika ukurasa wa 7]
Yesu Kristo alitabiri mambo mengi tunayoona yakiripotiwa katika magazeti leo
[Picha katika ukurasa wa 8]
Mambo yanayoripotiwa katika magazeti huthibitisha unabii wa Biblia
[Hisani]
FAO photo/B. Imevbore
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Watu waliothibitisha vyanzo vya mafundisho ya mtume Paulo walisifiwa, hivyo basi ni jambo la hekima pia mtu kufanya hivyo anaposoma habari zisizo za kawaida
-