-
Uganda2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Ofisi ya tawi ilituma mapainia wawili, Robert Nisbet na David Norman, kuhubiri eneo hilo kubwa ambalo leo ni Kenya, Uganda, na Tanzania.
Ndugu hao waliazimia kuhubiri habari njema ya Ufalme mpaka vijijini. Walianza kampeni yao Dar es Salaam mnamo Agosti 31, 1931 wakiwa na katoni 200 za vitabu. Kisha wakaelekea Zanzibar na baadaye bandari ya Mombasa, wakiwa njiani kuelekea nyanda za juu za Kenya. Walisafiri kwa gari-moshi, wakihubiri katika miji iliyokuwa njiani mpaka walipofika ufuo wa mashariki wa Ziwa Victoria. Kisha mapainia hao wawili wenye ujasiri wakaabiri meli na kusafiri hadi Kampala, mji mkuu wa Uganda. Baada ya kugawa vitabu na magazeti mengi, na pia kupata maandikisho ya gazeti la The Golden Age, ndugu hao wawili waliendelea na safari yao kwa gari mpaka ndani zaidi nchini.
Miaka minne baadaye, mwaka wa 1935, mapainia wengine wanne kutoka Afrika Kusini walifunga safari ya kuja Afrika Mashariki. Mapainia hao ni Gray Smith na mke wake, Olga, pamoja na Robert Nisbet na ndugu yake mdogo, George. Wakiwa na magari mawili makubwa ambayo yangeweza kutumiwa kama makao, mapainia hao wajasiri walipitia barabara mbovu na vichakani. “Mara nyingi walilala msituni,” yasema ripoti moja, “wakapata kionjo halisi cha Afrika na kuishi pamoja na wanyama-mwitu. Waliwasikia simba wakinguruma usiku, punda-milia na twiga wakilisha kwa utulivu, hali kadhalika wanyama wakubwa kama vifaru na tembo.” Yote hayo hayakuwazuia kutembelea miji mbalimbali ambayo kamwe haikuwa imepata ujumbe wa Ufalme.
Gray na Olga Smith waliamua kukaa Tanganyika (ambako leo ni Tanzania), naye Robert na George Nisbet wakaelekea Nairobi, Kenya.
-
-
Uganda2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Picha katika ukurasa wa 69]
David Norman na Robert Nisbet walileta habari njema Afrika Mashariki
[Picha katika ukurasa wa 71]
George na Robert Nisbet na Gray na Olga Smith wakiwa na magari yao kwenye chelezo tayari kuvuka mto
-