-
Norway2012 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Norway
KNUD PEDERSON HAMMER, akiwa amesimama kwenye sitaha ya meli, alijawa na furaha nyingi alipoitazama pwani ya Norway. Awali, alihudumu katika Kanisa moja la Baptisti huko North Dakota, Marekani. Lakini mwaka mmoja mapema, Knud alikuwa amejiunga na Wanafunzi wa Biblia (ambao sasa ni Mashahidi wa Yehova). Sasa, katika mwaka wa 1892, alikuwa anarudi katika nchi alimozaliwa ili kuwahubiria marafiki na watu wa ukoo.
Wengi kati ya watu milioni mbili walioishi Norway walikuwa washiriki wa Kanisa la Kilutheri la Serikali. Knud alitamani sana kuwasaidia watu wanyoofu wa Norway kumjua Mungu wa kweli, Yehova, na pia kuwasaidia waelewe kwamba Mungu huyo mwenye upendo hawaadhibu watenda dhambi katika moto wa mateso. Alitaka pia kuwafundisha kuhusu Utawala wa Miaka Elfu wa Kristo utakaoigeuza dunia kuwa paradiso.
Meli ilipokaribia pwani, Knud alitazama kwa makini nchi hii maridadi—nchi nyembamba yenye milima mirefu iliyofunikwa kwa theluji, mikono-bahari yenye kupendeza na misitu mikubwa. Alitambua kwamba haingekuwa rahisi kufikia maeneo yenye watu wachache sana na ambayo yalikuwa na madaraja na barabara chache tu. Ingawa watu wengi wa Norway waliishi katika miji iliyokuwa ikipanuka siku baada ya siku, wengine waliishi katika maeneo ya mashambani, vijiji vya wavuvi, au katika visiwa vingi katika pwani ya Norway. Matokeo ya kazi ya Knud ya kuhubiri, na vilevile ukuzi wa ibada safi nchini Norway licha ya matatizo, yanaimarisha imani na kuwachochea watu wa Mungu kila mahali.
MBEGU YA UFALME YAZAA MATUNDA
Ingawa watu fulani walipendezwa na ujumbe wake, Knud hakukaa sana Skien, jiji la nyumbani. Alilazimika kurudi kwa familia yao nchini Marekani. Hata hivyo, mnamo 1899, alirudi tena Norway baada ya kuombwa na Charles T. Russell aliyekuwa msimamizi wa kazi ya Wanafunzi wa Biblia wakati huo. Ndugu Russell alitaka Knud aanzishe kutaniko nchini Norway. Knud alibeba nakala kadhaa za mabuku mawili ya kwanza ya vitabu Millennial Dawn (baadaye viliitwa Studies in the Scriptures), ambayo yalikuwa yametafsiriwa katika mchanganyiko wa Kinorway na Kidenishi. (Wakati huo, maandishi ya Kinorway yalifanana na ya Kidenishi, na machapisho yangeweza kusomwa nchini Denmark na Norway.) Knud aliwahubiria watu wengi na kuwaachia vitabu, lakini baada ya muda alilazimika kurudi Marekani tena.
Mwaka uliofuata, Ingebret Andersen, ambaye aliishi karibu na jiji la Skien, alipata kitabu The Plan of the Ages, ambacho huenda kilikuwa mojawapo ya nakala ambazo Knud alileta Norway. Kwa muda mrefu, Ingebret alipendezwa na habari kuhusu kuja kwa Kristo kwa “mara ya pili,” na sasa yeye na mke wake Berthe, walivutiwa na mambo waliyosoma. Punde si punde, Ingebret akaanza kuhubiri. Hata alienda kwenye mikutano ya kidini ili kuwaambia watu kuhusu Utawala wa Miaka Elfu wa Kristo. Baadaye, aliwatembelea watu waliopendezwa, na muda si muda kukawa na kutaniko la angalau Wanafunzi wa Biblia kumi jijini Skien.
Knud alipoambiwa na mtu wa ukoo kuhusu kutaniko hilo dogo jijini Skien, alirudi Norway mwaka wa 1904 kumtafuta Ingebret. Alisimama barabarani na kumuuliza mwanamume fulani, “Je, unamfahamu Ingebret Andersen?” Mwanamume huyo akajibu, “Ndiyo, ni mimi.” Knud alisisimka sana hivi kwamba alifungua mkoba wake papo hapo katikati ya barabara, na akaanza kumwonyesha Ingebret vitabu alivyokuwa navyo. Ingebret naye alifurahi kukutana na Knud na kuona machapisho hayo mengi.
Knud aliwaambia kwa shauku waamini wenzake wa Norway kuhusu tengenezo na kazi ya kuhubiri. Kufikia wakati aliporudi kwa familia yake, ambayo kwa sasa waliishi Kanada, kutaniko la Skien lilikuwa limetiwa moyo sana kusonga mbele.
KUYAFIKIA MAENEO MENGINE YA NORWAY
Kazi ya kuhubiri nchini Norway ilipata nguvu zaidi mwaka wa 1903 wakati makolpota (wahubiri wa wakati wote) watatu wenye bidii walipofika kusaidia. Watatu hao walikuwa Fritiof Lindkvist, Viktor Feldt, na E. R. Gundersen. Fritiof aliamua kuishi jijini Kristiania (ambalo sasa ni Oslo), na mwaka wa 1904 nyumba yake ilifanywa ofisi ya Watch Tower Society, ambapo maagizo ya machapisho na maandikisho ya Zion’s Watch Tower yalishughulikiwa.
Mwishoni mwa mwaka wa 1903, Ndugu Gundersen alipokuwa anahubiri eneo la Trondheim, alizungumza na Lotte Holm, ambaye alikubali machapisho. Baadaye mwanamke huyo alienda nyumbani huko Narvik, eneo lililo juu ya Mzingo wa Aktiki, na akawa mhubiri wa kwanza kaskazini mwa Norway. Baada ya hapo, Viktor Feldt alienda Narvik, akawahubiria wanaume fulani wawili na wake zao, na wote wakawa Wanafunzi wa Biblia. Walimtafuta Lotte na baada ya muda mfupi, wakawa wanakutana pamoja kujifunza Biblia. Hallgerd, dada ya Lotte, pia alikubali kweli na baadaye wote wawili wakawa mapainia wenye bidii katika sehemu mbalimbali nchini Norway.
Ndugu Feldt na Gundersen walikuwa na matokeo mazuri sana walipohubiri Bergen mwaka wa 1904 na 1905. Gazeti la Zion’s Watch Tower la Machi 1, 1905 liliripoti hivi: “Mhubiri mashuhuri wa kanisa la Free Mission la [Bergen] amesadikishwa kabisa na nuru iliyo wazi, na sasa anawaeleza wengine kuhusu Injili yote na iliyo ya kweli.”
Mhubiri huyo alikuwa Theodor Simonsen, ambaye baadaye alifukuzwa kutoka Kanisa la Free Mission kwa sababu ya kufundisha kweli nzuri mpya ambazo alijifunza katika machapisho yetu. Hata hivyo, Wanafunzi wa Biblia walimkaribisha Ndugu Simonsen. Watu wa Yehova walimpenda Theodor sana na pia alikuwa msemaji mzuri. Mwishowe, Ndugu Theodor aliamua kuishi Kristiania ambapo kulikuwa na kutaniko lililokuwa likiongezeka.
-
-
Norway2012 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Picha katika ukurasa wa 88]
Knud Pederson Hammer
-