-
Malengo ya Olimpiki YanazorotaAmkeni!—2000 | Septemba 8
-
-
Malengo ya Olimpiki Yanazorota
BARON Pierre de Coubertin alipopendekeza kuanzishwa upya kwa Michezo ya Olimpiki, aliweka malengo fulani yanayofaa. Hata, kanuni inayoongoza michezo ya Olimpiki ya kisasa, inayodhaniwa kuwa ilibuniwa na Coubertin, hutaarifu hivi: “Jambo muhimu zaidi katika Michezo ya Olimpiki si kushinda bali kushiriki . . . Jambo la maana si kutia fora bali kupambana vyema.”
Coubertin aliamini kwamba kushiriki mashindano yafaayo kungeweza kusitawisha sifa bora, kudumisha akili timamu, na kuendeleza mwenendo mnyoofu. Hata alitaja ‘dini ya michezo.’ Yeye alidhani kwamba Michezo ya Olimpiki ingeweza kufunza watu kuishi kwa amani.
Lakini kufikia wakati Coubertin alipokufa mwaka wa 1937, matumaini ya kufikia malengo hayo yalikuwa yamedidimia. Tayari michezo hiyo ilikuwa imeahirishwa pindi moja kwa sababu ya vita ya ulimwengu, na kulikuwa na wasiwasi mkubwa wa kuzuka kwa vita nyingine kuu. Leo, malengo ya michezo ya Olimpiki yamezorota hata zaidi. Mbona yanazorota?
Michezo ya Olimpiki na Dawa za Kulevya
Kwa miongo mingi wanariadha wametumia dawa za kulevya ili kuwawezesha kutia fora, na Michezo ya Olimpiki imekumbwa na tatizo hilo pia. Kwa kweli, sasa miaka 25 tangu kuanzishwa kwa ule unaoonwa kuwa upimaji makini wa matumizi ya dawa za kulevya, wanariadha katika Michezo ya Olimpiki wangali wanaendelea kutumia dawa za kulevya zilizopigwa marufuku.
Baadhi ya wanariadha hutumia steroidi za kuongeza nguvu mwilini ili kuwashinda wenzao. Wengine hutumia dawa zinazochochea utendaji wa mwili. Homoni za ukuzi wa binadamu hutumiwa mno na wakimbiaji wa mbio za masafa mafupi na wanariadha wengine wa mashindano magumu sana kwa sababu huwasaidia kupata nguvu haraka baada ya mazoezi makali, pia hujenga misuli. Wakati huohuo, wakimbiaji wa masafa marefu, waogeleaji, na wale wanaoteleza thelujini kwa safari ndefu hupenda kutumia homoni iliyogeuzwa maumbile ya erythropoietin kwa sababu inazidisha ustahimilivu wao kwa kuchochea damu itokeze chembe nyingi nyekundu.
Ndiyo sababu, Dakt. Robert Voy, aliyekuwa mkurugenzi wa upimaji wa matumizi ya dawa za kulevya wa Kamati ya Olimpiki ya Marekani, anawaita wanariadha “maabara inayotembea.” Yeye aongezea hivi: “Michezo ya Olimpiki imekuwa mahali pa majaribio kwa wanasayansi, wanakemia, na madaktari wasio na ujuzi.” Vipi juu ya upimaji? Dakt. Donald Catlin, mkurugenzi wa maabara moja ya kupima utumiaji wa dawa za kulevya huko Marekani, asema: “Mwanariadha anayejiona kuwa na busara na anayetaka kutumia dawa za kulevya amegeukia dawa nyingine tusizoweza kupima.”
Rushwa na Ufisadi
Kwa kuwa ni majiji machache tu yanayoweza kufaulu kupata kibali cha kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki, baadhi yake hufanya juu chini ili kupata fursa hiyo. Miaka miwili hivi iliyopita, Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki (IOC) ilikumbwa na kashfa. Maadili ya wale waliohusika katika uteuzi yalitiliwa shaka kwa sababu ya madai ya kwamba washiriki wa IOC walipokea rushwa ya dola 400,000 za Marekani ili kukubali ombi la Jimbo la Salt Lake la kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi Kali ya mwaka wa 2002.
Mara nyingi si rahisi kubainisha ukarimu na rushwa ya peupe kwani majiji yanayowania nafasi ya kuwa mwenyeji wa michezo huwakabidhi zawadi kemkemu wale wanaoteua mahali pa kufanyia michezo hiyo. Washiriki wapatao 20 wa IOC walituhumiwa katika kashfa ya Jimbo la Salt Lake, na 6 kati yao waliachishwa kazi hatimaye. Kwa habari ya Michezo ya mwaka wa 2000 itakayofanyika Australia, jitihada yote ya kudumisha sifa njema ilitokomea wakati msimamizi wa Kamati ya Olimpiki ya Australia alipokiri hivi: “Kwa kweli, hatukufaulu kupata fursa hiyo kwa sababu ya umaridadi wa jiji wala wa vifaa vya michezo peke yake.”
Maisha ya ubadhirifu ya baadhi ya maofisa wakuu wa IOC yamezidisha shaka. Mswisi aliyekuwa msimamizi wa Shirikisho la Kimataifa la Upigaji-Makasia, Tommy Keller, pindi moja alisema kwamba kwa maoni yake maofisa fulani wa michezo huona Michezo ya Olimpiki kuwa njia ya “kutosheleza fahari yao ya kibinafsi.” Aliongezea kusema kwamba yaonekana wanachochewa na “pupa ya fedha na tamaa ya makuu.”
Uchumaji wa Fedha Nyingi Sana
Hakuna mtu awezaye kubisha kuwa Michezo ya Olimpiki huchuma fedha nyingi sana. Kwa kawaida, huvutia watazamaji wa televisheni chungu nzima na matangazo ya kibiashara yenye kuleta faida, ni mambo yanayowaletea wafadhili wa michezo hiyo kiasi kikubwa sana cha fedha.
Fikiria Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 1988, iliyodhaminiwa na makampuni tisa ya kimataifa ambayo yalilipa IOC jumla ya zaidi ya dola milioni 100 za Marekani ili kupata idhini ya kutangaza michezo hiyo ulimwenguni pote. Michezo ya mwaka wa 1996 ya Majira ya Kiangazi huko Atlanta ilichuma jumla ya dola milioni 400 za Marekani kutokana na matangazo. Bila kutia ndani idhini kwa vituo vya televisheni. Kituo kimoja cha mfumo wa televisheni huko Marekani kililipa zaidi ya dola bilioni 3.5 za Marekani ili kupata idhini ya kutangaza Michezo ya Olimpiki kati ya mwaka wa 2000 na 2008, na iliripotiwa kwamba wafadhili 11 ulimwenguni pote watahitaji kulipa dola milioni 84 za Marekani kila mmoja kwa kipindi cha miaka minne. Hivyo, watu fulani wamesema kwamba ijapokuwa hapo awali Michezo ya Olimpiki ilikuwa ikidhihirisha ufanisi wa mwanadamu, leo michezo hiyo huwapa wanadamu wenye pupa fursa ya kuchuma fedha nyingi sana.
Mbona Kuna Kasoro?
Baadhi ya wataalamu husema kwamba kuzorota kwa Michezo ya Olimpiki kulisababishwa na matukio mawili makuu mapema miaka ya 1980. La kwanza ni uamuzi wa kuidhinisha kila shirikisho la kimataifa la michezo kuweza kuteua wanariadha wanaofaa kushiriki Olimpiki. Ijapokuwa IOC ilikuwa imeruhusu tu wanariadha wasiolipwa kushiriki, mashirikisho hayo yalianza kuruhusu wanariadha wanaolipwa kushiriki mashindano mbalimbali ya Olimpiki. Lakini wanariadha wanaolipwa walijiona kuwa bora. Hungeweza kupokea donge nono kutoka kwa watangazaji kwa ‘kupambana vyema’ tu, kwa hiyo punde si punde ushindi ukawa jambo muhimu kupita yote. Si ajabu kwamba wazo hilo limeendeleza matumizi ya dawa za kulevya za kuwawezesha kutia fora.
Jambo la pili kuu lilitukia mwaka wa 1983 wakati IOC iliponuia kuchuma faida kwa kutumia kile kilichoitwa na mtaalamu wake wa uuzaji, “alama muhimu zaidi isiyopata kutumiwa ulimwenguni”—duara za Olimpiki. Alama hiyo ilizua mashindano makali ya kibiashara ambayo yamekuwa ya kawaida katika Michezo ya Olimpiki. Jason Zengerle alisema: “Licha ya matumaini yote ya kudumisha amani na kuunganisha ulimwengu wote . . . , kwa kweli Michezo ya Olimpiki ni sawa tu na . . . mashindano mengineyo mashuhuri ya michezo.” Lakini je, hilo lamaanisha kwamba malengo yaliyopendekezwa na chama cha Olimpiki hayawezi kutimizwa?
-
-
Kutimiza Hayo MalengoAmkeni!—2000 | Septemba 8
-
-
Kutimiza Hayo Malengo
NIA njema, udugu, amani ya kimataifa—ni nani ambaye hawezi kusifu malengo bora kama hayo? Baron Pierre de Coubertin, aliyeanzisha upya Michezo ya Olimpiki, aliamini kwamba michezo hiyo ingeshinda chuki za kitaifa kwa kudumisha staha ya washiriki bila kujali jamii, dini, au jinsia. Alihisi kwamba “ulimwengu bora ungeweza kuletwa tu na watu walio bora.” Lakini je, michezo yaweza kuleta amani ulimwenguni? Hatuna budi kujibu la, tuchunguzapo historia yake.
Ingawa michezo ina sehemu yake, elimu ya Biblia ndiyo ufunguo wa kudumisha amani ya kweli. Kwa kweli, kanuni za Biblia zaweza kutokeza “watu walio bora,” kama walivyoitwa na Coubertin. Chunguza maandiko kadhaa yanayoweza kudumisha amani miongoni mwa watu wanaoyatumia, bila kujali taifa lao.
“Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.”—Yohana 13:35.
“Ikiwezekana, kwa kadiri itegemeavyo nyinyi, iweni wenye kufanya amani na watu wote.”—Waroma 12:18.
“Maadamu tuna wakati wenye kufaa kwa ajili ya hilo, acheni sisi tufanye lililo jema kuelekea wote.”—Wagalatia 6:10.
“Bila kufanya jambo lolote kwa ugomvi au kwa majisifu ya bure, bali kwa hali ya akili ya kujishusha chini mkifikiria kwamba wengine ni wakubwa kuliko nyinyi.”—Wafilipi 2:3.
“Mazoezi ya kimwili ni yenye manufaa kidogo; lakini ujitoaji-kimungu ni wenye manufaa kwa mambo yote, kwa kuwa una ahadi ya uhai wa sasa na ule utakaokuja.”—1 Timotheo 4:8.
Je, kweli kanuni hizo za kimaandiko hufanya kazi? Fikiria jambo lililotukia huko Munich, Ujerumani. Mnamo mwaka wa 1974, miaka miwili tu baada ya michezo ya Olimpiki iliyofanyika katika jiji hilo kuvurugwa na ugaidi na mauaji, Mashahidi wa Yehova walikuwa na mkusanyiko wa kimataifa katika Uwanja wa Olimpiki. Baadhi ya wajumbe waliohudhuria walitoka Ugiriki na Uturuki—nchi zilizokuwa zikipigana. Wakati huohuo wa kiangazi, wanajeshi wa Ugiriki na Uturuki walikuwa wakigombania kisiwa cha Cyprus. Je, hilo lingeathiri Wakristo waliokuwa wakihudhuria mkusanyiko huo? La! Iligusa moyo kama nini kuona Wagiriki na Waturuki wakikumbatiana na kuitana ndugu na dada!
Mashahidi wa Yehova wanajulikana ulimwenguni pote kwa sababu ya kuwa na mahusiano ya amani yanayokiuka mipaka ya kitaifa, kimbari, na kikabila. Bila shaka, wao hawadai kwamba wametimiza kikamili lengo la muungano na ushirikiano wa ulimwenguni pote. Kama mtu yeyote yule, ni sharti wajitahidi kufuata shauri la mtume Mkristo Paulo: “Uvueni utu wa zamani pamoja na mazoea ya huo, na mjivike wenyewe utu mpya.” (Wakolosai 3:9, 10) Hata hivyo, wao huamini kwa dhati kwamba kufuata kanuni za Biblia kwaweza kuwasaidia watu ‘watafute sana amani na kuifuatia.’—1 Petro 3:11.
Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi wamedhihirisha sifa mbaya sana licha ya malengo bora ya Michezo ya Olimpiki. Kinyume cha hilo, Neno la Mungu lenye nguvu husaidia watu wawe na sifa bora zaidi, na kudumisha nia njema na amani ya kimataifa.
-