-
Kwa Nini Nitunze Afya Yangu?Amkeni!—2010 | Juni
-
-
Kula Vizuri—Uwe na Afya Nzuri!
Biblia inatuhimiza tuwe na kiasi katika mazoea yetu. Methali 23:20 inasema hivi: “Usiwe . . . kati ya watu wanaokula . . . kwa ulafi.” Si rahisi kufuata himizo hilo.
● “Kama vijana wengi, mimi huhisi njaa kila wakati. Wazazi wangu wamefananisha tumbo langu na shimo lisilo na mwisho!”—Andrew, 15.
● “Kwa sasa sioni ubaya wa kula chakula fulani kwa kuwa sihisi madhara yake.”—Danielle, 19.
Je, unahitaji kudhibiti jinsi unavyokula? Yafuatayo ni mambo yaliyowasaidia vijana wenzako.
Sikiliza tumbo lako. “Nilikuwa nikihesabu kalori, lakini sasa mimi huacha kula ninapohisi nimeshiba,” anasema Julia, mwenye umri wa miaka 19.
Epuka chakula kisicho na lishe bora. “Nilipoacha kunywa soda, nilipunguza kilo tano baada ya mwezi mmoja,” anasema Peter, mwenye umri wa miaka 21.
Badili mazoea yako ya kula. “Mimi hujaribu sana nisiongeze chakula,” anasema Erin, mwenye umri wa miaka 19.
Siri ya Kufanikiwa: Usikose kula hata mlo mmoja! Ukikosa utahisi njaa na huenda ukashawishika kula chakula kingi.
-
-
Kwa Nini Nitunze Afya Yangu?Amkeni!—2010 | Juni
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
“NILIBADILI MAISHA YANGU”
“Nilipokuwa na umri wa miaka sita, nilikuwa mzito kidogo ikilinganishwa na umri wangu. Kisha, polepole niliacha kuonjaonja chakula mara kwa mara na nikaanza kula wakati wote hasa vyakula visivyo na lishe bora! Kwa kuwa sikupenda kutumia nguvu, sikufanya kazi yoyote ngumu. Bila kutambua nikawa mnene kupita kiasi, jambo ambalo sikutaka. Nilihuzunishwa sana na jinsi nilivyoonekana na kuhisi! Mara kadhaa nilijaribu kupunguza uzito kwa kula chakula maalumu lakini baada ya muda nilinenepa tena. Mwishowe nilipokuwa na umri wa miaka 15 niliamua kubadili maisha yangu. Nilitaka kupunguza uzito kwa njia inayofaa—njia ambayo ningeweza kudumisha katika maisha yangu yote. Nilinunua kitabu kilichozungumzia kanuni za msingi za lishe na kufanya mazoezi, na nikaanza kufanyia kazi kile nilichosoma. Niliazimia kuendelea hata ikiwa nitashindwa kula chakula kinachofaa na kufanya mazoezi au hata kama ningevunjika moyo. Matokeo? Nilifaulu! Baada ya mwaka mmoja nilipunguza kilo 25. Nimedumisha uzito huo kwa miaka miwili. Sikufikiri ningefaulu! Nafikiri nilifaulu kwa kuwa sikula tu chakula fulani maalumu bali pia nilibadili maisha yangu. Nilipoelewa kuwa hali hiyo ingeathiri kila sehemu ya maishani yangu, nilikuwa tayari kufanya mabadiliko yaliyohitajika.”—Catherine, 18.
-