Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Papua New Guinea
    2011 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • KUHUBIRI KATIKA “KIJIJI KIKUBWA”

      Katika Septemba 22, 1951, miaka 12 baadaye, Tom Kitto, Mwaustralia mrefu mwenye umri wa miaka 47, alitua kwa ndege huko Port Moresby, eneo lenye joto jingi na unyevunyevu. Alikuwa amekubali mwito uliowataka wajitoleaji waanze kuhubiri katika visiwa vya Pasifiki. Mke wake, Rowena, alijiunga naye majuma sita baadaye. Eneo lao lilikuwa nchi yote ya Papua New Guinea.

      Kitto na mke wake walitambua kwamba watu wengi kutoka Ulaya walikuwa na ubaridi kuelekea ujumbe wa Ufalme. Kisha wakakutana na Geoff Bucknell, Mwaustralia mwenzao ambaye alikuwa amefifia kutoka kwenye kweli alipokuwa kijana. Geoff alikubali kujifunza na baadaye akawa Shahidi mwaminifu, pamoja na mke wake, Irene.

      Kisha Tom na Rowena wakahamia Hanuabada, jina linalomaanisha “Kijiji Kikubwa” katika lugha ya wenyeji ya Motu. Kijiji hicho kilifika hadi kwenye Bandari ya Port Moresby na kilikuwa na mamia ya nyumba zilizotengenezwa juu ya nguzo za mbao na kuunganishwa na vijia virefu vya mbao vinavyofika hadi ufuoni. “Watu walituzunguka ili wasikilize habari njema,” anaandika Rowena. “Watu wengi sana walipendezwa hivi kwamba tulirudi kila jioni kuongoza mafunzo ya Biblia, tulikosa kurudi jioni mbili tu katika miezi miwili.” Tom anaongeza hivi: “Tumaini la ufufuo na kuishi katika paradiso duniani liliwavutia sana watu hawa. Wamishonari wa dini zinazodai kuwa za Kikristo na polisi wa eneo hilo walijaribu kuwafanya waache kujifunza, lakini waliendelea kuwa imara. Kweli ilikuwa imeingia ndani sana ya mioyo yao.”

      Raho na Konio Rakatani, Oda Sioni, Geua Nioki na mume wake, Heni Heni aliyekuwa amepata vichapo kutoka kwa wahubiri waliowasili katika mashua inayoitwa Lightbearer miaka 16 mapema, ni baadhi ya wale ambao walichukua msimamo imara kwa ajili ya kweli. Punde si punde, watu 30 hivi walikuwa wakihudhuria mikutano kwa ukawaida katika nyumba ya Heni Heni. “Wanaume waliketi upande mmoja na wanawake upande ule mwingine katika chumba hicho,” anakumbuka Oda Sioni, ambaye alikuwa kijana wakati huo. “Wanawake walivalia sketi za nyasi na hawakuwa na blauzi na waliwabeba watoto katika mifuko yenye kuvutia iliyofumwa kwa nyuzi na ilining’inizwa kwenye nguzo za chumba hicho. Baada ya kuwanyonyesha watoto, waliwatia ndani ya mifuko hiyo na kuibembeza polepole hadi watoto walipolala.”

      Tom Kitto aliongoza mikutano hiyo akisaidiwa na mtafsiri. Nyakati nyingine mambo yalienda mrama. “Katika mkutano mmoja, ndugu ya Heni Heni, Badu Heni, alikuwa akitafsiri,” anaeleza Don Fielder, aliyefika huko katika mwaka wa 1953. “Mwanzoni ilionekana kwamba mambo yalikuwa shwari, kwa kuwa Badu alitafsiri maneno ya Tom na hata aliiga ishara zake. Baadaye tu ndipo Badu alimwambia Tom kuwa hakuelewa chochote ambacho alikuwa akisema. Alisema tu kweli alizokuwa amejua hapo awali na kuiga ishara za Tom ili ionekane kwamba hivyo ndivyo hotuba ilivyosema.” Licha ya hali hizo ngumu, kikundi hicho kilikua upesi, na baada ya muda kikundi cha pili kilianzishwa katika nyumba ya Raho Rakatani, ambayo pia ilikuwa kwenye kijiji cha Hanuabada.

      “NJOO UWAFUNDISHE WATU WANGU”

      Mapema katika mwaka wa 1952, Bobogi Naiori, chifu wa eneo la Koiari ambaye pia alikuwa mchawi maarufu, alimtembelea Heni Heni, kwani alikuwa wantok wake, au mtu wa kabila lake, na akahudhuria mkutano katika nyumba yake. Kwa kuwa alivutiwa na mambo aliyoona na kusikia, baadaye Bobogi alimwendea Tom Kitto na kumsihi: “Tafadhali, njoo uwafundishe watu wangu kuhusu kweli!”

      Muda mfupi baadaye, Tom na Rowena walisafiri kwa gari lao kuukuu kupitia barabara za udongo kufika nyumbani kwa Bobogi huko Haima, kijiji kidogo kilicho umbali wa kilomita 25 hivi kaskazini ya Port Moresby. Tom aliwahubiria wanakijiji waliokuwa wamekusanyika na Bobogi akatafsiri. Kuanzia wakati huo, watu 30 hivi wakaanza kujifunza Biblia.

      Baadaye katika mwezi huo, kikundi kilichokuwa huko Haima kilijenga jumba dogo kwa ajili ya mikutano ya Kikristo. “Jumba hilo lilikuwa na kiunzi cha mbao, paa lililoezekwa kwa nyasi, na kuta zilizofika kiunoni zilizofumwa kwa mianzi,” anakumbuka Elsie Horsburgh ambaye baadaye alihudhuria mikutano huko. “Ndani kulikuwa tu na viti vya mbao, taa ya mafuta, na ubao mweusi mdogo.” Jengo hilo la hali ya chini likawa Jumba la Ufalme la kwanza nchini Papua New Guinea.

      Bobogi alitaka watu wa kabila yake walioishi katika milima ya karibu wasikie habari njema. Kwa hiyo, yeye na Tom walitembea kwenye barabara iliyokuwa kwenye mwinuko mkali hadi kwenye uwanda wa juu wa Sogeri. Baada ya muda mfupi walikuwa wakijifunza na zaidi ya watu 90 katika vijiji vitatu huko.

  • Papua New Guinea
    2011 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • ◼ DADA yangu mkubwa alipowaona Tom na Rowena Kitto wakihubiri kwenye vijia vya mbao vya kijiji cha Hanuabada, aliniambia nihudhurie mikutano yao ili niweze kuchunguza hiyo “dini mpya.” Wakati huo mikutano ilikuwa ikifanywa nyumbani mwa Heni Heni Nioki, aliyekuwa akijifunza Biblia.

      Nilikuwa na umri wa miaka 13 na nilikuwa mwenye haya sana. Nilienda nyumbani kwa Heni Heni ambako wanakijiji 40 hivi walikuwa wamekusanyika, na nikaketi kimya nyuma ya kila mtu nikiwa nimefunika uso wangu kwa mikono. Nilifurahia mambo niliyosikia na hivyo nikarudi tena na tena. Baada ya muda, Heni Heni akaniomba nimtafsirie Tom Kitto kutoka Kiingereza hadi Kimotu, lugha iliyozungumzwa na wengi kati ya waliohudhuria.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki