Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Papua New Guinea
    2011 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • Raho na Konio Rakatani, Oda Sioni, Geua Nioki na mume wake, Heni Heni aliyekuwa amepata vichapo kutoka kwa wahubiri waliowasili katika mashua inayoitwa Lightbearer miaka 16 mapema, ni baadhi ya wale ambao walichukua msimamo imara kwa ajili ya kweli. Punde si punde, watu 30 hivi walikuwa wakihudhuria mikutano kwa ukawaida katika nyumba ya Heni Heni. “Wanaume waliketi upande mmoja na wanawake upande ule mwingine katika chumba hicho,” anakumbuka Oda Sioni, ambaye alikuwa kijana wakati huo. “Wanawake walivalia sketi za nyasi na hawakuwa na blauzi na waliwabeba watoto katika mifuko yenye kuvutia iliyofumwa kwa nyuzi na ilining’inizwa kwenye nguzo za chumba hicho. Baada ya kuwanyonyesha watoto, waliwatia ndani ya mifuko hiyo na kuibembeza polepole hadi watoto walipolala.”

  • Papua New Guinea
    2011 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 83, 84]

      “Niliacha Kuwa Mwenye Haya”

      ODA SIONI

      ALIZALIWA 1939

      ALIBATIZWA 1956

      MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Painia wa kwanza kati ya wenyeji wote wa Papua New Guinea. Sasa anatumika akiwa painia wa pekee katika Kutaniko la Hohola Motu, huko Port Moresby.

      ◼ DADA yangu mkubwa alipowaona Tom na Rowena Kitto wakihubiri kwenye vijia vya mbao vya kijiji cha Hanuabada, aliniambia nihudhurie mikutano yao ili niweze kuchunguza hiyo “dini mpya.” Wakati huo mikutano ilikuwa ikifanywa nyumbani mwa Heni Heni Nioki, aliyekuwa akijifunza Biblia.

      Nilikuwa na umri wa miaka 13 na nilikuwa mwenye haya sana. Nilienda nyumbani kwa Heni Heni ambako wanakijiji 40 hivi walikuwa wamekusanyika, na nikaketi kimya nyuma ya kila mtu nikiwa nimefunika uso wangu kwa mikono. Nilifurahia mambo niliyosikia na hivyo nikarudi tena na tena. Baada ya muda, Heni Heni akaniomba nimtafsirie Tom Kitto kutoka Kiingereza hadi Kimotu, lugha iliyozungumzwa na wengi kati ya waliohudhuria.

      Miaka kadhaa baadaye, nilipoanza kufanya kazi katika hospitali ya karibu nikiwa na mradi wa kuwa daktari, John Cutforth alizungumza nami faraghani na kuniambia hivi, “Ukiwa daktari wa kitiba, utawasaidia watu kimwili, lakini ukiwa ‘daktari’ wa kiroho, unaweza kuwasaidia kupata uzima wa milele.” Juma hilohilo nikaanza kufanya upainia.

      Mgawo wangu wa kwanza ulikuwa huko Wau. Nilikuwa nimetembelea mji huo na nikapata watu kadhaa wanaopendezwa na kweli. Mwanamume mmoja anayeitwa Jack Arifeae, aliniomba nikahubiri katika kanisa la Kilutheri la eneo hilo. Nilichagua kuzungumzia sheria ya Mungu kuhusu damu. Watu 600 waliohudhuria walinisikiliza kwa makini, kwa kuwa wengi wao waliamini kwamba iwapo wangekula damu ya mtu mwingine basi roho yake ingetawala mwili wao. Kasisi alikasirika sana na kuwaambia wasikilizaji kwamba hawapaswi kushirikiana nami hata kidogo. Lakini wengi wao walifurahia mambo waliyosikia na wakafanya maendeleo ya kiroho.

      Mwaka mmoja hivi baadaye, nilipewa mgawo huko Manu Manu, kilomita 50 hivi kaskazini-magharibi ya Port Moresby. Nilikutana na chifu wa eneo hilo, Tom Surau ambaye aliniomba nihubiri katika kijiji chake. Baada ya kujifunza na wanakijiji kwa siku tatu, walivunja-vunja sanamu yao ya mbao ya Bikira Maria na kuitupa ndani ya mto.

      Watu waliokuwa wakiishi eneo la chini zaidi walikusanya vipande hivyo na kuvipeleka kwa makasisi Wakatoliki katika kijiji chao, wakisema, “Wamemwua Maria!” Makasisi wawili walikuja kwangu. Mmoja wao alinijia moja kwa moja na kunipiga ngumi usoni na pete yake ikanikata usoni. Wanakijiji walipokuja kunisaidia, makasisi hao walitoroka.

      Nilisafiri hadi Port Moresby ili jeraha langu likashonwe na ili nipige ripoti kwa polisi. Baadaye, makasisi hao walilazimika kulipa faini na wakaondolewa katika wadhifa wao. Wakati huo, nilirudi kijijini na kuanzisha kikundi katika eneo hilo la mbali. Kwa msaada wa Yehova, niliacha kuwa mwenye haya.

      [Picha]

      Mikutano ya kwanza ilifanywa katika nyumba ya Heni Heni

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki