-
Papua New Guinea2011 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Kazi ya kuhubiri ya Don na Shirley ilimkasirisha sana kasisi wa Kanisa la United la eneo hilo, ambaye alimshinikiza mwenye shamba awaamuru waondoe nyumba yao kutoka kwenye shamba lake. “Watu wa kijiji cha karibu waliposikia jambo hilo, walikasirika sana kwa sababu hawakutaka tuondoke,” anasema Don. “Watu 20 hivi walitusaidia kuhamisha nyumba yote kutia ndani msingi wake, hadi kwenye shamba lingine lililokuwa la kijiji chao.”
Kasisi huyo aliyekasirika hakukata tamaa. Alijitahidi kuwashinikiza wenye mamlaka wa Port Moresby watupige marufuku tusijenge nyumba yetu popote katika wilaya hiyo. “Badala ya kuondoka katika mgawo wetu,” anasema Don, “tulimwomba Alf Green, fundi stadi wa mbao, achukue mbao za nyumba hiyo yetu na kujenga chumba kidogo juu ya mtumbwi wetu. Kisha tukatia nanga katika kinamasi cha mikoko karibu na mlango wa mto uliokuwa karibu. Tuliishi na kufanya upainia tukiwa mahali hapo penye mbu wengi na mamba kwa miaka miwili na nusu iliyofuata.”
-
-
Papua New Guinea2011 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Wanaume hao waliporudi nyumbani kwa ajili ya likizo, Lance na Jim Chambliss waliamua kuwatembelea kwa majuma mawili na hivyo kufikisha habari njema huko Kerema.
“Kijiji chote kilikusanyika ili kutusikiliza,” akaandika Lance. “Wakati tulipokuwa tukizungumza, kasisi wa Sosaiti ya Wamishonari ya London aliingia ghafula na kumshambulia mtafsiri wetu na kumpiga ngumi mara kadhaa kabla ya wanakijiji kumzuia. Alisisitiza kwamba watu wa eneo hilo hawakutaka tuwe katika eneo lao na akatuamuru tuondoke eneo ‘lake.’ Basi tukasema kwamba wale waliotaka kutusikiliza watufuate hadi upande ule mwingine wa kijiji, na wale wengine wabaki naye. Kijiji chote kilitufuata.
“Asubuhi iliyofuata, tulienda kumwona mkuu wa wilaya ili turipoti kile kilichokuwa kimetendeka. Njiani tulikutana na mwanamke aliyekuwa mgonjwa sana. Tulimwambia kwamba tungempeleka hospitali, lakini aliogopa kwenda. Baada ya kumbembeleza sana alikubali kuandamana nasi. Tulimwacha na daktari kisha tukaenda kumwona mkuu wa wilaya ambaye kwa wazi hakufurahi kutuona. Hata alitushtaki kwa ukali kwamba tuliwafundisha watu wasikubali matibabu! Hata hivyo, wakati huohuo daktari yule wa hospitali aliingia na kumsikia akitushtaki hivyo. Alimwambia mkuu huyo kwamba tulikuwa tumemsadikisha mwanamke mgonjwa aende hospitalini akatibiwe. Kwa kupendeza, mkuu huyo aliomba msamaha mara moja. Alituambia kwamba kasisi Mkatoliki wa eneo hilo alikuwa amemtembelea na kumwambia uwongo kuhusu imani yetu. Alitupa polisi wawili waliojihami watulinde ili tusishambuliwe tena. Ilikuwa ajabu kwetu kuwa na polisi wawili wenye bunduki wakiketi pamoja nasi katika mafunzo yetu ya Biblia!”
-