-
Je, Elementi Zilitokea kwa Nasibu?Amkeni!—2000 | Oktoba 8
-
-
Vipi kani zinazoshikanisha chembe hizo za atomu? “Kuanzia chembe yake ndogo sana hadi galaksi kubwa zaidi, kila kitu katika Ulimwengu hufuata sheria zinazotajwa kuwa sheria za fizikia,” chaeleza kichapo The Encyclopedia of Stars & Atoms. Hebu wazia kile ambacho kingetukia iwapo mojawapo ya sheria hizo ingebadilika. Mathalani, vipi ikiwa tungebadilisha kani inayofanya elektroni zizunguke kiini cha atomu?
Kani Zilizopimwa kwa Usahihi Kabisa
Fikiria matokeo endapo kani ya sumaku-umeme ingefanywa dhaifu. “Elektroni hazingeshikamana na atomu,” asema Dakt. David Block katika kitabu chake Star Watch. Hilo lingemaanisha nini? “Utendaji wa kemikali haungeweza kutukia ulimwenguni!” aongezea. Twapaswa kuwa wenye shukrani kama nini kwa sababu ya sheria madhubuti zinazowezesha utendaji wa kemikali utukie! Mathalani, atomu mbili za hidrojeni huungana na atomu moja ya oksijeni ili kufanyiza molekuli muhimu sana ya maji.
Kani ya sumaku-umeme ni dhaifu mara 100 hivi kuliko kani ya nyuklia yenye nguvu ambayo hushikanisha kiini cha atomu. Ni nini kingetukia iwapo uwiano huo ungebadilishwa? “Kama uwiano kati ya kani ya nyuklia na kani ya sumaku-umeme ungebadilishwa kidogo tu, atomu za kaboni zingetokomea,” waeleza wanasayansi John Barrow na Frank Tipler. Uhai ungekoma kuwapo pasipo kaboni. Kaboni hufanyiza asilimia 20 ya uzani wa viumbe wote walio hai.
Jambo jingine muhimu zaidi ni nguvu za kani ya sumaku-umeme ilinganishwapo na nguvu za uvutano. “Badiliko kidogo sana la uwiano wa nguvu za uvutano na kani ya sumaku-umeme,” laeleza gazeti New Scientist, “lingefanya nyota kama Jua kuwa na joto kali kupindukia au kuwa na mwangaza hafifu mno [kiasi cha kutoweza kutegemeza uhai].”
Kani nyingine, ile kani dhaifu ya nyuklia, hudhibiti kasi ya utendaji wa nyuklia katika jua. “Ni dhaifu kiasi tu cha kuwezesha hidrojeni iliyo katika jua ichomeke polepole kwa kiwango kilekile,” aeleza mwanafizikia Freeman Dyson. Twaweza kutoa mifano mingine mingi inayoonyesha kwamba uhai wetu unategemea hali na sheria tata zenye usawaziko zilizo katika ulimwengu. Mwandikaji wa sayansi Profesa Paul Davies alilinganisha hali na sheria za ulimwengu na seti ya vifundo kisha akasema: “Yaonekana kwamba ni lazima vifundo hivyo tofauti vipimwe kwa usahihi kabisa ikiwa ulimwengu utakuwa katika hali itakayofanya uhai usitawi.”
Zamani za kale kabla Sir Isaac Newton hajagundua sheria ya nguvu za uvutano, Biblia ilirejezea amri au sheria hizo madhubuti. Mwanamume aitwaye Yobu aliulizwa hivi: “Je! unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia?” (Ayubu 38:33) Maswali mengine yenye kunyenyekeza aliyoulizwa yalikuwa, “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi?” na, “Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua?”—Ayubu 38:4, 5.
-
-
Je, Elementi Zilitokea kwa Nasibu?Amkeni!—2000 | Oktoba 8
-
-
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 7]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Kani hizo nne zimepimwaje kwa usahihi kabisa?
KANI YA SUMAKU-UMEME
KANI YENYE NGUVU YA NYUKLIA
NGUVU ZA UVUTANO
KANI DHAIFU YA NYUKLIA
Molekuli ya maji
Kiini cha atomu
Nyota yenye joto kali kupindukia
Nyota yenye joto hafifu
Jua
-