Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ulimwengu Wetu Ulitokeaje?—Ubishi Uliopo
    Je, Kuna Muumba Anayekujali?
    • Uthibitisho huo watia ndani vipimo sahihi kabisa vya kani nne za msingi ambazo zinaathiri vitu vyote na mabadiliko yote katika ulimwengu. Kwa kutaja tu kani za msingi, huenda wengine wakasita, wakifikiri, ‘Hiyo inahusu wataalamu wa fizikia pekee.’ La hasha. Inafaa kuchunguza mambo ya msingi kwa sababu hayo yanatuhusu.

      Vipimo Sahihi Kabisa

      Kani nne za msingi zinahusika katika ulimwengu wote na katika vitu vidogo sana vya atomu. Ndiyo, kila kitu tuonacho kinahusika.

      Elementi zilizo muhimu kwa uhai wetu (hasa kaboni, oksijeni, na chuma) hazingekuwapo kama si vipimo sahihi kabisa vya zile kani nne za msingi ambazo kwa wazi zimo katika ulimwengu. Tayari tumetaja kani moja, ile nguvu ya uvutano. Nyingine ni kani ya sumaku-umeme. Kama kani ya sumaku-umeme ingalikuwa dhaifu kidogo tu, elektroni hazingaliweza kukusanywa kuzunguka kiini (nyuklia) cha atomu. ‘Je, hilo lingetokeza tatizo zito?’ huenda wengine wakauliza. Ndiyo, kwa sababu atomu hazingaliweza kujikusanya ili kufanyiza molekuli. Kwa upande mwingine, kama kani ya sumaku-umeme ingalikuwa yenye nguvu zaidi, elektroni zingenaswa katika kiini cha atomu. Hakungalikuwa na utendaji wowote kati ya atomu mbalimbali—jambo linalomaanisha kwamba hakungekuwa na uhai. Hata kutokana na hali hii, ni wazi kwamba uhai wetu wategemea kipimo sahihi kabisa cha nguvu za sumaku-umeme.

      Na ebu fikiria ukubwa wa ulimwengu: Tofauti ndogo tu katika kani za sumaku-umeme ingehusisha jua na hivyo kuathiri nuru inayofikia dunia, jambo ambalo lingefanya iwe vigumu sana au hata isiwezekane kwa usanidimwanga (njia ya mimea kujifanyizia chakula). Pia ingenyang’anya maji vitu vyake muhimu, ambavyo ni muhimu kwa uhai. Basi tena, kipimo sahihi kabisa cha kani za sumaku-umeme huamua kama tutaishi au hatutaishi.

      Jambo muhimu sana pia ni kadiri ya kani za sumaku-umeme kwa kulinganisha na zile kani nyinginezo tatu. Kwa kielelezo, wataalamu fulani wa fizikia wanaona kani hiyo kuwa nyingi kuliko nguvu ya uvutano mara 10,000,000,000,000,000,000,000,000,000,000,000,- 000,000 (yaani nambari 1 inayofuatwa na sufuri 40). Inaweza kuonekana kuwa badiliko dogo kuongeza sufuri moja tu kwenye tarakimu hiyo (iwe nambari 1 inayofuatwa na sufuri 41). Lakini, hiyo ingemaanisha kwamba nguvu za uvutano zinakuwa dhaifu kwa kulinganisha, na Dakt. Reinhard Breuer aeleza juu ya hali iwezayo kutokea: “Nguvu za uvutano zikipungua basi nyota zingekuwa ndogo, na msongo wa nguvu za uvutano ndani ya nyota haungetokeza joto la kuweza kuwasha utendaji wa nyuklia: hilo lingefanya jua lishindwe kuangaza.” Unaweza kuwazia jinsi ambavyo tungeathiriwa!

      Namna gani ikiwa kani za uvutano zingekuwa zenye nguvu zaidi kwa kulinganisha, ili ile tarakimu iwe na sufuri 39 pekee? “Kwa rekebisho hilo dogo tu,” aendelea kusema Breuer, “nyota iliyo kama jua ingekuwa na maisha mafupi sana.” Na wanasayansi wengine hufikiria kwamba vile vipimo sahihi kabisa vya zile kani nne ni sahihi hata zaidi ya vile ambavyo tumeona.

      Kwa kweli, sifa mbili zenye kutokeza za jua letu na nyota nyinginezo ni kwamba hizo ni thabiti na zina uwezo wa kutenda daima. Ebu fikiria mfano rahisi. Twajua kwamba ili injini ya gari ifanye kazi vizuri, inahitaji usawaziko mzuri wa mchanganyiko wa mafuta na hewa; wahandisi hufanyiza mifumo tata ya kiufundi na ya kompyuta ili injini iweze kufanya vizuri. Ikiwa ndivyo ilivyo na injini tu, namna gani nyota “zenye kuwaka” kwa njia bora kama vile jua letu? Zile kani kuu zinazohusika zimepimwa kwa usahihi kabisa, zikifanya kazi kwa njia bora zaidi ili kuendeleza uhai. Je, vipimo hivyo vilivyo sahihi kabisa vilitokea vyenyewe tu? Yule mtu wa kale Yobu aliulizwa: “Je, ulizitangaza kanuni zinazoongoza mbingu, au kujua sheria za asili zilizo duniani?” (Ayubu 38:33, The New English Bible) Hakuna mwanadamu aliyepata kufanya hivyo. Basi ni nani aliyeweka hivyo vipimo vilivyo sahihi kabisa?

      Kani Mbili za Nyuklia

      Muundo wa ulimwengu wahusisha mengi zaidi ya vipimo sahihi kabisa vya nguvu za uvutano na kani za sumaku-umeme. Kani nyinginezo mbili zinahusika na uhai wetu.

      Kani hizo mbili zinatenda katika kiini cha atomu, nazo huonyesha kwamba ziliwekwa hapo na mtu mwenye kufikiri. Fikiria kani ya nyuklia yenye nguvu, ambayo hushikanisha protoni na nutroni pamoja katika kiini cha atomu. Kwa sababu ya mshikano huo, elementi kadhaa zaweza kufanyizwa—zile nyepesi (kama vile heli na oksijeni) na zile nzito (kama vile dhahabu na risasi). Inaonekana kwamba kama nguvu hiyo yenye kushikanisha ingekuwa dhaifu kwa asilimia 2 tu, ni hidrojeni pekee ambayo ingekuwako. Kwa upande mwingine, kama hii kani ingeongeza nguvu kidogo tu, ni zile elementi nzito pekee ambazo zingekuwako, lakini hidrojeni haingepatikana. Je, uhai wetu ungeathiriwa? Naam, kama ulimwengu ungekosa hidrojeni, jua letu halingepata kitu ambacho linahitaji ili kuwaka na kuendeleza uhai. Na, bila shaka, hatungekuwa na maji wala chakula, kwa kuwa hidrojeni ni sehemu muhimu ya maji na chakula.

      Kani ya nne katika mazungumzo haya, inayoitwa kani dhaifu ya nyuklia, hupunguza atomu za vitu vyenye mnururisho. Pia inahusika na utendaji katika jua letu. ‘Je, kani hiyo imepimwa kwa usahihi kabisa?’ huenda ukauliza. Mtaalamu wa hesabu aliye pia mtaalamu wa fizikia Freeman Dyson aeleza: “Ile [kani] dhaifu ni dhaifu mara mamilioni kuliko nguvu za nyuklia. Ni dhaifu kiasi tu cha kuwezesha hidrojeni iliyo katika jua ichomeke polepole kwa kiwango kilekile. Kama hii [kani] dhaifu ingekuwa na nguvu zaidi au kuwa dhaifu zaidi ya ilivyo, aina yoyote ya uhai inayotegemea nyota zilizo kama jua zingepata matatizo.” Ndiyo, kiwango kifaacho kabisa cha kuchomeka hudumisha dunia yetu ikiwa na joto—lakini bila kuteketea—na kuendeleza uhai wetu.

      Isitoshe, wanasayansi huamini kwamba ile kani dhaifu huchangia ile milipuko mikubwa sana ya nyota, ambayo kulingana na wanasayansi ni utaratibu wa kutokeza na kusambaza elementi nyingi. “Kama kani hizo za nyuklia zingalikuwa tofauti kidogo na jinsi zilivyo hasa, nyota hazingaliweza kutengeneza elementi ambazo zimekufanyiza wewe na mimi,” aeleza mtaalamu wa fizikia John Polkinghorne.

      Mengi zaidi yaweza kusemwa, lakini yaelekea unaelewa jambo kuu. Zile kani nne za msingi zimepimwa kwa usahihi kabisa kwa njia ya kustaajabisha sana. “Kotekote, yaonekana twaona uthibitisho wa kwamba asili ilijua kufanya mambo kwa usahihi kabisa,” akaandika Profesa Paul Davies. Ndiyo, vipimo sahihi kabisa vya zile kani nne za msingi vimefanya iwezekane kuwako kwa jua letu na utendaji wake, kuwako kwa dunia yetu ikiwa na maji yake yenye kuendeleza uhai, anga letu ambalo ni muhimu sana kwa uhai, na vitu vingi vya kemikali vyenye thamani duniani. Lakini, ebu jiulize, ‘Kwa nini kukawa na vipimo hivyo vilivyo sahihi kabisa, navyo vilipimwa na nani?’

  • Ulimwengu Wetu Ulitokeaje?—Ubishi Uliopo
    Je, Kuna Muumba Anayekujali?
    • [Sanduku katika ukurasa wa 17]

      Kani Kuu Nne

      1. Nguvu za uvutano—ni kani dhaifu sana kwa atomu. Hiyo ina uvutano kwa vitu vikubwa—sayari, nyota, na makundi ya nyota.

      2. Sumaku-umeme—kani kuu ivutiayo protoni na elektroni, ikiwezesha molekuli ifanyizwe. Radi ni uthibitisho mmoja wa uwezo wake.

      3. Kani ya nyuklia yenye nguvu—kani ishikanishayo protoni na nutroni pamoja katika kiini cha atomu.

      4. Kani dhaifu ya nyuklia—kani ambayo hupunguza atomu za elementi zenye mnururisho na kufanya kuwe na utendaji mzuri katika jua.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki