-
Wasichana Wenye WatotoAmkeni!—2004 | Oktoba 8
-
-
Wasichana Wenye Watoto
“Mpenzi wangu alikuwa mwenye kuvutia. Alikuwa na pesa, nasi tulikuwa tukitembelea sehemu mbalimbali na kujifurahisha. Nilitambua kwamba nina mimba nilipokosa kupata hedhi. Sikujua nitakavyomwambia mama yangu. Sikuamini kwamba nimepatwa na jambo hilo. Nilikuwa na umri wa miaka 16 tu, nami sikujua la kufanya.”—Nicole.
SASA Nicolea ana umri wa miaka 30 na kitu, naye ni mama ya watoto watatu mwenye uhakika na bidii. Mtoto wake wa kwanza ana umri wa miaka 20. Naam, miaka kadhaa iliyopita alikuwa mmoja wa mamilioni ya vijana wanaopata mimba kabla ya kufunga ndoa. Sawa na akina mama wengine wachanga, alikabili magumu mengi, maamuzi mazito, na wasiwasi kuhusu wakati ujao.
Mara nyingi Nicole haelezi jinsi alivyoshtuka, alivyokataa kukubali hali yake, alivyoogopa, alivyokasirika, na alivyofadhaika katika miaka yake ya ujana, huku vijana wenzake wakihangaikia mavazi na maksi za shule. Hata hivyo, Nicole alikuwa na tumaini. Familia yao ilikuwa yenye upendo na alikuwa amefundishwa maadili bora. Ingawa kwa muda alipuuza maadili hayo na kupata matokeo mabaya, baadaye maadili hayohayo yalimsaidia afanikiwe maishani. Sikuzote alichochewa na maneno haya: “Bado kuna tumaini.”
Inasikitisha kwamba si akina mama wote wachanga wanaotegemezwa na familia zao au kuwa na mtazamo unaofaa. Wengi hutumbukia katika umaskini. Wengine hulazimika kuvumilia maumivu ya kihisia yanayotokana na kubakwa na jeuri.
Mambo hayo huwaathiri watoto wa mama hao wachanga. Kitabu Teen Moms—The Pain and the Promise, kinasema kwamba watoto wa akina mama wachanga “mara nyingi huzaliwa wakiwa na uzani mdogo, hupatwa na magonjwa mengi ya watoto, hufa wakiwa wachanga, hawapati matibabu yanayofaa, huteseka kutokana na njaa na kukosa chakula kinachofaa, hukabili jeuri zaidi, nao hukua polepole kuliko watoto waliozaliwa na akina mama wenye umri mkubwa.” Kwa hakika, kuna uwezekano mkubwa kwa binti za akina mama wachanga kupata watoto wakiwa wachanga kuliko binti za akina mama wenye umri mkubwa.
Tatizo la akina mama wachanga limeenea kadiri gani? Mama hao wanaweza kukabilianaje na magumu ya kuwalea watoto wao? Je, kuna njia ya kuwasaidia vijana kuepuka matatizo hayo? Makala zinazofuata zinajibu maswali hayo.
[Maelezo ya Chini]
a Baadhi ya majina katika mfululizo huu yamebadilishwa.
-
-
Wasichana Wanaopata Mimba Tatizo la Ulimwenguni PoteAmkeni!—2004 | Oktoba 8
-
-
Wasichana Wanaopata Mimba Tatizo la Ulimwenguni Pote
TATIZO la vijana kupata mimba limeenea sana. Hata hivyo, uzito wa tatizo hilo huonekana wakati msichana anaposhtuka kwamba amepata mimba. Maisha ya msichana huyo hubadilika sana na kumwathiri yeye, familia yake, na wapendwa wake.
Vijana walio kati ya umri wa miaka 13 hadi 19 wako katika kipindi ambacho Biblia hukiita “upeo wa ujana,” yaani, wakati ambapo hamu ya ngono ni yenye nguvu sana. (1 Wakorintho 7:36) Hata hivyo, kudhania kwamba mimba za vijana zinasababishwa na kutotumia njia ya kupanga uzazi tu, ni kupunguza uzito wa jambo hilo. Uthibitisho unaonyesha kwamba vijana wachanga hupata mimba kwa sababu ya hali mbalimbali za kijamii na kihisia.
Visababishi
Utafiti unaonyesha kwamba akina mama wengi wachanga hutoka katika familia zilizovunjika. Vijana wengi wanaopata mimba wakiwa wachanga husema hivi: “Laiti familia yetu ingekuwa na wazazi wote wawili.” Hivyo, kuvunjika kwa familia kunaweza kuchangia vijana wapate mimba. Mradi mmoja wa kuwasaidia akina mama wachanga uligundua kwamba mara nyingi vijana hao “huwa na uhusiano mbaya na mama zao na hawana uhusiano wowote na baba zao.” Anita aliyepata mtoto akiwa na umri wa miaka 18 anakumbuka kwamba ingawa mama yake ambaye hakuwa na mwenzi wa ndoa alijitahidi kumtimizia mahitaji yake ya msingi, bado alihisi pengo fulani kwa kukosa baba yake.
Wasichana wengine hupata mimba kwa sababu ya kubakwa. Baadaye maishani, baadhi ya wasichana wanaobakwa wanaweza kuumia sana kihisia na kujihusisha na mambo yanayoweza kuharibu maisha yao. Kwa mfano, Jasmine alibakwa alipokuwa na umri wa miaka 15. Anasema hivi: “Baada ya tukio hilo, sikujali chochote. Nilipata mimba nikiwa na umri wa miaka 19.” Kutendewa vibaya kingono pia kunaweza kumfanya mtu ahisi kwamba hafai. Jasmine anakumbuka hivi kwa majonzi: “Nilihisi kuwa sifai kitu.” Anita pia alipatwa na hali kama hiyo yenye kuhuzunisha. Anasema: “Nilipokuwa kati ya umri wa miaka 7 na 11, nilibakwa na kijana fulani. Nilijichukia na kujilaumu.” Alipata mimba akiwa na umri wa miaka 17.
Kwa upande mwingine, vijana fulani hupata mimba kwa sababu ya kujiamini kupita kiasi na kuwa wadadisi. Nicole aliyenukuliwa katika makala iliyotangulia anakubali hivi: “Nilifikiri ninajua kila kitu na kwamba ninaweza kufanya chochote. Inasikitisha pia kwamba ningeweza kupata mtoto.” Carol, ambaye pia alipata mimba akiwa mchanga, alichochewa na udadisi kufanya ngono. Anasema: “Nilihisi kwamba kuna mambo ninayokosa.”
Kisababishi kingine ni kutofahamu matokeo ya kufanya ngono. Kulingana na wanasoshiolojia, Karen Rowlingson na Stephen McKay, huko Uingereza, vijana fulani ‘hawajui matokeo ya kuingia katika mahusiano wala matokeo ya kupata mimba.’ Inaonekana vijana wengine hawajui kwamba kufanya ngono kunaweza kutokeza mimba. Katika uchunguzi mmoja, akina mama wengi wachanga “waliripoti kwamba walishtuka au kushangaa walipogundua kwamba wana mimba ingawa hawakuwa wametumia njia za kupanga uzazi.”
Hata hivyo, kubadilika kwa maoni ya watu kuhusu ngono ndiyo sababu kubwa zaidi ya vijana kupata mimba wakiwa wachanga. Tunaishi wakati ambapo watu ‘wanapenda raha badala ya kumpenda Mungu.’ (2 Timotheo 3:1-4) Watafiti wa Australia, Ailsa Burns na Cath Scott, wanasema “viwango vya kijamii, kidini, na vya kiuchumi vinavyopinga watu kufanya ngono nje ya ndoa vimelegezwa.” Kupata mtoto nje ya ndoa si jambo la kuaibikia kama ilivyokuwa zamani. Huenda vijana katika maeneo fulani wakaona kwamba kupata mtoto ni jambo linalomfanya mtu aheshimiwe au kusifiwa!
Kuathiriwa Kihisia
Mambo yanayowapata akina mama wachanga ni tofauti sana na maoni ambayo vijana huwa nayo. Mara nyingi, wasichana husumbuka sana kihisia wanapogundua kwamba wana mimba. Wengi husema kwamba wameshtuka. Chama cha Marekani cha Matatizo ya Akili ya Watoto na Vijana kinasema: “Mara nyingi wao hukasirika, huhisi hatia, na hawakubali kwamba wana mimba.” Hata hivyo, kutokubali hali ni hatari kwani kunaweza kumfanya msichana asiende kupata matibabu yanayohitajiwa.
Elvenia anapokumbuka hisia alizokuwa nazo alipokabili matokeo ya kufanya ngono anasema hivi: “Niliogopa sana.” Wasichana wengi waja-wazito hukosa mtu wa kueleza jinsi wanavyohisi au wanaona haya sana kuzungumzia hali yao. Basi, si ajabu kwamba wengine hulemewa na hisia za hatia na woga. Pia wengi wao hushuka moyo sana. “Sikujali kuishi au kufa,” asema Jasmine.a
Ingawa msichana anaweza kuwa na hisia mbalimbali anapopata mimba, bado atahitaji kufanya maamuzi mazito yanayomhusu yeye na mtoto wake. Makala inayofuata itazungumzia jinsi msichana anavyoweza kufanya maamuzi hayo kwa hekima.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari kuhusu kukabiliana na hisia za kutaka kujiua, ona makala “Uhai Una Thamani,” katika toleo la Amkeni! la Oktoba 22, 2001.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Habari Zenye Kushtua Kuhusu Vijana Wanaopata Mimba
Ingawa habari zifuatazo zinaonyesha jinsi hali ilivyo huko Marekani, zinaonyesha pia matatizo ambayo vijana wanaopata mimba wanakabili ulimwenguni pote.
● Wasichana 4 kati ya 10 hupata mimba kabla ya kufikia umri wa miaka 20, na hizo ni zaidi ya mimba 900,000 kila mwaka.
● Asilimia 40 hivi ya wasichana wenye watoto hawajafikia umri wa miaka 18.
● Watoto wa wazazi wachanga hutendewa vibaya na kupuuzwa kuliko watoto wa wazazi waliokomaa.
● Asilimia 40 tu ya akina mama walio chini ya umri wa miaka 18 ndio humaliza shule ya sekondari.
● Asilimia 80 hivi ya wanaume hawaoi wasichana wanaowatunga mimba.
● Asilimia 30 tu ya akina mama wachanga wanaoolewa baada ya kupata mtoto ndio wanaobaki katika ndoa hizo; uwezekano wa kuvunjika kwa ndoa za vijana ni mara mbili zaidi ya uwezekano wa kuvunjika kwa ndoa zinazofungwa mwanamke anapokuwa na angalau miaka 25.
● Watoto wa akina mama wachanga hukabili uwezekano mkubwa wa kuzaliwa kabla ya wakati na wakiwa na uzani mdogo, na hivyo kuongeza uwezekano wa kufa wakiwa wachanga, kuwa vipofu, kuwa viziwi, kupata magonjwa hatari ya kupumua, magonjwa ya akili, mtindio wa ubongo, kutoweza kusoma, na kukosa utulivu.
[Hisani]
Habari hiyo inategemea Not Just Another Single Issue: Teen Pregnancy Prevention’s Link to Other Critical Social Issues, The National Campaign to Prevent Teen Pregnancy, February 2002.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Vijana Hupata Mimba Ulimwenguni Pote
BRAZILI: Inasemekana kwamba “wasichana 698,439 walio chini ya umri wa miaka 19 walijifungua mwaka wa 1998 kwa kutumia Mfumo wa Afya wa Kitaifa wa Brazili . . . wasichana 31,857 kati yao walikuwa watoto waliokuwa kati ya umri wa miaka 10 na 14, na kwa hakika huo ni umri mdogo sana kupata mtoto.”—Folha de S. Paulo, Agosti 25, 1999.
UINGEREZA: “Vijana wengi zaidi hupata watoto nchini Uingereza kuliko katika nchi nyingine yoyote ya Ulaya Magharibi . . . Katika mwaka wa 1997 wasichana 90,000 walipata mimba huko Uingereza. Inakadiriwa kwamba wasichana watatu kati ya watano walijifungua (56,000) na asilimia 90 ya vijana waliojifungua mwaka wa 1997, hawakuwa wamefunga ndoa (50,000 hivi).”—Lone Parent Families, 2002.
MALASIA: “Idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa nchini humo imeongezeka tangu mwaka wa 1998, na mama wengi wakiwa wanakaribia miaka 20.”—New Straits Times–Management Times, Aprili 1, 2002.
URUSI: “Kulingana na habari za serikali, karibu thuluthi moja ya watoto waliozaliwa huko Urusi, walizaliwa na akina mama ambao hawajafunga ndoa, na hiyo ni mara mbili ya wale waliozaliwa miaka 10 kabla ya hapo na ndiyo idadi kubwa zaidi tangu Vita vya Pili vya Ulimwengu. Zaidi ya asilimia 40 ya watoto hao walizaliwa na wasichana wachanga.”—The Moscow Times, Novemba 29, 2001.
MAREKANI: “Licha ya kupungua kwa idadi ya wasichana wachanga wanaopata mimba, wasichana 4 kati ya 10 hupata mimba angalau mara moja kabla ya kufikisha umri wa miaka 20.”—Whatever Happened to Childhood? The Problem of Teen Pregnancy in the United States, 1997.
[Picha katika ukurasa wa 5]
Wazazi wanapotengana, uwezekano wa vijana kupata mimba huongezeka
[Picha katika ukurasa wa 6]
Inaonekana vijana wengine hawajui kwamba kufanya ngono kunaweza kutokeza mimba
[Picha katika ukurasa wa 6]
Msichana anapopata mimba, hilo humwathiri sana na vilevile wapendwa wake
-
-
Kukabili Magumu ya Kuwa Mama MchangaAmkeni!—2004 | Oktoba 8
-
-
Kukabili Magumu ya Kuwa Mama Mchanga
MSICHANA mchanga anapopata mimba, analazimika kukabili maamuzi ambayo watu wazima hukabili. Mama mmoja mchanga alisema hivi: “Ni kana kwamba nina miaka 40. Sikufurahia maisha yangu ya utotoni.” Kwa hakika, msichana mchanga anapogundua kwamba ana mimba anaweza kuogopa na kuhangaika sana.
Ikiwa wewe ni msichana mchanga na una mimba, unaweza kuhisi hivyo. Hata hivyo, hutatimiza chochote ukiruhusu hisia zisizofaa zikulemee. Biblia inasema, “Anayeuangalia upepo hatapanda mbegu; naye anayetazama mawingu hatavuna.” (Mhubiri 7:8; 11:4) Mkulima anayehangaishwa sana na hali ya hewa hatachukua hatua zinazohitajiwa. Usiruhusu mahangaiko yakuzuie kutenda. Muda si muda itakubidi uendelee kufanya shughuli za kawaida na kutimiza madaraka yako.—Wagalatia 6:5.
Utafanyaje? Huenda watu fulani wakakushauri utoe mimba. Lakini watu wanaotaka kumpendeza Mungu hawatoi mimba, kwani Biblia husema kwamba kutoa mimba ni kinyume cha sheria ya Mungu. (Kutoka 20:13; 21:22, 23; Zaburi 139:14-16) Machoni pa Mungu, uhai wa kila kiini-tete—hata ikiwa mimba imetungwa nje ya ndoa—ni wenye thamani.
Vipi kuolewa na baba ya mtoto wako na kumlea mtoto huyo mkiwa pamoja? Huenda ukafikiri kwamba ndoa inaweza kukuondolea aibu. Lakini hata baba mchanga akihisi kwamba ana daraka la kusaidia kumlea mtoto wake, mara nyingi ndoa si suluhisho linalofaa.a Hata ingawa kijana anaweza kutunga mimba, haimaanishi kwamba yuko tayari kihisia na kiakili kuwa mume na baba mzuri. Wala haimaanishi kwamba anaweza kumruzuku mke na mtoto wake. Isitoshe, ikiwa hamko katika dini moja na kijana huyo, kufunga ndoa naye kutakuwa kukiuka shauri la Biblia la kuoa “katika Bwana tu.” (1 Wakorintho 7:39) Imeonekana kwamba kukimbilia ndoa haraka-haraka, ambayo huenda haitadumu, kunaweza kusababisha maumivu na kuteseka zaidi.
Vipi kumkabidhi mtoto atunzwe na wengine? Ijapokuwa hatua hiyo ni afadhali kuliko kutoa mimba, unapaswa kukumbuka kwamba licha ya hali ngumu unazokabili, bado una nafasi ya kumtunza na kumlea mtoto wako.
Kukabili Magumu
Ni kweli kwamba si rahisi kumlea mtoto bila mwenzi. Hata hivyo, kwa kufuata kanuni za Biblia kadiri uwezavyo na kwa kumtegemea Mungu akuimarishe na kukuongoza, unaweza kufanikiwa kukabiliana na magumu mengi. Zifuatazo ni baadhi ya hatua zitakazokusaidia kukabiliana na magumu hayo.
● Rekebisha uhusuano wako na Mungu. Tambua kwamba kufanya ngono kabla ya ndoa ni dhambi mbele za Mungu, ni kuvunja viwango vyake vya juu vya adili. (Wagalatia 5:19-21; 1 Wathesalonike 4:3, 4) Hivyo, hatua ya kwanza muhimu ni kutubu na kumwomba Mungu msamaha. (Zaburi 32:5; 1 Yohana 2:1, 2) Ni kweli kwamba huenda ukaona hustahili kupata msaada wake. Hata hivyo, Yehova anaahidi kwamba atatusamehe, naye huwasaidia wale wanaotubu dhambi zao. (Isaya 55:6, 7) Kwenye Isaya 1:18, Yehova anasema: “Hata dhambi zenu zikiwa nyekundu [nzito sana], zitafanywa kuwa nyeupe kama theluji [zitasafishwa kabisa].” Biblia hutia moyo watenda-dhambi wawaendee wazee waliowekwa rasmi kutanikoni ili kupata msaada wa kiroho.—Yakobo 5:14, 15.
● Acha kufanya ngono kabla ya ndoa. Huenda hiyo ikamaanisha kuvunja uhusiano kati yako na baba ya mtoto wako. Kuendeleza uhusiano huo kabla ya kufunga ndoa kunaweza kukufanya uendelee kujihusisha na mambo yanayomchukiza Mungu. Usisahau kamwe kwamba ingawa sheria za Mungu ni thabiti, zinatulinda. Nicole aliyenukuliwa mapema katika mfululizo huu anakiri hivi: “Nimetambua kwamba Mungu husema kweli. Anataka tufaidike.”—Isaya 48:17, 18.
● Waambei wazazi wako. Huenda ukaogopa kwamba wazazi wako watakukasirikia. Ni kweli kwamba watakasirika na kuhangaika wanapojua una mimba. Huenda wakahisi kwamba wameshindwa kutimiza madaraka yao na hata wanaweza kujilaumu kwa sababu ya mwenendo wako mbaya. Hata hivyo, ikiwa kwa kweli wazazi wako wanamcha Mungu, muda si muda wataacha kuhuzunika. Wao ni wazazi wako na wanakupenda licha ya makosa yako. Wanapoona kwamba umetubu, bila shaka watamwiga baba ya mwana mpotevu na watakusamehe kwa upendo.—Luka 15:11-32.
● Toa shukrani. Mara nyingi wazazi, watu wa ukoo, na marafiki husaidia sana. Kwa mfano, wazazi wako wanaweza kuhakikisha kwamba unapata matibabu. Baada ya kupata mtoto, wanaweza kukusaidia kujua jinsi ya kumtunza mtoto mchanga; pia wanaweza kujitolea kuwa yaya wa mtoto wako. Nicole anasema hivi kuhusu mama yake: “Nilipata mtoto, lakini mama yangu ndiye aliyenisaidia sana.” Huenda pia marafiki wakakusaidia. Kwa busara wanaweza kukupatia nguo za mtoto na vitu vingine vinavyoweza kukusaidia. (Methali 17:17) Unapotendewa kwa fadhili, fuata shauri la Biblia la ‘kuonyesha shukrani.’ (Wakolosai 3:15) Ukisema asante, hawatahisi kwamba umepuuza fadhili zao.
● Jifunze kuwa mzazi. Bila shaka, hungependa kutegemea familia yenu na marafiki zako daima. Kwa hiyo, jifunze stadi zitakazokusaidia kumtunza mtoto wako na kushughulikia mambo ya nyumbani. Ni kazi ngumu kujifunza jinsi ya kumtunza mwanadamu mwenye mahitaji mengi sana. Kuna mambo mengi unayopaswa kujifunza kuhusu chakula, afya, na mambo mengine yanayohusiana na kumtunza mtoto. Inapendeza kwamba Biblia inawasihi wanawake Wakristo wenye umri mkubwa wawaelimishe wanawake vijana kuwa “wafanyakazi nyumbani.” (Tito 2:5) Bila shaka, mama yako—na labda washiriki wengine wenye umri mkubwa katika kutaniko la Kikristo—wanaweza kukupa mazoezi muhimu ya kushughulikia mambo hayo.
● Tumia pesa kwa hekima. Biblia inasema kwamba “pesa ni ulinzi.” (Mhubiri 7:12) Mtoto anapozaliwa, kunakuwa na mahitaji mengi ya kifedha.
Huenda ikafaa utafute msaada unaoandaliwa kwa umma. Hata hivyo, mara nyingi msichana bado atahitaji kutegemea wazazi wake kifedha. Ikiwa ndivyo ilivyo kwako, basi, ni jambo la hekima na upendo kupunguza gharama zako kwa kadiri iwezekanavyo. Ingawa ungependa mtoto wako awe na vitu vipya, unaweza kuokoa pesa kwa kununua bidhaa ambazo tayari zimetumiwa.
● Jaribu kupata elimu. Andiko la Methali 10:14 linasema: “Wenye hekima ndio wanaoweka hazina ya ujuzi.” Ingawa maneno hayo yanahusu hasa ujuzi wa Biblia, yanatumika pia kuhusu elimu ya kilimwengu. Unahitaji kupata stadi za kujiruzuku.
Ni kweli kwamba si rahisi kwenda shule huku ukimtunza mtoto. Hata hivyo, kukosa elimu ya msingi kunaweza kukufanya wewe na mtoto wako muishi maisha ya umaskini, kutegemea misaada ya umma, kuwa na mapato madogo, kuishi katika nyumba za hali ya chini, na kukosa chakula kinachofaa. Kwa hiyo, ikiwa inawezekana, endelea kupata elimu. Mama ya Nicole alisisitiza kwamba amalize shule, na hivyo Nicole akapata mazoezi ambayo yalimwezesha kuwa msaidizi wa wakili na kujiruzuku.
Kwa nini usichunguze ikiwa kuna masomo ya ziada unayoweza kupata? Ikiwa ni vigumu kwako kwenda shuleni, chunguza ikiwa unaweza kusomea nyumbani. Kwa mfano, kupata elimu kupitia mawasiliano ya barua kunaweza kukufaa sana.
Unaweza Kufanikiwa
Kumlea mtoto nje ya ndoa si jambo rahisi kwa msichana mchanga. Lakini unaweza kufanikiwa! Ukiwa na subira, nia, na msaada wa Yehova Mungu, unaweza kuwa mzazi mwenye upendo na ustadi, ambaye anatimiza madaraka yake. Na watoto wa akina mama wasio na wenzi wanaweza kukua na kuwa watu wazima wenye sifa nzuri. Ama kwa hakika, utafurahi kuona mtoto wako akikubali msaada na mazoezi unayompa na kumpenda Mungu.—Waefeso 6:4.
Nicole anasema hivi: “Licha ya magumu, kwa msaada wa Mungu, nilifurahia kumsaidia msichana wangu mdogo awe mtu mzima mwenye fadhili na heshima, na anayechukua madaraka kwa uzito. Ninapomtazama, mimi hukumbuka siku nilizokosa usingizi lakini pia mimi hufurahi sana.”
Hata hivyo, watu wazima wanapaswa kuwatendeaje akina mama wachanga pamoja na watoto wao? Je, kuna njia yoyote ya kuwasaidia vijana kuepuka matatizo yanayotokana na kupata mimba wakiwa wachanga?
[Maelezo ya Chini]
a Unaweza kupata habari zaidi kuhusu madaraka na matatizo yanayowapata akina baba wachanga ambao bado hawajafunga ndoa katika makala za “Vijana Huuliza . . . ” katika matoleo ya Amkeni! ya Aprili 22, 2000, na Mei 22, 2000.
[Picha katika ukurasa wa 9]
Mama wachanga hukabili magumu mengi ya kulea watoto wao
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kukimbilia ndoa kabla ya wakati si suluhisho
[Picha katika ukurasa wa 10]
Wazee Wakristo wanaweza kuwasaidia vijana waliofanya dhambi kurekebisha uhusiano wao na Mungu
[Picha katika ukurasa wa 11]
Ni jambo la hekima akina mama wasio na wenzi kupata elimu ya msingi
-
-
Jinsi ya Kuwasaidia na Kuwalinda VijanaAmkeni!—2004 | Oktoba 8
-
-
Jinsi ya Kuwasaidia na Kuwalinda Vijana
INAHUZUNISHA sana msichana mchanga anapopata mimba kabla ya kuolewa. Hata hivyo, tatizo la wasichana wachanga kupata mimba limeenea sana, nalo huathiri kila mtu kwa njia fulani. Matokeo mabaya ya tatizo hilo yanathibitisha kwamba amri hii ya Mungu inafaa: “Ukimbieni uasherati.”—1 Wakorintho 6:18.
Hata hivyo, nyakati nyingine msichana ambaye amefundishwa njia za Mungu huchagua kuzipuuza au kuzikataa. Anafanya ngono na kupata mimba. Wakristo wa kweli wanapaswa kutendaje? Kijana huyo aliyefanya dhambi anapotubu, wazazi wake na washiriki wengine wa kutaniko wanapaswa kumsaidia na kumtegemeza kwa upendo.
Fikiria tena kisa cha Nicole. Wazazi wake walikuwa wakimsaidia awe Shahidi wa Yehova. Hivyo, alipopata mimba nje ya ndoa walivunjika moyo sana. Hata hivyo, Nicole anakumbuka hivi: “Wakristo wenzangu walikuwa wakija nyumbani na kunitia moyo nijifunze Biblia na kuwa na uhusiano wa karibu na Yehova.”
Mashahidi wa Yehova hawakubali kamwe ukosefu wa adili katika ngono. Lakini wanatambua kwamba kwa kutumia kanuni za Biblia, watenda dhambi wanaweza ‘kugeuzwa.’ (Waroma 12:2) Wanaamini kabisa kwamba Mungu huwasamehe watenda-dhambi wanaotubu. (Waefeso 1:7) Pia wanatambua kwamba mtoto hana hatia, hata kama amezaliwa nje ya ndoa. Kwa hiyo, badala ya kumshutumu mtoto huyo, washiriki wa kutaniko la Kikristo humtendea kwa upendo, huruma, na fadhili, sawa na vile wangewatendea watoto wengine.—Wakolosai 3:12.
Mama mmoja asiye na mwenzi wa ndoa alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Alikubali haraka ujumbe wa Biblia na kufanya mabadiliko makubwa maishani mwake. Alisema hivi kuhusu Mashahidi: “Wote walipendezwa na mimi na watoto wangu kikweli. Walinipa chakula, mavazi, na kunitegemeza kifedha ilipohitajika. Walijitolea kuwa yaya wa mtoto wangu nilipoanza kuhubiri na Mashahidi wa Yehova. Walifanya yote wawezayo kunisaidia kumpenda Yehova kikweli.”
Kuzuia
Hata hivyo, ni afadhali zaidi kuwasaidia vijana kuepuka matatizo hayo. Hivyo, Mashahidi wa Yehova hujitahidi sana kufanya familia iwe yenye uchangamfu na upendo kwa ajili ya watoto wao. Mashahidi hujaribu kuwafundisha watoto wao kumpenda Yehova Mungu na sheria zake badala ya kuwatisha kwamba watapata UKIMWI au mimba. (Zaburi 119:97) Wanaamini kwamba watoto wanapaswa kuelezwa habari sahihi kuhusu ngono. Zaidi ya hilo, wanaamini kwamba watoto wanahitaji kufundishwa kanuni za maadili zilizo katika Biblia. (2 Timotheo 3:15) Mafundisho hutolewa kwenye Majumba ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, wazazi Mashahidi wanatiwa moyo kuwafundisha watoto wao Biblia, wao wenyewe. Vitabu kama vile Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, vimechapishwa ili kuwasaidia wazazi kuwafundisha watoto wao.a
Watu wanaofuata viwango thabiti vya Biblia huwa tofauti na watu ambao hufanya mambo yaliyopotoka kiadili ambayo yameenea sana ulimwenguni. Lakini kufuata viwango hivyo kunaweza kusaidia mamilioni ya wasichana wachanga waepuke matatizo yanayowapata wasichana wachanga wenye mimba.
[Maelezo ya Chini]
a Kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Wakristo wa kweli huwatendea kwa upendo na kwa fadhili akina mama wasio na wenzi
-