-
Rumania2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Mnamo Septemba 1, 1944, vikosi vya Ujerumani vilipoanza kurudi nyuma, mimi, nilikuwa kati ya ndugu 152 na wafungwa wengine walioondolewa kwenye kambi ya mateso ya Bor, huko Serbia, ili wapelekwe Ujerumani. Hatukula kwa siku kadhaa. Tulipopata chakula kidogo, kama vile viazi-sukari vilivyoachwa kando ya barabara karibu na mashamba, tulikila pamoja. Iwapo mmoja alikuwa dhaifu sana asiweze kutembea, wale waliokuwa na nguvu walimbeba kwenye mkokoteni.
Hatimaye, tulifika kwenye kituo cha gari-moshi, tukapumzika kwa saa nne hivi, kisha ili tupate nafasi ya kusafiria tuliondoa mizigo kutoka kwenye mabehewa mawili ya gari-moshi ambayo hayakuwa na paa. Kulikuwa na nafasi ya kusimama tu, nasi hatukuwa na nguo nzito za kujikinga na baridi, bali kila mmoja alikuwa na blanketi alilolitumia kujifunika mvua ilipoanza kunyesha. Tulisafiri katika hali hiyo usiku kucha. Tulipofika kwenye kijiji fulani saa 4:00 asubuhi siku iliyofuata, ndege mbili zilipiga kichwa cha gari-moshi letu kwa mabomu nasi tukalazimika kusimama. Ijapokuwa mabehewa yetu yalikuwa nyuma tu ya kichwa hicho, hakuna aliyeuawa. Kichwa kingine cha gari-moshi kiliunganishwa na behewa letu nasi tukaendelea na safari.
Baada ya kusafiri kilometa 100 hivi, tulisimama kwa saa mbili katika kituo fulani. Tukiwa hapo, tuliwaona wanaume na wanawake fulani waliobeba viazi kwa vikapu. Tulidhani wao ni wachuuzi wa viazi. Lakini tulikosea. Walikuwa ndugu na dada zetu wa kiroho waliokuwa wamesikia kutuhusu na kujua kwamba tulikuwa na njaa. Walimpa kila mmoja wetu viazi vitatu vikubwa vilivyochemshwa, kipande cha mkate, na chumvi kidogo. Hiyo ‘mana kutoka mbinguni’ ilitutegemeza kwa siku nyingine mbili hadi tulipofika Szombathely, Hungaria, mwanzoni mwa mwezi wa Desemba.
Tulikaa Szombathely wakati wa baridi kali, na tulikula hasa mahindi yaliyokuwa yamefunikwa kwa theluji. Katika mwezi wa Machi na Aprili mwaka wa 1945, mji huo maridadi ulipigwa kwa mabomu, na maiti zilizokatwakatwa zikatapakaa barabarani. Watu wengi waliangukiwa na vifusi, na mara kwa mara tuliwasikia wakililia msaada. Tulitumia vijiko na vifaa vingine kuokoa baadhi yao.
Majengo yaliyokuwa karibu na makao yetu yalipigwa kwa mabomu, lakini jengo letu halikupigwa. Kila mara king’ora kilipolia kutahadharisha kwamba mabomu yangeangushwa, watu wote waliogopa sana na kukimbilia usalama. Mwanzoni, sisi pia tulikuwa tukikimbia, lakini baada ya muda hatukuona tena uhitaji wa kufanya hivyo kwa kuwa hakukuwa na mahali salama pa kujificha. Hivyo, tulikaa tu na kujitahidi kutulia. Muda si muda, walinzi wakawa wakibaki nasi. Walisema kwamba Mungu wetu angeweza kuwaokoa wao pia! Mnamo Aprili 1, usiku wetu wa mwisho katika mji wa Szombathely, mabomu mengi sana yaliangushwa katika mji huo kuliko wakati mwingine wowote. Licha ya hilo, tulikaa katika jengo letu huku tukimsifu Yehova kwa nyimbo na kumshukuru kwa sababu ya kuwa na amani ya moyoni.—Flp. 4:6, 7.
Siku iliyofuata tuliamriwa tuanze safari ya kwenda Ujerumani. Tulikuwa na magari mawili yanayokokotwa na farasi, hivyo, tulisafiri kwa magari hayo na pia kwa miguu kwa kilometa 100 hivi hadi tulipofika kwenye msitu fulani uliokuwa kilometa 13 kutoka mahali ambapo majeshi ya Urusi yalikuwa. Tulikaa katika shamba la tajiri fulani usiku kucha, na siku iliyofuata walinzi wetu wakatuachilia. Tulimshukuru Yehova kwa sababu alikuwa ametutunza kimwili na kiroho, kisha tukitokwa na machozi tukaagana na wenzetu na kwenda makwetu. Baadhi yetu tulitembea kwa miguu na wengine wakasafiri kwa gari-moshi.
-
-
Rumania2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
jeshi la Ujerumani lilivamia nchi hiyo mnamo Oktoba 1940. Katika hali hizo ngumu mawasiliano yalikatishwa kati ya Rumania na Ofisi ya Tawi ya Ulaya ya Kati huko Uswisi.
Martin Magyarosi alitoka Bucharest na kuhamia TirguMures, Transylvania, kwa sababu Mashahidi wengi wa Yehova waliishi katika mkoa huo. Mke wake Maria tayari alikuwa amehamia Tirgu-Mures kwa sababu ya matatizo ya afya. Pamfil na Elena Albu, ambao pia walikuwa wamefanya kazi kwenye ofisi huko Bucharest, wakahamia Baia-Mare, sehemu ya kaskazini. Walipokuwa katika miji hiyo miwili, Ndugu Magyarosi na Albu walipanga upya kazi ya kuhubiri na ya kuchapa Mnara wa Mlinzi kisiri. Mfanyakazi mwenzao Teodor Morăraş, alibaki Bucharest, naye alisimamia kazi katika sehemu iliyobaki ya Rumania hadi alipokamatwa mwaka wa 1941.
Ndugu waliendelea kuhubiri kwa bidii, na waligawa vitabu vinavyozungumzia Biblia kila walipopata nafasi, lakini kwa tahadhari sana. Kwa mfano, waliacha vijitabu kwenye sehemu za umma kama vile mikahawa, vituo vya gari-moshi, na sehemu nyinginezo, wakitumaini kwamba mtu fulani angevutiwa navyo. Waliendelea pia kutii agizo la Maandiko la kukutanika pamoja ili kutiana moyo kiroho, huku wakijihadhari wasitambuliwe. (Ebr. 10:24, 25) Kwa mfano, katika sehemu za mashambani, wakulima walikuwa na desturi ya kusaidiana kuvuna na kusherehekea mavuno kwa kusimulia hadithi za vichekesho. Ndugu walifanya mikutano ya Kikristo badala ya karamu hizo za kitamaduni.
‘Walikazwa Katika Kila Njia’
Ndugu Magyarosi alikamatwa mnamo Septemba 1942 lakini akaendelea kupanga kazi ya kuhubiri akiwa gerezani. Ndugu na Dada Albu walikamatwa pia, pamoja na ndugu na dada wengine 1,000 hivi. Wengi wao waliachiliwa baada ya kupigwa na kufungwa kwa karibu majuma sita. Mashahidi 100, wakiwemo akina dada, walihukumiwa vifungo vya miaka 2 hadi 15 kwa sababu hawakuunga mkono jeshi. Ndugu watano walihukumiwa kifo, lakini adhabu hiyo ikabadilishwa kuwa vifungo vya maisha. Polisi wenye silaha waliwakamata hata mama na watoto wadogo usiku, na kuacha mifugo na nyumba zao bila ulinzi, ili wezi wapore.
Walipofika gerezani ndugu “walikaribishwa” na kikundi cha walinzi ambao walimfunga kila mmoja miguu na kumlaza sakafuni na kumshikilia kwa nguvu huku mmoja wao akimpiga nyayo kwa rungu gumu la mpira. Mifupa ilivunjika, kucha za vidole zikatoka, na ngozi ikawa nyeusi na kubambuka kama tu maganda ya mti. Makasisi waliotembelea magereza hayo waliwadhihaki kwa kusema: “Yehova wenu yuko wapi sasa awaokoe?”
Ndugu ‘walikazwa katika kila njia lakini hawakuachwa bila msaada.’ (2 Kor. 4:8, 9) Waliwafariji wafungwa wengine kwa kuwaeleza ujumbe wa Ufalme, na baadhi yao wakaukubali. Fikiria kisa cha Teodor Miron kutoka kijiji cha Topliţa, kaskazini-mashariki mwa Transylvania. Kabla ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, Teodor alielewa kwamba Mungu anakataza mauaji, kwa hiyo akakataa kujiunga na jeshi. Hivyo, mnamo Mei 1943, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano. Muda mfupi baadaye, alimkuta Martin Magyarosi, Pamfil Albu, na Mashahidi wengine gerezani naye akakubali kujifunza Biblia. Teodor alifanya maendeleo kwa haraka na baada ya majuma machache akajiweka wakfu kwa Yehova. Lakini alibatizwaje?
Nafasi ilitokea wakati Teodor na Mashahidi wengine 50 Warumania hivi walipokuwa wakipelekwa kwenye kambi ya Wanazi huko Bor, Serbia. Walipokuwa safarini kuelekea Bor, walikaa kwa muda mfupi huko Jászberény, Hungaria, ambako ndugu Wahungaria zaidi ya mia moja walijiunga nao. Walipokuwa huko walinzi waliwatuma ndugu kadhaa waende mtoni wakajaze pipa la maji. Walinzi hawakwenda nao kwa sababu waliwaamini. Teodor alijiunga nao na akabatizwa mtoni. Kutoka Jászberény wafungwa walipelekwa hadi Bor kwa gari-moshi na mashua.
Katika kambi ya Bor kulikuwa na Wayahudi 6,000; Wasabato 14; na Mashahidi 152. Ndugu Miron anasema hivi: “Hali zilikuwa mbaya, lakini Yehova alitusaidia. Mlinzi fulani aliyetupenda alitumwa Hungaria mara kwa mara, naye alituletea vitabu. Baadhi ya Mashahidi ambao aliwajua na kuwaamini walitunza familia yake alipokuwa safarini, kwa hiyo akawa kama ndugu yao. Mtu huyo aliyekuwa luteni alituonya kulipokuwa na hatari. Kambini kulikuwa na wazee 15 wa kutaniko, kama wanavyoitwa leo, nao walipanga mikutano mitatu kila juma. Watu 80 waliihudhuria mikutano zamu zao za kazi zilipowaruhusu. Pia tuliadhimisha Ukumbusho.”
Wenye mamlaka katika kambi fulani waliwaruhusu Mashahidi wasiofungwa wawaletee ndugu zao waliokuwa wamefungwa chakula na vitu vingine. Kati ya mwaka wa 1941 na 1945, Mashahidi 40 hivi kutoka Bessarabia, Moldova, na Transylvania walipelekwa kwenye kambi ya mateso huko Şibot, Transylvania. Kila siku walifanya kazi katika kiwanda cha mbao kilichokuwa nje ya kambi. Kwa sababu chakula kilikuwa haba kambini, Mashahidi walioishi karibu na kiwanda hicho waliwaletea chakula na nguo kila juma. Ndugu waligawa vitu hivyo kulingana na uhitaji.
Ndugu hao waliwatolea wafungwa wenzao na walinzi ushahidi mzuri kwa matendo yao. Walinzi walitambua pia kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wenye kutegemeka na kuaminika. Kwa hiyo, walipewa uhuru fulani ambao wafungwa wengine hawakuwa nao. Hata mlinzi mmoja huko Şibot akawa Shahidi.
-