-
Mambo Yenye Kupendeza Jijini RomaAmkeni!—2001 | Julai 8
-
-
Mambo Yenye Kupendeza Jijini Roma
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA
“Nadhani kwamba Romulus [mmojawapo wa waanzilishi wa Roma katika mwaka wa 753 K.W.K. kulingana na hadithi za kubuniwa] alifunuliwa kimbele na Mungu kwamba jiji hilo lingekuja kuwa makao makuu ya milki yenye nguvu.”—CICERO, MSEMAJI MROMA NA MWANASIASA ALIYEHESHIMIWA WA KARNE YA KWANZA K.W.K.
JIJI la Roma limebadilika mara nyingi kama majiji mengine ambayo yamekuwapo kwa maelfu ya miaka, na katika jiji hilo kuna mambo mengi yanayoonyesha mabadiliko hayo. Ungependa kuyaona? Huu ndio wakati unaofaa, hasa ikiwa umealikwa kuhudhuria mojawapo ya mikusanyiko ya Mashahidi wa Yehova ambayo itafanywa Agosti 10-12, 2001 huko Roma, Bari, Turin, na Milan.
Basi, unataka kuona nini? Kuna mambo ya Roma la kale, ya jamhuri ya Roma, na ya milki ya Roma. Mambo mapya zaidi ni yale yanayohusu Roma la Enzi ya Kati, Roma la Kipindi cha Mwamko (Renaissance), Roma lenye mapambo ya kupita kiasi (baroque), na vilevile Roma la kisasa. Kisha kuna Roma la Papa, Roma la watu wa kawaida, na Roma la watu wa tabaka ya juu. Kotekote katika jiji hilo kubwa kuna mambo yanayoshangaza.
Roma la Kale
Makao ya kale zaidi yalikuwa vijiji vya vibanda vya kipindi ambacho watu walianza kutumia chuma. Yaelekea vijiji hivyo vilijengwa mapema kabla ya karne ya nane K.W.K., kwenye vilima vya Roma vilivyozunguka eneo la chini karibu na sehemu isiyo na kina kirefu ya Mto Tiber. Zamani vilima vilivyozunguka sehemu hiyo vilionekana kwa urahisi, kwa hiyo ilisemekana kwamba jiji hilo lilijengwa kwenye vilima saba vinavyoitwa Quirinal, Viminal, Esquiline, Caelian, Aventine, Palatine, na Capitoline. Hata leo sehemu fulani za jiji hilo zinaitwa kwa majina ya baadhi ya vilima hivyo.
Ukiamua kutembelea Roma, usisahau ramani na kitabu cha kuongoza wasafiri. Yamkini utaona mambo yaleyale ambayo huenda ikawa Mroma aliyeishi miaka 2,000 iliyopita aliona.
Tutembelee Eneo la Baraza
Kitabu kimoja chasema kwamba, “eneo la baraza lilikuwa eneo la vitovu vya siasa na biashara, na mahakama ya Roma la kale.” Mlango mkuu wa eneo la baraza upo kwenye barabara ya Via dei Fori Imperiali. Gari la moshi la chini ya ardhi linaloitwa Metro na mabasi kadhaa yatakupeleka kule.
Uwanja wa Colosseum, ambao unajulikana pia kama Uwanja-Duara wa Maonyesho wa Flavian, upo pia katika eneo hilo. Uwanja huo ulijengwa katika enzi ya wamaliki na ni mojawapo ya vitu vya kale vinavyojulikana sana. Urefu wake wa meta 48 ni sawa na urefu wa jengo la kisasa lenye orofa 16. Upande mmoja wa uwanja huo una upana wa meta 190 hivi, na upana wa upande wa pili ni meta 155 hivi. Ulikuwa na milango 80, na ulitoshea watazamaji 55,000! Maliki Vespasian alitoa amri ya kuujenga uwanja huo katika mwaka wa 72 W.K. Fikiria jambo hilo unaposimama karibu nalo. Ikiwa kuta zingeweza kuongea . . .
Uchunguzi mbalimbali wa hivi majuzi unaonyesha kwamba huenda jengo hilo lilimalizika kujengwa kwa kutumia mali zilizoporwa ambazo vikosi vya Roma vilileta baada ya ushindi huko Yudea. Kilele cha ushindi huo kilikuwa uharibifu wa Yerusalemu mwaka wa 70 W.K. (Mathayo 24:1, 2; Luka 21:5, 6) Kwa muda wa karne nyingi mapigano ya kikatili kati ya watu au kati ya mtu na mnyama yalionyeshwa humo. Hata hivyo, yaelekea kwamba hakuna Mkristo aliyekufa humo kwa sababu ya imani yake, kama vile ambavyo watu wengi huamini.a
Karibu na Colosseum kuna Tao la Tito, ambalo lilijengwa kuwa ukumbusho wa ushindi huo. Ndani ya tao hilo unaweza kuona michoro ya maandamano ya ushindi, ambayo inaonyesha vyombo vitakatifu vya hekalu na Wayahudi mateka. Yamkini Wayahudi hao walipita hapohapo!
Hekalu la Pantheon ni hekalu maarufu la kale lenye kuvutia ambalo limedumu bila kuharibika. Awali, hekalu hilo liliwekwa wakfu kwa miungu yote; leo ni kanisa la Kikatoliki. Maliki Hadrian (76 W.K.-138 W.K.), anayejulikana kwa kujenga ukuta wa kinga sehemu ya kaskazini mwa Uingereza, alisanifu ujenzi wa hekalu hilo katika mwaka wa 118 W.K. hadi 128 W.K., nalo ni kazi bora ya wahandisi Waroma. Urefu na kipenyo za jengo hilo lenye paa la duara zina kipimo sawa—meta 43.4.
Kiwanja cha Maonyesho cha Maximus, Mlima Palatine na maeneo na majengo mengineyo yatuonyesha jinsi hali ilivyokuwa zamani. Kotekote jijini kuna minara mirefu yenye pembe nne na nguzo zenye michoro, kama zile za maliki Trajan na Marcus Aurelius, ambazo zinatukumbusha fahari ya miliki ya sita inayotajwa katika Biblia.
Roma la Enzi ya Mitume
Tunaweza kuona mambo machache yaliyohusu maisha ya Wakristo wa kwanza jijini Roma ijapokuwa baada ya muda mfupi tu Jumuiya ya Wakristo yenye kuasi imani ilichukua mahali pa Ukristo uliofundishwa na mitume. Kwa mfano tunapotazama barabara iitwayo Barabara ya Apia, tunakumbuka jinsi mtume Paulo alivyosindikizwa na ndugu zake Wakristo hadi jijini. (Matendo 28:14-16) Hata hivyo, tunapaswa kuwa waangalifu tusikubali masimulizi yote bila kuthibitisha yaliyo ya kweli. Kwa mfano, karibu na eneo la baraza, kuna gereza liitwalo Mamertine Prison. Inasemekana kwamba Petro alifungwa hapo. Lakini Biblia haisemi kwamba Petro alisafiri mpaka Roma.
Ukiwa katika eneo la Barabara ya Apia, huenda ungetaka kutembelea zile catacomb, ambazo ni njia za chini ya ardhi zilizotumiwa kama makaburi. Njia hizo zina urefu wa mamia ya kilometa. Uchunguzi mbalimbali wa makaburi haya umefichua mambo yanayohusu ibada ya wafu na wafia-imani, na dhana kuhusu nafsi isiyoweza kufa. Kwa hiyo, wale waliotumia makaburi hayo hawakuwa wafuasi wa kweli wa mafundisho ya awali ya Yesu.b
Jinsi Kipindi cha Mwamko Kilivyobadili Roma
Roma lilibadilika sana katika Kipindi cha Mwamko (kuanzia karne ya 14 hadi 16). Ongezeko la sifa na mamlaka za Papa lilichangia mabadiliko hayo. Wasanii, wasanifu wa ujenzi, na mafundi waliitwa kwenye makazi ya Papa. Mmoja anayejulikana sana alikuwa Michelangelo. Baadhi ya kazi zake za sanaa zimehifadhiwa huko Vatican City. Ukiingia katika kanisa dogo la Sistine Chapel kupitia Jumba la Ukumbusho la Vatikani unaweza kutazama mchoro wake mashuhuri wa “Hukumu ya Mwisho,” na michoro yake mingine kwenye dari la kanisa hilo. Inafaa kuzingatia kwamba mchoro huo “Hukumu ya Mwisho” hauonyeshi toharani.
Kazi nyingine bora ya sanaa ya Michelangelo ni sanamu ya Musa, nayo inapatikana katika kanisa la Roma linaloitwa Mtakatifu Petro Aliyefungwa kwa Minyororo. Katika Basilika ya Mtakatifu Petro kuna baadhi ya kazi bora za sanaa za Michelangelo. Mojawapo ni sanamu iitwayo “Pietà,” nayo inaonyesha Kristo aliyekufa mikononi mwa mamake. Kuna vitu vingine bora vya sanaa pia katika kanisa hilo.
Jambo linalopendeza Mashahidi wa Yehova ni kwamba jina la Mungu, Yehova, limeandikwa kwa herufi za Kiebrania katika sehemu kadhaa za kanisa hilo. Litazame kwenye kaburi la Clement wa 13 na katika Kanisa Dogo la Kukabidhi.
Roma Lenye Mapambo Mengi
Yamkini, mambo ya Roma yanayopendeza zaidi ni yale yaliyoundwa kwa kufuata mtindo wa baroque (mtindo wenye mapambo mengi sana). Kichapo kimoja kinasema kwamba mtindo wa baroque “una mambo mbalimbali yenye kupendeza.” Mtindo huo ulianza mwisho-mwisho mwa karne ya 16 na kufikia karne ya 18 ulikuwa umebadilika kuwa mtindo wa rococo. Bernini alifuata mtindo wa baroque alipojenga kaburi la Papa Alexander wa Saba katika kanisa la Mtakatifu Petro. Bernini alikuwa msanii aliyependwa sana na Mapapa. Alifanya mabadiliko katika makanisa, majumba ya kifalme, sanamu, na chemchemi za Roma. Tazama ua ulio mbele ya Kanisa la Mtakatifu Petro. Ua huo unazungukwa na safu yenye fahari ya Bernini. Au tazama ua uitwao Piazza del Popolo ambao ‘ni kama chumba kikubwa kinachoelekeza mtu katikati ya jiji la Roma.’ Kazi za Bernini na sanaa nyingine za mtindo wa baroque zipo kila mahali! Hakikisha umeona jinsi Chemchemi ya Trevi inavyorembesha mazingira. Au zile chemchemi kwenye Piazza Navona kama vile Fontana dei Fiumi (Chemchemi ya Mito Minne) na Fontana del Moro (Chemchemi ya Mmoori) ambazo ni kazi za Bernini.
Jiji la Kisasa
Siku hizi si kawaida kuona mabadiliko jijini Roma. Badiliko la mwisho lilifanywa katika miaka ya 1930 wakati mtaa uitwao Esposizione Universale di Roma (E.U.R.) ulipojengwa. Mtaa huo ulijengwa kwa sifa ya Ufashisti wakati wa utawala wa Mussolini.
Wasimamizi wa jiji hilo sasa wananuia kuhifadhi na kukazia umuhimu wa sanaa za Roma zenye thamani kubwa sana. Sanaa za Roma hazipatikani tu kwenye barabara na nyua za jiji bali pia katika majumba ya ukumbusho 100 yaliyopo jijini. Kabla ya kuondoka kwenda kwenye majumba ya ukumbusho, machimbo ya akiolojia, au kwenda kutazama vitu mbalimbali vya ukumbusho, huenda likawa jambo la hekima kujua saa za kufungua na kufunga vituo hivyo kwa kuchunguza kitabu cha kuongoza wasafiri au kupitia Internet.
Ingawa Roma linajulikana hasa kwa sababu ya Vatikani, kuna dini nyingine nyingi katika jiji hilo. Kuna ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova na Jumba moja la Kusanyiko huko. Kuna Mashahidi 10,000 hivi jijini, ambao hukutanika katika makutaniko na vikundi 130. Wanafanya mikutano yao katika lugha 12, mbali na Kiitalia. Umekaribishwa kwenye Sala del Regno (Jumba la Ufalme) lolote.
Basi, tunakukaribisha Roma, utembee sehemu ile ambayo inakupendeza zaidi, kwa kuwa mwandishi Johann Wolfgang von Goethe aliandika, ‘unaweza kujua Roma tu, ukiwapo Roma.’
[Maelezo ya Chini]
a Soma toleo la Amkeni!, la Kiingereza, la Aprili 8, 1991, ukurasa 24-27.
b Soma toleo la Agosti 8, 1995 la Amkeni!, ukurasa wa 16-20.
-
-
Mambo Yenye Kupendeza Jijini RomaAmkeni!—2001 | Julai 8
-
-
[Picha katika ukurasa wa 14]
Tao la Tito, lenye michoro ya mali zilizoporwa za hekalu la Yerusalemu
[Picha katika ukurasa wa 14]
Uwanja wa Colosseum
[Picha katika ukurasa wa 15]
Nguzo iliyochongwa na Marcus Aurelius
[Picha katika ukurasa wa 15]
Barabara ya Apia
[Picha katika ukurasa wa 15]
Pantheon, hekalu la kipagani lililowekwa wakfu kwa miungu yote, sasa ni kanisa la Kikatoliki
[Picha katika ukurasa wa 16]
Sehemu ya mchoro wa “Hukumu ya Mwisho,” wa Michelangelo katika kanisa dogo la Sistine Chapel
[Picha katika ukurasa wa 16]
Chemchemi ya Mito Minne iliyochongwa na Bernini
[Picha katika ukurasa wa 17]
Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova
[Picha katika ukurasa wa 17]
Chemchemi ya Trevi
[Picha katika ukurasa wa 17]
Hekaya inasema kwamba Romulus na Remus, waanzilishi wa jiji la Roma, walinyonyeshwa na mbwa-mwitu wa kike
-