Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Rwanda
    2012 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • MAUAJI YA JAMII NZIMA-NZIMA YAANZA!

      Jioni ya Aprili 6, ndege fulani ililipuliwa kwa kufyatuliwa risasi karibu na mji wa Kigali. Ilikuwa imebeba rais wa Rwanda na wa Burundi. Abiria wote walikufa. Watu wachache tu ndio waliojua jambo hilo; stesheni rasmi ya redio haikutoa tangazo lolote.

      Wale wamishonari watatu, Ndugu na Dada Bint, na Henk hawatasahau kamwe siku zilizofuata. Ndugu Bint aeleza: “Tulipoamka asubuhi ya Aprili 7, tulisikia sauti za bunduki na milipuko ya mabomu ya mkononi. Haikushangaza kwani katika miezi iliyokuwa imepita hali ya kisiasa nchini ilikuwa yenye msukosuko sana. Hata hivyo, tulipokuwa tukitayarisha kiamsha-kinywa, tulipokea simu. Emmanuel Ngirente, aliyekuwa katika ofisi ya tafsiri, alituambia kwamba stesheni ya redio ya kitaifa ilikuwa imetangaza kifo cha marais wawili waliokuwa katika ndege iliyolipuliwa. Wizara ya Ulinzi ikawaonya watu mjini Kigali wasitoke nyumbani.

      “Saa tatu asubuhi, tuliwasikia waporaji wakivunja nyumba ya jirani yetu. Wakaiba gari na kumuua mama mwenye nyumba.

      “Punde si punde, askari na waporaji hao wakaja kwetu, wakaligonga lango la chuma na kupiga kengele. Tukakaa kimya. Kwa sababu fulani, hawakujaribu kuvunja lango bali waliondoka na kwenda kwa nyumba nyingine. Milio ya risasi na milipuko ilisikika kila mahali, kwa hiyo hatukuthubutu kuondoka. Milio ya bunduki ilisikika karibu na nyumba yetu, hivyo tukaenda kwenye sehemu iliyo katikati ya vyumba ili kukwepa risasi. Tulitambua kwamba hali haitabadilika karibuni, kwa hiyo, tukajaribu kuhifadhi chakula kwa kutayarisha mlo mmoja tu kwa siku. Siku iliyofuata, tulipokuwa tu tumemaliza kula chakula cha mchana na tunasikiliza habari za kimataifa kwenye redio, Henk akasema, ‘Ndio hao kwenye ua wetu!’

      “Hatukuwa na wakati wa kupoteza. Tuliingia bafuni na kujifungia humo. Kisha, tukasali pamoja tukimwomba Yehova atusaidie tuvumilie chochote kitakachotokea. Kabla ya kumaliza kusali, tuliwasikia wanamgambo na waporaji wakivunja madirisha na milango. Baada ya dakika chache, walikuwa ndani, wakipiga kelele na kuvunja fanicha. Walikuwa waporaji 40 hivi—wanaume, wanawake, na watoto—pamoja na wanamgambo. Pia, tulisikia risasi zikifyatuliwa huku wakipigania vitu walivyopata.

      “Baada ya muda huo ulioonekana kuwa mrefu sana—ingawa ilikuwa dakika 40 hivi—wakajaribu kufungua bafu. Kisha, kwa sababu mlango ulikuwa umefungwa kwa funguo, wakajaribu kuuvunja. Sasa tukatambua kwamba tunapaswa kujisalimisha. Wanaume hao walitenda kiwazimu na walikuwa wametumia dawa za kulevya. Wakatutisha kwa mapanga na visu. Jennie alimlilia Yehova kwa sauti. Mwanamume mmoja akatoa panga na kumpiga Henk shingoni kwa upande ulio bapa. Henk akaanguka bafuni. Kwa njia fulani, nilifanikiwa kupata pesa na kuwapa washambuliaji hao. Wakazipigania.

      “Ghafula, tulimwona kijana mmoja akitukazia macho. Ingawa hatukumjua, alitutambua, labda kwa sababu ya kazi yetu ya kuhubiri. Akatusukuma ndani ya bafu na kutuambia tufunge mlango. Akasema kwamba angetuokoa.

      “Kelele za waporaji ziliendelea kwa dakika 30 hivi, na hatimaye kukatulia. Baadaye, kijana huyo alirudi na kutuambia kwamba tunaweza kutoka nje. Akisisitiza kwamba tuondoke mara moja, alitusindikiza kutoka nyumbani. Hatukuchukua chochote. Tulishtuka kuona miili ya baadhi ya jirani zetu waliokuwa wameuawa. Washiriki wawili wa Walinzi wa Rais walitusindikiza hadi kwenye nyumba ya ofisa fulani wa jeshi iliyokuwa karibu. Kisha, ofisa huyo akatusindikiza hadi kwenye Hoteli ya Mille Collines, ambapo watu wengi walikuwa wamekimbilia. Hatimaye, mnamo Aprili 11, tukahamishiwa Kenya, baada ya kuhangaika kwa saa nyingi na kusafirishwa na wanajeshi kutoka mjini kupitia njia isiyo ya moja kwa moja hadi kwenye uwanja wa ndege. Tulifika kwenye eneo la mapokezi la Betheli ya Nairobi tukiwa wachafu. Henk, aliyekuwa ametenganishwa nasi wakati wa kuhamishwa, aliwasili saa kadhaa baadaye. Familia ya Betheli ilituhangaikia sana na kututia moyo.”

      SALA YA MSICHANA MDOGO YAWAOKOA

      Siku moja baada ya ndege iliyowaua marais wa Rwanda na Burundi kuanguka, askari sita wa serikali walienda kwa Ndugu Rwakabubu. Macho yao yalikuwa mekundu sana, walinuka pombe, na walijiendesha kwa njia iliyoonyesha kwamba walikuwa wametumia dawa za kulevya. Wakaamuru wapewe silaha. Ndugu Rwakabubu akawaambia kwamba yeye na familia yake ni Mashahidi wa Yehova na hivyo hawana silaha.

      Askari hao walijua kwamba kwa sababu Mashahidi wa Yehova hawaungi mkono upande wowote, walikataa kuunga mkono serikali, na hawakuwasaidia wanajeshi kifedha. Hilo liliwakasirisha. Gaspard na Melanie Rwakabubu, si Watutsi, lakini wapiganaji wa Interahamwe waliwaua pia Wahutu ambao hawakuwa na msimamo mkali, hasa ikiwa walidhaniwa kuwa wanawahurumia Watutsi au jeshi lililopinga serikali.

      Askari hao waliwapiga Gaspard na Melanie kwa vijiti na kuwapeleka pamoja na watoto wao watano katika chumba cha kulala. Wakaondoa mashuka kitandani na kuanza kuwafunika nayo. Baadhi yao walikuwa na makombora mikononi, hivyo ilikuwa wazi walitaka kuwaua. Gaspard akawauliza, “Tunaweza kusali tafadhali?”

      Kwa dharau, askari mmoja alikataa ombi lao. Kisha, baada ya mazungumzo fulani askari hao wakakubali, lakini shingo upande. Wakawaambia “Sawa, tunawapa dakika mbili msali.”

      Wakasali kimya-kimya, lakini Deborah Rwakabubu, aliyekuwa na umri wa miaka sita, akasali kwa sauti: “Yehova, watu hawa wanataka kutuua, lakini tutawarudiaje watu niliowahubiria na kuwaachia magazeti matano nikiwa na Baba? Wanasubiri tuwarudie na wanahitaji kujua kweli. Nakuahidi kwamba tusipouawa, nitakuwa mhubiri, nibatizwe, na kuwa painia! Yehova, tuokoe!”

      Waliposikia sala hiyo, askari hao wakashangaa. Mwishowe, mmoja wao akasema: “Kwa sababu ya sala ya huyu msichana mdogo, hatutawaua. Wengine wakija, waambie kwamba tayari tumekuwa hapa.”b

      HALI YAZIDI KUZOROTA

      Pole kwa pole vita vilizidi kadiri majeshi yaliyopinga serikali (Rwandan Patriotic Front) yalivyozidi kukaribia mji wa Kigali. Hilo liliwachochea wapiganaji wa Interahamwe kuendeleza mauaji zaidi.

      Kulikuwa na vizuizi vya barabarani kotekote mjini na katika makutano ya barabara. Vizuizi hivyo vilikuwa chini ya ulinzi wa wanajeshi na wapiganaji wa Interahamwe wenye silaha pamoja na wenyeji. Wanaume wote wenye nguvu pamoja na wapiganaji wa Interahamwe walilazimika kulinda vizuizi hivyo mchana na usiku. Kusudi la vizuizi hivyo lilikuwa kuwatambua na kuwaua Watutsi.

      Kadiri mauaji yalivyoendelea kotekote nchini, ndivyo mamia ya maelfu ya wakaaji wa Rwanda walivyoacha makao yao. Wengi wao, kutia ndani Mashahidi wa Yehova, walitafuta usalama nchini Kongo na Tanzania.

      KUKABILI VITA NA KIFO

      Yafuatayo ni masimulizi ya ndugu na dada zetu wakati mauaji ya jamii nzima-nzima yalipoanza. Kumbuka kwamba Mashahidi wa Yehova nchini Rwanda walikuwa wamepitia majaribu makali yaliyoimarisha na kuboresha imani yao na kuwapa ujasiri katika miaka ya 1980. Imani yao iliwasaidia ‘kutokuwa sehemu ya ulimwengu’ kwa kutoshiriki katika uchaguzi, kutotumia silaha ili kujilinda, na kutojiingiza katika siasa. (Yoh. 15:19) Kwa sababu ya kutojihusisha katika mambo hayo, walikabili dhihaka, vifungo, mateso, na kifo. Hata hivyo, ujasiri wao uliwasaidia katika hali hizo zote. Mbali na kutojihusisha katika mauaji, sifa hizo zilizojaribiwa pamoja na upendo wao kwa Mungu na jirani, ziliwasaidia Mashahidi wa Yehova kuhatarisha uhai wao ili kuwalinda wenzao.

      Kuna mambo mengi ambayo hayajatajwa. Ndugu wengi wangependa kusahau mambo hayo yenye kutisha, kwa kuwa hawatafuti kulipiza kisasi. Tunatumaini kwamba masimulizi haya ya imani yao yatatuchochea sote tuonyeshe kikamili upendo unaowatambulisha wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo.—Yoh. 13:34, 35.

      KISA CHA JEAN NA CHANTAL

      Jean de Dieu (John) Mugabo, ndugu mchangamfu na mwenye kujali, alianza kujifunza na Mashahidi wa Yehova mnamo 1982. Kabla ya kubatizwa katika mwaka wa 1984, alikuwa tayari amefungwa gerezani mara tatu kwa sababu ya msimamo wake kama Shahidi wa Yehova. Mke wake, Chantal, alibatizwa pia mwaka wa 1984, na wakafunga ndoa mwaka wa 1987. Mauaji ya jamii nzima-nzima yalipoanza, walikuwa na watoto watatu, wote wasichana. John na Chantal waliishi na kitinda-mimba wao mwenye umri wa miezi sita huku wale watoto wengine wakiishi na wazazi wa Chantal katika eneo lingine.

      Siku ya kwanza ya mauaji, Aprili 7, 1994, askari na wapiganaji wa Interahamwe walianza kuvamia nyumba zote za Watutsi. John alikamatwa na kupigwa kwa marungu; lakini akafanikiwa kutoroka na kukimbilia Jumba la Ufalme lililo karibu akiwa pamoja na ndugu mwingine. Chantal naye, bila kujua kilichompata mumewe, alijaribu kuondoka mjini pamoja na mtoto wao mdogo ili kwenda kuungana na watoto wao wengine.

      John asimulia mambo yaliyompata: “Jumba la Ufalme lilikuwa na dohani kubwa kwa maana jengo hilo lilikuwa duka la kuokea mikate hapo awali. Kwa juma moja, tulijificha katika Jumba la Ufalme lenyewe, na dada mmoja Mhutu alituletea chakula ilipokuwa salama kufanya hivyo. Baadaye, tulijificha kwenye paa, kati ya mabati na dari, ambapo kulikuwa na joto sana jua lilipowaka. Tulitaka sana kupata mahali pazuri zaidi pa kujificha, kwa hiyo tulibomoa sehemu fulani ya dohani hilo la matofali, tukaingia na kukaa huko kwa zaidi ya mwezi mmoja tukiwa tumechutama.

      “Karibu na hapo, wapiganaji wa Interahamwe walikuwa wameweka kizuizi cha barabarani na mara nyingi waliingia ndani ya Jumba la Ufalme kuzungumza au kujikinga mvua. Tungewasikia wakiongea. Dada huyo aliendelea kutuletea chakula ilipowezekana. Wakati mwingine, nilihisi sitaweza kuvumilia tena, lakini tuliendelea kumwomba Yehova atusaidie kustahimili. Mwishowe, mnamo Mei 16, dada huyo alitujulisha kwamba wanajeshi wa Rwandan Patriotic Front wamechukua udhibiti wa eneo hilo la mji, na hivyo hakuna haja ya kujificha tena.”

      Naye Chantal, mke wa John, alipatwa na nini? Anaeleza: “Nilifaulu kutoroka kutoka nyumbani pamoja na mtoto wetu mnamo Aprili 8. Nilikutana na Immaculée, ambaye kitambulisho chake kilionyesha kwamba yeye ni Mhutu, na Suzanne, ambaye ni Mtutsi. Tulitaka kufika Bugesera, mji ulio umbali wa kilomita 50, ambapo wazazi wangu waliishi pamoja na watoto wetu. Kwa kuwa tulisikia kwamba kuna vizuizi katika barabara zote za kuelekea nje ya mji, tuliamua kwenda kwenye kijiji kilicho karibu na mji wa Kigali, ambako Immaculée alikuwa na mtu wa ukoo aliyeitwa Gahizi, na ambaye pia alikuwa Shahidi wa Yehova. Gahizi, aliyekuwa Mhutu, alitukaribisha na licha ya vitisho kutoka kwa majirani, alifanya yote aliyoweza ili kutusaidia. Askari wa serikali na wapiganaji wa Interahamwe waliposikia kwamba Gahizi alikuwa anawalinda Watutsi, walimpiga risasi.

      “Baada ya kumwua Gahizi, askari hao walitupeleka mtoni ili kutuua. Tukiwa na hofu nyingi, tulisubiri kuuawa. Ghafula, kukazuka bishano kali kati ya askari hao, na mmoja wao akasema: ‘Usiue wanawake. Tukiwaua, tutapatwa na mkosi. Huu ni wakati wa kuua wanaume tu.’ Baada ya hapo, André Twahirwa, mmoja wa ndugu waliokuwa wakitufuata na ambaye alikuwa amebatizwa juma lililotangulia, akatupeleka kwake nyumbani licha ya kukatazwa na majirani. Siku iliyofuata, akaandamana nasi hadi Kigali, ambapo alinuia kututafutia mahali salama pa kukaa. Alitusaidia kupita vizuizi kadhaa vya barabarani vilivyokuwa hatari sana. Immaculée alibeba mtoto wangu ili tukikamatwa, aweze kumwokoa. Mimi na Suzanne tulipasua vitambulisho vyetu ili tusigunduliwe.

      “Katika kizuizi kimoja, Interahamwe walimgonga Immaculée na kusema, ‘Mbona unasafiri na Watutsi hawa?’ Mimi na Suzanne tulizuiwa tusipite. Hivyo Immaculée na André walitangulia hadi nyumbani kwa Ndugu Rwakabubu. André na ndugu wengine wawili, Simon na Mathias, walihatarisha uhai wao sana ili kutusaidia kupita kizuizi hicho cha mwisho na kunipeleka kwa Ndugu Rwakabubu, naye Suzanne akaenda kwa mmoja wa watu wake wa ukoo.

      “Hata hivyo, ilikuwa hatari sana kwangu kuendelea kuishi kwa Ndugu Rwakabubu, hivyo, kwa shida nyingi, ndugu walinisaidia kwenda kwenye Jumba la Ufalme ambapo Mashahidi wengine walifichwa. Kufikia wakati huo, ndugu na dada kumi ambao ni Watutsi walikuwa wamejificha humo. Immaculée alikataa kuniacha. Alisema, ‘Wakikuua nami ninusurike, nitamwokoa mtoto wako.’”c

      Wakati huo, Védaste Bimenyimana, ndugu aliyeishi karibu na ambaye alikuwa na mke Mtutsi, alikuwa tu amefaulu kupeleka familia yake mahali salama. Baadaye, akarudi kwenye Jumba la Ufalme kuwasaidia ndugu kukimbilia mahali salama. Inapendeza kwamba wote waliokoka.

      Baada ya mauaji, John na Chantal walipata habari kwamba wazazi wao kutia ndani binti zao wawili wenye umri wa miaka miwili na mitano, ambao waliishi pamoja na wazazi hao, walikuwa wameuawa pamoja na watu wengine 100 wa ukoo. Walihisije baada ya kufiwa na watu wengi hivyo? “Mwanzoni, haikuwa rahisi kuvumilia,” asema Chantal. “Tulihisi tumekufa ganzi. Hakuna aliyewazia kwamba watu wengi hivyo wangekufa. Tuliacha yote mikononi mwa Yehova, tukiwa na tumaini la kuwaona watoto wetu tena wakati wa ufufuo.”

      WAFICHWA KWA SIKU 75!

      Tharcisse Seminega alibatizwa nchini Kongo mwaka wa 1983. Wakati wa mauaji alikuwa akiishi Butare, Rwanda, kilomita 120 hivi kutoka Kigali. Asema, “Baada ya ndege iliyombeba rais kuanguka huko Kigali, tulisikia kwamba amri ilitolewa ya kuwaua Watutsi wote. Ndugu wawili walijaribu kutusaidia tukimbilie Burundi, lakini wapiganaji wa Interahamwe walikuwa wanalinda barabara na vijia vyote.

      “Tulikuwa wafungwa katika nyumba yetu wenyewe, na hatukujua twende wapi. Askari wanne walikuwa nje ya nyumba yetu na mmoja wao alisimama mita 180 kutoka nyumba yetu akiwa ametuelekezea bunduki ya rasharasha. Nilisali: ‘Ee Yehova, hatuwezi kufanya chochote ili kujiokoa. Ni wewe tu unayeweza kutusaidia!’ Jioni hiyo, ndugu fulani alikuja nyumbani akihofia kwamba tumeshakufa. Wanajeshi hao walimruhusu kuingia ndani ya nyumba na kukaa kwa dakika chache. Alifurahi sana kupata tuko hai, na akafanikiwa kwenda kwake na watoto wetu wawili. Kisha, akawajulisha ndugu wengine wawili, Justin Rwagatore na Joseph Nduwayezu, kwamba tulikuwa mafichoni na tulihitaji msaada. Wakaja usiku huo; na licha ya shida na hatari, wakatupeleka kwa Justin.

      “Hatukukaa kwa Justin sana kwa sababu siku iliyofuata, watu walijua kwamba tumejificha huko. Siku hiyohiyo, mwanamume fulani anayeitwa Vincent alikuja kutuonya kuwa Interahamwe walikuwa wanajitayarisha kutuvamia na kutuua. Mwanamume huyo alikuwa amejifunza Biblia pamoja na Justin lakini hakuwa amechukua msimamo katika kweli. Vincent alipendekeza kwamba tujifiche kwanza katika kichaka kilichokuwa karibu na nyumba ya Justin. Kisha, usiku huo akatupeleka kwake. Alituficha katika kibanda cha mbuzi. Kibanda hicho kilikuwa cha matope, chenye sakafu ya udongo, paa la nyasi, na hakikuwa na dirisha.

      “Siku zilionekana kuwa ndefu sana katika kibanda hicho kilichokuwa karibu na makutano ya barabara, na hatua chache tu kutoka soko lenye shughuli nyingi zaidi katika eneo hilo. Tungewasikia wapita-njia wakiongea kuhusu mambo waliyofanya siku hiyo, kutia ndani masimulizi yenye kutisha ya mauaji waliyotekeleza na mambo waliyopanga kufanya. Hofu yetu ilizidi, na tuliendelea kusali tusiuawe.

      “Vincent alifanya yote aliyoweza ili kutuandalia mahitaji yetu. Tulikaa hapo kwa mwezi mmoja, na kuelekea mwishoni mwa mwezi wa Mei, mahali hapo pakawa hatari sana kwetu kwa sababu wapiganaji wa Interahamwe walikuwa wakikimbilia eneo hilo kutoka Kigali. Ndugu waliamua kutuhamisha hadi kwa ndugu mmoja aliyekuwa na chumba fulani cha chini ya ardhi ndani ya nyumba yake. Tayari alikuwa anawaficha ndugu watatu ndani ya chumba hicho. Tulitembea usiku kwa muda wa saa nne na nusu na safari hiyo ilikuwa hatari. Mvua kubwa ilinyesha, na kwa sababu hiyo wauaji hawakutuona.

      “Maficho yetu mapya yalikuwa shimo lenye urefu wa mita 1.5 na mlango wa ubao. Ili kuingia shimoni, tuliteremka kwa ngazi, na kisha tukachutama na kutambaa kupitia mtaro fulani mpaka tulipofika kwenye sehemu wazi yenye ukubwa wa mita mbili mraba. Kulikuwa na harufu ya kuvu, na ni mwangaza kidogo tu uliotufikia kupitia ufa fulani. Tulikaa hapo pamoja na mke wangu Chantal, watoto wetu watano, na watu wengine watatu. Sote kumi tuliishi kwa woga ndani ya shimo hilo dogo kwa majuma sita. Hatukuthubutu kuwasha mshumaa, kwa kuwa mwangaza ungetusaliti. Hata hivyo, katika shida na kuteseka huko kwote, Yehova alitutegemeza. Ndugu walihatarisha maisha yao kuja kutuletea chakula, dawa, na kututia moyo. Wakati mwingine tuliwasha mshumaa mmoja wakati wa mchana ili kusoma Biblia, gazeti la Mnara wa Mlinzi, au andiko la siku.

      “Kila hadithi ina mwisho wake,” Tharcisse aendelea kusema. “Hadithi hiyo ilifikia mwisho Julai 5, 1994. Vincent alitufahamisha kwamba jeshi lililokuwa linawafukuza wapiganaji wa Interahamwe lilikuwa limedhibiti eneo la Butare. Tulipotoka ndani ya chumba hicho cha chini ya ardhi, watu wengine hawakudhani sisi ni Wanyarwanda, tulikuwa tumegeuka rangi na kuwa weupe sana kwa sababu ya kukosa jua. Isitoshe, kwa muda fulani hatungeweza kuzungumza kwa sauti, tulinong’ona tu. Ilituchukua majuma kadhaa kurudia hali ya kawaida.

      “Matukio hayo yote yalibadili sana maoni ya mke wangu, ambaye kwa miaka kumi alikataa kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Lakini sasa, alianza kujifunza Biblia. Watu walipomwuliza kwa nini, alijibu: ‘Nilivutiwa na upendo tulioonyeshwa na akina ndugu na pia jinsi walivyojidhabihu ili kutuokoa. Pia, niliona mkono wenye nguvu wa Yehova, ambaye alituokoa kutoka kwa panga za wauaji.’ Alijiweka wakfu kwa Yehova na akabatizwa katika kusanyiko la kwanza baada ya vita.

      “Tunawathamini sana akina ndugu na dada ambao walitusaidia kuokoka kupitia matendo yao na sala zao za kutoka moyoni. Tumejionea wenyewe upendo wao mkubwa unaotoka moyoni, na ambao unashinda tofauti za kijamii.”

      KUMSAIDIA ALIYESAIDIA

      Baadaye, Justin Rwagatore, mmoja wa akina ndugu waliosaidia familia ya Ndugu Seminega, alihitaji msaada. Mwaka wa 1986 alifungwa gerezani kwa sababu ya kutojiingiza katika siasa za serikali iliyokuwa mamlakani. Miaka kadhaa baada ya kuilinda familia ya Ndugu Seminega, Justin na ndugu wengine walikamatwa tena kwa sababu ya msimamo wao wa kutounga mkono upande wowote. Ndugu Seminega alikuwa mmoja wa ndugu walioenda kukutana na wenye mamlaka kuhusu msimamo wa Mashahidi wa Yehova wa kutojiingiza katika siasa. Aliwaeleza wenye mamlaka jinsi Justin alivyofanya mengi ili kuiokoa familia yake. Hivyo, ndugu wote wakaachiliwa.

      Mfano mzuri wa ndugu zetu wakati wa mauaji uliwachochea wengine kuikubali kweli. Suzanne Lizinde, mwanamke Mkatoliki mwenye umri wa miaka 60 na kitu, aliona jinsi dini yake ilivyounga mkono mauaji hayo. Alichochewa kufanya maendeleo ya haraka alipoona mwenendo wa Mashahidi wa Yehova katika eneo la kwao wakati wa mauaji na pia upendo uliopo miongoni mwao. Suzanne alibatizwa Januari 1998 na hakuwahi kukosa mikutano hata kama alilazimika kutembea umbali wa kilomita 5 katika eneo lenye vilima. Pia, aliisaidia familia yake kujifunza kweli. Leo mwana wake mmoja ni mzee wa kutaniko, na mjukuu mmoja ni mtumishi wa huduma.

      MAMIA YA MAELFU WATOROKA

      Henk van Bussel, mmishonari aliyetumwa Rwanda mwaka wa 1992, alikimbilia Kenya mnamo Aprili 1994, na mara kwa mara alisafiri hadi Goma, mashariki mwa Kongo, ili kusaidia katika juhudi za kutoa misaada kwa wakimbizi wa Rwanda. Wakiwa upande wa Kongo, ndugu walitembea-tembea karibu na vivukio vya mpakani wakiwa wameshika machapisho ya Biblia na wakiimba nyimbo za Ufalme ili Mashahidi waliokuwa wakivuka kutoka Rwanda wawatambue.

      Hofu ilitanda kila mahali. Huku vita kati ya vikosi vya serikali na Rwandan Patriotic Front vikiendelea, mamia ya watu walikimbilia nchi ya Kongo na Tanzania. Ndugu waliokimbilia mji wa Goma walikusanyika katika Jumba la Ufalme. Baadaye, kambi ya wakimbizi ilijengwa nje ya mji na ingetoshea zaidi ya watu 2,000—Mashahidi wa Yehova pekee, watoto wao, na watu wenye kupendezwa. Ndugu walianzisha kambi nyingine kama hizo katika maeneo mengine ya mashariki mwa Kongo.

      Ijapokuwa watu waliokimbia walikuwa hasa Wahutu walioogopa adhabu, Mashahidi waliokimbia pamoja walikuwa Wahutu na Watutsi. Ilikuwa hatari sana kwa Watutsi kuvuka mpaka na kuingia Goma, kwa kuwa mauaji ya Watutsi yaliendelea. Wakati mmoja, iligharimu dola 100 za Marekani kumsafirisha ndugu mmoja Mtutsi nje ya nchi kisiri.

      Wakiwa nchini Kongo, akina ndugu walitaka kukaa pamoja. Hawakutaka kushirikiana kwa vyovyote na Interahamwe, waliokuwa wanaendeleza utendaji wao katika kambi zilizoanzishwa na Umoja wa Mataifa. Isitoshe, wakimbizi wengi wasio Mashahidi waliiunga mkono serikali iliyokuwa inaondolewa mamlakani. Watu hao, na hasa Interahamwe, hawakuwapenda Mashahidi wa Yehova kwa kuwa Mashahidi hawakushirikiana nao. Akina ndugu walitaka kujitenga nao ili pia wawalinde ndugu zao Watutsi.

      Wakimbizi hao wa Rwanda walihitaji msaada kwa kuwa waliacha vitu vyao vyote. Mashahidi wa Yehova kutoka Kenya, Kongo, Ubelgiji, Ufaransa, na Uswisi walisaidia kwa pesa, dawa, chakula, mavazi na pia madaktari na wauguzi. Mojawapo ya ndege za kwanza za msaada, ilibeba mahema mengi madogo kutoka ofisi ya tawi ya Ufaransa. Baadaye, ofisi ya tawi ya Ubelgiji ilituma mahema makubwa, ambayo yangetoshea familia nzima-nzima. Pia, vitanda vinavyoweza kubebwa kwa urahisi na vile vya kutiwa hewa ndani vilitumwa. Ofisi ya tawi ya Kenya nayo ilituma zaidi ya tani mbili za nguo na blanketi zaidi ya 2,000.

      MLIPUKO WA KIPINDUPINDU

      Baada ya kukimbia Rwanda, zaidi ya Mashahidi 1,000 na watu wenye kupendezwa waliishi katika Jumba la Ufalme la Goma na katika sehemu ya ardhi iliyopakana na Jumba hilo. Inasikitisha kwamba kwa sababu ya idadi kubwa ya wakimbizi kulitokea mlipuko wa maradhi ya kipindupindu mjini Goma. Upesi, ofisi ya tawi ya Kongo (Kinshasa) ilituma dawa, na Ndugu Van Bussel akapeleka makatoni 60 ya dawa kutoka Nairobi hadi Goma. Kwa muda, Jumba la Ufalme lilitumiwa kama hospitali, na jitihada zilifanywa ili kuwatenga wagonjwa. Loic Domalain na ndugu mwingine, wote wawili madaktari, pamoja na Aimable Habimana, daktari msaidizi kutoka Rwanda, walifanya kazi mfululizo. Pia, Ndugu Hamel kutoka Ufaransa alisaidia sana na vilevile ndugu na dada wengi wenye ujuzi wa kimatibabu walijitolea kuwatunza wagonjwa.

      Licha ya jitihada kubwa za kuzuia ugonjwa huo, zaidi ya ndugu na watu wenye kupendezwa 150 waliathirika, na 40 hivi wakafa kabla ya ugonjwa huo wenye kufisha kukomeshwa. Baadaye, ndugu walikodi sehemu kubwa ya ardhi ambayo ingetumiwa kama kambi ya Mashahidi wa Yehova. Mamia ya mahema madogo-madogo yalisimamishwa, na hema moja kubwa kutoka Kenya lilitumiwa kama hospitali. Wafanyakazi wa afya kutoka Marekani walivutiwa na usafi na mpangilio walioona katika kambi hiyo.

      Kufikia mapema Agosti 1994, halmashauri ya kutoa misaada mjini Goma ilikuwa ikiwatunza wakimbizi 2,274—Mashahidi, watoto, na watu wenye kupendezwa. Wakati huohuo, kulikuwa na ndugu wengine wakimbizi katika miji ya Bukavu na Uvira, iliyo mashariki mwa Kongo, na pia nchini Burundi. Wengine 230 walikuwa katika kambi moja ya wakimbizi nchini Tanzania.

      Ndugu katika ofisi ya kutafsiri mjini Kigali walipolazimika kukimbilia Goma, walikodi nyumba ili kuendelea na kazi ya kutafsiri. Wakati wa vita akina ndugu walifaulu kuficha kompyuta na jenereta moja na wakazihamisha kutoka Kigali hadi Goma.

      Mjini Goma, hamkuwa na huduma za simu wala za kutuma au kupokea barua. Hata hivyo, kwa msaada wa Mashahidi waliofanya kazi katika uwanja wa ndege, ndugu walituma makala walizotafsiri na pia barua nyingine kwa ndege kila juma kutoka Goma hadi Nairobi. Nayo ofisi ya tawi ya Kenya iliwatumia barua kupitia njia hiyohiyo.

      Emmanuel Ngirente na watafsiri wengine wawili waliendea kufanya yote waliyoweza ijapokuwa hali zilikuwa ngumu. Hawakutafsiri makala zote za Mnara wa Mlinzi kwa sababu ya vita, lakini makala hizo zilitafsiriwa baadaye na kuchapishwa katika broshua za pekee ambazo ndugu walijifunza katika Funzo la Kitabu la Kutaniko.

      MAISHA KATIKA KAMBI ZA WAKIMBIZI

      Huku watu wengi wakikimbia kutoka Kigali, Francine, ambaye alikuwa amekimbia na kwenda Goma baada ya mume wake Ananie kuuawa, alihamishwa na kupelekwa katika kambi moja ya Mashahidi. Anasema hivi kuhusu maisha katika kambi: “Kila siku, akina ndugu na dada fulani walipewa mgawo wa kutayarisha chakula. Tulitayarisha uji wa mtama au mahindi kwa ajili ya kiamsha kinywa. Pia, tulipika chakula cha mchana. Baada ya kumaliza kazi, tulienda kuhubiri. Tuliwahubiria hasa watu wa familia zetu ambao si Mashahidi na pia watu walioishi nje ya kambi. Hata hivyo, baada ya muda, wapiganaji wa Interahamwe ambao walikuwa katika kambi nyingine, walikasirika kuona kwamba Mashahidi walikuwa katika kambi tofauti na wakimbizi wengine, na hilo likafanya hali ziwe hatari sana.”

      Kufikia Novemba 1994, ilidhihirika wazi kwamba ni salama kwa ndugu kurudi Rwanda. Kwa kweli, ingefaa sana kurudi kwa sababu ya ukosefu wa usalama katika kambi za watu wasio Mashahidi zilizokuwa Kongo. Lakini ingekuwa vigumu kurudi. Interahamwe walinuia kujipanga tena na kuivamia Rwanda, na hivyo, mtu yeyote aliyerudi Rwanda kutoka Kongo alionwa kuwa msaliti.

      Ndugu waliijulisha serikali ya Rwanda kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuunga mkono vita wala kushiriki katika mauaji ya Watutsi, na walitaka kurudishwa Rwanda. Serikali iliwashauri wazungumze na Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi (UNHCR), kwa kuwa ilikuwa na magari yanayoweza kutumiwa kuwarudisha nyumbani. Hata hivyo, kwa sababu Interahamwe wangewazuia kurudi Rwanda, ilibidi ndugu watumie maarifa.

      Ndugu walitangaza kwamba kutakuwa na kusanyiko la pekee mjini Goma, na wakatayarisha mabango ya kusanyiko. Kisha wakawajulisha Mashahidi kisiri kuhusu mipango ya kurudishwa Rwanda. Ili kuepuka kutokeza shaka, ndugu waliagizwa kuacha vitu vyao vyote na kubeba tu Biblia zao na vitabu vya nyimbo kana kwamba wanaenda kusanyikoni.

      Francine anakumbuka kwamba walitembea kwa saa kadhaa kisha wakapata malori yaliyowabeba hadi mpakani. Walipovuka mpaka na kuingia Rwanda, tume ya UNHCR iliwasafirisha mpaka Kigali na kisha kwenye maeneo ya nyumbani kwao. Hivyo, ndugu wengi, familia zao, na watu wenye kupendezwa walirudi Rwanda mnamo Desemba 1994. Gazeti moja la Ubelgiji, Le Soir, la Desemba 3, 1994, liliripoti: “Wakimbizi 1,500 wa Rwanda waliamua kuondoka Zaire [Kongo] kwa sababu walihofia usalama wao. Hao ni Mashahidi wa Yehova ambao walikuwa na kambi yao wenyewe karibu na kambi ya Katale. Mashahidi wa Yehova walinyanyaswa sana na serikali iliyopita kwa sababu walikataa kubeba silaha na kushiriki katika mikutano ya kisiasa.”

      Baada ya kurudi Rwanda, Francine alifanikiwa kuhudhuria kusanyiko la wilaya mjini Nairobi. Akiwa amefarijiwa baada ya kifo cha mume wake na kuimarishwa na ushirika wa akina ndugu na dada, Francine alirudi kwenye ofisi ya kutafsiri ambayo ilikuwa imefunguliwa tena huko Kigali. Baadaye, aliolewa na Emmanuel Ngirente, na wanaendelea kutumika katika ofisi ya tawi.

      Francine alikabilije hisia zake wakati wa vita? Asema: “Tulikuwa na jambo moja tu akilini wakati huo— lazima tuvumilie hadi mwisho. Tuliamua kutofikiria sana mambo mabaya yaliyokuwa yanaendelea. Nilifarijiwa na andiko la Habakuki 3:17-19, linaloongea kuhusu kupata shangwe wakati wa hali ngumu. Ndugu na dada walinitia moyo sana. Hata wengine waliniandikia barua. Hilo lilinisaidia kuwa na mtazamo unaofaa na wa kiroho. Nilikumbuka jinsi Shetani alivyo mjanja. Tukikazia fikira aina moja ya matatizo, huenda atunase kupitia aina nyingine. Tusipokaa macho, tunaweza kuwa dhaifu katika njia moja au nyingine.”

  • Rwanda
    2012 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • Mashahidi wa Yehova 400 hivi waliuawa, kutia ndani Wahutu ambao waliuawa kwa sababu ya kuwalinda ndugu na dada zao Watutsi. Hakuna Shahidi aliyeuawa na mwamini mwenzake.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki