-
Je, Kitabu Hiki Chaafikiana Na Sayansi?Kitabu kwa Ajili ya Watu Wote
-
-
Dunia Ina Umbo Jipi?
Swali hilo limevutia wanadamu sana kwa maelfu ya miaka. Maoni ya kawaida katika nyakati za kale yalikuwa kwamba dunia ilikuwa tambarare. Kwa kielelezo, Wababiloni waliamini kwamba ulimwengu wote mzima ulikuwa sanduku au chumba ambacho dunia ilikuwa sakafu yacho. Makuhani wa Kivedi wa India waliwazia kwamba dunia ilikuwa tambarare na kwamba upande mmoja tu wayo ulikuwa umekaliwa na watu. Kabila la kikale katika Asia liliiona dunia kuwa sinia kubwa ya kubebea vikombe vya chai.
Mapema sana kuanzia karne ya sita K.W.K., mwanafalsafa Mgiriki Pythagoras alitoa nadharia kwamba kwa kuwa mwezi na jua ni tufe, lazima dunia pia iwe tufe. Aristotle (karne ya nne K.W.K.) aliafiki baadaye, akifafanua kwamba hali ya dunia kuwa tufe inathibitishwa na kupatwa mbalimbali kwa mwezi. Kivuli cha dunia kwenye mwezi ni mviringo.
Hata hivyo, dhana ya dunia tambarare (ikiwa imekaliwa na watu kwenye sehemu yayo ya juu tu) haikutoweka kabisa. Watu fulani hawakuweza kukubali lile dokezo la kupatana na akili la dunia iliyo duara—dhana ya antipodi.a Lactantius, mtetea-imani Mkristo wa karne ya nne W.K., alidhihaki hilo wazo lenyewe. Alisababu hivi: “Je, kuna mtu aliye mpumbavu sana aweze kuamini kwamba kuna watu ambao nyayo zao ziko juu kuliko vichwa vyao? . . . kwamba mimea na miti hukua kuelekea chini? kwamba mvua, na theluji, na mvua-barafu huanguka kuelekea juu?”2
Dhana ya antipodi ilitokeza hali ya kutatanisha kwa wanatheolojia wachache. Nadharia fulani zilishikilia kwamba ikiwa kulikuwa na watu wanaoishi katika upande ule mwingine wa dunia, wasingeweza kuwasiliana hata kidogo na wanadamu wajulikanao ama kwa sababu bahari ilikuwa pana mno isiweze kusafiriwa ama kwa sababu kanda yenye joto kali isiyoweza kupitika iliizunguka ikweta. Basi watu walioishi kwenye ule upande mwingine wa dunia wangeweza kuwa walitoka wapi? Kwa kutatanishwa, wanatheolojia fulani walipendelea kuamini kwamba kusingeweza kuwa na watu wanaoishi kwenye ule upande mwingine wa dunia, au hata, kama alivyojadili Lactantius, kwamba dunia hata isingeweza kuwa tufe!
Bado, dhana ya kwamba dunia ni tufe ilienea, na hatimaye ilikubaliwa na watu wengi sana. Hata hivyo, ni baada tu ya enzi ya anga kuanza katika karne ya 20, ndipo imewezekana kwa wanadamu kusafiri mbali angani vya kutosha kuthibitisha kwa kujionea moja kwa moja kwamba dunia ni tufe.b
Na msimamo wa Biblia ulikuwa nini katika suala hili? Katika karne ya nane K.W.K., wakati maoni yaliyoenea yalipokuwa kwamba dunia ilikuwa tambarare, karne kadhaa kabla ya wanafalsafa wa Kigiriki kutoa nadharia kwamba dunia yamkini ilikuwa tufe, na maelfu ya miaka kabla ya wanadamu kuiona dunia ikiwa tufe kutoka angani, nabii Mwebrania Isaya alitaarifu hivi kwa usahili wa ajabu: “Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia.” (Isaya 40:22, italiki ni zetu.) Neno la Kiebrania chugh, linalotafsiriwa hapa “duara,” laweza pia kufasiriwa kuwa “tufe.”3 Tafsiri nyingine za Biblia husema, “tufe la dunia” (Douay Version) na “dunia mviringo.”—Moffatt.c
Mwandikaji wa Biblia Isaya aliepuka ngano za kawaida juu ya dunia. Badala ya hivyo, aliandika taarifa ambayo haikutishwa na maendeleo ya uvumbuzi wa kisayansi.
-
-
Je, Kitabu Hiki Chaafikiana Na Sayansi?Kitabu kwa Ajili ya Watu Wote
-
-
Ni Nini Kinachoitegemeza Dunia?
Katika nyakati za kale, wanadamu walitatanishwa na maswali mengine juu ya ulimwengu: Dunia inakalia nini? Jua, mwezi, na nyota hutegemezwa na nini? Hawakuwa na ujuzi wowote juu ya sheria ya nguvu za uvutano za ulimwengu wote mzima, zilizofanyizwa na Isaac Newton na kuchapishwa mwaka wa 1687. Wazo la kwamba kwa kweli, magimba ya kimbingu huning’inia katika anga tupu pasipo kitu halikujulikana kwao. Hivyo, mafafanuzi yao mara nyingi yalidokeza kwamba vitu au dutu zenye kugusika ziliitegemeza dunia na magimba mengine ya kimbingu huko juu.
Kwa kielelezo, nadharia moja ya kale, labda yenye kuanzishwa na watu walioishi kwenye kisiwa fulani, ilikuwa kwamba dunia ilizungukwa na maji na kwamba ilielea katika maji hayo. Wahindu waliwazia kwamba dunia ilikuwa na misingi kadhaa, mmoja juu ya mwingine. Ilikalia ndovu wanne, hao ndovu walisimama juu ya kobe mkubwa mno, huyo kobe alisimama juu ya nyoka mkubwa sana, na nyoka huyo aliyejikunja alielea juu ya maji ya ulimwengu wote mzima. Empedocles, mwanafalsafa Mgiriki wa karne ya tano K.W.K., aliamini kwamba dunia ilikalia kisulisuli na kwamba kisulisuli hicho kilikuwa ndicho kisababishi cha mwendo wa magimba ya kimbingu.
Miongoni mwa maoni yenye uvutano zaidi yalikuwa yale ya Aristotle. Ingawa alitoa nadharia kwamba dunia ni tufe, alikana kwamba ingeweza kwa vyovyote kuning’inia katika anga tupu. Katika maandishi yake On the Heavens, alipokuwa akikanusha dhana ya kwamba dunia hukalia maji, alisema hivi: “Si asili ya maji, sawa na vile si asili ya dunia, kuning’inia hewani: lazima yakalie kitu.”4 Kwa hiyo, dunia ‘hukalia kitu gani’? Aristotle alifundisha kwamba jua, mwezi, na nyota zilikuwa zimeshikamana na sehemu ya juu ya tufe zito, jangavu. Tufe moja lilikuwa ndani ya jingine, dunia ikiwa—bila kujongea —katikati. Matufe hayo yalipozunguka moja likiwa ndani ya jingine, vitu vilivyokuwa juu yayo—jua, mwezi, na sayari —vilijongea kuivuka anga.
Ufafanuzi wa Aristotle ulionekana kuwa wenye kupatana na akili. Ikiwa magimba ya kimbingu hayakuwa yameshikamana imara na kitu fulani, yangeweza kukaa juu kwa njia gani nyingine? Maoni ya Aristotle aliyestahiwa yalikubaliwa kuwa jambo la hakika kwa miaka ipatayo 2,000. Kulingana na The New Encyclopædia Britannica, katika karne ya 16 na ya 17 mafundisho yake “yalifikia kiwango cha kuwa fundisho la kidini” machoni pa kanisa.5
Darubini-upeo ilipobuniwa, waastronomia walianza kutilia shaka nadharia ya Aristotle. Bado, jibu liliwaepuka mpaka Sir Isaac Newton alipofafanua kwamba sayari zinaning’inia katika anga tupu, zikiwa zimeshikiliwa katika mizingo yao na kani isiyoonekana—nguvu za uvutano. Ilionekana kutosadikika, na baadhi ya wafanyakazi wa Newton waliona ni vigumu kuamini kwamba anga lingeweza kuwa tupu, bila dutu yoyote kwa ujumla.d6
Biblia ina mambo gani ya kusema juu ya swali hilo? Miaka karibu 3,500 iliyopita, Biblia ilitaarifu kwa uwazi usio wa kawaida kwamba dunia inaning’inia “pasipo na kitu.” (Ayubu 26:7, BHN) Katika Kiebrania cha awali, neno litumiwalo hapa kwa “pasipo na kitu” (beli-mahʹ) humaanisha kihalisi “bila kitu.”7 Union Version ya Kiswahili hutumia maneno, “nafasi isiyo na kitu.”
Watu walio wengi katika siku hizo hawakuifikiria hata kidogo dunia kuwa sayari inayoning’inia katika “nafasi isiyo na kitu.” Hata hivyo, kimbele sana kuliko wakati wake, mwandikaji wa Biblia alirekodi taarifa iliyo thabiti kisayansi.
-