-
Kufumbua Fumbo la Ule Mti MkubwaSikiliza Unabii wa Danieli!
-
-
UTIMIZO WA KWANZA WA NDOTO
15. (a) Nebukadreza aliendelea kuonyesha mtazamo gani? (b) Maandishi yafunua nini juu ya utendaji mbalimbali wa Nebukadreza?
15 Nebukadreza aliendelea kuwa na kiburi. Akitembea huku na huku kwenye paa ya jumba la kifalme miezi 12 baada ya ndoto yake, alijivuna hivi: “Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?” (Danieli 4:28-30) Nimrodi alikuwa ameujenga Babiloni (Babeli), lakini Nebukadreza aliupa fahari. (Mwanzo 10:8-10) Katika mojawapo ya maandishi yake ya kikabari, ajisifu hivi: “Nebukadreza, Mfalme wa Babiloni, aliyejenga upya Esagila na Ezida, mwana wa Nabopolasa ndimi. . . . Ngome ya Esagila na ya Babiloni niliziimarisha na kuliweka jina la utawala wangu milele.” (Kichapo Archaeology and the Bible, kilichoandikwa na George A. Barton, 1949, ukurasa wa 478-479) Maandishi mengine hurejezea mahekalu yapatayo 20 ambayo alirekebisha au kujenga upya. “Chini ya utawala wa Nebukadreza,” chasema kichapo The World Book Encyclopedia, “Babiloni lilipata kuwa mojawapo ya majiji yenye fahari sana ya ulimwengu wa kale. Katika rekodi zake mwenyewe, alitaja utendaji wake wa kijeshi mara chache sana, lakini aliandika juu ya ujenzi wake mwingi na ibada yake kwa miungu ya Babilonia. Huenda Nebukadreza ndiye aliyejenga Bustani Zenye Kuning’inia za Babiloni, mojawapo ya Maajabu Saba ya Ulimwengu wa Kale.”
16. Nebukadreza alikuwa amekaribia kudhiliwaje?
16 Ingawa alijivuna, Nebukadreza mwenye kiburi alikuwa akikaribia kudhiliwa. Simulizi lililopuliziwa lasema hivi: “Neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako. Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.”—Danieli 4:31, 32.
17. Ni nini kilichompata Nebukadreza mwenye kiburi, na mara moja akajikuta katika hali gani?
17 Papo hapo Nebukadreza akarukwa na akili. Akafukuzwa mbali na wanadamu, na kula majani “kama ng’ombe.” Akiwa miongoni mwa wanyama wa kondeni, haielekei kwamba aliketi tu kwenye majani katika aina fulani ya paradiso, akifurahia kupunga hewa siku baada ya siku. Katika Iraki ya leo, yalipo magofu ya Babiloni, kiwango cha joto hupanda hadi digrii 50 Selsiasi katika miezi ya kiangazi na kushuka chini ya kiwango cha kuganda wakati wa majira ya baridi kali. Kwa kuwa hazikutunzwa na kwa sababu ya hali ya hewa, nywele ndefu za matimutimu za Nebukadreza zilifanana na manyoya ya tai nazo kucha zake ndefu za mikono na miguu zikawa kama kucha za ndege. (Danieli 4:33) Mtawala huyo wa ulimwengu mwenye kiburi alikuwa amedhiliwa kama nini!
18. Wakati wa zile nyakati saba, ni nini kilichotokea kwa kiti cha ufalme cha Babiloni?
18 Katika ndoto ya Nebukadreza, ule mti mkubwa uliangushwa na kisiki cha shina lake kikafungwa pingu kizuiwe kukua kwa nyakati saba. Vivyo hivyo, Nebukadreza “aliuzuliwa katika kiti chake cha enzi” Yehova alipompiga kwa kichaa. (Danieli 5:20) Hilo hasa lilibadili moyo wa mfalme uliokuwa wa binadamu ukawa wa ng’ombe. Hata hivyo, Mungu alimhifadhia Nebukadreza kiti cha ufalme hadi nyakati saba zilipoisha. Ingawa huenda Evil-merodaki alitawala kwa muda, Danieli alikuwa ‘mkubwa juu ya uliwali wote wa Babeli, na liwali mkuu juu ya wote wenye hekima wa Babeli.’ Wale waandamani wake watatu waliendelea kushiriki katika kusimamia mambo ya wilaya hiyo. (Danieli 1:11-19; 2:48, 49; 3:30) Wahamishwa hao wanne walingojea kurudishwa kwa Nebukadreza kwenye kiti cha ufalme akiwa mfalme timamu ambaye amejifunza kwamba “Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.”
KURUDISHWA KWA NEBUKADREZA
19. Baada ya Yehova kumrudishia Nebukadreza fahamu, mfalme huyo wa Babiloni alitambua nini?
19 Yehova alirudisha utimamu wa Nebukadreza mwishoni mwa zile nyakati saba. Kisha akimkiri Mungu Aliye Juu, mfalme huyo alisema hivi: “Hata mwisho wa siku hizo, mimi, Nebukadreza, nikainua macho yangu kuelekea mbingu, fahamu zangu zikanirudia; nikamhimidi Yeye aliye juu, nikamsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme wake hudumu toka kizazi hata kizazi; na watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu; naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, Unafanya nini wewe?” (Danieli 4:34, 35) Naam, Nebukadreza alikuja kufahamu kwamba Aliye Juu ndiye kwa kweli Mtawala Mwenye Enzi Kuu katika ufalme wa wanadamu.
20, 21. (a) Kuondolewa kwa pingu ya metali iliyofunga kisiki cha shina kulilinganaje na yaliyompata Nebukadreza? (b) Nebukadreza alikiri nini, na je, kufanya hivyo kulimfanya awe mwabudu wa Yehova?
20 Nebukadreza aliporudi kwenye kiti chake cha ufalme, ilikuwa kana kwamba ile pingu ya metali iliyofunga kisiki cha shina la mti ulioonekana kwenye ndoto ilikuwa imeondolewa. Kuhusu kurudishwa kwake, alisema hivi: “Basi wakati uo huo fahamu zangu zikanirudia, na kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu, enzi yangu na fahari yangu zikanirudia; na mawaziri wangu, na madiwani wangu, wakaja kunitafuta; nami nikathibitika katika ufalme wangu, nikaongezewa enzi kupita kiasi.” (Danieli 4:36) Ikiwa maofisa wowote walikuwa wamemdharau mfalme aliyerukwa na akili, sasa walikuwa ‘wakimtafuta’ ili kumsaidia.
21 Mungu Aliye Juu alikuwa amefanya “ishara na maajabu” kama nini! Si ajabu kwamba mfalme wa Babiloni aliyerudishwa alisema hivi: “Basi mimi, Nebukadreza, namhimidi Mfalme wa mbinguni, namtukuza na kumheshimu; maana matendo yake yote ni kweli, na njia zake ni za adili; na wale waendao kwa kutakabari, yeye aweza kuwadhili.” (Danieli 4:2, 37) Hata hivyo, kukiri huko hakukumfanya Nebukadreza awe mwabudu wa Yehova, asiye Myahudi.
JE, KUNA UTHIBITISHO WA KILIMWENGU?
22. Watu fulani wamesema kichaa cha Nebukadreza kilikuwa ugonjwa gani, lakini twapaswa kutambua nini kuhusu kisababishi cha kichaa hicho?
22 Watu fulani wamesema kwamba kichaa cha Nebukadreza kilikuwa ugonjwa uitwao lycanthropy. Kamusi moja ya kitiba yasema hivi: “LYCANTHROPY . . . latokana na [lyʹkos], lupus, mbwa-mwitu; [anʹthro·pos], homo, mwanadamu. Jina hilo lilipewa ugonjwa wa watu ambao wanaamini kwamba wamegeuka na kuwa mnyama, na ambao huiga sauti na milio, umbo au tabia za mnyama huyo. Kwa kawaida watu hao hujiwazia wamegeuka kuwa mbwa-mwitu, mbwa au paka; nyakati nyingine kuwa fahali [ng’ombe], kama katika kisa cha Nebukadreza.” (Dictionnaire des sciences médicales, par une société de médicins et de chirurgiens, Paris, 1818, Buku la 29, ukurasa wa 246) Dalili za ugonjwa huo zafanana na zile za kichaa cha Nebukadreza. Hata hivyo, kwa kuwa ugonjwa wake wa akili ulitokana na amri ya Mungu, hauwezi kutambulishwa waziwazi kuwa ugonjwa fulani ujulikanao.
23. Ni ushuhuda gani wa kilimwengu uliopo unaothibitisha kichaa cha Nebukadreza?
23 Msomi John E. Goldingay ataja mambo fulani yanayopatana na kichaa na kurudishwa kwa Nebukadreza. Kwa mfano, ataarifu hivi: “Yaonekana kipande fulani cha maandishi ya kikabari charejezea aina fulani ya ugonjwa wa akili wa Nebukadreza, na huenda kupuuza kwake Babiloni na kuiacha.” Goldingay ataja hati iitwayo “Yobu wa Babiloni” na kusema kwamba hiyo “yatoa ushuhuda juu ya kutiwa adabu na Mungu, ugonjwa, kudhiliwa, kutafuta fasiri ya ndoto yenye kuogofya, kutupwa kama mti, kuwekwa nje, kula majani, kupoteza uelewevu, kuwa kama fahali, kunyeshewa na Marduki, kucha kuharibika, nywele kukua, na kufungwa pingu, kisha kurudishwa ambako yuamsifia mungu.”
-
-
Kufumbua Fumbo la Ule Mti MkubwaSikiliza Unabii wa Danieli!
-
-
[Picha katika ukurasa wa 91]
-