Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Linda Ngozi Yako!
    Amkeni!—2005 | Juni 8
    • Kansa ya Ngozi Ni Tatizo Kubwa Leo

      Kichapo The Merck Manual kinasema kwamba hiyo ndiyo kansa inayopata watu wengi sana ulimwenguni. Nchini Marekani, mtu 1 kati ya kila watu 6 hadi 7 hupatwa na aina fulani ya kansa ya ngozi. Lakini idadi ya watu wanaopatwa na kansa hiyo inaongezeka. Katika kitabu The Skin Cancer Answer, Dakt. I. William Lane anasema: “Sasa inakadiriwa kwamba asilimia 50 ya watu ambao hufikisha umri wa miaka 65 watapatwa na aina fulani ya kansa ya ngozi.” Kulingana na Taasisi ya Magonjwa ya Ngozi ya Marekani, kansa ya ngozi inayoathiri chembe za ndani za ngozi husababisha vifo 7,500 hivi kila mwaka nchini humo na idadi hiyo inazidi kuongezeka. Si rahisi kwa watu wenye ngozi nyeusi kupatwa na kansa ya ngozi, lakini wao pia wamo hatarini.

      Kwa nini kansa ya ngozi imeenea hivyo? Ingawa huenda ikasababishwa na mambo mengi kama vile mwinuko kutoka usawa wa bahari, latitudo, kiasi cha mawingu, na hali ya tabaka la ozoni, huenda kisababishi kikuu kikawa kupigwa na jua kwa muda mrefu. Mitindo ya maisha imebadilika. Imekuwa rahisi kwa watu wengi wanaofanya kazi ofisini kwenda likizo kwenye fuo na kufurahia tafrija kama vile kupanda mlima na kuteleza kwenye barafu. Mitindo ya mavazi imebadilika. Ingawa zamani wanaume na wanawake walivaa nguo ndefu za kuogelea, siku hizi nguo za kuogelea hazifuniki sehemu kubwa ya mwili. Kwa sababu hiyo kansa ya ngozi imeongezeka. Huenda watu walioishi jangwani kama vile Wabedui walijua jambo hilo na ndio sababu walivalia kanzu ndefu na vilemba.

      Kansa ya Ngozi Ni Hatari!

      Aina tatu za kansa ya ngozi ambazo huwapata sana watu ni kansa inayoathiri chembe za katikati za ngozi, kansa ya chembe za juu za ngozi, na kansa ya chembe za ndani za ngozi ambayo ni hatari sana. Kansa ya chembe za katikati na za juu ya ngozi huanza katika tabaka la juu la ngozi ambalo lina unene wa milimita moja tu kwa wastani. Yaonekana kansa hizo ambazo si hatari sana husababishwa na kupigwa na jua kwa muda mrefu sana, kama vile watu wanaofanya kazi chini ya jua, nazo hutokea hasa kwenye sehemu za mwili zinazopigwa na jua kama vile uso na mikono.a Aina hizo za kansa huelekea kuanza kama uvimbe mdogo kwenye ngozi ambao hukua, huvuja damu mara nyingi na hauponi kabisa. Unaweza kuanza kuenea na kuathiri tishu zinazouzunguka. Asilimia 75 hivi ya kansa za ngozi huwa kansa zinazoathiri chembe za katikati za ngozi. Ingawa kansa inayoathiri chembe za juu za ngozi si ya kawaida, huenda ikaenea na kuathiri sehemu nyingine za mwili. Ni muhimu kansa za aina hiyo zingunduliwe mapema kwani ingawa zinaweza kutibiwa, zikiachwa kwa muda mrefu bila kutibiwa zinaweza kusababisha kifo.

      Kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi ambayo hupata asilimia 5 tu ya watu wanaougua kansa ya ngozi, pia huanza katika sehemu ya juu ya ngozi. Inaonekana kwamba mojawapo ya visababishi vikuu vya aina hii ya kansa ni kujianika juani kwa vipindi virefu sana kama vile watu wanaofanya kazi za ofisini hufanya wanapoenda likizo. Asilimia 50 hivi ya aina hiyo ya kansa hutokana na mabaka meusi hasa kwenye sehemu ya juu ya mgongo na sehemu ya chini ya miguu.

      Aina hii ya kansa ndiyo hatari zaidi kwa kuwa isipotibiwa mapema, inaweza kuvamia tabaka la ndani la ngozi, ambako kuna mishipa ya damu na limfu. Kuanzia hapo, inaweza kuenea haraka. Mtalaamu wa matibabu ya uvimbe Dakt. Larry Nathanson anasema: “Jambo la kushangaza ni kwamba kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi inaweza kutibiwa kwa urahisi inapogunduliwa mapema. Kwa upande mwingine, inapoenea haiwezi kutibiwa kwa dawa au mnururisho.” Kwa kweli, ni asilimia 2 au 3 tu ya wagonjwa wenye kansa hiyo iliyoenea ambao huweza kuishi kwa miaka mitano. (Ona dalili za mapema za kansa hiyo kwenye sanduku katika ukurasa wa 7.)

      Ni nani wanaoweza kupata kansa ya ngozi? Mbali na watu ambao wamewahi kupigwa na jua kwa muda mrefu sana, au wale wanaojianika juani kwa vipindi virefu sana, wale walio na ngozi nyeupe, nywele na macho ya rangi hafifu, wenye mabaka na madoadoa, na wale ambao mtu fulani katika familia yao amekuwa na ugonjwa huo, wanaweza kuupata. Si rahisi kwa watu wenye ngozi nyeusi kupatwa na kansa ya ngozi. Je, hii inamaanisha kwamba kadiri ngozi yako inavyounguzwa na jua na kuwa nyeusi ndivyo inavyokuwa vigumu kupatwa na kansa ya ngozi? Sivyo, kwa sababu ingawa ngozi hujigeuza rangi na kuwa nyeusi ili kujikinga na mnururisho wa miale ya urujuanimno, inapofanya hivyo hiyo huathirika, na inapoathirika mara nyingi kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kupata kansa ya ngozi.

  • Linda Ngozi Yako!
    Amkeni!—2005 | Juni 8
    • Linda Ngozi Yako!

      “Watu hawatambui hatari kubwa inayosababishwa na jua . . . na jinsi linavyoweza kudhuru chembe za urithi za ngozi. Madhara ya muda mrefu yanaweza kutokeza kansa ya ngozi baadaye.” —Dakt. Mark Birch-Machin, mtaalamu wa kansa ya ngozi.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki