-
Nchi Ambazo Zilikuwa Sehemu ya Yugoslavia2009 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Baraza Linaloongoza lilipotoa idhini ya kujenga ofisi mpya ya tawi nchini Slovenia, akina ndugu walianza kutafuta uwanja unaofaa. Baada ya kuchunguza viwanja karibu 40, ndugu walichagua uwanja ulio karibu na mji wa Kamnik, kilomita 20 kutoka kwenye mji mkuu, chini ya safu yenye kuvutia ya milima. Muda si muda, walitimiza matakwa yote ya ujenzi, wakapata vibali vya ujenzi, uwanja ukanunuliwa, wakafanya makubaliano pamoja na kampuni ya ujenzi, kisha watumishi wa kimataifa wakaitwa ili washiriki katika ujenzi huo. Walikuwa tayari kabisa kuanza ujenzi.
Hata hivyo, habari kuhusu mradi huo zilipoenea, majirani waliandamana haraka ili kupinga ujenzi huo. Siku ya kuanza ujenzi ilipofika, watu waliandamana na kufunga njia ya kuingia kwenye uwanja huo. Kisha wakabeba mabango ya kupinga mradi huo. Siku sita baadaye, karibu saa sita mchana, polisi 30 hivi walikuja kuwalinda wafanyakazi wa baraza la jiji waliotumwa kuondoa vizuizi vya waandamanaji; waandamanaji hao waliwatukana polisi. Kazi ya ujenzi ilikuwa imeahirishwa, basi hakuna ndugu wala mfanyakazi yeyote wa kampuni ya ujenzi aliyefika mahali pa ujenzi siku hiyo. Upinzani ulianza kupungua baada ya ujenzi kuahirishwa, na ndugu zetu walijaribu kusuluhisha tatizo hilo kwa amani.
Ua wa uwanja huo ulikuwa umebomolewa mara tatu na wapinzani, lakini mwishowe kazi ya ujenzi ilianza tena baada ya mwezi na kuendelea bila kuvurugwa. Kwa kweli, hatua hiyo ya kuwashambulia watu wa Yehova mwishowe ilileta baraka kwa sababu ilitangazwa sana na vyombo vya habari. Ripoti zaidi ya 150 kuhusu ujenzi huo zilitangazwa kwenye televisheni na redio na katika magazeti. Ujenzi ulikamilika baada ya miezi 11, na mnamo Agosti 2005, familia ya Betheli ilihamia majengo hayo mapya.
Tangu wakati huo, uhusiano kati ya ndugu na majirani wao umebadilika kabisa. Majirani wengi wametembelea ofisi ya tawi. Mtu mmoja aliyekuwa mpinzani baadaye alipendezwa sana na ujenzi huo. Alituuliza sisi ni nani na ni kazi gani itakayofanywa katika ofisi hiyo. Alipotembelea ofisi ya tawi, alivutiwa sana kuona akikaribishwa kwa urafiki na alivutiwa pia na usafi wa jengo hilo. Aliwaambia hivi akina ndugu: “Majirani wananiuliza ikiwa sasa nimejiunga nanyi. Nami ninawajibu hivi: ‘Hata ingawa niliwapinga vikali Mashahidi wa Yehova mwanzoni, sasa ninawaunga mkono kwa sababu ni watu wazuri.’”
Agosti 12, 2006 ilikuwa siku yenye furaha kwa sababu Theodore Jaracz wa Baraza Linaloongoza alitoa hotuba ya wakfu iliyosikilizwa na watu 144 kutoka katika nchi 20 hivi. Katika mkutano wa pekee huko Ljubljana, aliwahutubia wasikilizaji 3,097 kutoka sehemu mbalimbali za Slovenia, na pia kutoka Kroatia na Bosnia na Herzegovina.
-
-
Nchi Ambazo Zilikuwa Sehemu ya Yugoslavia2009 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Picha katika ukurasa wa 253]
Ofisi ya tawi huko Kamnik, Slovenia, 2006
-