-
Linda Ngozi Yako!Amkeni!—2005 | Juni 8
-
-
Jifunze Kuhusu Jinsi ya Kujikinga na Madhara ya Jua
Ni muhimu kujifunza tangu utotoni kuhusu kujikinga na madhara ya kupigwa na jua. Kulingana na Taasisi ya Kansa ya Ngozi, ‘watu wengi hupigwa na asilimia 80 hivi ya kiasi cha jua wanachohitaji maishani kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Kuunguzwa sana na jua na kupatwa na malengelenge mara moja tu utotoni, huzidisha maradufu uwezekano wa kupatwa na kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi baadaye maishani.’ Hii ni kwa sababu kansa ya ngozi inaweza kuchukua miaka 20 au zaidi kukua. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 8 ili kupata madokezo ya kujikinga na madhara ya kupigwa na jua.)
Australia ina kiwango cha juu cha visa vya ugonjwa wa kansa ya ngozi, hasa ile inayoathiri chembe za ndani za ngozi.b Hii ni kwa sababu wakazi wengi wa nchi hiyo ambao walihama kutoka Ulaya Kaskazini wana ngozi yenye rangi hafifu, na wengi wao huishi pwani yenye fuo zenye jua. Uchunguzi waliofanyiwa wahamiaji hao unadokeza kwamba wale wanaohamia Australia wakiwa wachanga hukabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kansa inayoathiri chembe za ngozi za ndani, jambo linaloonyesha umuhimu wa kujifunza tangu utotoni kuhusu madhara ya kupigwa na jua. Serikali ya Australia imeanzisha kampeni kali ya kuwafunza watu kuhusu hatari za jua kwa kuwaambia wavae t-shati, kofia, na kujipaka losheni ya kujikinga na jua. Mabadiliko hayo madogo katika mtindo wa maisha yamekuwa na matokeo makubwa katika kuzuia kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi kati ya vijana nchini humo.
Losheni ya kujikinga na jua inayofaa ni ile inayoweza kukinga miale ya mnururisho ya UVA na UVB. Ni muhimu kujipaka losheni hiyo hata siku zenye mawingu mengi kwa kuwa asilimia 85 ya mnururisho wa miale ya urujuanimno inaweza kupenya mawingu. Pia miale hiyo inaweza kupenya majini. Wataalamu fulani wanapendekeza losheni ya kujikinga na jua yenye kinga (SPF) ya angalau namba 15. Ili kujua losheni hiyo inaweza kukukinga kwa kiasi gani, hesabu dakika ambazo kwa kawaida wewe huchukua kuunguzwa na jua kisha uzizidishe kwa 15. Mtu anapaswa kujipaka losheni hiyo angalau baada ya kila saa mbili, lakini kufanya hivyo hakuzidishi maradufu muda ambao utakuwa umekingwa na jua.
Isitoshe, kitabu The Skin Cancer Answer kinaonya kwamba hupaswi kufikiri kwamba uko salama eti kwa sababu tu unatumia losheni ya kujikinga na jua. Hakuna losheni ya kujikinga na jua inayoweza kuzuia kikamili kuunguzwa na jua, wala kuzuia kansa ya ngozi. Kwa kweli, kutumia losheni kama hizo kunaweza kuongeza uwezekano wa kupatwa na kansa ya ngozi kwa njia isiyo ya moja kwa moja ikiwa kuzitumia kutafanya ukae muda mrefu zaidi kwenye jua. Kitabu hicho kinasema: “Njia pekee ya kujikinga ni kufuata madokezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na madhara ya kupigwa na jua. Kuvaa mavazi ya kujikinga na kukaa ndani ya nyumba wakati jua linapokuwa kali, huonwa kuwa mbinu ‘zenye matokeo’ za kujikinga na kansa ya ngozi.”
Namna gani kujigeuza rangi kwa kutumia taa na vitanda vinavyotokeza mnururisho wa jua ukiwa ndani ya nyumba? Inakadiriwa kwamba kutumia dakika 20 tu katika chumba kama hicho, ni sawa na kujianika kwenye jua kwa saa nne hivi. Ilidhaniwa kwamba kujaribu kugeuza rangi ya ngozi ndani ya nyumba ni salama kwa sababu mnururisho wa miale ya UVA uliotumiwa hasa, ulionekana kuwa hauunguzi ngozi. Lakini kitabu The Skin Cancer Answer kinasema: “Sasa inajulikana kwamba miale ya UVA hupenya ndani zaidi katika ngozi kuliko miale ya UVB, inaweza kusababisha kansa ya ngozi, na huenda ikadhoofisha mfumo wa kinga.” Uchunguzi mmoja ulioripotiwa katika toleo la kimataifa la The Miami Herald ulionyesha kwamba wanawake ambao huenda kwenye vyumba vya kugeuza rangi ya ngozi mara moja kwa mwezi au zaidi “waliongeza uwezekano wao wa kupatwa na kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi kwa asilimia 55.”
Hivyo, ni muhimu kujifunza jinsi ya kujikinga na madhara ya kupigwa na jua. Kumbuka kwamba ukiunguzwa na jua leo, huenda ukapatwa na kansa ya ngozi miaka 20 au zaidi baadaye.
-
-
Linda Ngozi Yako!Amkeni!—2005 | Juni 8
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
MADOKEZO YA JINSI YA KULINDA NGOZI YAKO
1. Usikae kwenye jua sana hasa kati ya 4:00 asubuhi na saa 10:00 jioni, wakati kuna mnururisho mwingi wa miale hatari ya urujuanimno.
2. Chunguza ngozi yako kuanzia wayo hadi utosini angalau mara moja kila miezi mitatu.
3. Unapokuwa nje, tumia losheni ya kujikinga na jua yenye kinga (SPF) namba 15 au zaidi. Jipake losheni nyingi dakika 30 kabla ya kujianika juani na baada ya kila saa mbili. (Watoto walio chini ya umri wa miezi sita hawapaswi kupakwa losheni ya kujikinga na jua.)
4. Wafunze watoto wako jinsi ya kujikinga na jua wakiwa wangali wachanga, kwa kuwa madhara ambayo husababisha kansa ya ngozi kwa watu wazima huanza utotoni.
5. Vaa nguo za kujikinga kama vile suruali ndefu, shati zenye mikono mirefu, kofia pana, na miwani inayoweza kuzuia miale ya urujuanimno.
-