Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Watu Wanazidi Kuchukia Kodi?
    Amkeni!—2003 | Desemba 8
    • Je, Watu Wanazidi Kuchukia Kodi?

      “Ninapochuma kwa jasho, mimi hupokonywa.”—Methali ya Babiloni, karibu mwaka wa 2300 K.W.K.

      “Katika ulimwengu huu, hakuna kitu kilicho hakika kama kifo na kodi.”—Mwanasiasa Mmarekani, Benjamin Franklin, mwaka wa 1789.

      REUBEN ni afisa wa mauzo. Kila mwaka karibu thuluthi moja ya mshahara wake ambao ameutolea jasho huishia katika kodi. Analalamika hivi: “Sijui pesa hizo huenda wapi. Kwa kuwa serikali imepunguza matumizi yake, sasa tunapata huduma chache kuliko wakati mwingine wowote.”

      Hata hivyo, tupende tusipende, kodi ni sehemu ya maisha. Mwandishi Charles Adams anasema: “Serikali zimetoza kodi ya mapato kwa njia nyingi tangu jamii ilipostaarabika.” Kodi zimewachukiza watu mara nyingi na nyakati nyingine zimechochea uasi. Waingereza wa kale walipigana na Waroma, wakisema hivi: “Ni afadhali tuuawe kuliko kulemezwa na kodi!” Nchini Ufaransa, watu walichukizwa na kodi ya chumvi na hilo likasababisha Mapinduzi ya Ufaransa, ambapo watoza-kodi waliuawa. Pia, vita vya uhuru vya Marekani dhidi ya Uingereza vilisababishwa kwa kadiri fulani na kodi.

      Haishangazi kwamba watu wanachukia kodi hata leo. Wataalamu wanasema kwamba katika nchi zinazoendelea, mara nyingi sheria za kodi “hazifanyi kazi vizuri” na “zinakandamiza.” Kulingana na mtafiti mmoja, nchi moja maskini ya Afrika ilikuwa na “zaidi ya kodi 300, na ilikuwa vigumu kutoza kodi hizo hata kukiwa na wafanyakazi stadi. Huenda hakuna mfumo bora wa kukusanya kodi na kuhakikisha inatumiwa vizuri ama mfumo huo hautumiwi ipasavyo, . . . na hivyo pesa zinatumiwa vibaya.” Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliripoti kwamba katika nchi moja ya Asia “maafisa wa serikali walitoza . . . kodi nyingi zisizo halali kwa wakulima wa ndizi na hata kwa kuchinja nguruwe ili kuongeza mapato ya serikali au kuingiza pesa mifukoni mwao.”

      Tofauti kati ya matajiri na maskini huwafanya wengi wachukie kodi. Gazeti Africa Recovery la Umoja wa Mataifa linasema: “Mojawapo ya tofauti nyingi za kiuchumi kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ni kwamba nchi zilizoendelea huwapa wakulima msaada wa kifedha hali zile zinazoendelea huwatoza wakulima kodi. . . . Uchunguzi uliofanywa na Benki ya Dunia unadokeza kwamba misaada ya kifedha inayotolewa kwa wakulima wa Marekani pekee hupunguza mapato ambayo Afrika Magharibi hupata kila mwaka kwa kuuza pamba kwa dola [milioni] 250.” Kwa hiyo, huenda wakulima katika nchi zinazoendelea wakaudhika wakati serikali zinapowatoza kodi na kupunguza mapato yao madogo sana. Mkulima mmoja huko Asia anasema: “Kila mara tulipowaona [maafisa wa serikali] hapa tulijua kwamba wanatafuta pesa.”

      Hivi majuzi pia, watu waliudhika nchini Afrika Kusini wakati serikali ilipoanza kuwatoza wakulima kodi ya shamba. Wakulima walitisha kwenda mahakamani. Msemaji wa wakulima hao alisema kwamba kodi hiyo “itawafilisisha wakulima na wafanyakazi wengi zaidi wa mashambani watakosa kazi.” Hata leo, jeuri hutokea nyakati nyingine kwa sababu ya kuchukia kodi. Shirika la BBC linasema: “Wakulima wawili [Waasia] waliuawa mwaka uliopita wakati polisi walipovuruga maandamano katika kijiji kimoja ambako wakulima walipinga kodi za juu.”

      Lakini, si maskini tu wanaochukia kodi. Uchunguzi uliofanywa nchini Afrika Kusini ulionyesha kwamba matajiri wengi wanaolipa kodi “hawataki kulipa kodi zaidi hata kama jambo hilo litasababisha serikali ishindwe kuboresha huduma zinazowafaidi.” Imeripotiwa kwamba mabingwa wa muziki, sinema, michezo, na wanasiasa mashuhuri wamehepa kodi. Kitabu The Decline (and Fall?) of the Income Tax kinasema: “Inasikitisha kwamba hata maafisa wakuu serikalini, marais, hawajawawekea raia mfano mzuri wa kulipa kodi.”

      Labda unahisi kwamba kodi zenu ni za juu mno, zinakandamiza, na kulemea. Basi, unapaswa kuwa na maoni gani juu ya kulipa kodi? Je, zinatimiza kusudi lolote? Ni kwa nini mara nyingi mifumo ya kodi huwa tata sana na huonekana kuwa inakandamiza? Makala zinazofuata zitazungumzia maswali hayo.

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      Katika nchi zinazoendelea maskini wanaweza kulemewa na kodi

      [Hisani]

      Godo-Foto

  • Je, Kodi Hulipwa ili Kuwe na “Maendeleo”?
    Amkeni!—2003 | Desemba 8
    • Je, Kodi Hulipwa ili Kuwe na “Maendeleo”?

      “Sisi hulipa kodi ili kuwe na maendeleo.”—Maandishi kwenye jengo la Huduma za Malipo ya Kodi, Washington, D.C.

      SERIKALI husema kwamba kodi ni muhimu ingawa zinawalemea watu—zinalipwa ili kuwe na “maendeleo.” Iwe unakubaliana na taarifa hiyo au la, ni wazi kwamba kwa kawaida watu hutumia pesa nyingi kulipa kodi.

      Kodi zinaweza kugawanywa katika makundi mawili: kodi zinazotozwa moja kwa moja na zisizotozwa moja kwa moja. Kodi ya mapato, kodi ya shirika, na kodi ya rasilimali ni baadhi ya kodi zinazotozwa moja kwa moja. Kati ya hizo, kodi ya mapato ndiyo inayochukiwa zaidi. Ni hivyo hasa katika nchi ambako kodi ya mapato hutozwa kulingana na mapato ya mtu—hivyo ikiwa mapato yako ni ya juu, utalipa kodi ya juu. Watu wanaopinga ulipaji wa kodi fulani wanasema kwamba kodi inapotozwa hivyo, hilo huwaadhibu watu wanaofanya kazi kwa bidii na waliofanikiwa.

      Kitabu OECD Observer cha Shirika la Ushirikiano na Maendeleo ya Kiuchumi kinasema kwamba “huenda wafanyakazi wakatozwa kodi ya mapato na serikali za mtaa, za wilaya, au za majimbo kuongezea kodi ya mapato inayotozwa na serikali kuu. Ndivyo ilivyo huko Hispania, Iceland, Japan, Kanada, Korea, Marekani, katika nchi za Skandinavia, Ubelgiji, na Uswisi.”

      Kodi zisizotozwa moja kwa moja zinatia ndani kodi ya mauzo, kodi inayotozwa vileo na sigara, na ushuru wa forodhani. Tofauti na kodi zinazotozwa moja kwa moja, watu hawatambui kuwa wanatozwa kodi hizo waziwazi, lakini zinaweza kuwalemea watu, hasa maskini. Katika gazeti Frontline la India, mwandishi Jayali Ghosh anasema kwamba si kweli kuwa matajiri na watu wanaochuma mapato ya kadiri hulipa sehemu kubwa ya kodi nchini India. Ghosh anasema: “Kodi zisizotozwa moja kwa moja ni zaidi ya asilimia 95 ya kodi zote zinazokusanywa na serikali za Majimbo. . . . Huenda watu maskini zaidi ndio hutumia sehemu kubwa ya mapato yao kulipa kodi kuliko matajiri.” Huenda tofauti hiyo husababishwa na kodi za juu zinazotozwa bidhaa zinazonunuliwa na watu wengi kama vile sabuni na chakula.

      Serikali hutumiaje pesa zinazokusanywa?

      Pesa Hutumiwaje?

      Ni kweli kwamba serikali hutumia pesa nyingi kutoa huduma muhimu. Kwa mfano, nchini Ufaransa, mtu 1 kati ya 4 ameajiriwa na serikali. Hiyo inatia ndani walimu, wafanyakazi wa posta, wafanyakazi wa majumba ya makumbusho na hospitali, polisi, na wengineo. Kodi zinahitajiwa ili kuwalipa mishahara. Kodi pia hutumiwa kutengeneza barabara, shule, na hospitali na vilevile kulipia gharama za kukusanya takataka na kutuma barua.

      Kodi hutumiwa pia kugharimia matumizi ya kijeshi. Katika mwaka wa 1799, Waingereza matajiri walitozwa kodi ya kwanza ya mapato ili kugharimia vita dhidi ya Wafaransa. Lakini wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, serikali ya Uingereza ilianza kuwatoza wafanyakazi kodi ya mapato. Leo, pesa nyingi hutumiwa kugharimia shughuli za kijeshi hata wakati wa amani. Shirika la Stockholm la Utafiti wa Amani ya Kimataifa lilikadiria kwamba gharama za kijeshi ulimwenguni pote katika mwaka wa 2000, zilikuwa dola bilioni 798 hivi za Marekani.

      Kutoza Kodi Ili Kubadili Mazoea ya Watu

      Kodi hutozwa pia ili kuwachochea watu waache mazoea mabaya au wafanye mema. Kwa mfano, kodi ya vileo hutozwa ili kupunguza unywaji wa kupita kiasi. Kwa hiyo, katika nchi nyingi, asilimia 35 hivi ya bei ya kileo huwa kodi.

      Sigara pia hutozwa kodi za juu sana. Nchini Afrika Kusini, asilimia 45 hadi 50 ya bei ya sigara huwa kodi. Hata hivyo, nyakati nyingine serikali hutoza kodi hizo kwa sababu tofauti mbali na kufaidi jamii. Kama mwandishi Kenneth Warner anavyosema katika gazeti Foreign Policy, sigara “huleta mamia ya mabilioni ya dola kila mwaka kupitia mauzo, na mabilioni zaidi kupitia kodi.”

      Mfano mmoja wa jinsi kodi inavyoweza kubadili mazoea ulitukia mapema katika karne ya 20. Wabunge wa Marekani walitaka kupunguza familia za matajiri. Jinsi gani? Kwa kuanzisha kodi ya mali. Tajiri anapokufa, kodi ya juu hutozwa ili kupunguza sana mali alizokusanya. Watetezi wa kodi hiyo wanasema kwamba “inaondoa mali kutoka kwa familia na watu wachache na kuzielekeza kwa umma na serikali.” Labda hilo ni kweli, lakini matajiri wamebuni mbinu nyingi za kuhepa kodi hiyo.

      Kodi huendelea kutumiwa kuendeleza mipango ya kijamii, kama vile kuhifadhi mazingira. Gazeti The Environmental Magazine linaripoti: “Hivi majuzi, nchi tisa za Ulaya Magharibi zimeanzisha kodi fulani ili kuhifadhi mazingira, hasa kwa kupunguza vichafuzi vya hewa.” Kodi inayotozwa kwa kutegemea kiasi cha mapato, ambayo ilitajwa mwanzoni, pia ni mfano wa kodi inayokusudiwa kubadili mazoea. Inakusudiwa kupunguza tofauti kati ya matajiri na maskini. Serikali fulani pia huwapunguzia kodi watu wanaotoa misaada au wenzi walio na watoto.

      Kwa Nini Sheria za Kodi Zinatatanisha?

      Wabunge wanapopendekeza kodi mpya, wao hujaribu kuwazuia watu wasiihepe kwa vyovyote kwani pesa nyingi zinaweza kupotea. Tokeo ni nini? Sheria za kodi huwa tata sana. Makala moja katika gazeti Time ilieleza kwamba matatizo mengi yanayofanya sheria za kodi za Marekani ziwe tata “hutokana na kubainisha mapato,” yaani, kujua kiasi kinachopaswa kutozwa. Magumu mengine yanatokana na kanuni nyingi “zinazowaruhusu watu kupunguziwa na kutolipa kodi fulani.” Hata hivyo, si Marekani tu yenye sheria tata za kodi. Sheria ya kodi iliyotungwa hivi majuzi nchini Uingereza ilichukua kurasa 9,521 zilizojaza mabuku kumi.

      Ofisi ya Utafiti wa Sheria za Kodi katika Chuo Kikuu cha Michigan inaripoti hivi: “Kila mwaka walipa-kodi nchini Marekani hutumia zaidi ya saa bilioni tatu wakijaza fomu za malipo ya kodi. . . . Kwa ujumla, wakati na pesa ambazo walipa-kodi wa Marekani hutumia [kujaza fomu za malipo ya kodi] hugharimu dola bilioni 100 kila mwaka, au asilimia 10 hivi ya kodi zinazotozwa. Gharama hizo nyingi husababishwa na utata wa sheria za kodi ya mapato.” Reuben, aliyetajwa mwanzoni mwa makala ya kwanza anasema: “Hapo zamani, nilikuwa ninajaza fomu hizo mwenyewe, lakini ilinichukua wakati mwingi, na nilihisi kwamba ninalipa pesa nyingi kuliko inavyostahili. Kwa hiyo sasa nimemwajiri mhasibu afanye kazi hiyo.”—Ona sanduku “Kutii Sheria za Kodi,” kwenye ukurasa wa 8.

      Watu Wanaolipa, Wanaoepuka, na Wanaohepa Kodi

      Watu wengi wanaweza kukubali shingo upande kwamba kodi hufaidi jamii. Msimamizi wa Idara ya Kodi ya Uingereza alieleza hivi: “Hakuna mtu anayefurahia kulipa kodi ya mapato, lakini wengi wanakubali kwamba inatufaidi.” Wengine wanakadiria kwamba asilimia 90 ya watu nchini Marekani hulipa kodi. Shirika moja la kodi linakiri hivi: “Idadi kubwa ya watu ambao hawalipi kodi hufanya hivyo kwa sababu hawaelewi sheria na utaratibu, si kwamba wanahepa kimakusudi.”

      Hata hivyo, watu wengi hutafuta njia za kuepuka kulipa kodi fulani. Kwa mfano, fikiria yale ambayo makala moja katika gazeti U.S.News & World Report ilisema hivi kuhusu kodi ya shirika: “Mashirika mengi hutumia sheria kuepuka kiasi kikubwa cha kodi—na wakati mwingine kodi yote—kwa kuomba wapunguziwe kodi na kwa kutumia ujanja.” Makala hiyo ilitoa mfano huu kuonyesha mbinu ya ujanja: “Shirika moja la Marekani linaweza kuanzisha ofisi katika nchi ya kigeni isiyotoza kodi nyingi. Halafu, linaweza kufanya shirika lililoko Marekani liwe tawi la ofisi hiyo.” Kwa hiyo shirika hilo huepuka kulipa kodi za Marekani, ambazo zinaweza kufikia asilimia 35, hata ingawa “huenda makao hayo makuu ni ofisi tu yenye kabati ya faili na sanduku la posta.”

      Kisha kuna kuhepa kodi kabisa-kabisa. Inaripotiwa kwamba katika nchi moja ya Ulaya watu hupenda kuhepa kodi. Kulingana na uchunguzi uliofanywa nchini Marekani, asilimia 58 tu ya wanaume walio kati ya umri wa miaka 25 na 29 ndio wanaoamini kwamba haifai kudanganya kuhusu mapato yao. Waandishi wa ripoti hiyo wanakiri hivi: “Ripoti hiyo inaonyesha kwamba tabia na maadili ya jamii yetu yamezorota.” Nchini Mexico, inakadiriwa kwamba asilimia 35 hivi ya watu huhepa kodi.

      Hata hivyo, kwa ujumla, watu hutambua umuhimu wa kulipa kodi, na hawaoni ubaya kuzilipa. Lakini, maneno haya yanayojulikana sana, ambayo huenda yalisemwa na Kaisari Tiberio, ni ya kweli: “Mchungaji mwema huwanyoa kondoo lakini hawachuni ngozi.” Iwapo unaona kwamba unakandamizwa na mfumo wa kodi unaolemea, usio wa haki, na unaotatanisha sana, unapaswa kuwa na maoni gani kuhusu kulipa kodi?

      [Sanduku katika ukurasa wa 7]

      Fikiri Kabla ya Kuhama!

      Mifumo ya kodi hutofautiana katika nchi mbalimbali. Hata kodi za mapato zinaweza kutofautiana sana katika nchi ileile. Je, inafaa kuhamia eneo linalotoza kodi nafuu? Labda, lakini unapaswa kufikiri kabla ya kuhama.

      Kwa mfano, makala moja katika gazeti OECD Observer inawakumbusha wasomaji kwamba hawapaswi kuangalia tu kiwango cha kodi ya mapato. Inasema hivi: “Kodi halisi huathiriwa na viwango mbalimbali vya kupunguza kodi.” Kwa mfano, nchi fulani hazitozi kodi kubwa ya mapato. Lakini “hazipunguzi kodi sana na haziwaruhusu watu wasilipe kodi fulani.” Kwa hiyo, mtu anaweza kulipa kodi zaidi huko kuliko katika nchi ambazo zinatoza kodi ya juu na ambazo zinawaruhusu watu wapunguziwe au wasilipe kodi fulani.

      Nchini Marekani, watu fulani hufikiria kuhamia majimbo ambayo hayatozi kodi ya mapato. Lakini je, kufanya hivyo huokoa pesa? Sivyo kulingana na kitabu Kiplinger’s Personal Finance, kinachosema: “Katika visa fulani, uchunguzi wetu unaonyesha kwamba majimbo ambayo hayatozi kodi ya mapato hupata pesa kwa kutoza kodi za juu za mali, za mauzo, na kodi nyingine.”

      [Sanduku katika ukurasa wa 8]

      Kutii Sheria za Kodi

      Kwa wengi wetu, kulipa kodi ni mzigo mzito na wenye kulemea. Kwa hiyo Amkeni! lilimwomba mtaalamu wa kodi atoe madokezo kadhaa.

      “Omba mashauri yenye kutegemeka. Hilo ni muhimu kwa sababu sheria za kodi zinaweza kuwa tata, na mara nyingi kutojua sheria si udhuru wa kutolipa kodi. Ingawa huenda mlipa-kodi akawaona maafisa wa kodi kuwa maadui, wanaweza kumpa maelezo sahihi na sahili ambayo yanaweza kumsaidia kushughulikia masuala ya kodi. Mashirika ya kodi hutaka ujaze fomu za kulipa kodi kwa usahihi unapoanza kulipa kodi. Hawakusudii kukushtaki kwa kutolipa.

      “Ikiwa unapata ugumu kufanya hesabu ya kodi yako, omba mashauri kutoka kwa mtaalamu wa kodi. Lakini jihadhari! Ingawa wataalamu wengi wa kodi ni wazuri, kuna wengi wanaotumia hila. Omba mashauri kutoka kwa rafiki au mfanyabishara anayeaminika ili akusaidie kujua sifa za mtaalamu huyo.

      “Tenda haraka. Watu wanaochelewa kulipa kodi huadhibiwa vikali.

      “Weka rekodi nadhifu. Hata iwe unatumia njia gani kuweka rekodi, hakikisha zina habari za karibuni zaidi. Hivyo, hutatumia wakati mwingi kufanya hesabu za kodi wakati wa kulipa unapofika. Pia hutatatanika iwapo rekodi zako zitakaguliwa.

      “Uwe mnyofu. Huenda ukashawishiwa kudanganya au kuvunja sheria kidogo. Lakini maafisa wa kodi wana mbinu nyingi za kugundua udanganyifu. Kwa hiyo ni vizuri kuwa mnyofu nyakati zote.

      “Jihusishe. Mtaalamu wa kodi akiwasilisha rekodi zisizo sahihi, wewe ndiwe unayewajibika. Kwa hiyo, hakikisha mtaalamu uliyeajiri anafuata matakwa yako.”

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Katika nchi nyingi bidhaa za tumbaku na vileo hutozwa kodi za juu

      [Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      Kodi hulipia huduma nyingi ambazo nyakati nyingine hatuzitilii maanani

  • Je, Unapaswa Kulipa Kodi?
    Amkeni!—2003 | Desemba 8
    • Je, Unapaswa Kulipa Kodi?

      “Wapeni wote haki zao, yeye anayetaka kodi, kodi; yeye anayetaka ushuru, ushuru; yeye anayetaka woga, woga huo; yeye anayetaka heshima, heshima hiyo.”—Waroma 13:7.

      KWA KUWA kodi zinaongezeka, inaweza kuwa vigumu kutii shauri lililo hapa juu. Hata hivyo, hayo ni maneno ya mtume Paulo, na yameandikwa katika Biblia. Bila shaka unaiheshimu Biblia. Lakini huenda ukauliza, ‘Je, Wakristo wanapaswa kulipa kodi zote, hata zile ambazo wengine wanaona kuwa hazifai au si za haki?’

      Fikiria shauri ambalo Yesu aliwapa wanafunzi wake. Alijua kwamba Wayahudi wenzake walichukia sana kodi zilizotozwa na serikali ya Roma. Ingawa hivyo, Yesu alisema: “Mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari, lakini Mungu vitu vya Mungu.” (Marko 12:17) Waona, Yesu aliagiza watu walipe kodi kwa serikali ambayo ingemuua baada ya muda mfupi.

      Miaka michache baadaye, Paulo alitoa shauri lililonukuliwa mwanzoni. Aliwahimiza watu walipe kodi, ingawa kiasi kikubwa cha pesa za kodi kilitumiwa kugharimia shughuli za kijeshi za Waroma na kuwategemeza maliki Waroma waliokuwa na mwenendo mbaya na maisha ya anasa. Kwa nini Paulo alitoa shauri hilo ambalo halikupendwa na wengi?

      Mamlaka Zilizo Kubwa

      Fikiria muktadha wa maneno ya Paulo. Aliandika hivi kwenye Waroma 13:1: “Kila nafsi na ijitiishe kwa mamlaka zilizo kubwa, kwa maana hakuna mamlaka isipokuwa kwa njia ya Mungu; mamlaka zilizopo zimesimamishwa na Mungu katika vyeo vyao vya kadiri.” Wakati taifa la Israeli lilipokuwa na watawala wanaomwogopa Mungu, ilikuwa rahisi kutambua kwamba kutegemeza taifa kifedha ni wajibu wa kiraia na wa kidini. Lakini je, Wakristo walikuwa na wajibu huohuo wakati watawala waliabudu sanamu? Ndiyo! Maneno ya Paulo yalionyesha kwamba Mungu aliwapa watawala “mamlaka” ya kutawala.

      Serikali mbalimbali hujitahidi sana kudumisha amani. Hilo huwaruhusu Wakristo waendelee na shughuli zao za kiroho. (Mathayo 24:14; Waebrania 10:24, 25) Ndiyo sababu Paulo alisema hivi kuhusu mamlaka za serikali za wakati huo: “Ni mhudumu wa Mungu kwako kwa faida yako.” (Waroma 13:4) Paulo mwenyewe alifaidika kutokana na ulinzi wa serikali ya Roma. Kwa mfano, wakati umati ulipomshambulia, aliokolewa na maaskari Waroma. Baadaye alikata rufani kwa mfumo wa sheria wa Roma ili aendelee kuwa mishonari.—Matendo 22:22-29; 25:11, 12.

      Hivyo, Paulo alitoa sababu tatu za kulipa kodi. Kwanza, alizungumzia jinsi serikali zinavyowahukumu kwa “ghadhabu” watu wanaovunja sheria. Pili, alieleza kwamba dhamiri ya mtu anayemtii Mungu inaweza kuathiriwa sana akihepa kodi. Mwishowe, alisema kwamba kodi ni malipo ya huduma ambazo serikali hutoa zikiwa ‘watumishi kwa watu wote.’—Waroma 13:1-6.

      Je, Wakristo walioishi wakati wa Paulo walitii maneno hayo? Inaonekana walifanya hivyo, kwa sababu katika karne ya pili mwandishi aliyedai kuwa Mkristo, Justin Martyr (karibu mwaka wa 110 hadi 165 W.K.), alisema kwamba Wakristo walilipa kodi “kwa hiari kuliko watu wote.” Leo, serikali zinapodai malipo, iwe ni wakati au pesa, bado Wakristo hutii kwa hiari.—Mathayo 5:41.a

      Bila shaka, Wakristo wanaruhusiwa kutumia maandalizi ya kisheria ya kupunguziwa kodi. Katika visa fulani, huenda wakafaidika na maandalizi ya kupunguziwa kodi yanayotolewa kwa wale wanaotoa michango kwa mashirika ya kidini. Hata hivyo, Wakristo wa kweli hawapaswi kuhepa kodi kwa kuwa wanatii Neno la Mungu. Wao hulipa kodi, na kuachia serikali wajibu wa kutumia pesa hizo itakavyo.

      Utozaji wa kodi ya juu ni mojawapo ya njia ambazo “mwanadamu amemtawala mwanadamu kwa kumuumiza.” (Mhubiri 8:9) Mashahidi wa Yehova hufarijiwa na ahadi ya Biblia kwamba karibuni watu wote watatendewa kwa haki chini ya serikali ya Mungu—serikali ambayo haitawalemeza watu na kodi zinazokandamiza.—Zaburi 72:12, 13; Isaya 9:7.

      [Maelezo ya Chini]

      a Shauri la Yesu la kulipa “Kaisari vitu vya Kaisari” halikumaanisha kulipa kodi tu. (Mathayo 22:21) Kitabu Critical and Exegetical Hand-Book to the Gospel of Matthew cha Heinrich Meyer kinaeleza: “[Vitu vya Kaisari] . . . si kodi ya serikali tu, lakini vitu vyote ambavyo tunapaswa kumlipa Kaisari akiwa mtawala halali.”

      [Blabu katika ukurasa wa 11]

      Wakristo wa mapema walilipa kodi “kwa hiari kuliko watu wote.”—JUSTIN MARTYR

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Wakristo wa kweli hutii sheria za kodi

      [Picha katika ukurasa wa 11]

      Yesu alisema: “Mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari”

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

      © European Monetary Institute

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki