-
Usahihi wa Biblia Unathibitishwa na Maktaba ya Kale ya UrusiMnara wa Mlinzi—2005 | Julai 15
-
-
Usahihi wa Biblia ulijadiliwa vikali hasa nchini Ujerumani. Profesa mmoja kijana aliyeishi huko aliacha maisha yake ya starehe na elimu na kufunga safari ambayo ilimwezesha kugundua hati muhimu zaidi za Biblia. Aliitwa Konstantin von Tischendorf. Yeye alikuwa msomi wa Biblia aliyepinga uchambuzi wa Biblia na hatimaye akafanikiwa kutetea usahihi wa maandishi ya Biblia. Alipata mafanikio katika safari yake ya kwanza ya kwenda kwenye jangwa la Sinai katika mwaka 1844. Alipochungulia kikapu cha takataka katika makao ya watawa, aliona Septuajinti, ambayo ni tafsiri ya kale ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania. Nakala hiyo aliyopata ndiyo iliyokuwa ya kale zaidi kuwahi kupatikana!
Tischendorf alifurahi sana na akafaulu kupata sehemu 43 za hati hizo za kale. Ijapokuwa alikuwa na hakika kwamba kulikuwa na sehemu nyingine za hati hiyo, alipata tu kipande kidogo aliporudi mwaka wa 1853. Zile sehemu nyingine zilikuwa wapi? Pesa zake zilikuwa zimekwisha na Tischendorf akamwomba tajiri fulani msaada wa kifedha na kuamua kutoka nchi yao tena ili aende akatafute hati nyingine za kale za Biblia. Hata hivyo, kabla ya kufunga safari hiyo akamwomba maliki wa Urusi msaada wa kutimiza mradi huo.
Maliki Aunga Mkono
Yamkini Tischendorf alijiuliza kama yeye aliyekuwa msomi Mprotestanti angekaribishwa nchini Urusi, kwani katika nchi hiyo kubwa watu wengi walikuwa wafuasi wa Kanisa Othodoksi la Urusi. Hata hivyo, mabadiliko makubwa yalikuwa yakitukia nchini Urusi. Elimu ilitiliwa maanani, na katika mwaka wa 1795 Malkia Katerina wa Pili (anaitwa pia Katerina Mkuu) akaanzisha Maktaba ya Milki ya St. Petersburg. Hiyo ilikuwa maktaba ya kwanza ya umma nchini Urusi na iliwawezesha watu wengi sana kusoma vitabu vingi vilivyokuwa huko.
Maktaba hiyo ilionwa kuwa mojawapo ya maktaba bora huko Ulaya, hata hivyo ilikosa kitu fulani. Miaka 50 baada ya kuanzishwa, maktaba hiyo ilikuwa na hati sita tu za kale za Kiebrania. Kwa kuwa watu wengi nchini Urusi walipendezwa na lugha za Biblia na tafsiri zake, hati hizo chache hazingetosheleza tamaa yao. Malkia Katerina wa Pili alikuwa amewapeleka wasomi wakajifunze Kiebrania kwenye vyuo vikuu huko Ulaya. Waliporudi, masomo ya lugha ya Kiebrania yalianzishwa katika seminari za Kanisa Othodoksi la Urusi, na kwa mara ya kwanza, wasomi Warusi wakaanza kutafsiri nakala sahihi ya Biblia katika Kirusi wakitegemea maandishi ya kale ya Kiebrania. Lakini hawakuwa na fedha za kutosha, na viongozi wa kanisa wasiotaka mabadiliko waliwapinga. Wakati wa kuielewa Biblia vizuri haukuwa umefika.
Maliki Aleksanda wa Pili, alielewa upesi umuhimu wa mradi wa Tischendorf na akaamua kumsaidia kifedha. Licha ya “wivu na upinzani” wa watu fulani, Tischendorf alienda Sinai na akarejea akiwa na zile sehemu nyingine za Septuajinti.a Bado hati hiyo ya Septuajinti, ambayo baadaye ilikuja kuitwa Kodeksi ya Sinai, ni mojawapo ya hati za kale zaidi za Biblia ambazo zimewahi kupatikana. Aliporudi St. Petersburg, Tischendorf alienda moja kwa moja kwenye Jumba la Maliki la Majira ya Baridi. Alimpendekezea maliki aunge mkono “mmojawapo wa miradi mikubwa zaidi ya kuchunguza na kujifunza maandishi ya Biblia,” yaani, kutayarisha nakala ya hati hiyo iliyopatikana karibuni na kuichapisha. Baadaye nakala hiyo iliwekwa kwenye Maktaba ya Milki. Maliki alikubali upesi na baadaye Tischendorf aliyekuwa na furaha akaandika hivi: “Kwa mapenzi ya Mungu kizazi chetu kimepewa . . . Biblia ya Sinai ambayo inathibitisha kikamili na waziwazi usahihi wa maandishi ya Neno la Mungu, na kutusaidia kutetea kweli ya Biblia kwa kuonyesha jinsi ilivyokuwa awali.”
-
-
Usahihi wa Biblia Unathibitishwa na Maktaba ya Kale ya UrusiMnara wa Mlinzi—2005 | Julai 15
-
-
[Picha katika ukurasa wa 11]
Konstantin von Tischendorf (katikati)
-