Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ustahimilivu—Kutoka Mwisho Mmoja Hadi Ule Mwingine
    Amkeni!—1997 | Januari 22
    • Ustahimilivu—Kutoka Mwisho Mmoja Hadi Ule Mwingine

      MANDHARI zenye kuvutia za Bonde la Kashmir zilichochea mwanafalsafa wa karne ya 16 apaaze sauti hivi: “Ikiwa kuna paradiso mahali popote, ni hapa!” Kwa wazi, hakuwa na wazo lolote kuhusu kile ambacho kingetokea baadaye katika sehemu hii ya ulimwengu. Katika kipindi cha miaka mitano ambayo imepita, angalau watu 20,000 wameuawa huko katika vita kati ya vikundi vya kupigania uhuru na Jeshi la India. Gazeti la habari la Ujerumani Süddeutsche Zeitung sasa hufafanua eneo hilo kuwa “bonde la machozi.” Bonde la Kashmir huandaa somo sahili lakini lenye thamani: Ukosefu wa ustahimilivu waweza kuharibu sehemu iwezayo kuwa paradiso.

      Yamaanisha nini kuwa mstahimilivu? Kulingana na Collins Cobuild English Language Dictionary, “ikiwa wewe ni mstahimilivu, wewe huruhusu watu wawe na mitazamo na itikadi zao wenyewe, au waenende kwa njia fulani, hata ikiwa wewe hukubali au hupendelei jambo hilo.” Ni sifa nzuri kama nini ya kudhihirisha! Kwa hakika sisi huhisi tukiwa tumestareheka tukiwa na watu ambao hustahi itikadi na mitazamo yetu hata ikiwa inatofautiana na yao.

      Kutoka Ustahimilivu Hadi Ushupavu

      Kinyume cha ustahimilivu ni ukosefu wa ustahimilivu, ambao huwa na viwango tofauti-tofauti vya mkazo. Ukosefu wa ustahimilivu waweza kuanza na kutokubali kwa akili iliyofungika mwenendo au njia ya mtu mwingine ya kufanya mambo. Kuwa na akili iliyofungika huzuia kufurahia maisha na kufanya akili ya mtu isipate mawazo mapya.

      Kwa kielelezo, huenda mtu mgumu akachukizwa na idili nyingi za mtoto. Huenda kijana akachoshwa na njia za kutafakari za mtu mwenye umri mkubwa kupita wake. Mwulize mtu mwenye hadhari afanye kazi bega kwa bega na mtu ambaye hupenda sana kujasiria, na wote watachokozeka. Kwa nini mtu achukizwe, achoshwe, na achokozeke? Kwa sababu, katika kila kisa, mtu huona likiwa jambo gumu kustahimili mtazamo na mwenendo wa yule mwingine.

      Mahali ambapo ukosefu wa ustahimilivu husitawi, kuwa na akili iliyofungika kwaweza kuongezeka kufikia ubaguzi, ambao ni kujiepusha na kikundi, jamii, au dini fulani. Ulio mbaya zaidi kuliko ubaguzi ni ushupavu, ambao waweza kujidhihirisha kwa chuki yenye jeuri. Tokeo ni taabu na umwagikaji wa damu. Fikiria kile ambacho ukosefu wa ustahimilivu ulitokeza wakati wa zile Krusedi! Hata leo, ukosefu wa ustahimilivu ni kisababishi kikuu cha mapambano katika Bosnia, Rwanda, na Mashariki ya Kati.

      Ustahimilivu huhitaji usawaziko, na kudumisha usawaziko ufaao si jambo rahisi. Tuko kama pinduli ya saa, ikibembea kutoka upande mmoja hadi ule mwingine. Nyakati fulani, sisi huonyesha ustahimilivu mchache sana; nyakati nyingine, ustahimilivu mwingi sana.

      Kutoka Ustahimilivu Hadi Ukosefu wa Adili

      Je, inawezekana kuwa mstahimilivu kupita kiasi? Mbunge wa Marekani Dan Coats, alipokuwa akizungumza katika 1993, alifafanua “bishano juu ya maana na udhihirishaji wa ustahimilivu.” Alimaanisha nini? Mbunge huyo aliomboleza kwamba kwa kutoa udhuru kwamba ni ustahimilivu, wengine “wameacha itikadi katika ukweli wa adili—katika jema na baya, lililo sawa na lisilo sawa.” Watu kama hao wanahisi kwamba jamii haina haki ya kuhukumu ni upi ulio mwenendo mwema na upi ulio mbaya.

      Katika 1990, mwanasiasa Mwingereza Lord Hailsham aliandika kwamba “adui mbaya sana wa maadili si uatheisti, uagnosti, ufuatiaji wa vitu vya kimwili, pupa wala chochote cha visababishi vinginevyo vinavyokubaliwa. Adui wa kweli wa maadili ni unihili, ikisemwa wazi kabisa, kutoitikadi chochote.” Kwa wazi, tusipoitikadi chochote, hatuna viwango vya mwenendo ufaao na kila kitu chaweza kustahimiliwa. Lakini ni jambo linalofaa kustahimili kila namna ya mwenendo?

      Mkuu wa shule ya sekondari aliye Mdenmark hakufikiri hivyo. Yeye aliandika makala ya gazeti la habari katika miaka ya mapema ya 1970, akilalamika kuhusu matangazo ya biashara katika vyombo vya habari kwa maonyesho ya kiponografia yenye kuonyesha tendo la ngono kati ya wanyama na wanadamu. Matangazo haya yaliruhusiwa kwa sababu ya “ustahimilivu” wa Denmark.

      Kwa wazi, matatizo huzuka si kutokana na kuonyesha tu ustahimilivu mchache bali pia ustahimilivu mwingi kupita kiasi. Kwa nini ni jambo gumu kuepuka kupita kiasi na kubaki katika usawaziko ufaao? Tafadhali soma makala ifuatayo.

  • Usawaziko Ufaao Waweza Kufanya Maisha Yako Yapendeze
    Amkeni!—1997 | Januari 22
    • Usawaziko Ufaao Waweza Kufanya Maisha Yako Yapendeze

      USTAHIMILIVU ni kama sukari katika kikombe cha chai. Kiwango kifaacho chaweza kuongeza utamu katika maisha. Lakini ingawa twaweza kuwa wakarimu na sukari, mara nyingi hatuwi wakarimu na ustahimilivu. Kwa nini?

      “Wanadamu hawataki kuwa wastahimilivu,” akaandika Arthur M. Melzer, profesa mshiriki kwenye Chuo Kikuu cha Jimbo la Michigan. “Wanadamu wana mwelekeo wa asili wa kuonyesha . . . ubaguzi.” Kwa hiyo ukosefu wa ustahimilivu si tu kasoro ya utu ambayo hupata wachache tu; kuwa wenye akili iliyofungika hutupata sote kiasili kwa kuwa wanadamu wote si wakamilifu.—Linganisha Waroma 5:12.

      Wenye Uwezekano wa Kuwa Wadadisi

      Katika 1991, gazeti Time liliripoti juu ya hali inayoendelea kuongezeka ya akili iliyofungika Marekani. Makala hiyo ilifafanua “mtindo-maisha wa wadadisi,” watu ambao hujaribu kulazimisha kila mtu afuate viwango vyao wenyewe. Wasiokubaliana wamehasiriwa. Kwa mfano, mwanamke mmoja katika Boston alifutwa kazi kwa sababu ya kukataa kutumia virembeshi. Mwanamume mmoja katika Los Angeles alifutwa kazi kwa sababu ya kuwa mnene kupita kiasi. Kwa nini jitihada hiyo yote ya kufanya wengine wakubaliane?

      Watu wenye akili iliyofungika hawakubali sababu, ni wenye ubinafsi, wenye shingo ngumu, na wenye kutaka watu wafuate maoni yao tu. Lakini je, watu wengi si ni wenye kukosa kukubali sababu, wenye ubinafsi, wenye shingo ngumu, au wenye kutaka maoni yao tu yafuatwe kwa kiwango fulani? Tabia hizi zikipata mizizi mizuri katika utu wetu, tutakuwa watu wenye akili iliyofungika.

      Namna gani wewe? Je, wewe hudhihirisha hali ya kutokubali kwa habari ya ladha ya mtu mwingine ya chakula? Katika mazungumzo, je, kwa kawaida wewe hutaka kuwa mwenye neno la mwisho? Unapofanya kazi mkiwa kikundi, je, wewe hutarajia wengine wafuate njia yako ya kufikiri? Ikiwa ndivyo, lingekuwa jambo zuri kuongeza sukari kidogo katika chai yako!

      Lakini, kama ilivyotajwa katika makala iliyotangulia, ukosefu wa ustahimilivu waweza kuja katika namna ya ubaguzi wenye uhasama. Jambo moja liwezalo kufanya ukosefu wa ustahimilivu uongezeke ni hangaiko baya.

      “Hisi Yenye Kina ya Kukosa Uhakika”

      Wataalamu wa jamii na asili za wanadamu wamechunguza wakati uliopita wa mwanadamu ili wajue ni wakati gani na mahali gani ambapo ubaguzi wa jamii ulikuwa wazi. Walipata kwamba aina hii ya ukosefu wa ustahimilivu haiwi wazi wakati wote, wala haijidhihirishi katika kila nchi kwa kiwango kilekile. Gazeti la Ujerumani la sayansi ya asili GEO huripoti kwamba mikwaruzano ya kijamii hujitokeza katika wakati wa tatizo wakati ambapo “watu wana hisi yenye kina ya kukosa uhakika na kuhisi kwamba utambulisho wao umo hatarini.”

      Je, hiyo “hisi yenye kina ya kukosa uhakika” imeenea sana leo? Bila shaka. Zaidi ya wakati mwingineo wote, wanadamu wanasumbuliwa na tatizo moja baada ya jingine. Ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, kupanda kwa gharama ya maisha, idadi ya watu yenye kupita kiasi, kupungua kwa tabaka la ozoni, uhalifu majijini, uchafuzi wa maji ya kunywa, kuongezeka kwa joto tufeni pote—hofu yenye kusumbua ya lolote la mambo hayo huongeza hangaiko. Matatizo husababisha hangaiko, na hangaiko lisilofaa huongoza kwenye ukosefu wa ustahimilivu.

      Ukosefu huo wa ustahimilivu hujidhihirisha, kwa mfano, mahali ambapo vikundi vya kikabila na tamaduni tofauti huchangamana, kama ilivyo katika nchi fulani za Ulaya. Kulingana na ripoti moja iliyotolewa na National Geographic katika 1993, nchi za Ulaya Magharibi wakati huo zilikuwa na wahamiaji zaidi ya milioni 22 kutoka nchi nyinginezo. Watu wengi wa ulaya “walihisi wamelemezwa na kuja kwa wingi wa wageni” wa lugha, tamaduni, au dini tofauti. Kumekuwa na ongezeko la maoni yaliyo dhidi ya wageni katika Austria, Hispania, Italia, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani.

      Namna gani viongozi wa ulimwengu? Katika kipindi cha miaka ya 1930 na 1940, Hitler alifanya ukosefu wa ustahimilivu uwe sera ya serikali. Kwa kuhuzunisha, viongozi fulani wa kisiasa na wa kidini leo hutumia ukosefu wa ustahimilivu ili kupata malengo yao. Ndivyo imekuwa katika mahali kama vile Austria, Ireland, Marekani, Rwanda, Ufaransa, na Urusi.

      Epuka Mtego wa Ubaridi

      Kukiwa na sukari chache sana katika chai yetu twahisi kwamba kuna kitu kinachokosekana; kukiwa na sukari nyingi mno twahisi ladha ya utamu isiyofurahisha kinywani mwetu. Ndivyo ilivyo na ustahimilivu. Fikiria ono la mwanamume mmoja afundishaye katika chuo fulani Marekani.

      Miaka kadhaa iliyopita David R. Carlin, Jr., alipata njia rahisi lakini yenye matokeo ya kufanya mazungumzo ya darasani yawe yenye kusisimua. Alikuwa akitokeza taarifa iliyokusudiwa kutoa wito wa ushindani kwa maoni ya wanafunzi wake, akijua kwamba wangepinga. Matokeo yalikuwa kwamba kulikuwa na mazungumzo moto-moto. Hata hivyo, katika 1989, Carlin aliandika kwamba njia iyo hiyo haikuwa na matokeo tena. Kwa nini? Ingawa wanafunzi bado hawakukubaliana na kile alichosema, hawakushughulika kubishana. Carlin alieleza kwamba walikuwa wamekuwa na “mtazamo wa mtu mwenye kushuku na kuachilia mambo”—mtazamo wa kutojali kabisa.

      Je, mtazamo wa kutojali ni sawa na ustahimilivu? Ikiwa hakuna mtu anayejali kile ambacho mtu mwingine hufikiri au kufanya, hakuna viwango kabisa. Ukosefu wa viwango ni ubaridi—ukosefu kamili wa upendezi. Hali kama hiyo yaweza kutokeaje?

      Kulingana na Profesa Melzer, ubaridi waweza kuenea katika jamii ambayo hukubali viwango vingi tofauti vya mwenendo. Watu huja kuamini kwamba aina yote ya mwenendo inakubalika na kwamba kila kitu ni jambo tu la uchaguzi wa kibinafsi. Badala ya kujifunza kufikiri na kutilia shaka kinachokubalika na kisichokubalika, watu “mara nyingi hujifunza kutofikiri kabisa.” Wanakosa nguvu ya maadili inayomsukuma mtu kukinza kwa ujasiri ukosefu wa ustahimilivu wa wengine.

      Namna gani wewe? Je, wewe hujipata ukiwa na mtazamo wa kutojali? Je, wewe hucheka vichekesho visivyo safi au vya ubaguzi wa jamii? Je, wewe huruhusu mwana au binti yako tineja atazame vidio ambazo huchochea pupa na ukosefu wa adili? Je, wahisi kwamba ni sawa watoto wako wakicheza michezo yenye jeuri ya kompyuta?

      Kukiwa na ustahimilivu wa kupita kiasi, familia au jamii itavuna maumivu makali, kwa kuwa hakuna mtu anayejua—au anayejali—kilicho sawa na kisicho sawa. Mbunge wa Marekani Dan Coats alionya kuhusu “mtego wa kuunga mkono ustahimilivu kumbe ni ubaridi.” Ustahimilivu waweza kuongoza kwenye kuwa mtu mwenye akili iliyofunguka; ustahimilivu wa kupita kiasi waweza kuongoza kwenye—ubaridi—kuwa na kichwa kitupu.

      Kwa hiyo, tustahimili nini na tukatae nini? Ni nini iliyo siri ya kupata usawaziko ufaao? Hiyo ndiyo itakayokuwa habari ya makala ifuatayo.

  • Wenye Kubadilikana, Hata Hivyo Wenye Wajibu Kuelekea Viwango vya Kimungu
    Amkeni!—1997 | Januari 22
    • Wenye Kubadilikana, Hata Hivyo Wenye Wajibu Kuelekea Viwango vya Kimungu

      “WATU wastahimilivu si wapumbavu kamwe, na watu wapumbavu si wastahimilivu kamwe,” yasema methali moja ya Kichina. Kuna mengi ya kweli katika methali hii, kwa sababu kuwa mstahimilivu ni jambo gumu, lenye kuhitaji kuwa na wajibu kwa viwango vifaavyo vya mwenendo. Lakini twapaswa kujiwajibisha kwa viwango gani? Je, halingekuwa jambo la akili kufuata viwango vilivyowekwa na Mfanyi wa wanadamu, kama vinavyoelezwa katika Neno lake, Biblia Takatifu? Mungu mwenyewe huweka kielelezo cha kufuata viwango vyake.

      Muumba—Kielelezo Chetu Kikuu

      Mungu Mweza Yote, Yehova, amesawazika kabisa katika ustahimilivu, akionyesha ustahimilivu usio mwingi kupita kiasi wala usio mchache kupita kiasi. Kwa maelfu ya miaka, amestahimili wale wanaoharibia sifa jina lake, wanadamu wafisadi, na wale wanaoitumia dunia vibaya. Mtume Paulo aliandika, kama ilivyorekodiwa kwenye Waroma 9:22, kwamba Mungu “alivumilia kwa ustahimilivu mwingi vyombo vya hasira ya kisasi vilivyofanywa kufaa kwa ajili ya uharibifu.” Kwa nini Mungu amekuwa mstahimilivu kwa muda mrefu hivyo? Kwa sababu ustahimilivu wake una kusudi.

      Mungu ni mwenye subira kuelekea wanadamu “kwa sababu hataki yeyote aangamizwe bali hutaka wote wafikie toba.” (2 Petro 3:9) Muumba amepatia wanadamu Biblia na amepatia watumishi wake utume wa kujulisha kila mahali viwango vyake vya mwenendo. Wakristo wa kweli wanawajibika kwa viwango hivi. Lakini je, hilo lamaanisha kwamba ni lazima watumishi wa Mungu wawe wagumu katika kila hali?

      Wenye Uthabiti, Hata Hivyo Wenye Kubadilikana

      Yesu Kristo alitia moyo wale wanaotafuta uhai wa milele ‘waingie kupitia lango jembamba.’ Lakini kuingia kupitia lango jembamba hakumaanishi kuwa na akili iliyofungika. Ikiwa tuna mwelekeo wa kutawala au kutaka watu wafuate maoni yetu tunapokuwa na wengine, kwa hakika itafanya maisha yawe yenye kufurahisha kwa kila mtu ikiwa tutazuia mwelekeo huu. Lakini jinsi gani?—Mathayo 7:13; 1 Petro 4:15.

      Theofano, mwanafunzi Mgiriki, aliyeeleza kwamba wakati uliotumiwa pamoja na watu wa malezi tofauti-tofauti uliongoza katika kuwafahamu vizuri zaidi, alisema: “Ni jambo la muhimu kwamba tujaribu kuona jinsi wanavyofikiri badala ya kuwalazimisha kufuata njia yetu ya kufikiri.”Kwa hiyo, kwa kupata kumjua mtu vyema zaidi, twaweza kugundua kwamba ladha yake katika chakula na hata lahaja yake si ya ajabu kama tulivyofikiri. Badala ya nyakati zote kuwa na mengi ya kusema kuliko wengine au kusisitiza kusema neno la mwisho, twajifunza mambo yenye mafaa kwa kusikiliza maoni ya mwingine. Kwa hakika, watu wenye akili iliyofunguka hupata maisha yakiwa yenye kuthawabisha sana.

      Wakati wowote upendezi wa kibinafsi unapohusika, twapaswa kuwa wenye kubadilikana na kuruhusu wengine wafurahie chaguo lao wenyewe. Lakini wakati mwenendo ni jambo la utii kwa Muumba wetu, twapaswa kuwa thabiti. Mungu Mweza Yote havumilii aina zote za mwenendo. Alionyesha hili kwa shughuli zake pamoja na watumishi wake wakati uliopita.

      Mtego wa Kuwa Mstahimilivu Kupita Kiasi

      Eli, kuhani mkuu wa taifa la kale la Israeli, alikuwa mtumishi wa Mungu ambaye alinaswa katika mtego wa kuwa mstahimilivu kupita kiasi. Waisraeli walikuwa wameingia katika uhusiano wa kiagano pamoja na Mungu, wakikubali kutii sheria zake. Lakini wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwa wenye pupa na wasio na adili na walikosa staha sana kwa Mweza Yote. Eli, ingawa aliijua vema sana Sheria ya Mungu, alitoa karipio pole tu na alilegea katika kutoa nidhamu. Alifanya kosa la kufikiri kwamba Mungu angestahimili uovu. Muumba hutofautisha udhaifu na uovu. Kwa sababu ya kuasi kimakusudi Sheria ya Mungu, wana waovu wa Eli waliadhibiwa vikali—na ilikuwa hivyo kwa kufaa.—1 Samweli 2:12-17, 22-25; 3:11-14; 4:17.

      Lingekuwa jambo la huzuni kubwa kama nini kwetu kuwa wenye ustahimilivu kupita kiasi katika familia yetu kwa kujifanya hatuoni makosa yenye kurudiwa ya watoto wetu! Ni jambo zuri zaidi kama nini kuwalea “katika nidhamu na rekebisho la akilini la Yehova”! Hili lamaanisha kwamba ni lazima tushikamane na viwango vya kimungu vya mwenendo sisi wenyewe na kuvikaza katika watoto wetu.—Waefeso 6:4.

      Vivyo hivyo, kutaniko la Kikristo haliwezi kustahimili uovu. Ikiwa mshiriki azoea kutenda makosa na kukataa kutubu, ni lazima aondoshwe. (1 Wakorintho 5:9-13) Hata hivyo, nje ya mzingo wa familia na kutaniko, Wakristo wa kweli hawajaribu kubadili jamii kwa ujumla.

      Uhusiano Imara Pamoja na Yehova

      Ukosefu wa ustahimilivu hutokea katika mazingira ya hangaiko. Hata hivyo, ikiwa tuna uhusiano wa karibu pamoja na Mungu, sisi hufurahia hisi ya usalama ambayo hutusaidia kudumisha usawaziko ufaao. “Jina la BWANA ni ngome imara; mwenye haki huikimbilia akawa salama,” ndivyo tusomavyo kwenye Mithali 18:10. Kwa hakika hakuna madhara yawezayo kutupata au kupata wapendwa wetu ambayo Muumba hatayashughulikia kwa wakati wake.

      Mtu aliyenufaika sana kutokana na uhusiano mzuri pamoja na Mungu alikuwa mtume Paulo. Akiwa Myahudi aliyeitwa Sauli, yeye aliwanyanyasa wafuasi wa Yesu Kristo na alikuwa na hatia ya umwagaji wa damu. Lakini Sauli mwenyewe alikuja kuwa Mkristo, na akiwa mtume Paulo, baadaye alieneza evanjeli kwa wakati wote. Paulo alidhihirisha mtazamo wa akili iliyofunguka kwa kuhubiria watu wote, “kwa Wagiriki na kwa Wabaribari pia, kwa wenye hekima na kwa wasio na akili pia.”—Waroma 1:14, 15; Matendo 8:1-3.

      Yeye alifauluje kubadilika? Kwa kupata ujuzi sahihi wa Maandiko na kukua katika upendo kwa Muumba, ambaye hana upendeleo. Paulo alijifunza kwamba Mungu ni mwenye haki katika njia ya kwamba Yeye huhukumu watu wakiwa mtu mmoja-mmoja, si kulingana na utamaduni au jamii, lakini kulingana na kile alicho mtu na anachofanya. Ndiyo, kwa Mungu, matendo ni ya muhimu. Petro alitaja kwamba “Mungu si mwenye ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake.” (Matendo 10:34, 35) Mungu Mweza Yote hana upendeleo. Ni tofauti na viongozi fulani wa ulimwengu, ambao huenda wakatumia ukosefu wa ustahimilivu kimakusudi kwa makusudi yao wenyewe.

      Nyakati Zinabadilika

      Kulingana na John Gray, wa Chuo Kikuu cha Oxford katika Uingereza, ustahimilivu ni “sifa ambayo siku hizi imekuwa nadra sana kupatikana.” Lakini hilo litabadilika. Ustahimilivu uliosawazishwa na hekima ya kimungu utaenea.

      Katika ulimwengu mpya wa Mungu ulio karibu, ukosefu wa ustahimilivu utatoweka. Namna mbaya za ukosefu wa ustahimilivu, kama vile ubaguzi na ushupavu, zitatoweka. Kuwa na akili iliyofungika hakutazuia tena furaha katika maisha. Kisha, kutakuwa na paradiso tukufu sana kuliko yoyote ile ambayo imewezekana kuwapo katika Bonde la Kashmir.—Isaya 65:17, 21-25.

      Je, unatazamia kuishi katika ulimwengu huo mpya? Ni pendeleo lililoje na litafurahisha kama nini!

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki