Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Faida za Kutembelea Majumba ya Ukumbusho
    Amkeni!—2005 | Machi 8
    • Kando ya jengo hilo, kuna jengo lingine la pekee linalowavutia watalii wengi kutoka sehemu zote za ulimwengu. Jengo hilo lilifunguliwa katika mwaka wa 1993. Hilo ni Jumba la Ukumbusho la Maangamizi Makubwa la Marekani.

      Jumba la Ukumbusho la Maangamizi Makubwa

      Jina la jumba hilo, yaani Holocaust, linatokana na neno la Kigiriki linalotumiwa katika Biblia na linalomaanisha toleo zima la kuteketezwa. (Waebrania 10:6) Hata hivyo, kuhusiana na jumba hilo la ukumbusho, neno Holocaust hutumiwa kurejelea “mateso na mauaji ya Wayahudi wa Ulaya yaliyopangwa na kutekelezwa na serikali ya Nazi ya Ujerumani na washiriki wake katika mwaka wa 1933 hadi 1945.” Wayahudi hasa ndio walioshambuliwa, hata hivyo, sera ya serikali ilihusisha kuangamiza makabila mawili ya Wagypsy, yaani Roma na Sinti, kuangamiza wasiojiweza, Wapoland, wafungwa wa vita wa Sovieti, walawiti, Mashahidi wa Yehova, na waasi wa kisiasa.

      Huwezi kuvutiwa na chochote uingiapo katika jumba hilo. Kambi za mateso za Nazi zilikusudiwa kuwatisha watu. Jumba hilo la ukumbusho linaonyesha jinsi hali ilivyokuwa katika kambi hizo. Jumba hilo ni jengo refu linalotisha lililojengwa kwa chuma na matofali nalo hufanana na kiwanda. Ukiwa katika Jumba la Ushahidi, ambalo liko kwenye orofa ya kwanza, unaweza kuona paa ya chuma na kioo iliyo juu ya orofa ya tatu. Broshua moja husema kuwa mtu akitazama juu anaweza kufikiri kwamba vitu vilivyomo “vimepindika, vimekunjamana, na kuegemea upande.” Mhandisi wa jumba hilo alitaka watalii wahisi kwamba “kuna kasoro fulani humo.”

      Jumba hilo la ukumbusho lina orofa tano, lakini watu hutembelea hasa orofa ya pili, ya tatu, na ya nne. Inapendekezwa uanze matembezi yako kwenye orofa ya nne. Huenda ukachukua saa mbili au tatu kutembea katika jumba hilo na huhitaji kuongozwa na mtu. Kwa kuwa kuna picha za kushtua zinazoonyesha jinsi watu walivyonyanyaswa na kuuawa, inapendekezwa watoto walio chini ya umri wa miaka 11 wasitembelee sehemu inayoitwa Permanent Exhibition. Katika orofa ya kwanza, kuna eneo lililotengewa watoto ambalo huitwa Hadithi ya Daniel. Linaonyesha jinsi mtoto aliyeishi huko Ujerumani wakati wa utawala wa Nazi alivyoyaona hayo Maangamizi Makubwa.

      Lifti zinazoenda kwenye orofa ya nne ni kama vyombo baridi vya chuma vinavyotisha. Historia ya Maangamizi Makubwa huonyeshwa kuanzia kwenye orofa hiyo nayo huhusisha “Mashambulizi ya Wanazi” ya mwaka wa 1933 hadi 1939. Ukiwa huko utaona jinsi habari za uwongo ambazo zilienezwa na Wanazi zilivyowaathiri raia wa Ujerumani na kuwaogopesha hasa Wayahudi wa Ujerumani. Kuna nini kwenye orofa ya tatu?

      Kwenye orofa hiyo utaona kichwa hiki chenye kushtua, “Final Solution” (“Suluhisho la Mwisho”)—1940-1945. Kitabu kimoja cha kuwaongoza wageni kinasema kwamba sehemu hiyo “inaonyesha makao ya Wayahudi, uhamisho, kazi ngumu, kambi za mateso, na jinsi ‘Suluhisho la Mwisho’ [kuangamizwa kwa Wayahudi na watu wengine] lilivyotekelezwa kwa kutumia njia mbalimbali kama vile vikosi vya wauaji waliosafiri na kambi za vifo.”

      Orofa ya pili ina kichwa kinachopendeza, yaani, “Last Chapter” (“Sura ya Mwisho”). Inaonyesha historia ya “uokoaji, upinzani, kuwekwa huru, na jitihada za waokokaji za kuanza upya maisha yao.” Kwenye upande mmoja wa orofa hiyo kuna Kituo cha Kujifunzia cha Wexner, kilicho na jambo fulani linalowapendeza Mashahidi wa Yehova. Kwa kutumia kompyuta watalii wanaweza kuchunguza historia ya baadhi ya Mashahidi walioteswa au kuuawa.

      Kwa mfano, unaweza kuchunguza yaliyompata Helene Gotthold, aliyeishi Dortmund, Ujerumani. Mama huyo aliyekuwa na watoto wawili, aliendelea kuhudhuria mikutano ya Kikristo licha ya Wanazi kupiga marufuku mikutano hiyo. Aliuawa kwa kukatwa kichwa mnamo Desemba 1944. Unaweza kuchunguza masimulizi ya watu wengine wengi ambao walinyanyaswa na kuuawa katika kambi za mateso.

      Vilevile katika orofa hiyo kuna Tower of Life (Mnara wa Uhai) ambao pia huitwa Tower of Faces (Mnara wa Nyuso) ambao huinuka hadi kwenye orofa ya nne. Mnara huo hufanyizwa kwa mamia ya picha za Wayahudi walioishi Eishyshok, mji mdogo nchini Lithuania ambao sasa unaitwa Eisiskes. Picha hizo zilipigwa kati ya mwaka wa 1890 na 1941. Hizo ni picha za jamii fulani ya Wayahudi iliyokuwa na ufanisi kwa kipindi cha miaka 900. Katika mwaka wa 1941, kwa siku mbili tu, wauaji wanaosafiri wa kikosi cha SS (Einsatzkommando) waliua jamii hiyo nzima ya Wayahudi! Kulingana na rekodi za serikali ya Nazi, jumla ya Wayahudi 3,446 waliuawa, wakiwemo wanaume 989, wanawake 1,636, na watoto 821. Wanazi waliangamiza jamii nzima.

      Vilevile kwenye orofa ya pili kuna Hall of Remembrance (Jumba la Kumbukumbu), na katika kuta zake za marumaru kuna maandiko fulani ya Biblia, kama vile Kumbukumbu la Torati 30:19 na Mwanzo 4:9, 10. Pia kuna vitu mbalimbali vinavyoonyesha kwamba Mashahidi wa Yehova waliteswa kama vile pembe tatu ya rangi ya zambarau ambayo walihitaji kuwa nayo ili kuwatambulisha. Ukiwa makini utaona vitu hivyo unapotembea. Kuna vitu vingi unavyoweza kuchunguza kutia ndani sehemu kubwa ya kufanya utafiti iliyo kwenye orofa ya tano.

      Moyo wako utatulia ukitoka nje ya jumba hilo la ukumbusho. Hebu sasa tutembelee jumba jipya zaidi kati ya majumba ya ukumbusho ya Washington. Jumba hilo linatukumbusha jambo tofauti sana na pia jitihada ya kuangamiza jamii nzima.

  • Faida za Kutembelea Majumba ya Ukumbusho
    Amkeni!—2005 | Machi 8
    • [Picha katika ukurasa wa 16]

      Mnara wa Uhai una orofa tatu

      [Picha katika ukurasa wa 16]

      Mavazi ya kambi ya mateso yaliyovaliwa na Shahidi wa Yehova

      [Picha katika ukurasa wa 17]

      Jumba la Ukumbusho la Maangamizi Makubwa la Marekani

      [Picha katika ukurasa wa 17]

      Helene Gotthold

      [Hisani]

      USHMM, courtesy of Martin Tillmans

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki