Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kile Ambacho Nadharia ya Mshindo Mkubwa Hueleza—Na Kile Ambacho Haielezi
    Amkeni!—1996 | Januari 22
    • Ulimwengu Wote Mzima Wenye Kutisha

      Kile Ambacho Nadharia ya Mshindo Mkubwa Hueleza—Na Kile Ambacho Haielezi

      KILA asubuhi ni muujiza. Ndani kabisa katika jua la asubuhi, hidrojeni inayeyushwa kuwa heli katika halijoto ya mamilioni ya digrii. Miali-X na miali-gama ambayo ni yenye nguvu sana inamiminika kutoka kitovu cha jua hadi kwenye tabaka za jua zinazolizingira. Jua lingelikuwa lenye wangavu, miali hii ingelipasua ikiwa na joto jingi hadi kwenye sehemu ya nje ya jua kwa sekunde chache. Badala ya hivyo, huanza kuruka-ruka kutoka atomu zilizofungwa kwa uthabiti hadi atomu za “uhami” wa jua, pole pole zikipoteza nishati. Siku, majuma, karne nyingi, hupita. Maelfu ya miaka baadaye, unururishi huo ambao wakati mmoja ulikuwa hatari hatimaye huibuka kwenye sehemu ya nje ya jua ukiwa nuru nyanana ya manjano yenye kuburudisha—ikiwa haidhuru tena bali ikifaa kwa ajili ya kupasha joto dunia kwa ujoto wayo.

      Kila usiku ni muujiza pia. Jua nyinginezo hutumwekea-mwekea zikivuka anga pana ya galaksi yetu. Zina ushelabela wa marangi, saizi, halijoto, na mikondo mbalimbali. Nyingine ni kubwa mno hivi kwamba ikiwa moja lingekuwa mahali pa jua letu, kile kingebaki kwa sayari yetu kingekuwa ndani ya nyota hiyo kubwa mno. Jua nyinginezo ni ndogo mno, vijinyota vyeupe hivi—vidogo kuliko dunia yetu, lakini vyenye uzito wa jua letu. Nyingine huchipua mwendo kwa amani kwa mabilioni ya miaka. Nyingine zaelekea kwenye ukingo wa milipuko ya supanova ambao utaziharibu, kwa kipindi kifupi zikiangaza kuliko galaksi zote.

      Watu wa kikale walisimulia kuhusu madubwana wa baharini na miungu yenye kupigana, kuhusu majoka na makasa na ndovu, kuhusu maua ya yungiyungi na miungu yenye kuota ndoto. Baadaye, wakati wa ile iliyoitwa Enzi ya Kusababu, miungu ilitupiliwa mbali na “ulozi” mpya wa kanuni za kalkula na Newton. Sasa twaishi katika enzi ambayo haina ushairi na hekaya za kale. Watoto wa enzi ya leo ya atomu wamechagua kama kigezo chao cha uumbaji, si dubwana wa kale wa baharini, si “mashine” ya Newton, bali ile ishara yenye kunasa mno ya karne ya 20—bomu la atomu. “Muumba” wao ni mlipuko fulani. Wao huuita mlipuko wao wa ulimwengu wote mzima, mshindo mkubwa.

      Kile Ambacho Mshindo Mkubwa “Hueleza”

      Fasiri iliyo maarufu sana ya mtazamo wa kizazi hiki kuhusu uumbaji hutaarifu kwamba miaka ipatayo bilioni 15 hadi 20 iliyopita, ulimwengu wote mzima haukuwapo, wala utupu wa anga. Hakukuwa na wakati, hakukuwa na mata—hakuna chochote ila uzito mdogo, sehemu ndogo mno iitwayo umosi, ambayo ililipuka kuwa ulimwengu wote mzima wa sasa. Mlipuko huo ulitia ndani kipindi kifupi katika sehemu ndogo ya sekunde wakati ulimwengu wote mzima mchanga ulipanuka, au kutanuka, kwa kasi mno kuliko mwendo wa nuru.

      Wakati wa dakika chache za kwanza za mshindo mkubwa, uyeyunganishaji wa kinyukilia ulitukia kwa mweneo wa ulimwengu wote mzima, hilo likisababisha vile vipimo vya sasa vya ukolevu wa hidrojeni na heli na angalau sehemu ya lithi katika uvukwe wa anga za kinyota. Labda baada ya miaka 300,000, joto lenye kuenea kote katika ulimwengu wote mzima lilipungua kuliko joto la uso wa jua, likiruhusu elektroni kutulia kwenye mizunguko kuzunguka atomu na kuachilia mmweko wa photoni, au nuru. Mmweko huo wa awali waweza kupimwa leo, hata ingawa umepoa mno, kwa unururishi wa awali wa ulimwengu wote mzima kwenye kasimawimbi ya kijiwimbi ulinganao na halijoto la Kelvini 2.7.a Kwa hakika, ilikuwa ni uvumbuzi wa unururishi huu wa awali katika miaka ya 1964-1965 ambao ulisadikisha wanasayansi wengi kwamba kulikuwa na ukweli fulani kuhusu nadharia ya mshindo mkubwa. Hiyo nadharia pia hudai kueleza kwa nini ulimwengu wote mzima huonekana kupanuka kuelekea pande zote, magalaksi ya mbali yakionekana kutukimbia au kukimbizana kwa mwendo wa kasi mno.

      Kwa kuwa nadharia ya mshindo mkubwa huonekana kueleza mambo mengi sana, kwa nini tuitilie shaka? Kwa kuwa pia kuna mengi ambayo haielezi. Kutolea kielezi: Mwastronomia wa kale Tolemi alikuwa na nadharia kwamba jua na sayari zilizunguka dunia katika miviringo mikubwa, zikifanyiza miviringo midogo kwa wakati uleule, iitwayo vijiviringo. Hiyo nadharia ilionekana kueleza mwendo wa sayari. Kadiri waastronomia kwa karne nyingi walivyokusanya habari zaidi, wanaanga wa Kitolemi sikuzote wangeweza kuongezea vijiviringo vya ziada kwenye vile vijiviringo vingine vyao na “kueleza” hiyo habari mpya. Lakini hilo halikumaanisha kwamba hiyo nadharia ilikuwa sahihi. Mwishowe kulikuwa na habari nyingi mno zilizohitaji kufafanuliwa, na nadharia nyinginezo, kama vile maoni ya Copernicus kwamba dunia ilizunguka jua, zilieleza mambo vizuri zaidi na kwa usahili zaidi. Leo ni vigumu kupata mwastronomia anayefuata nadharia ya Tolemi!

      Profesa Fred Hoyle alifananisha jitihada za wanaanga wa Kitolemi za kujaribu kuunga upya nadharia yao iliyosambaratishwa na mavumbuzi mapya na zile jitihada za waamini wa mshindo mkubwa leo za kuweza kuidumisha nadharia yao. Yeye aliandika katika kitabu chake The Intelligent Universe: “Jitihada kubwa za wachunguzi zimekuwa kuficha migongano katika nadharia ya mshindo mkubwa, ili kujenga oni fulani ambalo limekuwa tata zaidi na lenye kulemea.” Baada ya kurejezea utumizi usiofaulu wa vijiviringo vya Tolemi ili kuokoa nadharia yake, Hoyle aliendelea: “Sisiti-siti kusema kwamba kwa sababu ya hayo, wingu jeusi laning’inia juu ya nadharia ya mshindo mkubwa. Kama nilivyotaja awali, wakati kigezo cha kweli kinapoelekezwa dhidi ya nadharia, kwa kawaida si rahisi hiyo ipone.”—Ukurasa 186.

      Gazeti la New Scientist, la Desemba 22/29, 1990, lilirudia maoni kama hayo: “Mbinu ya Tolemi imetumiwa mno kwa . . . kiolezo cha kianga cha mshindo mkubwa.” Kisha makala hiyo yauliza: “Twaweza kupataje maendeleo halisi katika fizikia ya nishati na sayansi ya anga? . . . Ni lazima tuwe wanyoofu na kusema waziwazi zaidi kuhusu uhalisi wa makisio ya baadhi ya mengi ya madhanio yetu tuyahaziniyo.” Uchunguzi mpya sasa wamiminika.

      Maswali Ambayo Mshindo Mkubwa Haujibu

      Ugumu mkuu kwa mshindo mkubwa umetokana na wachunguliaji wakitumia lenzi zilizosahihishwa za Darubiniupeo ya Angani ya Hubble kupima umbali wa magalaksi mengineo. Hiyo habari mpya inawatia hofu wananadharia!

      Mwastronomia Wendy Freedman na wengine hivi majuzi walitumia Darubiniupeo ya Angani ya Hubble kupima umbali wa galaksi katika jamii ya nyota ya Mashuke, na kipimo chake chadokeza kwamba ulimwengu wote mzima unapanuka kwa kasi zaidi, na hivyo ni mchanga zaidi, kuliko ilivyodhaniwa hapo awali. Kwa hakika, hiyo “yaonyesha umri wa ulimwengu wote mzima kuwa mchanga kufikia miaka bilioni nane,” likaripoti gazeti Scientific American Juni uliopita tu. Ingawa miaka bilioni nane yasikika kuwa wakati mrefu sana, ni karibu nusu tu ya umri wa sasa uliokadiriwa wa ulimwengu wote mzima. Hili husababisha tatizo maalumu, kwani, kama hiyo ripoti inavyoendelea kusema, “habari nyinginezo huonyesha kwamba nyota fulani zina umri wa angalau miaka bilioni 14.” Makadirio ya Freedman yakithibitika kuwa kweli, nyota hizo za kale mno zitakuwa na umri mkubwa zaidi kupita mshindo mkubwa wenyewe!

      Tatizo jingine bado la mshindo mkubwa limetokana na uthibitisho wenye kuongezeka kwa haraka wa “utupu-tupu” katika ulimwengu wote mzima ambao una ukubwa na miaka-nuru bilioni 100, ukiwa na magalaksi kwenye upande wa nje na utupu wa ndani. Margaret Geller, John Huchra, na wengineo kwenye Kitovu cha Astrofizikia katika Harvard-Smithsonian wamepata kile wanachokiita ukuta mkubwa wa magalaksi wenye urefu upatao miaka-nuru milioni 500 kuvuka anga la kaskazini. Kikundi kingine cha waastronomia, ambacho kilikuja kuitwa Seven Samurai, kimepata uthibitisho wa mkusanyo tofauti ya kianga, ambao wanauita Mvutani Mkuu, ambao uko karibu na kilimia cha kusini cha Hydra na Centaurus. Waastronomia Marc Postman na Tod Lauer waamini kwamba ni lazima kuna kitu fulani kikubwa zaidi kilichoko mbele ya kilimia cha Orioni, kinachosababisha mamia ya magalaksi, kutia ndani na yetu, kufuliza kuelekea upande huo kama vyelezo kwenye “mto angani.”

      Muundo huu wote wamakisha. Wanasayansi wa anga wasema huo mlipuko kutoka kwa mshindo mkubwa ulikuwa mwanana mno na wenye kufululiza, ikitegemea unururishi ambao hudaiwa ulisalia nyuma. Mwanzo mwanana kama huo ungeweza kufuatishaje muundo mkubwa na tata kama huo? “Uvumbuzi mpya wa hivi majuzi wa kuta na vivutaji ulizidisha hilo fumbo la jinsi muundo mkubwa kama huo ungetokea mnamo umri wa miaka bilioni 15 wa ulimwengu wote mzima,” lakiri Scientific American—tatizo ambalo huzidi kuwa baya Freedman na wengineo wanapopunguza zaidi umri uliokadiriwa wa ulimwengu wote mzima.

      “Tunakosa Visababishi Fulani vya Kimsingi”

      Ramani za Geller zenye mipanuko mitatu ya maelfu ya mkusanyo wa kigalaksi, uliofungamana pamoja, kupitana-pitana, na wenye kuenea imebadili jinsi wanasayansi wanavyouona ulimwengu wote. Yeye hajifanyi kuelewa kile akionacho. Uvutano pekee huonekana kutoweza kueleza chanzo cha ule ukuta wake mkubwa. “Angalabu mimi huhisi tunakosa visababishi fulani vya msingi katika jaribio letu la kufahamu muundo huu,” yeye akiri.

      Geller aliongezea hivi kuhusu mashaka yake: “Kwa wazi hatujui jinsi ya kueleza miundo mikubwa katika muktadha wa Mshindo Mkubwa.” Mafasiri ya muundo wa kianga kwa msingi wa uchoraji wa sasa wa mbingu uko mbali na kuwa hakika—ni kama vile kujaribu kuchora ramani ya ulimwengu wote kwa kutegemea habari kidogo sana. Geller akaendelea: “Siku moja huenda tutagundua kwamba hatukuwa tukieleza mambo kwa njia ifaayo, na tukifanya hivyo, hiyo itakuwa dhahiri sana hivi kwamba tutashangaa kwa nini hatukuwa tumefikiria hilo mapema zaidi.”

      Hilo laongoza kwenye swali lililo kubwa kuliko yote: Ni nini kinachofikiriwa kuwa kilisababisha mshindo mkubwa wenyewe? Si mwingine ila Andrei Linde, mmoja wa waanzilishi wa fasiri tutumuvu ya nadharia ya mshindo mkubwa, akiriye waziwazi kwamba nadharia ya mshindo mkubwa haijibu maswali haya ya msingi. “Tatizo la kwanza, na lililo muhimu, ni kule kuwapo kwa mshindo mkubwa,” yeye asema. “Mmoja huenda akauliza, Ni nini kilitokea kwanza? Ikiwa wakati-anga haukuwapo, kila kitu kingewezaje kutokea kutoka kwa utupu? . . . Kuelezea umosi huu wa mwanzoni—mahali na wakati ulipoanza—bado hubaki likiwa tatizo lisiloweza kutatuliwa la taaluma ya anga ya kisasa.”

      Makala fulani katika gazeti Discover hivi majuzi ilifikia mkataa kwamba “hakuna mwanaanga mwenye kusababu angedai kwamba Mshindo Mkubwa ndiyo nadharia pekee katika huo msururu.”

      Sasa acheni tutoke nje na tutafakari umaridadi na fumbo la dari ya kinyota.

      [Maelezo ya Chini]

      a Kelvini ni kizio cha kupima halijoto ambacho digrii zacho ni sawa na digrii kwenye kipimio cha halijoto cha Selsiasi, isipokuwa kwamba kipimio cha Kelvini huanzia sufuri kamili, yaani 0 K.—ulingano wa digrii -273.16 Selsiasi. Maji huganda kwenye 273.16 K. na huchemka kwenye 373.16 K.

      [Sanduku katika ukurasa wa5]

      Miaka-Nuru—Timazi ya Kianga

      Ulimwengu wote mzima ni mkubwa hivi kwamba kuupima kwa maili au kilometa ni kama kupima umbali kutoka London hadi Tokyo kwa mikrometa. Kizio kifaacho zaidi cha kupima ni miaka-nuru, umbali ambao nuru husafiri kwa mwaka, au kilometa 9,460,000,000,000 hivi. Kwa sababu nuru ndiyo kitu chenye mwendo wa kasi mno katika ulimwengu wote mzima na huhitaji sekunde 1.3 tu kusafiri hadi mwezini na karibu dakika 8 hivi hadi kwenye jua, mwaka-nuru ungeonekana kuwa mkubwa kweli!

  • Wa Kifumbo, na Bado ni Maridadi Mno
    Amkeni!—1996 | Januari 22
    • Ulimwengu Wote Mzima Wenye Kutisha

      Wa Kifumbo, na Bado ni Maridadi Mno

      WAKATI huu mwakani, anga la usiku huvutia kwa ufahari wenye kujaa johari. Juu kabisa Orioni kakamavu yachapua mwendo, ikionekana kwa urahisi mnamo jioni za Januari kutoka Anchorage, Alaska, hadi Cape Town, Afrika Kusini. Je, hivi majuzi umepata kuchungulia hazina za anga zipatikanazo katika vilimia maarufu, kama vile Orioni? Waastronomia walichungulia si kitambo sana wakitumia Darubiniupeo ya Angani ya Hubble iliyorekebishwa hivi majuzi.

      Kutoka kwa nyota tatu za ukanda wa Orioni waning’inia upanga wayo. Nyota yenye mwangaza mwangavu katikati ya hicho kisu si nyota halisi kamwe bali ni Orioni Nebula iliyo mashuhuri, kitu chenye umaridadi wenye kuvutia hata kitazamwapo kwa darubiniupeo ndogo. Hata hivyo, wangavu wayo wa kianga, si sababu ya uvutio wacho kwa waastronomia wa kitaaluma.

      “Waastronomia huchunguza Orioni Nebula pamoja na nyota zayo nyingi changa kwa sababu ndilo eneo kubwa zaidi na lenye kutokeza zaidi nyota katika sehemu yetu ya Galaksi,” aripoti Jean-Pierre Caillault katika gazeti Astronomy. Nebula yaonekana kuwa chumba cha kuzalishia cha angani! Darubiniupeo ya Hubble ilipopiga picha Orioni Nebula, ikinasa mambo ya kindani ambayo hayakuwa yamepata kuonekana awali, waastronomia waliona si nyota na gesi zenye kuwaka tu bali kile Caillault alikifafanua kuwa “miviringo-yai midogo myangavu yenye alama kama nyuzinyuzi za rangi ya machungwa. Zafanana na vimego vya chakula cha mchana vilivyoanguka kiaksidenti kwenye picha.” Hata hivyo, wanasayansi wanaamini kwamba, badala ya kasoro za ukiwi, miviringo-yai hii ya nyuzinyuzi ni “chimbuko la diski za kisayari, mifumo ya jua ya kwanza ikiwa katika harakati za kutengenezwa ikionekana kutoka umbali wa miaka-nuru 1,500.” Je, nyota—kwa kweli, mifumo mizima ya jua—inazaliwa kwenye pindi hii katika Orioni Nebula? Waastronomia wengi huamini hufanya hivyo.

      Kutoka Chumba cha Kuzalishia Hadi Ziara la Nyota

      Kadiri Orioni anavyochipua mwendo kuelekea mbele, uta mkononi, yuaonekana kukabili kilimia cha Ng’ombe, yule fahali. Darubiniupeo ndogo itafunua, karibu na ncha ya pembe ya kusini ya fahali, kizio chenye nuru iliyofifia. Hicho chaitwa Kaa Nebula, na katika darubiniupeo kubwa, hicho chaonekana kama mlipuko unaoendelea, kama inavyoonyeshwa kwenye ukurasa 9. Ikiwa Orioni Nebula ni mahali pa kuzalia nyota, basi Kaa Nebula iliyo karibu tu huenda ikawa ziara la nyota yenye kupatwa na kifo kutokana na jeuri isiyowazika.

      Huo msiba wa kimbingu huenda ulipata kurekodiwa na waastronomia Wachina ambao walifafanua “Nyota Ngeni” katika Ng’ombe ambayo ilitokea kwa ghafula mnamo Julai 4, 1054, nayo ikang’aa kwa wangavu sana hivi kwamba ilionekana wakati wa mchana kwa siku 23. “Kwa majuma kadhaa,” akaonelea Robert Burnham, “hiyo nyota iliangaza kwa nuru ya jua zipatazo milioni 400.” Wanasayansi huita ujiuaji kimakusudi wa nyota ulio dhahiri kama huo supanova. Hata sasa, karibu miaka elfu moja baada ya kuonekana huko, vilipukaji kutoka kwa mlipuko huo vyazangaa angani kwa mwendo ukadiriwao kuwa kilometa milioni 80 kwa siku.

      Darubiniupeo ya Angani ya Hubble imekuwa ikichunguza nyanja hii pia, ikipekua ndani ya kitovu cha nebula na kuvumbua “mambo ya kindani katika Kaa ambayo waastronomia hawakutazamia kamwe,” kulingana na gazeti Astronomy. Mwastronomia Paul Scowen asema hayo mavumbuzi “lazima yatawafanya waastronomia wa kinadharia wafikirie sana kwa miaka mingi ijayo.”

      Waastronomia, kama vile Robert Kirshner wa Harvard, waamini kwamba kuelewa masalio ya supanova kama vile Kaa Nebula ni muhimu kwa sababu yaweza kutumiwa kupima umbali wa magalaksi mengineyo, ambayo sasa ni nyanja ya kufanyiwa utafiti sana. Kama tulivyoona, kutokubaliana juu ya umbali hadi magalaksi mengineyo hivi majuzi kumewasha mijadala mikali juu ya nadharia ya mshindo mkubwa kuhusu uumbaji wa ulimwengu wote mzima.

      Kuvuka Ng’ombe, lakini bado wenye kuonekana katika Nusu-Kizio cha Kaskazini katika anga la magharibi la Januari, ni wangavu mwanana wa kilimia cha Andromeda. Wangavu huo ni galaksi ya Andromeda, kitu kilicho mbali zaidi kiwezacho kuonekana kwa macho matupu. Maajabu ya Orioni na Ng’ombe yako katika ujirani wa ulimwengu wetu mzima—mnamo maelfu machache ya miaka-nuru kutoka Duniani. Hata hivyo, sasa twaangaza macho kuvuka miaka-nuru ikadiriwayo kuwa milioni mbili kwenye mvururo mkubwa wa nyota zikaribiazo kufanana na galaksi yetu, Njia ya Kimaziwa, lakini zilizo kubwa hata zaidi—miaka-nuru ipatayo 180,000 kuvuka. Kadiri unapotazama huo wangavu mwanana wa Andromeda, macho yako yaangazwa na nuru ambayo huenda ikawa ina umri wa zaidi ya miaka milioni mbili!

      Katika miaka ya hivi majuzi Margaret Geller na wengine wameanza programu kabambe ili kuchora ramani za galaksi zote zinazozunguka kwa mipanuko mitatu, na matokeo yametokeza maswali mazito kuhusu nadharia ya mshindo mkubwa. Badala ya kuona msambao mwanana wa magalaksi katika sehemu zote, wachora-ramani wa ulimwengu wote mzima walivumbua “utata wa kiusanii wa magalaksi” katika miundo ieneayo kwa mamilioni ya miaka-nuru. “Jinsi utata huo wa usanii ulivyofumwa kutoka kwa mata inayoelekea kufanana ya ulimwengu wote mzima uliozaliwa hivi ni moja ya maswali yenye kusumbua kichwa sana katika taaluma ya kianga,” kulingana na ripoti ya hivi majuzi katika jarida Science lenye kutambuliwa.

      Tulianza jioni hii kwa kutazama anga letu la usiku wa Januari na mara tukavumbua si tu umaridadi wenye kutwesha bali pia maswali na mambo yasiyoelezeka yanayohusiana na asili halisi na mwanzo wa ulimwengu wote mzima. Ulianzaje? Ulifikiaje hali yawo ya sasa ambayo ni tata? Ni nini kitapata maajabu ya kianga yanayotuzunguka? Je, kuna yeyote awezaye kusema? Acheni tuone.

      [Sanduku katika ukurasa wa8]

      Wanajuaje Ni Umbali Kiasi Gani?

      Waastronomia wanapotuambia kwamba galaksi ya Andromeda iko umbali wa miaka-nuru milioni mbili, kwa hakika wao hutupa kadirio la mawazio ya kisasa. Hakuna yeyote ambaye amepata kutokeza njia ya kupima moja kwa moja umbali kama huo wenye kutatanisha akili. Umbali kwenye nyota zilizoko karibu sana, zile ziko mnamo miaka-nuru 200 au kitu kama hicho, zaweza kupimwa moja kwa moja kupitia mlinganisho wa nyota, ambao huhusisha hesabu ya trigonomia sahili. Lakini hili hutumika kwa nyota ambazo ziko karibu sana na dunia zinazoonekana kusogea kidogo kadiri dunia inapozunguka jua. Nyota nyingi, na magalaksi yote, yako mbali zaidi. Tunapofikia umbali huo makisio huanza. Hata nyota zilizoko ujiranini, kama vile Betelgeuse kubwa mno na iliyo nyekundu katika Orioni, ni kazi ya makisio, ikiwa na umbali unaokisiwa kutoka miaka-nuru 300 hadi zaidi ya 1,000. Hivyo basi, haipasi kutushangaza kupata kutokubaliana miongoni mwa waastronomia kuhusu umbali wa magalaksi, ambao ni mara milioni mbali zaidi.

      [Sanduku katika ukurasa wa8]

      Supanova, Pulsa, na Mashimo Meusi

      Katika kitovu cha Kaa Nebula mna mojapo kitu cha ajabu kupita zote katika ulimwengu wote mzima unaojulikana. Kulingana na wanasayansi, kijizoga cha nyota iliyokufa, kikiwa kimebanwa ndani ya uzito usioaminika, huvurura katika kaburi lacho mara 30 kwa sekunde, kikitoa kasimawimbi za redio ambazo mara ya kwanza zilinaswa duniani katika 1968. Hicho huitwa pulsa, hufafanuliwa kuwa salio la supanova lenye kuvurura lililobanwa hivi kwamba elektroni na protoni katika atomu za nyota ya awali zimebanwa pamoja ili kutokeza nutroni. Wanasayansi husema kwamba wakati mmoja ilikuwa kiini kikubwa cha nyota kubwa mno kama ile ya Betelgeuse au Rigel katika Orioni. Hiyo nyota ilipolipuka na tabaka za nje kulipuliwa angani, ni kiini tu kilichobonyea ndicho tu kilibaki, kikiwa masao mangavu meupe, mioto yacho ya kinyukilia ilizima kitambo sana.

      Ebu wazia kuchukua nyota yenye ukubwa wa mawili ya majua yetu na kuibana ndani ya tufe lenye kipenyo cha kilometa 15 hadi 20! Ebu wazia kuchukua sayari Dunia na kuibana ndani ya meta 120. Sentimeta 16 mara tatu ya mata hii zingekuwa na uzito wa zaidi ya tani bilioni 16.

      Hata ufafanuzi huu hauonekani kuwa kamili juu ya mata iliyobanwa. Ikiwa tungeifanya dunia kuwa ndogo kama gololi, nguvu za uvutano za dunia hatimaye zingekuwa zenye nguvu sana hivi kwamba hakuna hata nuru ambayo ingeweza kuponyoka. Kufikia hapa dunia yetu ndogo ingeonekana kupotelea ndani ya kile kinachoitwa shimo jeusi. Ingawa waastronomia wengi huamini yapo, mashimo meusi bado hayajathibitishwa kuwapo, na hayaonekani kuwa ya ukawaida kama yalivyofikiriwa miaka michache iliyopita.

      [Sanduku katika ukurasa wa 10]

      Je, Rangi Hizo Ni Halisi?

      Watu ambao huchungua anga kwa kutumia darubiniupeo ndogo mara nyingi huhisi kutamauka mara ya kwanza wanapoona galaksi au nebula fulani maarufu. Ziko wapi zile rangi maridadi ambazo wameona katika picha? “Rangi za magalaksi haziwezi kuonekana kwa macho ya kibinadamu moja kwa moja, hata kwa kutumia darubiniupeo kubwa kuliko zote zilizopo,” aonelea mwastronomia na mwandikaji wa sayansi Timothy Ferris, “kwa kuwa nuru yazo imefifia sana kuweza kuchochea vipokezi rangi vya retina.” Hili limesababisha watu wengine kufikia mkataa kwamba rangi maridadi zinazoonekana katika picha za kiastronomia si halisi, zimeongezwa tu kwa njia fulani katika utokezaji wa picha. Hata hivyo, hiyo si kweli. “Rangi zenyewe ni halisi,” aandika Ferris, “na hizo picha huonyesha jitihada bora zaidi za waastronomia ya kuzitokeza upya kwa usahihi.”

      Katika kitabu chake Galaxies, Ferris aeleza kwamba hizo picha za vitu vya mbali vilivyofifia, kama magalaksi na zilizo nebula nyingi, “hutokana na kanda zilizolengwa kwa muda, zikipatikana kwa kuilenga darubiniupeo kwenye galaksi fulani na kuyafunua mabamba ya kipicha kwa saa kadhaa huku mwanga wa nyota ukinywelea ndani ya uoevu wa kipicha. Katika wakati huu mtambo wenye kujiendesha wasawazisha mzunguko wa dunia na kuweka darubiniupeo ikiwa imeelekezwa kwenye galaksi, huku waastronomia, ama katika hali nyinginezo mfumo fulani wa kuelekeza moja kwa moja, ukisawazisha kasoro ndogo sana.”

  • ‘Kitu Fulani Kinakosekana’—Kipi?
    Amkeni!—1996 | Januari 22
    • Ulimwengu Wote Mzima Wenye Kutisha

      ‘Kitu Fulani Kinakosekana’—Kipi?

      BAADA ya kuangaza macho kwenye nyota wakati wa usiku uliotakata, wenye giza, twarudi ndani ya nyumba, tukihisi baridi na macho yakiwa yanapepesa-pepesa, akili zetu zikitatanishwa na umaridadi mwingi na maswali chungu nzima. Kwa nini ulimwengu wote mzima upo? Huo ulitoka wapi? Huo waelekea wapi? Haya ndiyo maswali ambayo wengi hujaribu kujibu.

      Baada ya miaka mitano ya kufanya utafiti katika taaluma ya anga, ambayo ilimchukua kwenye makongamano ya kisayansi na vituo vya utafiti tufeni pote, mwandikaji wa sayansi Dennis Overbye alifafanua mazungumzo yake pamoja na mwanafizikia maarufu sana ulimwenguni Stephen Hawking hivi: “Hatimaye kile nilichotaka kujua kutoka kwa Hawking ni kile ambacho sikuzote nilitaka kujua kutoka kwa Hawking: Mahali ambapo sisi huenda tunapokufa.”

      Ingawa maneno hayo ni ya kukejeli, maneno haya hufunua mengi kuhusu enzi yetu. Maswali hayawi mengi sana kuhusu nyota zenyewe na nadharia na maoni yenye kupingana ya wanaanga ambao huzichungua. Watu leo bado wana tamaa ya kupata majibu ya maswali ya msingi ambayo yamesumbua wanadamu kwa mileani nyingi: Kwa nini tuko hapa? Je, kuna Mungu? Sisi huenda wapi tunapokufa? Majibu ya maswali haya yako wapi? Je, yatapatikana katika nyota?

      Mwandikaji mwingine wa sayansi, John Boslough, alionelea kwamba kwa kuwa watu wameacha dini, wanasayansi kama wanaanga wamekuja kuwa “makuhani kamili wa enzi ya kilimwengu. Wanasayansi, na si viongozi wa kidini, ndio ambao wangefunua siri zote za ulimwengu wote mzima hatua kwa hatua, si kwa mfanyizo wa ghafula wa kiroho bali katika aina ya milinganyo iliyofichika kwa wote isipokuwa kwa wateule.” Lakini je, watafunua siri zote za ulimwengu wote mzima na kujibu maswali yote ambayo yamesumbua wanadamu kwa enzi nyingi?

      Wanaanga wanafunua nini sasa? Wengi huunga mkono ile fasiri ya “theolojia” ya mshindo mkubwa, ambayo imekuwa dini ya kilimwengu ya wakati wetu, hata wanapobishana daima juu ya vijambo. “Hata hivyo,” Boslough akaonelea, “katika muktadha wa uchunguzi mpya na wenye kujipinga, nadharia ya mshindo mkubwa inaanza kuonekana kwa ubayana zaidi kuwa yafanana sana na ufafanuzi sahili ambao inatafuta kupatanisha maelezo ya uumbaji. Kufikia mapema katika miaka ya 1990 nadharia ya mshindo mkubwa ilikuwa . . . ikiendelea kushindwa kujibu mengi ya maswali ya msingi.” Yeye aliongezea kwamba “wananadharia wengi wametoa hoja kwamba hiyo haitaweza hata kudumu hadi mwishoni mwa miaka ya 1990.”

      Labda baadhi ya makisio ya sasa ya kianga yatakuja kuwa sahihi, labda sivyo—kama vile labda kuna sayari hasa zinazoibuka katika kilimia cha Orioni nebula, labda sivyo. Ukweli usiobishaniwa ni kwamba hakuna yeyote katika dunia hii kwa hakika anajua. Lakini kuna nadharia nyingi zinatokezwa, lakini watazamaji wenye unyoofu warudia ule uchunguzi wenye saburi wa Margaret Geller kwamba licha ya mazungumzo ya kijuu-juu, kitu fulani cha kimsingi chaonekana kinakosekana katika uelewevu wa sasa wa wanaanga.

      Wakosekana—Ule Utayari wa Kukubali Mambo ya Hakika

      Wanasayansi wengi—na hawa watia ndani wanaanga wengi—hupendelea nadharia ya mageuzi. Wao huona vigumu kukubali mazungumzo yanayoupa fungu weledi na kusudi katika uumbaji, nao hunyarafika Mungu atajwapo kuwa Muumba. Wao hukataa hata kutafakari uzushi kama huo. Zaburi 10:4 husema kwa kukashifu kuhusu mtu mwenye kujitutumua ambaye ‘hatafuti, jumla ya mawazo yake ni, hakuna Mungu.’ Mungu wake aliyejiumbia ni Nasibu. Lakini ujuzi unapoongezeka na nasibu na pia sadfa kuporomoka kwa uthibitisho wenye kuongezeka, wanasayansi huanza kugeukia zaidi na zaidi miiko yao kama weledi na usanii. Ebu fikiria vielelezo vifuatavyo:

      “Kijenzi fulani kwa wazi kimekuwa kikikosa katika machunguo ya kianga. Chimbuko la Ulimwengu Wote Mzima, kama vile suluhisho la kyubu ya Rubik, chahitaji weledi fulani,” akaandika mwastrofizikia Fred Hoyle katika kitabu chake The Intelligent Universe, ukurasa 189.

      “Kadiri ninavyochungua ulimwengu wote mzima na kuchunguza vijambo vidogo-vidogo vya ufundi wao, ndivyo ninavyopata uthibitisho zaidi kwamba ulimwengu wote mzima kwa njia fulani lazima ulijua kuhusu kuja kuwapo kwetu.”—Disturbing the Universe, kilichoandikwa na Freeman Dyson, ukurasa 250.

      “Ni sehemu zipi za Ulimwengu Wote Mzima zilizokuwa muhimu katika kutokea kwa viumbe kama sisi, na je, ilikuwa ni kupitia sadfa, au kupitia sababu isiyojulikana, kwamba Ulimwengu Wote Mzima wetu una sehemu hizi? . . . Je, kuna mipangilio fulani ya kina zaidi ambayo huhakikisha kwamba Ulimwengu Wote Mzima uliumbwa kwa ajili ya jamii ya kibinadamu?”—Cosmic Coincidences, kilichoandikwa na John Gribbin na Martin Rees, kurasa 14, 4.

      Fred Hoyle pia aeleza juu ya tabia hizi kwenye ukurasa 220 wa kitabu chake kilichonukuliwa hapo juu: “Tabia hizo zaonekana kuingiliana na ulimwengu wa asili kama mfanyizo wa aksidenti zenye kufurahisha. Lakini kuna nyingi ya hizi sadfa zinazohusu maisha zenye kuhitaji maelezo fulani ili kuzifafanua.”

      “Si kwamba tu mwanadamu amebadilishwa ili kufaa ulimwengu wote mzima. Ulimwengu mzima umebadilishwa ili kufaa mwanadamu. Ebu wazia ulimwengu wote mzima ambao katika huo moja au nyingineyo ya vima visivyobadilika vya msingi vya fizikia vyabadilishwa kwa asilimia ndogo kwa njia moja au nyingine? Mwanadamu hangeweza kamwe kuishi ndani ya ulimwengu wote mzima kama huo. Hicho ndicho kiini hasa cha kanuni ya mahusiano ya kuishi kwa binadamu. Kulingana na kanuni hii, kisababishi chenye kupatia uhai ni chimbuko la utaratibu mzima na usanii wa ulimwengu.”—The Anthropic Cosmological Principle, kilichoandikwa na John Barrow na Frank Tipler, ukurasa 7.

      Mungu, Usanii, na Vima Visivyobadilika vya Fizikia

      Ni vipi baadhi ya vima hivi visivyobadilika vya msingi vya fizikia ambavyo ni vya lazima ili uhai uwepo katika ulimwengu wote mzima? Ripoti fulani katika The Orange County Register la Januari 8, 1995, iliorodhesha vichache vya vima hivi visivyobadilika. Hiyo ilikazia jinsi sehemu hizi lazima ziwe zina upatano kabisa, ikitaarifu hivi: “Vile viwango vya kikiasi vya vima vingi vya kimaumbile visivyobadilika vinavyoainisha ulimwengu wote mzima—kwa kielelezo, badiliko la elektroni, au udumifu wa kasimwelekeo ya nuru, au uwiano wa nyezo za kani za msingi katika asili—kwa kushangaza vyapatana mno, nyingine kwa desimali 120. Ukuaji wa ulimwengu wote mzima wenye kutegemeza uhai kwa kuzidi umekuwa mnyetivu kwa vima hivyo mahususi. Badiliko lolote dogo—kuondoa sehemu moja ya bilioni ya sekunde hapa, kuongeza sehemu moja ya bilioni kumi ya meta moja pale—na ulimwengu wote mzima utakuwa mfu na mnyaufu.”

      Mwandikaji wa ripoti hii kisha alitaja kile ambacho kwa ukawaida huwa hakitajwi: “Yaonekana ni kusababu kunakofaa zaidi kudhania kwamba mwelekeo fulani usiojulikana watenda katika ukuaji wa ulimwengu wote mzima, labda katika utendaji wa uwezo fulani wenye weledi na ambao uliupatanisha ulimwengu wote mzima kwa kutayarisha kuwasili kwetu.”

      George Greenstein, profesa wa astronomia na taaluma ya anga, alitoa orodha ndefu zaidi ya vima hivi visivyobadilika vya kimaumbile katika kitabu chake The Symbiotic Universe. Miongoni mwa vilivyoorodheshwa mlikuwa na vima visivyobadilika vinavyopatana sana hivi kwamba ikiwa vingekuwa na kasoro ndogo sana, hakungekuwa na atomu, hakungekuwa na nyota, hakungekuwa na ulimwengu wote mzima. Vijambo vidogo-vidogo vya mahusiano haya vimeorodheshwa katika sanduku lililoambatanishwa. Ni lazima viwepo kwa ajili ya kuwezesha uhai wa kimaumbile. Vijambo hivyo ni tata na huenda visieleweke kwa wasomaji wote, lakini vyatambulika, pamoja na vinginevyo vingi, kwa wanafizikia wa anga waliozoezwa katika taaluma hizi.

      Kadiri orodha hii ilivyoendelea kuwa ndefu, Greenstein alishindwa. Yeye alisema “Lo! Sadfa nyingi mno! Kadiri ninavyosoma zaidi, ndivyo ninavyosadikishwa zaidi ‘sadfa’ kama hizo katu hazingeweza kutokea kwa nasibu. Lakini kadiri usadikisho huu ulivyokua, ndivyo jambo fulani jingine lilivyokua pia. Hata sasa ni vigumu kueleza ‘jambo hili fulani’ kwa maneno. Hilo lilikuwa kutamauka kwingi, na nyakati nyingine kulikuwa kwa kiasili. Ningeshtuka kihalisi kwa kukosa utulivu. . . . Je, yawezekana kwamba kwa ghafula, bila ya kunuia, kiaksidenti tumepata ithibati ya kuwapo kwa Kiumbe Kikuu Kuliko Vyote? Je, alikuwa Mungu ambaye alichukua hatua na kwa kufanya uandalizi akapanga ulimwengu wote mzima kwa faida yetu?”

      Akiwa ametamaushwa na kutishwa na hilo wazo, Greenstein mara moja alilitupilia mbali wazo hilo, na kushikilia imani ya dini ya kisayansi, na kupiga mbiu hivi: “Si Mungu.” Hii siyo sababu yenye kufaa—hilo wazo lilikuwa chungu sana hivi kwamba hangeweza kulistahimili!

      Uhitaji wa Kiasili wa Binadamu

      Hakuna lolote la maoni haya ambalo ni la kukashifu kazi ngumu ya unyoofu wa moyo ya wanasayansi, kutia ndani wanaanga. Hasa Mashahidi wa Yehova huthamini uvumbuzi wao mwingi kuhusu uumbaji ambao hufunua uwezo na hekima na upendo wa Mungu wa kweli, Yehova. Warumi 1:20 hutangaza hivi: “Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru.”

      Ule uchunguzi na kazi ngumu ya wanasayansi ni itikio la kiasili la binadamu kwa uhitaji ambao ni wa msingi kwa wanadamu kama vile uhitaji wa chakula, makao, na mavazi. Ni ule uhitaji wa kujua majibu kwa maswali fulani kuhusu wakati ujao na kusudi la uhai. Mungu ‘ameweka umilele katika mioyo ya wanadamu; hata hivyo hawawezi kuvumbua kile ambacho Mungu amefanya tangu mwanzo hadi mwisho.’—Mhubiri 3:11, The Holy Bible—New International Version.

      Hii si habari mbaya sana vile. Hiyo humaanisha kwamba wanadamu hawatajua mambo yote kamwe, lakini hawatakosa mambo mapya ya kujifunza: “Niliiona kazi yote ya Mungu, ya kuwa haitafutikani na mwanadamu kazi inayofanyika chini ya jua; kwa sababu mwanadamu na akijisumbua kadiri awezavyo kuitafuta, hata hivyo hataiona; naam, zaidi ya hayo, mwenye hekima ajapodhania ya kuwa ataijua, lakini yeye hataweza kuiona.”—Mhubiri 8:17.

      Wanasayansi wengine hupinga kwamba kumfanya Mungu kuwa “suluhisho” kwa tatizo fulani humaliza ile ari ya kufanya utafiti wa ziada. Hata hivyo, mtu ambaye hutambua Mungu kuwa Muumba wa mbingu na dunia ana vijambo vingi zaidi vidogo-vidogo vyenye kuvutia vya kuvumbua na mafumbo yenye kuvutia ambayo aweza kupekua. Ni kana kwamba ana idhini rasmi ya kuendelea na safari yenye kufurahisha ya kuvumbua na kujifunza!

      Ni nani anayeweza kukinza mwaliko wa Isaya 40:26? “Inueni macho yenu juu, mkaone.” Tumeinua macho yetu juu katika kurasa hizi chache, na kile tumeona ni ‘kitu fulani kimekosa’ ambacho kiliwaponyoka wanaanga. Pia tumepata majibu ya msingi ya maswali hayo yenye kujirudia ambayo yamesumbua akili ya mwanadamu katika enzi zote.

      Majibu Yapatikana Katika Kitabu Fulani

      Sikuzote majibu yamekuwapo, lakini kama vile wanadini wa siku ya Yesu, watu wengi wamefunga macho yao, wameziba masikio yao, na kufanya mioyo yao kuwa migumu kwa majibu ambayo hayakupatana na nadharia zao za kibinadamu au mtindo-maisha wao waliouchagua. (Mathayo 13:14, 15) Yehova ametueleza ulimwengu wote mzima ulikotoka, na jinsi dunia ilitokea, na wale ambao wataishi juu yake. Yeye ametuambia kwamba wakazi wa kibinadamu wa dunia ni lazima wailime na kutunza kwa upendo mimea na wanyama wanaoishiriki pamoja nao. Yeye pia ametueleza kile kinachotukia watu wanapokufa, kwamba wanaweza kuishi tena, na kile wapaswacho kufanya ili kuishi kwenye dunia milele.

      Ikiwa unapendezwa kupata majibu yakitolewa kwa lugha ya Neno la Mungu lililopuliziwa, Biblia, tafadhali soma maandiko yafuatayo: Mwanzo 1:1, 26-28; 2:15; Mithali 12:10; Mathayo 10:29; Isaya 11:6-9; 45:18; Mwanzo 3:19; Zaburi 146:4; Mhubiri 9:5; Matendo 24:15; Yohana 5:28, 29; 17:3; Zaburi 37:10, 11; Ufunuo 21:3-5.

      Kwa nini usisome maandiko haya pamoja na familia yako au pamoja na jirani au pamoja na kikundi cha marafiki katika nyumba yako jioni moja? Uwe na uhakika yatatokeza mazungumzo yenye kuarifu na kupendeza!

      Je, unasisimuliwa na mafumbo ya ulimwengu wote mzima na kuchochewa moyoni na umaridadi wao? Kwa nini usijifunze ili umjue vizuri zaidi Mmoja aliyeuumba? Mbingu ambazo haziwezi kusema hazina upendezi wowote katika udadisi na mshangao wetu, lakini Yehova Mungu, Muumba wazo, pia ni Muumba wetu, naye hujali wenye upole ambao wanapendezwa kujifunza kumhusu na uumbaji wake. Mwaliko sasa unatolewa duniani pote: “Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.”—Ufunuo 22:17.

      Huu ni mwaliko wenye kuchangamsha moyo kama nini kutoka kwa Yehova! Badala ya kutokea kwa mlipuko usio wa kiakili, wenye kukosa kusudi, ulimwengu wote mzima uliumbwa na Mungu mwenye weledi usio na mwisho na kusudi halisi ambaye alikufikiria wewe tangu mwanzoni. Akiba zake za nishati zisizo na mipaka zimedhibitiwa kwa umakini na sikuzote zapatikana ili kutegemeza watumishi wake. (Isaya 40:28-31) Kwa kumjua thawabu yako itakuwa bila mipaka kama ulimwengu wote mzima wenyewe, ambao ni wenye madaha!

      “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake.”—Zaburi 19:1.

      [Sanduku katika ukurasa wa13]

      Orodha ya Baadhi ya Vima Visivyobadilika Ambavyo Ni vya Lazima kwa Kuwapo kwa Uhai

      Nishati za elektroni na protoni ni lazima zilingane na ziwe kinyume; nutroni ni lazima ipite uzani wa protoni kwa asilimia ndogo sana; ulingano lazima uwepo kati ya halijoto ya jua na ufyonzaji wa klorofili kabla ya usanidimwanga kuweza kutukia; ikiwa kani yenye nguvu ingekuwa dhaifu kidogo, jua halingeweza kutokeza nishati kupitia kwa utendanaji wa nyukilia, lakini ingalikuwa yenye nguvu zaidi kidogo tu, fueli inayohitajiwa ili kutokeza nishati ingekosa usawaziko sana; bila udukiziwimbi aina mbili uliotengwa baina ya kiini katika vitovu vya nyota kubwa mno nyekundu, hakuna elementi yoyote isipokuwa heli ambayo ingeweza kufanyizwa; nafasi ingekuwa imepungua mipanuko mitatu, na miunganishio ya mtiririko wa damu na mfumo wa neva haingekuwapo; na ikiwa nafasi ingezidi mipanuko mitatu, sayari hazingeweza kuzunguka jua kwa usawaziko.—The Symbiotic Universe, kurasa 256-257.

      [Sanduku katika ukurasa wa14]

      Je, Kuna Yeyote Aliyepata Kuona Uzito Wangu Unaokosekana?

      Galaksi ya Andromeda, kama vile galaksi zote za mviringo, huzunguka kwa madaha angani kana kwamba ni tufani kubwa mno. Waastronomia wanaweza kuhesabu kima cha kuzunguka cha magalaksi mengi kutokana na spektra ya nuru, na wafanyapo hivyo, wao huvumbua kitu fulani chenye kutatanisha. Vima vya kuzunguka huonekana kutowezekana! Galaksi zote za mviringo huonekana kuzunguka kwa kasi mno. Hizo hutenda kana kwamba nyota zinazoonekana za galaksi zimefunganywa katika mvururo-nuru mkubwa zaidi wa mata nyeusi, isiyoonekana kwa darubiniupeo. “Hatujui mifanyizo ya hiyo mata nyeusi,” akakiri mwastronomia James Kaler. Wanasayansi wa anga hukadiria kwamba asilimia 90 ya uzito huo unaokosekana haujulikani ulipo. Wao wana hamu sana ya kuupata, ama katika mfanyizo wa neutrino kubwa ama aina ya mata isiyojulikana lakini iliyo nyingi mno.

      Ukiuona uzito unaokosekana, mjulishe mara moja mwanaanga wa mahali penu!

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki