Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kudumisha Wema wa Adili Katika Ulimwengu Uliojaa Upotovu wa Adili
    Mnara wa Mlinzi—1997 | Julai 15
    • Kudumisha Wema wa Adili Katika Ulimwengu Uliojaa Upotovu wa Adili

      “Fulizeni kufanya mambo yote bila manung’uniko na mabishano, ili mpate kuja kuwa bila lawama na wasio na hatia, watoto wa Mungu wasio na waa miongoni mwa kizazi kilicho kombo na kilichopotoka.”—WAFILIPI 2:14, 15.

      1, 2. Kwa nini Mungu alitaka Wakanaani waharibiwe kabisa?

      AMRI ya Yehova hairuhusu kuridhiana. Waisraeli walikuwa karibu kuingia Bara Lililoahidiwa nabii Musa alipowaambia hivi: ‘Waangamizeni kabisa, Wahiti, na Waamori, na Wakanaani, na Waperizi, na Wahivi, na Wayebusi, kama alivyowaamuru BWANA, Mungu wenu.’—Kumbukumbu la Torati 7:2; 20:17.

      2 Kwa kuwa Yehova ni Mungu mwenye rehema, kwa nini alitaka wakazi wa Kanaani waharibiwe kabisa? (Kutoka 34:6) Sababu moja ilikuwa ‘Wakanaani wasije wakawafunza Waisraeli kufanya mfano wa machukizo yao yote, waliyoifanyia miungu yao; hivyo itakuwa ni makosa juu ya BWANA, Mungu.’ (Kumbukumbu la Torati 20:18) Musa alisema hivi pia: “Ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA awafukuza nje mbele yako.” (Kumbukumbu la Torati 9:4) Wakanaani walikuwa mfano mkubwa zaidi wa upotovu wa adili. Upotovu wa ngono na ibada ya sanamu zilikuwa sifa bainifu za ibada yao. (Kutoka 23:24; 34:12, 13; Hesabu 33:52; Kumbukumbu la Torati 7:5) Ngono ya maharimu, ufiraji, na ngono na wanyama yalikuwa ‘matendo ya nchi ya Kanaani.’ (Mambo ya Walawi 18:3-25) Watoto wasio na hatia walitolewa kikatili wakiwa dhabihu kwa miungu isiyo ya kweli. (Kumbukumbu la Torati 18:9-12) Si ajabu kwamba Yehova aliona kuwapo tu kwa mataifa hayo kuwa tisho kwa hali njema ya kimwili, kiadili, kiroho ya watu wake!—Kutoka 34:14-16.

      3. Matokeo yalikuwa nini kwa sababu Waisraeli hawakutimiza kikamili maagizo ya Mungu kuhusu wakazi Wakanaani?

      3 Kwa sababu maagizo ya Mungu hayakutekelezwa kikamili, wakazi wengi wa Kanaani waliokoka ushindi wa Israeli wa Bara Lililoahidiwa. (Waamuzi 1:19-21) Baada ya muda fulani, uvutano wenye kudhuru kwa siri wa Wakanaani ulihisiwa, na ingeweza kusemwa hivi: “[Waisraeli] wakazikataa sheria zake [Yehova], na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao BWANA alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao.” (2 Wafalme 17:15) Naam, kwa miaka kadhaa Waisraeli wengi walizoea upotovu wa adili ambao ulimfanya Mungu aamuru kutoweka kabisa kwa Wakanaani—ibada ya sanamu, mazidio ya kingono, na hata kudhabihu watoto!—Waamuzi 10:6; 2 Wafalme 17:17; Yeremia 13:27.

      4, 5. (a) Ni nini kilichoyapata Israeli na Yuda yaliyokosa kuwa na uaminifu? (b) Ni himizo gani linalotolewa kwenye Wafilipi 2:14, 15, na ni maswali gani yanayotokezwa?

      4 Kwa hiyo nabii Hosea alitangaza hivi: “Lisikieni neno la BWANA, enyi wana wa Israeli; kwa maana BWANA ana mateto nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi. Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu hugusana na damu. Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa kondeni na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataondolewa.” (Hosea 4:1-3) Katika 740 K.W.K., ufalme wa kaskazini wenye ufisadi wa Israeli ulitiishwa na Ashuru. Kwa njia fulani, zaidi ya karne nzima baadaye, ufalme wa kusini wa Yuda usio mwaminifu ulishindwa na Babiloni.

      5 Matukio haya yatoa kielezi cha jinsi inavyoweza kuwa hatari kujiruhusu wenyewe tushindwe na upotovu wa adili. Mungu hukataa kabisa ukosefu wa uadilifu na hatauvumilia miongoni mwa watu wake. (1 Petro 1:14-16) Ni kweli kwamba twaishi katika “mfumo mwovu wa mambo uliopo,” katika ulimwengu ambao unaongezeka kuwa wenye ufisadi. (Wagalatia 1:4; 2 Timotheo 3:13) Ingawa hivyo, Neno la Mungu lawahimiza sana Wakristo wote waendelee kutenda katika njia ambayo watapata kuwa “bila lawama na wasio na hatia, watoto wa Mungu wasio na waa miongoni mwa kizazi kilicho kombo na kilichopotoka, ambao miongoni mwao [wanang’aa wakiwa] wamulikaji katika ulimwengu.” (Wafilipi 2:14, 15) Lakini twaweza kudumishaje wema wa adili katika ulimwengu huu uliojaa upotovu wa adili? Je, kweli yawezekana kufanya hivyo?

      Ulimwengu wa Roma Uliojaa Upotovu wa Adili

      6. Kwa sababu gani Wakristo wa karne ya kwanza walikabili ugumu wa kudumisha wema wa adili?

      6 Wakristo wa karne ya kwanza walikabili ugumu wa kudumisha wema wa adili kwa sababu upotovu wa adili ulienea katika kila upande wa jamii ya Roma. Mwana-falsafa Mroma Seneca alisema hivi kuhusu watu walioishi wakati uleule alioishi: “Wanadamu hujitahidi katika ushindani mkubwa wa uovu. Kila siku tamaa ya kutenda maovu ni kubwa zaidi, hofu ya kutotenda maovu ni ndogo zaidi.” Aliilinganisha jamii ya Kiroma na “jumuiya ya hayawani.” Basi, haishangazi kwamba, ili kujitumbuiza Waroma walitafuta mashindano ya kikatili ya kupigana na wanyama na maonyesho machafu ya kuigiza.

      7. Paulo alifafanuaje upotovu wa adili ambao ulikuwa umeenea miongoni mwa watu wengi katika karne ya kwanza W.K.?

      7 Huenda ikawa mtume Paulo alikumbuka kushuka kwa tabia kwa watu katika karne ya kwanza alipoandika hivi: “Mungu aliwaacha kwenye hamu za ngono yenye kufedhehesha, kwa maana watu wao wa kike walibadili utumizi wa kiasili wa wao wenyewe kuwa ule ulio kinyume cha asili; na hivyohivyo pia hata watu wa kiume waliacha utumizi wa kiasili wa aliye wa kike na kuwakiana tamaa kali katika uchu wao kuelekea mtu na mwenzake, watu wa kiume kwa watu wa kiume, wakifanya yaliyo yenye aibu na kupokea katika wao wenyewe malipo kamili, yaliyostahili kosa lao.” (Waroma 1:26, 27) Wakiazimia kufuatia tamaa zisizo safi za kimwili, jamii ya Waroma ilikuja kulemewa na upotovu wa adili.

      8. Watoto walitumiwaje mara nyingi kwa faida ya ubinafsi katika jamii ya Kigiriki na Kiroma?

      8 Historia haielezi waziwazi kadiri ambavyo ugoni-jinsia-moja ulienea miongoni mwa Waroma. Ingawa hivyo, bila shaka, walipatwa na uvutano wa watangulizi wao Wagiriki, ambao waliuzoea sana. Lilikuwa jambo la kawaida kwa wanaume wazee kufisidi wavulana wachanga, wakiwa kana kwamba wako chini ya mbawa zao katika uhusiano wa mwalimu na mwanafunzi ambao mara nyingi uliongoza vijana hao kuwa na tabia potovu za kingono. Bila shaka, Shetani na roho wake waovu walikuwa wakiongoza upotovu huo wa adili na kutendwa vibaya kwa watoto.—Yoeli 3:3; Yuda 6, 7.

      9, 10. (a) Ni katika njia gani ambayo 1 Wakorintho 6:9, 10 hushutumu matendo mbalimbali ya upotovu wa adili? (b) Malezi ya baadhi ya Wakristo katika kutaniko la Korintho yalikuwaje, na ni badiliko gani lililofanyika upande wao?

      9 Akiandika chini ya upulizio wa kimungu, Paulo aliwaambia Wakristo katika Korintho hivi: “Ama! Je, hamjui kwamba watu wasio waadilifu hawatarithi ufalme wa Mungu? Msiongozwe vibaya. Wala waasherati, wala waabudu-sanamu, wala wazinzi, wala wanaume watunzwao kwa makusudi yasiyo ya asili, wala wanaume walalao pamoja na wanaume, wala wezi, wala watu wenye pupa, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi hawatarithi ufalme wa Mungu. Na hata hivyo baadhi yenu ndivyo mlivyokuwa. Lakini mmeoshwa mkawa safi, lakini mmetakaswa, lakini mmetangazwa kuwa waadilifu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa roho ya Mungu wetu.”—1 Wakorintho 6:9-11.

      10 Hivyo barua zilizopuliziwa za Paulo zilishutumu ukosefu wa adili za kingono, akisema kwamba “waasherati” “hawatarithi ufalme wa Mungu.” Hata hivyo, baada ya kuorodhesha idadi kadhaa ya upotovu wa adili, Paulo alisema hivi: “Na hata hivyo baadhi yenu ndivyo mlivyokuwa. Lakini mmeoshwa mkawa safi.” Kwa msaada wa Mungu iliwezekana kwa wakosaji kuwa safi machoni pake.

      11. Wakristo wa karne ya kwanza waliendeleaje katika mazingira hayo maovu ya siku yao?

      11 Ndiyo, wema wa adili wa Kikristo ulisitawi hata katika ulimwengu uliojaa upotovu wa adili katika karne ya kwanza. Waamini ‘waligeuzwa umbo kwa kufanywa upya akili zao.’ (Waroma 12:2) Waliacha ‘njia yao ya kwanza ya mwenendo’ nao walikuwa ‘wanafanywa upya katika kani inayotendesha akili zao.’ Hivyo waliukimbia upotovu wa adili wa ulimwengu na “[kuvaa] utu mpya ulioumbwa kulingana na mapenzi ya Mungu katika uadilifu wa kweli na uaminifu-mshikamanifu.”—Waefeso 4:22-24.

      Ulimwengu wa Leo Uliojaa Upotovu wa Adili

      12. Ni badiliko gani ambalo limetokea ulimwenguni tangu 1914?

      12 Vipi siku yetu? Ulimwengu tunamoishi umejaa upotovu wa adili zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Hasa tangu 1914 kumekuwako na mshuko wa kiadili wa tufeni pote. (2 Timotheo 3:1-5) Wakikataa mawazo ya kidesturi juu ya wema wa adili, adili, heshima, na elimu-maadili, wengi wamekuwa wenye kujifikiria wenyewe katika kufikiri kwao na ‘wameishiwa na hisia zote za adili.’ (Waefeso 4:19) Gazeti Newsweek lilisema: “Tunaishi katika kizazi cha ukadirifu wa kiadili,” likiongezea kwamba tabia yenye kuonea ya kiadili “imeshusha mawazo yote yaliyo mema na mabaya kuhusu mapendezi ya kibinafsi, mapendezi ya kihisia-moyo au uchaguzi wa kitamaduni.”

      13. (a) Vitumbuizo vingi vya leo vinachocheaje upotovu wa adili? (b) Vitumbuizo vibaya vinaweza kuwa na matokeo gani mabaya kwa watu?

      13 Kama ilivyokuwa katika karne ya kwanza, vitumbuizo vilivyopotoka ni vya kawaida leo. Televisheni, redio, sinema, na vidio huandaa daima habari zinazohusiana na ngono. Upotovu wa adili hata umepenya katika mifumo ya kompyuta. Kulingana na uchunguzi mmoja wa chuo kikuu, ponografia ya kompyuta sasa ni “mojawapo ya matumizi ya tafrija makubwa zaidi (ikiwa si yaliyo makubwa zaidi) ya watumiaji wa mifumo ya kompyuta.” Matokeo ya haya yote ni nini? Mwandishi mmoja wa gazeti la habari asema hivi: “Wakati umwagikaji wa damu na ujeuri wa bure na ngono yenye ushaufu zinapojaza utamaduni wetu wenye kupendwa na wengi, twazoea umwagikaji wa damu na ujeuri wa bure na ngono yenye ushaufu. Sisi huchoshwa kabisa. Upotovu huvumilika kwa kuendelea kwa sababu huo hautushtui sana.”—Linganisha 1 Timotheo 4:1, 2.

      14, 15. Kuna uthibitisho gani kwamba adili za kingono zimeshuka ulimwenguni?

      14 Fikiria kwa uangalifu ripoti hii iliyo katika gazeti The New York Times: “Jambo ambalo lingeonekana kuwa lenye kushtua miaka 25 iliyopita sasa limekuwa mpango wa maisha wenye kukubalika. Idadi ya wenzi wanaochagua kuishi pamoja badala ya kuoana ilipanda hadi asilimia 80 [katika Marekani] kati ya mwaka wa 1980 na mwaka wa 1991.” Hilo si jambo la Amerika ya Kaskazini peke yake. Gazeti Asiaweek laripoti hivi: “Mjadala wa utamaduni unaendelea vikali katika nchi kotekote [Asia]. Suala ni kuhusu uhuru wa kingono dhidi ya viwango vya kidesturi, na misongo ya badiliko inaongezeka bila kukoma.” Takwimu zaonyesha ongezeko la kukubalika kwa uzinzi na ngono kabla ya ndoa katika nchi nyingi.

      15 Biblia ilitabiri kwamba utendaji wa kishetani ungekuwa mwingi katika siku yetu. (Ufunuo 12:12) Basi, haipasi kutushangaza kwamba upotovu unaenea kwa njia yenye kutia hofu. Kwa kielelezo, kutumia watoto kingono ili kupata faida kumefikia viwango vyenye kuenea sana.a Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa laripoti kwamba “biashara ya kutumia ngono ili kupata faida inawaharibu watoto katika karibu kila nchi ulimwenguni.” Kila mwaka “watoto zaidi ya milioni 1 ulimwenguni pote wanaripotiwa kulazimishwa katika umalaya wa watoto, wanasafirishwa na kuuzwa kwa makusudi ya kingono, na kutumiwa katika kufanyiza ponografia ya watoto.” Ugoni-jinsia-moja pia ni wa kawaida, wanasiasa na viongozi kadhaa wa kidini wakiongoza katika kuuchochea ukiwa “mtindo-maisha wa badala.”

      Kukataa Upotovu wa Ulimwengu

      16. Ni msimamo gani ambao Mashahidi wa Yehova huchukua kuhusu adili za kingono?

      16 Mashahidi wa Yehova hawakubaliani na wale wanaokubali viwango vyenye uendekevu vya adili za kingono. Andiko la Tito 2:11, 12 lasema hivi: “Fadhili isiyostahiliwa ya Mungu iletayo wokovu kwa watu wa namna zote imedhihirishwa, ikituagiza tukatae katakata kukosa kumwogopa Mungu na tamaa za kilimwengu na tuishi kwa utimamu wa akili na uadilifu na ujitoaji-kimungu katikati ya mfumo uliopo wa mambo.” Ndiyo, twasitawisha chuki ya kweli, karaha ya upotovu, kama ngono ya kabla ya ndoa, uzinzi, na matendo ya ugoni-jinsi-moja.b (Waroma 12:9; Waefeso 5:3-5) Paulo alitoa himizo hili: “Acha kila mtu anayeliita jina la Yehova akatae kabisa ukosefu wa uadilifu.”—2 Timotheo 2:19.

      17. Wakristo wa kweli huonaje matumizi ya vinywaji vya alkoholi?

      17 Wakristo wa kweli hukataa maoni ya ulimwengu juu ya yale yanayoonekana kuwa upotovu mdogo. Kwa kielelezo, watu wengi leo huona matumizi mabaya ya alkoholi kuwa burudisho lenye kuchangamsha. Lakini watu wa Yehova wanatii shauri la Waefeso 5:18: “Msiwe mkilewa divai, ambayo katika hiyo mna ufasiki, bali fulizeni kujazwa roho.” Mkristo akichagua kunywa, yeye hufanya hivyo kwa kiasi.—Mithali 23:29-32.

      18. Kanuni za Biblia huongozaje watumishi wa Yehova katika kuwatendea washiriki wa familia zao?

      18 Tukiwa watumishi wa Yehova, sisi pia twakataa maoni ya watu wengine katika ulimwengu ya kwamba kupiga mayowe na makelele kwa mwenzi wa mtu wa ndoa na watoto au kuwatukana kwa maneno yenye kuumiza ni tabia yenye kukubalika. Wakiwa wameazimia kufuatia mwendo wenye wema wa adili, waume na wake Wakristo hufanya bidii pamoja kutumia shauri hili la Paulo: “Acheni uchungu wote wenye nia ya kudhuru na hasira na hasira ya kisasi na kupiga kelele na usemi wenye kuudhi viondolewe mbali kutoka kwenu pamoja na ubaya wote. Bali iweni wenye fadhili nyinyi kwa nyinyi, wenye huruma kwa njia nyororo, mkisameheana kwa hiari mtu na mwenzake kama vile Mungu pia kupitia Kristo alivyowasamehe nyinyi kwa hiari.”—Waefeso 4:31, 32.

      19. Upotovu wa adili katika ulimwengu wa biashara umeeneaje?

      19 Ukosefu wa ufuatiaji haki, udanganyifu, uwongo, mbinu za biashara zenye mashindano makali sana, na kuiba pia ni mambo ya kawaida leo. Makala moja katika gazeti la biashara CFO yaripoti hivi: “Uchunguzi wa wafanyakazi 4,000 . . . ulipata kwamba asimilia 31 ya watu waliochunguzwa washuhudia ‘mwenendo usiofaa mkubwa sana’ wakati wa mwaka uliotangulia.” Mwenendo usiofaa huo ulitia ndani kuiba, rekodi zenye kudanganya, udhia wa kingono, na wizi. Ikiwa tutabaki safi kiadili machoni pa Yehova, lazima tuepuke mwenendo kama huo na tuwe wafuatiaji haki katika shughuli zetu za kifedha.—Mika 6:10, 11.

      20. Kwa nini Wakristo wanahitaji kujiepusha na “kupenda fedha”?

      20 Fikiria kwa uangalifu lililompata mwanamume mmoja aliyewazia kwamba angekuwa na wakati mwingi wa utumishi wa Mungu ikiwa angekuwa na faida kubwa sana katika kujasiria kifedha. Aliwavutia wengine katika mpango wa kitega uchumi kwa kutia chumvi sana matazamio ya faida yao. Mambo hayo yalipokosa kufaulu, alikuwa tayari kufanya lolote ili kulipa hasara kubwa zaidi alizopata hivi kwamba aliiba pesa alizokuwa amekabidhiwa. Kwa sababu ya matendo yake na mtazamo wa kutotubu, alitengwa na kutaniko la Kikristo. Kwa kweli hili onyo la Biblia ni la kweli: “Wale waazimiao kuwa matajiri huanguka ndani ya kishawishi na mtego na tamaa nyingi zisizo za akili na zenye kuumiza, ambazo hutumbukiza watu ndani ya uharibifu na uangamizo. Kwa maana kupenda fedha ni mzizi wa mambo mabaya ya namna zote, na kwa kujitahidi kufikilia kupenda huku wengine wameongozwa wapotee njia kutoka kwenye imani na wamejichoma wenyewe kotekote kwa maumivu mengi.”—1 Timotheo 6:9, 10.

      21. Ni tabia gani iliyo ya kawaida miongoni mwa watu walio na mamlaka ulimwenguni, lakini wale wenye madaraka ya nyadhifa katika kutaniko la Kikristo wanapaswa kujiendeshaje?

      21 Wanaume walimwengu wenye nguvu na wenye uvutano mara nyingi hukosa wema wa adili na huonyesha ukweli wa hii kanuni ya msingi, ‘Uwezo hufisidi.’ (Mhubiri 8:9) Katika nchi kadhaa, uhongaji na aina nyingine za ufisadi ni njia ya maisha miongoni mwa mahakimu, mapolisi, na wanasiasa. Hata hivyo, wale wanaoongoza katika kutaniko la Kikristo lazima wawe wenye wema wa adili na hawapaswi kupiga ubwana juu ya wengine. (Luka 22:25, 26) Wazee, pamoja na watumishi wa huduma, hawatumikii kwa “kupenda pato lisilo la haki.” Lazima wasiathiriwe na majaribio yoyote ya kuzuia au kuwa na uvutano kwa hukumu yao wakiwa na tarajio la kujitajirisha kibinafsi.—1 Petro 5:2; Kutoka 23:8; Mithali 17:23; 1 Timotheo 5:21.

      22. Makala ifuatayo itazungumza juu ya nini?

      22 Kwa ujumla, Wakristo wanakabiliana kwa mafanikio na magumu ya siku ya kisasa ya kudumisha wema wa adili katika ulimwengu wetu uliojaa upotovu wa adili. Hata hivyo, wema wa adili hutia mengi zaidi ya kuepuka uovu. Makala ifuatayo itazungumzia kinachotakikana hasa katika kusitawisha wema wa adili.

  • Je, Wafuatia Wema wa Adili?
    Mnara wa Mlinzi—1997 | Julai 15
    • Je, Wafuatia Wema wa Adili?

      “Wema wa adili wowote ulioko na jambo lolote la kustahili sifa likiwako, endeleeni kufikiria mambo haya.”—WAFILIPI 4:8.

      1. Upotovu wa adili ni nini, na kwa nini haujachafua ibada ya Yehova?

      UPOTOVU wa adili ni ubaya au ufisadi. Huenea katika ulimwengu tunamoishi. (Waefeso 2:1-3) Hata hivyo, Yehova Mungu hataruhusu ibada yake safi ichafuliwe. Vichapo vya Kikristo, mikutano, makusanyiko, na mikusanyiko hutupa sisi maonyo ya wakati unaofaa dhidi ya mwenendo usio wa uadilifu. Twapokea msaada ufaao wa Kimaandiko ‘tuambatane na lililo jema’ machoni pa Mungu. (Waroma 12:9) Kwa hiyo, wakiwa tengenezo, Mashahidi wa Yehova wanajitahidi kuwa safi, wenye wema wa adili. Lakini vipi sisi binafsi? Je, kwa kweli, wewe wafuatia wema wa adili?

      2. Wema wa adili ni nini, na kwa nini jitihada inahitajiwa ili kubaki wenye wema wa adili?

      2 Wema wa adili ni ubora wa kiadili, wema, kutenda na kufikiri ifaavyo. Si sifa baridi bali sifa tendaji, yenye kujenga. Wema wa adili hutia ndani zaidi ya kuepuka dhambi; humaanisha kufuatia lililo jema. (1 Timotheo 6:11) Mtume Petro aliwahimiza sana Wakristo wenzake hivi: “Jazeni kwenye imani yenu wema wa adili.” Jinsi gani? “Kwa kuchanga kwenu [kwa ahadi zenye thamani za Mungu] jitihada yote yenye bidii.” (2 Petro 1:5) Kwa sababu ya asili yetu yenye dhambi, twahitaji kujitahidi sana ili kubaki tukiwa wenye wema wa adili. Hata hivyo, watu wenye kumhofu Mungu wa zamani wamefanya hivyo, hata walipokabili vizuizi vikubwa mno.

      Alifuatia Wema wa Adili

      3. Mfalme Ahazi alikuwa na hatia ya matendo gani maovu?

      3 Maandiko yana masimulizi mengi ya wale waliofuatia wema wa adili. Mathalani, fikiria kwa uangalifu Hezekia mwenye wema wa adili. Baba yake, Mfalme Ahazi wa Yuda, kwa wazi aliabudu Moleki. “Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; wala hakufanya mema machoni pa BWANA Mungu wake, kama Daudi babaye. Lakini aliiendea njia ya wafalme wa Israeli, hata akampitisha mwanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Kisha akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti mbichi.” (2 Wafalme 16:2-4) Wengine hudai kwamba ‘kupitisha motoni’ kuliwakilisha aina fulani ya desturi ya utakaso na si dhabihu ya kibinadamu. Hata hivyo, kitabu Molech—A God of Human Sacrifice in the Old Testament kilichoandikwa na John Day, chasema hivi: “Kuna uthibitisho katika vyanzo vya fasihi ya kale na vya Carthage, pamoja na uthibitisho wa kiakiolojia, vya kuwapo kwa dhabihu za kibinadamu . . . katika ulimwengu wa Kikanaani, na hivyo hakuna sababu ya kushuku vidokezi vya Old Testament [vya dhabihu ya kibinadamu].” Zaidi ya hayo, 2 Mambo ya Nyakati 28:3 husema hususani kwamba Ahazi ‘aliwateketeza wanawe motoni.’ (Linganisha Kumbukumbu la Torati 12:31; Zaburi 106:37, 38.) Matendo maovu kama nini!

      4. Hezekia alijiendeshaje katika mazingira yaliyojaa upotovu wa adili?

      4 Hezekia aliendeleaje katika mazingira hayo yaliyojaa upotovu wa adili? Zaburi ya 119 inapendeza, kwa kuwa wengine huamini kwamba Hezekia aliitunga, akifanya hivi alipokuwa mkuu. (Zaburi 119:46, 99, 100) Kwa hiyo hali zake zaweza kuonyeshwa kwa maneno haya: “Wakuu nao waliketi wakaninena, lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako. Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito.” (Zaburi 119:23, 28) Akizungukwa na wazoeaji wa dini isiyo ya kweli, huenda Hezekia akawa alidhihakiwa sana miongoni mwa nyumba ya kifalme, hivi kwamba aliona shida kupata usingizi. Hata hivyo, alifuatia wema wa adili, baada ya muda fulani akawa mfalme, na “akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA . . . Alimtumaini BWANA, Mungu wa Israeli.”—2 Wafalme 18:1-5.

      Walibaki Wakiwa Wenye Wema wa Adili

      5. Ni majaribu gani ambayo Danieli na waandamani wake watatu walikabili?

      5 Pia Danieli na waandamani wake Waebrania watatu, walioitwa Hanania, Mishaeli, na Azaria walikuwa vielelezo bora vya wema wa adili. Walichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi yao ya nyumbani na kuhamishwa hadi Babiloni. Vijana hao wanne walipewa majina ya Kibabiloni—Belteshaza, Shadraka, Meshaki, na Abednego. Walipewa “chakula cha mfalme,” kutia ndani vyakula vilivyokatazwa na Sheria ya Mungu. Isitoshe, walilazimishwa kuwa na mtaala wa mazoezi wa miaka mitatu unaohusiana na “elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.” Hilo lilitia ndani zaidi ya kujifunza tu lugha nyingine, kwa kuwa yamkini neno “Wakaldayo” hapa hudhihirisha jamii ya wasomi. Hivyo, mafundisho yenye upotovu ya Kibabiloni yaliwekwa wazi kwa vijana hao Waebrania.—Danieli 1:1-7.

      6. Kwa nini twaweza kusema kwamba Danieli alifuatia wema wa adili?

      6 Ijapokuwa misongo mikubwa mno ya kujipatanisha, Danieli na waandamani wake watatu walichagua wema wa adili kuliko upotovu wa adili. Danieli 1:21 husema: “Danieli huyo akadumu huko hata mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi.” Ndiyo, Danieli “akadumu” akiwa mtumishi wa Yehova mwenye wema wa adili kwa miaka zaidi ya 80—hadi kuinuka na kuanguka kwa wafalme kadhaa wenye nguvu. Alibaki akiwa mwaminifu kwa Mungu licha ya hila na njama za kufisidi za wakuu wa serikali na upotovu wa adili kingono ulioenea katika dini ya Kibabiloni. Danieli aliendelea kufuatia wema wa adili.

      7. Twaweza kujifunza nini kutokana na mwendo uliofuatiwa na Danieli pamoja na waandamani wake watatu?

      7 Twaweza kujifunza mengi kutokana na Danieli na waandamani wake wenye kumhofu Mungu. Walifuatia wema wa adili nao wakakataa kufanywa wenyeji wa utamaduni wa Kibabiloni. Ijapokuwa walipewa majina ya Kibabiloni, hawakupoteza kamwe utambulisho wao wakiwa watumishi wa Yehova. Kwani, miaka ipatayo 70 hivi baadaye, mfalme Mbabiloni alimwita Danieli kwa jina lake la Kiebrania! (Danieli 5:13) Katika maisha yake yote marefu, Danieli alikataa kuridhiana hata katika mambo madogo. Akiwa kijana, “aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme.” (Danieli 1:8) Msimamo huo wa kutoridhiana uliochukuliwa na Danieli pamoja na waandamani wake watatu bila shaka uliwaimarisha kuokoka majaribu ya kufa na kupona waliyokabili baadaye.—Danieli, sura ya 3 na ya 6.

      Kufuatia Wema wa Adili Leo

      8. Vijana Wakristo wanaweza kukinzaje kufanywa wenyeji wa ulimwengu wa Shetani?

      8 Kama Danieli na waandamani wake watatu, watu wa Mungu leo hukinza kufanywa wenyeji wa ulimwengu mbovu wa Shetani. (1 Yohana 5:19) Ikiwa wewe ni kijana Mkristo, huenda ikawa unapata msongo mwingi kutoka kwa marika wako ili uige mapendezi yao yenye kupita kiasi ya mavazi, kujipamba, na muziki. Ingawa hivyo, badala ya kufuata kila mtindo wa muda tu au kila mtindo unaokuja, simama imara, na usijiache ‘ufanyizwe kulingana na mtindo wa mfumo huu wa mambo.’ (Waroma 12:2) ‘Kataa katakata kukosa kumwogopa Mungu na tamaa za kilimwengu na uishi kwa utimamu wa akili na uadilifu na ujitoaji-kimungu.’ (Tito 2:11, 12) Jambo la maana ni kibali cha Yehova si cha marika wako.—Mithali 12:2.

      9. Ni misongo gani ambayo Wakristo walio katika ulimwengu wa biashara huenda wakakabili, na wapaswa kujiendeshaje?

      9 Wakristo walio watu wazima pia hukabili misongo na lazima wawe wenye wema wa adili. Huenda wafanya-biashara Wakristo wakashawishiwa kutumia njia zenye kutilika shaka au kupuuza matakwa na kanuni za serikali za kodi. Hata hivyo, bila kujali mashindano ya kibiashara au jinsi ambavyo wafanyakazi wenzi hujiendesha, “twataka kujiendesha wenyewe kwa kufuata haki katika mambo yote.” (Waebrania 13:18) Tunahitajika Kimaandiko kuwa wafuatiaji haki na wenye usawaziko pamoja na waajiri, waajiriwa, wateja, na serikali za kilimwengu. (Kumbukumbu la Torati 25:13-16; Mathayo 5:37; Waroma 13:1; 1 Timotheo 5:18; Tito 2:9, 10) Pia acheni tujitahidi kuwa wenye utaratibu katika mambo yetu ya kibiashara. Kwa kuweka maandishi sahihi na kuandika maagano, mara nyingi twaweza kuzuia kutoelewana.

      Jihadhari!

      10. Kwa nini kuna uhitaji wa ‘kujihadhari’ inapohusu uchaguzi wetu wa muziki?

      10 Zaburi 119:9 hukazia upande mwingine wa kubaki tukiwa wenye wema wa adili machoni pa Mungu. Mtunga-zaburi aliimba: “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.” Mojawapo ya silaha za Shetani zenye matokeo zaidi ni muziki, ambao una nguvu ya kuchochea hisia-moyo. Kwa kusikitisha, baadhi ya Wakristo wameshindwa ‘kujihadhari’ inapohusu muziki, nao hujipata wamevutwa kwa aina zao zenye kupita kiasi, kama vile rapu na muziki wenye mdundo mzito. Huenda wengine wakabisha kwamba muziki huo hauwadhuru au kwamba hawasikilizi kwa uangalifu maneno yake. Wengine husema kwamba wao hufurahia tu mpigo mzito au mlio wa gita zenye sauti kubwa. Ingawa hivyo, kwa Wakristo, suala si kama jambo fulani linafurahisha. Hangaiko lao ni kama ni “lenye kukubalika kwa Bwana.” (Waefeso 5:10) Kwa ujumla, muziki wenye mdundo mzito na rapu huchochea upotovu wa adili kama vile maneno machafu, uasherati, na hata Ibada ya Shetania—mambo ambayo bila shaka hayaruhusiwi miongoni mwa watu wa Mungu. (Waefeso 5:3) Iwe tu wazee au vijana, kila mmoja wetu angefanya vizuri kufikiria swali hili, Je, mimi nafuatia wema wa adili au upotovu wa adili, kwa uchaguzi wangu wa muziki?

      11. Mkristo anaweza kujihadharije kuhusiana na vipindi vya televisheni, vidio, na sinema?

      11 Programu nyingi za televisheni, vidio, na sinema huendeleza upotovu wa adili. Kulingana na mtaalamu mmoja wa afya ya kiakili, ‘maisha ya anasa, utendaji wa kingono, jeuri, pupa, na ubinafsi’ huzidi katika sinema zilizo nyingi ambazo zinafanyizwa leo. Kwa hiyo, kujihadhari hutia ndani kuwa wateuzi juu ya yale tunayochagua kutazama. Mtunga-zaburi alisali hivi: “Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa.” (Zaburi 119:37) Kijana Mkristo aitwaye Joseph alitumia kanuni hii. Wakati filamu moja ilipoanza kuonyesha ngono na jeuri ya wazi, aliondoka kwenye jumba la maonyesho. Je, aliaibika kufanya hivyo? “La, hasha,” asema Joseph. “Nilimfikiria Yehova kwanza na nikafikiria kumpendeza yeye.”

      Lile Fungu la Funzo na Kutafakari

      12. Kwa nini funzo la kibinafsi na kutafakari kwahitajiwa ili kufuatia wema wa adili?

      12 Kuepuka mambo mabaya tu hakutoshi. Kufuatia wema wa adili hutia ndani pia kujifunza na kutafakari juu ya mambo mazuri yaliyorekodiwa katika Neno la Mungu ili kanuni zake zenye uadilifu ziweze kutumika maishani mwetu. “Sheria yako naipenda mno ajabu,” akasema kwa mkazo mtunga-zaburi. “Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.” (Zaburi 119:97) Je, funzo la kibinafsi la Biblia na vichapo vya Kikristo ni sehemu ya ratiba yako ya kila juma? Ni kweli, kuweka wakati kwa ajili ya funzo la bidii lenye kuendelea la Neno la Mungu na kutafakari kwa njia ya sala juu yalo laweza kuwa jambo gumu. Lakini mara nyingi yawezekana kununua wakati kutoka utendaji mwingine mbalimbali. (Waefeso 5:15, 16) Labda saa za asubuhi na mapema zaweza kufaa kwa ajili ya sala, funzo, na kutafakari.—Linganisha Zaburi 119:147.

      13, 14. (a) Kwa nini kutafakari ni kwenye thamani? (b) Ni kutafakari maandiko yapi kunakoweza kutusaidia tukirihi ukosefu wa adili katika ngono?

      13 Kutafakari ni kwenye thamani, kwa kuwa hutusaidia kushika yale tujifunzayo. La maana zaidi, kunaweza kutusaidia tuendeleze maoni ya kimungu. Kutoa kielezi: Ni rahisi kujua kwamba Mungu hukataza uasherati lakini ni vigumu ‘kukirihi lililo ovu, na kuambatana na lililo jema.’ (Waroma 12:9) Kwa kweli twaweza kuhisi vile Yehova huhisi kuhusu ukosefu wa adili katika ngono kwa kutafakari maandiko ya msingi ya Biblia, kama vile Wakolosai 3:5, ambayo husihi: “Kwa hiyo, fisheni viungo vya mwili wenu vilivyo juu ya dunia kwa habari ya uasherati, ukosefu wa usafi, hamu ya ngono, tamaa yenye kuumiza, na tamaa, ambako ni ibada ya sanamu.” Jiulize mwenyewe hivi: ‘Ni aina gani ya hamu ya ngono ambayo lazima niifishe? Ni jambo gani nipaswalo kuepuka ambalo huenda likaamsha tamaa isiyo safi? Je, kuna mabadiliko ambayo nahitaji kufanya katika shughuli zangu na watu wa jinsia tofauti?’—Linganisha 1 Timotheo 5:1, 2.

      14 Paulo awasihi sana Wakristo waepukane na uasherati na wajidhibiti ili “kwamba yeyote asifikie hatua ya kudhuru na kuziingilia haki za ndugu yake.” (1 Wathesalonike 4:3-7) Jiulize mwenyewe: ‘Kwa nini kufanya uasherati ni jambo lenye kudhuru? Ningefanya madhara gani kwangu au kwa mtu mwingine ikiwa ningefanya dhambi kwa habari hii? Ningeathiriwaje kiroho, kihisia-moyo, na kimwili? Vipi watu mmoja-mmoja katika kutaniko ambao wamevunja sheria ya Mungu na wamekuwa wasiotubu? Mambo yamekuwaje kwao?’ Kutii yale ambayo Maandiko husema juu ya mwenendo kama huo kwaweza kuongeza kina cha chuki yetu kwa yale yaliyo mabaya machoni pa Mungu. (Kutoka 20:14; 1 Wakorintho 5:11-13; 6:9, 10; Wagalatia 5:19-21; Ufunuo 21:8) Paulo asema kwamba mwasherati “anapuuza, si mwanadamu, bali Mungu.” (1 Wathesalonike 4:8) Ni Mkristo yupi wa kweli ambaye angempuuza Baba yake wa kimbingu?

      Wema wa Adili na Ushirika

      15. Ushirika una fungu gani katika kufuatia kwetu wema wa adili?

      15 Msaada mwingine wa kubaki wenye wema wa adili ni ushirika mzuri. Mtunga-zaburi aliimba: “Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao [Yehova], na wale wayatiio mausia yako.” (Zaburi 119:63) Twahitaji ushirika mzuri unaoandaliwa kwenye mikutano ya Kikristo. (Waebrania 10:24, 25) Tukijitenga wenyewe, huenda tukawa wenye ubinafsi katika kufikiri kwetu, na upotovu wa adili waweza kutushinda kwa urahisi. (Mithali 18:1) Hata hivyo, ushirikiano mchangamfu wa Kikristo, waweza kuimarisha azimio letu la kubaki tukiwa wenye wema wa adili. Bila shaka, lazima pia tujihadhari na mashirika mabaya. Twaweza kuwa wenye moyo mkunjufu kwa majirani, wafanyakazi wenzi, na wanafunzi wenzetu. Lakini tukitembea kwa hekima, tutaepuka kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na wale wasiofuatia wema wa adili wa Kikristo.—Linganisha Wakolosai 4:5.

      16. Utumiaji wa 1 Wakorintho 15:33 waweza kutusaidiaje tufuatie wema wa adili leo?

      16 Paulo aliandika hivi: “Mashirika mabaya huharibu mazoea yenye mafaa.” Kwa kutoa taarifa hii, alikuwa akiwaonya waamini kwamba wanaweza kupoteza imani yao kwa kushirikiana na waliodai kuwa Wakristo ambao walikataa fundisho la Kimaandiko juu ya ufufuo. Kanuni iliyomaanishwa na onyo la Paulo yatumika kwa mashirika yetu ndani na nje ya kutaniko. (1 Wakorintho 15:12, 33) Pasipo budi, hatutaki kuwaepuka ndugu na dada zetu kwa sababu hawakubaliani na maoni fulani ya kibinafsi tu ambayo sisi hushikilia. (Mathayo 7:4, 5; Waroma 14:1-12) Hata hiyo, tahadhari yahitajiwa ikiwa wengine katika kutaniko wajiingiza katika mwenendo wenye kutiliwa shaka au waonyesha roho ya uchungu na ya kulalamika. (2 Timotheo 2:20-22) Ni jambo lenye hekima kuwa na uhusiano wa karibu na wale wanaofurahia “badilishano la kitia-moyo.” (Waroma 1:11, 12) Hilo litatusaidia tufuatie mwendo wenye wema wa adili na tubaki tukiwa katika “njia ya uzima.”—Zaburi 16:11.

      Endelea Kufuatia Wema wa Adili

      17. Kulingana na Hesabu sura ya 25, ni msiba gani uliopata Waisraeli, na ni somo gani tunaloandaliwa?

      17 Punde tu baada ya Waisraeli kurithi Bara Lililoahidiwa, maelfu yao walichagua mwendo wa upotovu wa adili—nao wakapata msiba. (Hesabu, sura ya 25) Leo, watu wa Yehova wanasimama ukingoni mwa ulimwengu mpya wenye uadilifu. Kuingia huko kutakuwa pendeleo lenye baraka kwa wale wanaoendelea kukataa upotovu wa adili wa ulimwengu huu. Tukiwa wanadamu tusio wakamilifu, huenda tukawa na mielekeo mibaya, lakini Mungu anaweza kutusaidia tufuate miongozo ya uadilifu ya roho yake takatifu. (Wagalatia 5:16; 1 Wathesalonike 4:3, 4) Basi acheni tutii himizo la Yoshua kwa Israeli: “Mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli.” (Yoshua 24:14) Hofu yenye staha ya kutompendeza Yehova itatusaidia tufuatie mwenendo wenye wema wa adili.

      18. Kuhusu upotovu wa adili na wema wa adili, azimio la Wakristo wote lapaswa kuwa nini?

      18 Ikiwa una tamaa ya moyoni ya kumpendeza Mungu, azimia kutii himizo hili la Paulo: “Mambo yoyote yaliyo ya kweli, mambo yoyote yaliyo ya hangaikio zito, mambo yoyote yaliyo ya uadilifu, mambo yoyote yaliyo safi kiadili, mambo yoyote yaliyo ya kupendeka, mambo yoyote yaliyo ya kusemwa vema, wema wa adili wowote ulioko na jambo lolote la kustahili sifa likiwako, endeleeni kufikiria mambo haya.” Ukifanya hivyo, matokeo yatakuwa nini? Paulo alisema hivi: “Zoeeni kuyafanya haya; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.” (Wafilipi 4:8, 9) Ndiyo, kwa msaada wa Yehova unaweza kukataa upotovu wa adili na ufuatie wema wa adili.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki