Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kamchatka—Rasi Maridadi Kwenye Pasifiki
    Amkeni!—2007 | Machi
    • Volkano na Chemchemi za Maji Moto na za Mvuke

      Ikiwa kwenye Eneo la Pasifiki Lenye Volkano, Kamchatka ina volkano 30 hivi zilizo hai. Kilele cha volkano inayoitwa Klyuchevskaya kimefafanuliwa kuwa “kilele maridadi sana.” Kina urefu wa mita 4,750 juu ya usawa wa bahari, na hivyo kufanya mlima huo kuwa volkano kubwa zaidi iliyo hai katika mabara ya Ulaya na Asia. Tangu 1697, mwaka ambao wavumbuzi Warusi walifika Kamchatka, milipuko zaidi ya 600 imerekodiwa katika rasi hiyo.

      Katika miaka ya 1975/1976 milipuko ya volkano iliyotokea kwenye eneo la Tolbachik ilitokeza “mioto” iliyoruka mita 2,500! Kulikuwa na radi katikati ya mawingu ya majivu. Milipuko hiyo iliyoendelea kwa karibu mwaka moja na nusu bila kukoma ilitokeza milima minne ya volkano. Maziwa na mito ilitokomea, na majivu ya moto yaliteketeza misitu mizima mpaka kwenye mizizi. Maeneo makubwa yaligeuzwa kuwa jangwa.

      Jambo linalopendeza ni kwamba milipuko mingi ilitokea mbali na makazi ya watu, na ni watu wachache sana waliokufa. Lakini wageni wanapaswa kujihadhari hasa wanapoenda kwenye Bonde la Kifo, ambalo liko chini ya mlima wa volkano wa Kichpinych. Kunapokuwa hakuna upepo, na hasa wakati theluji inapoyeyuka, gesi zenye sumu za volkano hutanda kwenye bonde hilo na hivyo kuhatarisha maisha ya wanyama. Wakati mmoja, bonde hilo lilikuwa na mizoga ya dubu kumi na wanyama wengi wadogo.

      Bonde kubwa linaloitwa Uzon, lina shimo lenye matope yanayotokota na maziwa yenye maji moto yaliyo na miani yenye rangi nyingi.

  • Kamchatka—Rasi Maridadi Kwenye Pasifiki
    Amkeni!—2007 | Machi
    • [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

      BONDE MARIDADI SANA

      Bonde la Uzon, lililofanyizwa kutokana na volkano ya kale lina kipenyo cha kilomita kumi. Kitabu kimoja kinasema kwamba ndani ya bonde hilo mna “kila kitu kinachofanya Kamchatka kuwa maarufu.” Bonde hilo lina chemchemi za maji moto na baridi; mashimo yenye matope yanayotokota; vilima vya tope lenye moto; maziwa safi yenye samaki na bata-maji, na mimea mingi.

      Kitabu Miracles of Kamchatka Land kinasema kwamba “hakuna mahali popote pengine Duniani” ambapo majira ya kupukutika kwa majani huwa mafupi lakini maridadi sana. Nyanda nyekundu za eneo hilo hutofautiana sana na miti ya mibetula yenye rangi ya dhahabu na manjano. Wakati huohuo ardhi hutoa mvuke mweupe ambao huonekana waziwazi kwenye anga la bluu. Na mapema asubuhi, misitu “huimba” mamilioni ya majani yaliyo na umande yanapoanguka kwa sauti nyororo, kuonyesha kwamba majira ya baridi kali yanakaribia.

      [Sanduku katika ukurasa wa 19]

      ZIWA HATARI!

      Mnamo 1996, volkano iliyofikiriwa kuwa haitendi ililipuka chini ya Ziwa Karymsky, na kutokeza mawimbi yenye urefu wa mita kumi ambayo yaliangusha miti katika misitu inayozunguka ziwa hilo. Katika muda wa dakika chache tu, ziwa hilo likawa na asidi nyingi sana hivi kwamba hakuna kiumbe ambacho kingeendelea kuwa hai humo. Hata hivyo, hakuna wanyama waliopatikana wakiwa wamekufa karibu na ziwa hilo licha ya kwamba majivu ya volkano hiyo na mawimbi yalienea kotekote katika ufuo, anaeleza mtafiti Andrew Logan. “Kabla ya mlipuko huo,” anasema, “kulikuwa na mamilioni ya samaki (hasa salmoni na trauti) katika Ziwa Karymsky. Baada ya mlipuko huo hakukuwa na kiumbe yeyote katika ziwa hilo.” Hata hivyo, huenda samaki kadhaa waliokoka. Wanasayansi wanakisia kwamba huenda jambo fulani, kama vile kubadilika kwa maji, liliwaonya samaki na kuwafanya wakimbilie Mto Karymsky ulio karibu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki