-
Sehemu ya 3—Kuwa Mashahidi Hadi Sehemu ya Mbali Zaidi Sana ya DuniaMashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
-
-
Kuhubiri Katika Ulaya Ujapokuwa Mnyanyaso wa Wakati wa Vita
Kwa sababu hawangeweza kuacha imani yao na kazi yao ya kuhubiri, maelfu ya Mashahidi wa Yehova katika Austria, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, na Ujerumani walitiwa gerezani au wakapelekwa kwenye kambi za mateso za Nazi. Humo kutendwa kinyama kulikuwa jambo la kawaida sana. Wale waliokuwa bado kutiwa gerezani waliendelea na huduma yao kwa tahadhari. Mara nyingi walifanya kazi kwa kutumia Biblia pekee na kutoa fasihi nyingine wakati tu walipokuwa wakifanya ziara za kurudia kwa watu wenye kupendezwa. Ili kuepuka kukamatwa, Mashahidi walikuwa wakizuru nyumba moja katika ghorofa na kisha labda kwenda kwenye jengo jingine, au baada ya kuzuru nyumba moja tu wangeenda kwenye barabara nyingine kabla ya kuzuru nyumba nyingine. Lakini hawakuwa na woga hata kidogo wa kutoa ushahidi.
Katika Desemba 12, 1936, miezi michache tu baada ya Gestapo kukamata maelfu ya Mashahidi na watu wengine wenye kupendezwa katika jitihada ya taifa zima ya kukomesha kazi yao, Mashahidi walifanya kampeni yao wenyewe. Kwa mwendo kama wa umeme walitia makumi ya maelfu ya nakala za azimio lililochapwa katika masanduku ya posta na chini ya milango ya watu kotekote katika Ujerumani. Maazimio hayo yalipinga jinsi ndugu na dada zao Wakristo walivyokuwa wakitendewa. Katika muda wa saa moja baada ya ugawanyaji huo kuanza, polisi walikuwa wakienda huku na huku wakijaribu kukamata wagawanyaji, lakini waliweza kuwakamata kama kumi hivi tu nchini mwote.
Maofisa walishtuka kwamba kampeni kama hiyo ingeweza kufanywa baada ya yote ambayo serikali ya Nazi ilikuwa imefanya ili kukandamiza kazi. Zaidi ya hilo, walikuja kuwaogopa raia. Kwa nini? Kwa sababu wakati polisi na wakuu wengine waliovalia kirasmi walipozuru makao ya watu na kuwauliza kama walikuwa wamepokea kikaratasi kama hicho, wengi wao walikana jambo hilo. Kwa kweli, wengi wao hawakuwa wamekipokea. Nakala zilikuwa zimeachiwa familia mbili au tatu tu katika kila jengo. Lakini polisi hawakujua hivyo. Walidhani kwamba nakala iliachwa kwenye kila mlango.
Wakati wa miezi iliyofuata, wakuu wa Nazi walikataa katakata mashtaka yaliyofanywa katika azimio hilo lililochapwa. Kwa hiyo, katika Juni 20, 1937, Mashahidi waliokuwa wangali huru waligawanya ujumbe mwingine, barua iliyoandikiwa wakuu katika magazeti ya umma ambayo ilifichua wazi mambo mengi kwa urefu juu ya mnyanyaso huo, hati hiyo ilitaja majina ya maofisa na tarehe na mahali pa mnyanyaso. Mshangao ulikuwa mkuu miongoni mwa Gestapo juu ya mfichuo huo na juu ya uwezo wa Mashahidi wa kufanya ugawanyaji kama huo.
Mambo mengi yaliyoipata familia ya Kusserow, iliyotoka Bad Lippspringe, Ujerumani, yalidhihirisha nia hiyohiyo ya kutoa ushahidi. Kielelezo kimoja chahusu jambo lililotukia baada ya Wilhelm Kusserow kuuawa hadharani katika Münster na serikali ya Nazi kwa sababu ya kukataa kwake kuridhiana imani yake. Hilda, mama yake Wilhelm, alienda gerezani mara hiyo na kusihi sana apewe mwili ili ukazikwe. Aliambia familia yake hivi: “Tutatoa ushahidi mwingi kwa watu waliomjua.” Kwenye mazishi, Franz, baba ya Wilhelm, alitoa sala iliyoonyesha imani katika uandalizi wenye upendo wa Yehova. Kaburini, Karl-Heinz, ndugu mdogo wa Wilhelm alisema maneno ya kufariji kutoka katika Biblia. Kwa kufanya hivyo waliadhibiwa, lakini kwao jambo lililokuwa la maana lilikuwa kumheshimu Yehova kwa kutoa ushahidi kuhusu jina na Ufalme wake.
Kadiri mikazo ya wakati wa vita ilivyoongezeka katika Uholanzi, kwa hekima Mashahidi huko walirekebisha mipango yao ya mikutano. Sasa ilifanywa katika vikundi vya watu kumi au wachache zaidi katika makao ya watu binafsi. Mahali pa mikutano palibadilishwa mara nyingi. Kila Shahidi alihudhuria pamoja na kikundi chake tu, na hakuna yeyote angetoboa siri ya mahali pa funzo, hata kwa rafiki mwenye kutumainiwa. Katika pindi hiyo ya historia, wakati idadi nzimanzima za watu zilipokuwa zikifukuzwa kutoka makao yao kama tokeo la vita, Mashahidi wa Yehova walijua kwamba watu walihitaji sana ujumbe wenye kufariji upatikanao tu katika Neno la Mungu, nao waliushiriki pamoja nao bila woga. Lakini barua moja kutoka ofisi ya tawi iliwakumbusha akina ndugu juu ya tahadhari ambayo Yesu alionyesha katika pindi mbalimbali alipokabiliwa na wapinzani. (Mt. 10:16; 22:15-22) Kama tokeo, walipokutana na mtu aliyeonyesha uhasama, waliandika nambari ya nyumba kwa uangalifu ili tahadhari za pekee ziweze kuchukuliwa wakati wa kufanya kazi katika eneo hilo wakati ujao.
Katika Ugiriki wakazi walipatwa na mateso yenye kuenea sana wakati wa kukaliwa na Ujerumani. Hata hivyo, kutendwa vibaya sana kulikowapata Mashahidi wa Yehova kulikuja kama tokeo la kusingiziwa kikatili na makasisi wa Kanisa Orthodoksi la Kigiriki, waliosisitiza kwamba polisi na mahakama ziwachukulie hatua. Mashahidi wengi walitiwa gerezani au wakafukuzwa kutoka miji ya kwao na kupelekwa kwenye vijiji vya mbali au kufungwa chini ya hali mbaya sana katika visiwa visivyo na kitu. Hata hivyo, wao waliendelea kutoa ushahidi. (Linganisha Matendo 8:1, 4.) Mara nyingi jambo hilo lilifanywa kwa kuongea na watu katika bustani za umma, kwa kuketi kwenye mabenchi pamoja nao na kuwaambia juu ya Ufalme wa Mungu. Wakati kupendezwa kwa kweli kulipopatikana, mtu huyo aliazimwa fasihi fulani ya Biblia yenye thamani kubwa. Fasihi hiyo ilirudishwa baadaye ili itumiwe tena na tena. Wengi wapendao kweli walikubali kwa shukrani msaada uliotolewa na Mashahidi na hata wakajiunga pamoja nao katika kushiriki habari njema na wengine, ingawa kufanya hivyo kuliwaletea mnyanyaso mkali.
Jambo la maana katika ujasiri na ustahimilivu wa Mashahidi lilikuwa kujengwa kwao na chakula cha kiroho. Ingawa ugavi wa fasihi ya kugawiwa wengine hatimaye ilipata kupungua sana katika sehemu nyingine za Ulaya wakati wa vita, walifaulu kueneza miongoni mwao habari yenye kujenga imani iliyokuwa imetayarishwa na Sosaiti kwa ajili ya funzo la Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote. Kwa kuhatirisha maisha zao, August Kraft, Peter Gölles, Ludwig Cyranek, Therese Schreiber, na wengine wengi walishiriki kazi ya kurudufisha na kugawanya habari ya funzo iliyoingizwa katika Austria kisirisiri kutoka Chekoslovakia, Italia, na Uswisi. Katika Uholanzi, ni mlinzi wa gereza mwenye fadhili aliyesaidia kwa kupata Biblia kwa ajili ya Arthur Winkler. Ijapokuwa tahadhari yote iliyochukuliwa na maadui, maji ya kweli ya Biblia yenye kuburudisha kutoka kwa Mnara wa Mlinzi yalifika hata ndani ya kambi za mateso za Ujerumani na kuenezwa miongoni mwa Mashahidi humo.
Kufungiwa gerezani na katika kambi za mateso hakukuzuia Mashahidi wa Yehova wasiwe mashahidi. Wakati mtume Paulo alipokuwa gerezani katika Roma, aliandika hivi: “Ninavumilia uovu kufikia hatua ya vifungo vya gereza . . . Hata hivyo, neno la Mungu halifungwi.” (2 Tim. 2:9, NW) Ilithibitika kuwa vivyo hivyo kwa habari ya Mashahidi wa Yehova katika Ulaya wakati wa Vita ya Ulimwengu 2. Walinzi waliona mwenendo wao; baadhi yao waliuliza maswali, na wachache wao wakawa waamini wenzao, hata ingawa hiyo ilimaanisha kupoteza uhuru wao wenyewe. Wafungwa wengi waliofungwa pamoja na Mashahidi walikuwa wametoka nchi mbalimbali kama vile Urusi, ambako ni kazi ndogo sana ya kuhubiri habari njema ilikuwa imefanywa. Baada ya vita baadhi yao walirudi nchi za kwao wakiwa Mashahidi wa Yehova, wakiwa na hamu ya kueneza ujumbe wa Ufalme humo.
Mnyanyaso wa kinyama na athari za vita kamili havikuweza kuzuia ile kazi iliyotabiriwa ya kukusanya watu kwenye nyumba kuu ya kiroho ya Yehova kwa ajili ya ibada. (Isa. 2:2-4) Kuanzia 1938 hadi 1945, nchi nyingi za Ulaya zilionyesha maongezeko makubwa ya idadi ya waliokuwa wakishiriki hadharani katika ibada hiyo kwa kupiga mbiu ya Ufalme wa Mungu. Katika Finland, Ufaransa, Uingereza, na Uswisi, Mashahidi walipata maongezeko ya karibu asilimia 100. Katika Ugiriki, kulikuwa ongezeko la karibu mara saba. Katika Uholanzi, lilikuwa mara 12. Lakini kufikia mwisho wa 1945, habari kamili haikuwa imefika kutoka Ujerumani au Rumania, na ripoti ambazo hazikuwa zimekamilika zilitoka katika nchi nyingine chache.
Nje ya Ulaya Wakati wa Miaka Hiyo ya Vita
Katika nchi za Mashariki vilevile, vita ya ulimwengu ilitokeza magumu makubwa sana kwa Mashahidi wa Yehova. Katika Japani na Korea, walikamatwa na kupigwa na kuteswa kwa sababu walitetea Ufalme wa Mungu na hawakuabudu maliki wa Japani. Hatimaye mawasiliano yote na Mashahidi katika zile nchi nyingine yalikatwa kabisa. Kwa wengi wao, fursa pekee za kutoa ushahidi zilikuwapo wakati walipohojiwa au waliposhtakiwa mahakamani. Kufikia mwisho wa vita, huduma ya hadharani ya Mashahidi wa Yehova katika nchi hizo ilikuwa ni kama imekoma.
Wakati vita ilipofika Filipino, Mashahidi huko walitendwa vibaya na pande zote mbili kwa sababu wao hawakuunga mkono ama Wajapani ama wakinzani. Ili kuepuka kukamatwa, Mashahidi wengi waliacha makao yao. Lakini walipokuwa wakihamahama walihubiri—na kuwaazima wengine fasihi wakati zilipokuwa zinapatikana, na baadaye kwa kutumia Biblia pekee. Wakati vita viliposonga mbali, hata walitayarisha mashua kadhaa ili kusafirisha vikundi vikubwa vya Mashahidi kwenye visiwa ambavyo hakuna ushahidi uliokuwa umetolewa.
Katika Burma (sasa ni Myanmar), mkazo kutoka kwa makasisi Waanglikana, Wamethodisti, Wakatoliki wa Roma, na Wabaptisti Waamerika uliotumiwa juu ya maofisa wa kikoloni ndio uliosababisha kupigwa marufuku kwa fasihi za Mashahidi wa Yehova katika Mei 1941 wala si uvamizi wa Japani. Mashahidi wawili waliokuwa wakifanya kazi katika ofisi ya kebo waliona telegramu iliyowajulisha ni jambo gani lililokaribia kutukia, hivyo ndugu waliondoa haraka fasihi katika depo ya Sosaiti ili kuepuka isinyakuliwe na maofisa. Halafu jitihada ilifanywa ya kuipeleka China kupitia nchi kavu.
Wakati huo serikali ya Marekani ilikuwa ikisafirisha kwa malori kiasi kikubwa cha vifaa vya vita kupitia Barabara ya Burma ili kuunga mkono serikali ya Kitaifa ya China. Ndugu walijaribu kupata nafasi katika mojawapo malori hayo lakini wakakataliwa vikali. Jitihada za kupata gari kutoka Singapore zilishindwa pia. Hata hivyo, wakati Mick Engel, aliyekuwa msimamizi wa depo ya Sosaiti ya Rangoon (sasa ni Yangon), alipomwendea ofisa wa cheo cha juu wa Marekani, alipewa ruhusa ya kusafirisha fasihi hizo kwa malori ya kijeshi.
Hata hivyo, baada ya hapo wakati Fred Paton na Hector Oates walipomwendea ofisa aliyesimamia msafara uliokuwa ukienda China na kumuuliza awape nafasi, alipandwa sana na hasira! “Eti nini?” akapaaza sauti. “Nawezaje kuwapa nafasi yenye thamani sana katika malori yangu kwa ajili ya trakti zenu duni hali mimi sina nafasi hata kidogo kwa ugavi wenye kuhitajiwa sana wa kijeshi na kitiba unaoharibikia hapa nje?” Fred alitua, akatia mkono katika mkoba wake, akamwonyesha ile barua ya ruhusa, na kutaja kwamba lingekuwa jambo la hatari sana kupuuza mwelekezo uliotolewa na maofisa katika Rangoon. Si kwamba tu msimamizi huyo wa msafara alipanga kusafirisha tani mbili za vitabu bali pia aliwapa ndugu hao lori jepesi pamoja na dereva na ugavi wa mahitaji walitumie. Walielekea kaskazini-mashariki kupitia njia hiyo hatari ya milimani ya kwenda China wakiwa na shehena yao yenye thamani kubwa. Baada ya kutoa ushahidi katika Pao-shan, walisonga mbele hadi Chungking (Pahsien). Maelfu ya fasihi mbalimbali yenye kusema juu ya Ufalme wa Yehova iligawanywa wakati wa mwaka mmoja waliotumia katika China. Miongoni mwa wale waliotolea ushahidi binafsi alikuwa Chiang Kai-shek, rais wa serikali ya Kitaifa ya China.
Wakati huohuo, kadiri Burma ilivyozidi kushambuliwa kwa mabomu, Mashahidi wote isipokuwa watatu tu waliondoka nchini, wengi wao wakielekea India. Bila shaka, utendaji wa hao watatu waliobaki ulikuwa mdogo. Hata hivyo waliendelea kutoa ushahidi ki-vivi-hivi, na jitihada zao zilizaa matunda baada ya vita.
Katika Amerika Kaskazini vilevile, Mashahidi wa Yehova walikabiliwa na vizuizi vikubwa wakati wa vita. Jeuri ya wafanyaghasia yenye kuenea na matumizi yaliyo kinyume cha katiba ya sheria za mahalimahali vilileta mkazo juu ya kazi ya kuhubiri. Maelfu walitiwa gerezani kwa sababu ya kuchukua msimamo wao wakiwa Wakristo wasiokuwamo. Hata hivyo, jambo hilo halikupunguza huduma ya nyumba hadi nyumba ya Mashahidi. Zaidi ya hilo, kuanzia na Februari 1940, lilikuwa jambo la kawaida kuwaona barabarani katika wilaya za kibiashara wakitoa Mnara wa Mlinzi na Consolation (sasa ni Amkeni!). Bidii yao ikawa yenye nguvu hata zaidi. Ingawa walikuwa wakipatwa na mnyanyaso mkali usiopata kuonwa katika sehemu hiyo ya ulimwengu, Mashahidi waliongezeka zaidi ya mara mbili katika Marekani na Kanada pia tokea 1938 hadi 1945, na wakati waliotumia katika huduma yao ya hadharani uliongezeka mara tatu.
Katika nchi nyingi zilizohusiana na Jumuiya ya Madola ya Uingereza (katika Amerika Kaskazini, Afrika, Asia, na visiwa vya Karibea na vya Pasifiki) ama Mashahidi wa Yehova ama fasihi zao zilipigwa marufuku na serikali. Mojawapo nchi hizo ni Australia. Tangazo la serikali lililotangazwa huko katika Januari 17, 1941, kwa mwelekezo wa gavana mkuu, lilifanya iwe kinyume cha sheria kwa Mashahidi wa Yehova kukutana kwa ajili ya ibada, kueneza yoyote ya fasihi zao, au hata kuwa nayo. Chini ya sheria iliwezekana kupinga marufuku hiyo mahakamani, na jambo hilo lilifanywa mara moja. Lakini ilikuwa zaidi ya miaka miwili kabla Bw. Justice Starke wa Mahakama Kuu kujulisha kwamba kanuni ambazo marufuku hiyo ilitegemea zilikuwa “matumizi mabaya ya mamlaka, kinyume cha sheria, na yenye uonevu.” Washiriki wote wa Mahakama Kuu waliiondoa marufuku hiyo. Kwa wakati huohuo Mashahidi wa Yehova walifanya nini?
Kwa kuiga mitume wa Yesu Kristo, ‘walimtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.’ (Mdo. 4:19, 20; 5:29, NW) Waliendelea kuhubiri. Vijapokuwa vizuizi vingi, hata walipanga kuwa na mkusanyiko katika Hargrave Park, karibu na Sydney, Desemba 25-29, 1941. Wakati serikali ilipokataa kusafirisha baadhi ya wajumbe kwa reli, kikundi kimoja kutoka Australia Magharibi kilitia katika magari yao vifaa vyenye kutokeza gesi vyenye kutumia makaa na kuanza safari ya siku 14 ya kuvuka nchi, iliyotia ndani kutumia juma moja wakivuka ile Tambarare ya Nullarbor iliyo kavu sana. Waliwasili salama nao wakafurahia programu pamoja na wajumbe wengine elfu sita. Mwaka uliofuata, kusanyiko lingine lilifanywa, lakini wakati huu liligawanywa kuwa vikundi vidogo 150 katika majiji saba makubwa kotekote nchini, wasemaji wakisafiri toka mahali pamoja hadi pengine.
Kadiri hali katika Ulaya zilivyozorota katika 1939, baadhi ya wahudumu mapainia wa Mashahidi wa Yehova walijitolea kutumikia katika mashamba mengine. (Linganisha Mathayo 10:23; Matendo 8:4.) Mapainia watatu kutoka Ujerumani walitumwa kutoka Uswisi hadi Shanghai, China. Idadi fulani yao walienda Amerika Kusini. Miongoni mwa wale waliohamishwa kwenda Brazili alikuwa Otto Estelmann, aliyekuwa amekuwa akitembelea na kusaidia makutaniko katika Chekoslovakia, na Erich Kattner, aliyekuwa ametumikia kwenye ofisi ya Watch Tower Society katika Prague. Mgawo wao mpya haukuwa rahisi. Walipata kwamba, katika sehemu fulani za mashamba, Mashahidi walikuwa wakiamka mapema na kuhubiri hadi saa 1:00 asubuhi na kisha kufanya utumishi zaidi wa shambani wakati wa jioni sana. Ndugu Kattner akumbuka kwamba alipokuwa akitembea toka mahali pamoja hadi pengine, mara nyingi alilala nje, akitumia mkoba wake wa fasihi kama mto.—Linganisha Mathayo 8:20.
Wote wawili Ndugu Estelmann na Ndugu Kattner walikuwa wakiwindwa daima na polisi wa siri wa Nazi katika Ulaya. Je, kuhamia kwao Brazili kuliwaokoa na mnyanyaso? Kinyume cha hivyo, baada ya mwaka mmoja tu, walijipata wakiwa wamezuiliwa nyumbani na kufungwa kwa muda mrefu kwa uchochezi wa maofisa ambao kwa wazi walikuwa marafiki wa Nazi! Upinzani kutoka kwa makasisi Wakatoliki ulikuwa wa kawaida pia, lakini Mashahidi waliendelea na kazi yao waliyopewa na Mungu. Walijitahidi daima kufikia majiji na miji katika Brazili ambayo ujumbe wa Ufalme ulikuwa haujahubiriwa.
Pitio la hali ya dunia hufunua kwamba katika nchi nyingi ambako Mashahidi wa Yehova walikuwa wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, serikali ilipiga marufuku ama tengenezo lao ama fasihi zao. Ingawa walikuwa wamekuwa wakihubiri katika nchi 117 katika 1938, katika miaka ya vita (1939-1945) ama tengenezo lao au fasihi zao zilipigwa marufuku, au wahudumu wao wakarudishwa kwenye nchi zao, katika zaidi ya nchi 60 kati ya hizo. Hata mahali ambako hakukuwa na marufuku, walikabiliwa na umati wenye ghasia na walikamatwa mara nyingi. Yajapokuwa yote hayo, kazi ya kuhubiri habari njema haikukoma.
-
-
Sehemu ya 3—Kuwa Mashahidi Hadi Sehemu ya Mbali Zaidi Sana ya DuniaMashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 451-453]
Walikataa Kuacha Kutoa Ushahidi Hata Ingawa Walitiwa Gerezani
Walioonyeshwa hapa ni baadhi tu ya maelfu ya wale walioteseka kwa ajili ya imani yao katika magereza na kambi za mateso wakati wa Vita ya Ulimwengu 2
1. Adrian Thompson, New Zealand. Alifungwa katika 1941 nchini Australia; maombi yake ya kusihi asitiwe kwenye orodha ya wanajeshi yalikataliwa wakati Australia ilipopiga marufuku Mashahidi wa Yehova. Baada ya kuachiliwa kwake, akiwa mwangalizi asafiriye, aliimarisha makutaniko katika huduma yayo ya hadharani. Alitumikia akiwa mishonari na mwangalizi asafiriye wa kwanza katika Japani baada ya vita; aliendelea kuhubiri kwa bidii hadi kifo chake katika 1976.
2. Alois Moser, Austria. Alifungwa katika magereza na kambi saba za mateso. Yeye angali Shahidi mwenye bidii katika 1992 akiwa na umri wa miaka 92.
3. Franz Wohlfahrt, Austria. Kuuawa kwa babaye na nduguye hakukumzuia Franz. Alifungwa katika Kambi ya Rollwald katika Ujerumani kwa miaka mitano. Alikuwa angali akitoa ushahidi katika 1992 akiwa na umri wa miaka 70.
4. Thomas Jones, Kanada. Alifungwa katika 1944, kisha akafungwa katika kambi mbili za kazi ngumu. Baada ya miaka 34 ya utumishi wa wakati wote, aliwekwa katika 1977 kuwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi inayosimamia kazi ya kuhubiri katika Kanada yote.
5. Maria Hombach, Ujerumani. Alifungwa mara kwa mara; katika kifungo cha peke yake kwa miaka mitatu na nusu. Akiwa tarishi, alihatirisha maisha yake kupeleka fasihi za Biblia kwa Mashahidi wenzi. Katika 1992, yeye alikuwa mshiriki mwaminifu wa familia ya Betheli akiwa na umri wa miaka 90.
6. Max na Konrad Franke, Ujerumani. Baba na mwanaye, wote wawili wakifungwa mara kwa mara, na kwa miaka mingi. (Mke wa Konrad, Gertrud, alikuwa pia gerezani.) Wote waliendelea kuwa waaminifu-washikamanifu, watumishi wa Yehova wenye bidii, na Konrad alikuwa katika mstari wa mbele wa kuanzisha upya kazi ya kuhubiri ya Mashahidi katika Ujerumani ya baada ya vita.
7. A. Pryce Hughes, Uingereza. Alihukumiwa kifungo cha miaka miwili katika Wormwood Scrubs, London; pia amepata kufungwa kwa sababu ya imani yake wakati wa Vita ya Ulimwengu 1. Alikuwa katika mstari wa mbele katika kazi ya kuhubiri Ufalme katika Uingereza hadi kufikia kifo chake katika 1978.
8. Adolphe na Emma Arnold pamoja na binti yao Simone, Ufaransa. Baada ya Adolphe kufungwa, Emma na Simone waliendelea kutoa ushahidi, na pia kugawia Mashahidi wengine fasihi. Alipokuwa gerezani, Emma, alifungwa peke yake kwa sababu ya kuendelea kutolea wafungwa wengine ushahidi. Simone alipelekwa kwenye shule ya kurekebishia tabia. Wote waliendelea kuwa Mashahidi wenye bidii.
9. Ernst na Hildegard Seliger, Ujerumani. Wote wawili wamekuwa katika magereza na kambi za mateso kwa miaka zaidi ya 40 kwa ajili ya imani yao. Hata wakiwa gerezani waliendelea kushiriki na wengine kweli za Biblia. Walipoachiliwa huru walitumia wakati wao wote wakihubiri habari njema. Ndugu Seliger alikufa akiwa mtumishi wa Mungu mwaminifu-mshikamanifu katika 1985; Dada Seliger, alikufa katika 1992.
10. Carl Johnson, Marekani. Miaka mwili baada ya kubatizwa, alifungwa pamoja na mamia ya Mashahidi wengine katika Ashland, Kentucky. Ametumikia akiwa painia na akiwa mwangalizi wa mzunguko; katika 1992, alikuwa angali akiongoza katika huduma ya shambani akiwa mzee.
11. August Peters, Ujerumani. Akitenganishwa na mke wake na watoto wanne, alifungwa katika 1936-1937, pia katika 1937-1945. Baada ya kuachiliwa, badala ya kupunguza wakati wa mahubiri, aliuongeza, katika utumishi wa wakati wote. Katika 1992, akiwa na umri wa miaka 99, yeye alikuwa angali akitumikia akiwa mshiriki wa familia ya Betheli na alikuwa ameona idadi ya Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani ikikua hadi kufikia 163, 095.
12. Gertrud Ott, Ujerumani. Alifungwa katika Lodz, Poland, kisha katika kambi ya mateso ya Auschwitz, kisha katika Gross-Rosen na Bergen-Belsen katika Ujerumani. Baada ya vita alitumikia kwa bidii akiwa mishonari katika Indonesia, Iran, and Luxembourg.
13. Katsuo Miura, Japani. Miaka saba baada ya kukamatwa na kufungwa kwake katika Hiroshima, sehemu kubwa ya gereza alimokuwa amefungiwa iliharibiwa na bomu la atomi lililofanya jiji kuwa ukiwa. Hata hivyo, madaktari hawakupata ithibati yoyote kwamba aliathiriwa na minururisho. Alitumia miaka ya mwisho ya maisha yake akiwa painia.
14. Martin na Gertrud Poetzinger, Ujerumani. Miezi michache baada ya kufunga ndoa, walikamatwa na kutenganishwa kwa miaka tisa. Martin alipelekwa Dachau and Mauthausen; Gertrud, alipelekwa Ravensbrück. Wajapotendwa kikatili, imani yao haikuyumbayumba. Baada ya kuachiliwa walitoa jitihada zao zote kwa utumishi wa Yehova. Kwa miaka 29 alitumikia akiwa mwangalizi asafiriye kotekote katika Ujerumani; kisha, akawa mshiriki wa Baraza Linaloongoza hadi kifo chake katika 1988. Katika 1992, Gertrud aliendelea kuwa mweneza-evanjeli mwenye bidii.
15. Jizo na Matsue Ishii, Japani. Baada ya kugawanya fasihi za Biblia kotekote katika Japani kwa mwongo mmoja, wakafungwa. Ingawa kazi ya Mashahidi wa Yehova katika Japani ilikomeshwa wakati wa vita, Ndugu na Dada Ishii walitoa ushahidi tena kwa bidii baada ya vita. Kufikia 1992, Matsue Ishii alikuwa ameona idadi ya Mashahidi watendaji katika Japani imeongezeka kuwa zaidi ya 171,000.
16. Victor Bruch, Luxembourg. Alifungwa katika Buchenwald, Lublin, Auschwitz, na Ravensbrück. Akiwa na umri wa miaka 90, angali anatenda akiwa mzee wa Mashahidi wa Yehova.
17. Karl Schurstein, Ujerumani. Mwangalizi asafiriye kabla ya Hitler kupata mamlaka. Alifungwa kwa miaka minane, kisha akauawa na SS katika Dachau katika 1944. Hata ndani ya kambi, aliendelea kujenga wengine kiroho.
18. Kim Bong-nyu, Korea. Alifungwa kwa miaka sita. Akiwa na umri wa miaka 72, angali anawaambia wengine kuhusu Ufalme wa Mungu.
19. Pamfil Albu, Rumania. Baada ya kutendwa kikatili, alipelekwa kwenye kambi ya kazi ngumu katika Yugoslavia kwa miaka miwili unusu. Baada ya vita alifungwa mara mbili tena, kwa miaka mingine 12. Hakuacha kusema juu ya kusudi la Mungu. Kabla ya kifo chake alisaidia maelfu katika Rumania kutumikia pamoja na tengenezo la duniani pote la Mashahidi wa Yehova.
20. Wilhelm Scheider, Poland. Alikuwa katika kambi za mateso za Nazi katika 1939-1945. Katika magereza ya Wakomunisti katika 1950-1956, pia 1960-1964. Hadi kifo chake katika 1971, alitoa nishati zake bila kuyumbayumba katika kupiga mbiu ya Ufalme wa Mungu.
21. Harald na Elsa Abt, Poland. Wakati na baada ya vita, Harald alitumia miaka 14 gerezani na katika kambi za mateso kwa sababu ya imani yake lakini aliendelea kuhubiri huko pia. Elsa alitenganishwa na binti yao mdogo na kisha akazuiwa katika kambi sita katika Poland, Ujerumani, na Austria. Kujapokuwa na marufuku ya miaka 40 juu ya Mashahidi wa Yehova katika Poland hata baada ya vita, wote waliendelea kuwa watumishi wa Yehova wenye bidii.
22. Ádám Szinger, Hungaria. Wakati wa kusikizwa kwa kesi mara sita, alihukumiwa kifungo cha miaka 23, ambacho alitumikia miaka 8 1/2 gerezani na kambi za kazi ngumu. Alipoachiliwa, alitumikia akiwa mwangalizi asafiriye kwa jumla ya miaka 30. Yeye angali mzee wa kutaniko aliye mwaminifu-mshikamanifu akiwa na umri wa miaka 69.
23. Joseph Dos Santos, Filipino. Alikuwa ametumia miaka 12 akiwa mpiga-mbiu ya ujumbe wa Ufalme kwa wakati wote kabla ya kufungwa katika 1942. Alifufua utendaji wa Mashahidi wa Yehova katika Filipino baada ya vita na akaendelea katika utumishi wa painia hadi kifo chake katika 1983.
24. Rudolph Sunal, Marekani. Alifungwa katika Mill Point, West Virginia. Baada ya kuachiliwa alitumia wakati wote kueneza ujuzi wa Ufalme wa Mungu—akiwa painia, mshiriki wa familia ya Betheli, na mwangalizi wa mzunguko. Alikuwa angali akipainia katika 1992, akiwa na umri wa miaka 78.
25. Martin Magyarosi, Rumania. Alipotoka gerezani, katika 1942-1944, aliendelea kutoa mwelekezo kwa kazi ya kuhubiri habari njema katika Transylvania. Alipoachiliwa alisafiri mahali pengi ili kutia moyo Mashahidi wenzi katika kuhubiri kwao na yeye mwenyewe alikuwa Shahidi mwenye ujasiri. Alifungwa tena katika 1950, alikufa katika kambi ya kazi ngumu katika 1953, akiwa mtumishi mwaminifu-mshikamanifu wa Yehova.
26. R. Arthur Winkler, Ujerumani na Uholanzi. Alipelekwa kwanza katika kambi ya mateso ya Esterwegen; aliendelea kuhubiri kambini. Baadaye, katika Uholanzi, alipigwa na Gestapo hadi akawa hatambuliki. Mwishowe akapelekwa Sachsenhausen. Alikuwa Shahidi mwaminifu-mshikamanifu mwenye bidii hadi kifo chake katika 1972.
27. Park Ock-hi, Korea. Alifungwa miaka mitatu katika Gereza la Sodaemun, Seoul; aliteswa vibaya sana. Katika 1992, akiwa na umri wa miaka 91, yeye alikuwa angali akitoa ushahidi kwa bidii, akiwa painia wa pekee.
-