-
Rwanda2012 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Ndugu waliokimbilia mji wa Goma walikusanyika katika Jumba la Ufalme. Baadaye, kambi ya wakimbizi ilijengwa nje ya mji na ingetoshea zaidi ya watu 2,000—Mashahidi wa Yehova pekee, watoto wao, na watu wenye kupendezwa. Ndugu walianzisha kambi nyingine kama hizo katika maeneo mengine ya mashariki mwa Kongo.
Ijapokuwa watu waliokimbia walikuwa hasa Wahutu walioogopa adhabu, Mashahidi waliokimbia pamoja walikuwa Wahutu na Watutsi. Ilikuwa hatari sana kwa Watutsi kuvuka mpaka na kuingia Goma, kwa kuwa mauaji ya Watutsi yaliendelea. Wakati mmoja, iligharimu dola 100 za Marekani kumsafirisha ndugu mmoja Mtutsi nje ya nchi kisiri.
Wakiwa nchini Kongo, akina ndugu walitaka kukaa pamoja. Hawakutaka kushirikiana kwa vyovyote na Interahamwe, waliokuwa wanaendeleza utendaji wao katika kambi zilizoanzishwa na Umoja wa Mataifa. Isitoshe, wakimbizi wengi wasio Mashahidi waliiunga mkono serikali iliyokuwa inaondolewa mamlakani. Watu hao, na hasa Interahamwe, hawakuwapenda Mashahidi wa Yehova kwa kuwa Mashahidi hawakushirikiana nao. Akina ndugu walitaka kujitenga nao ili pia wawalinde ndugu zao Watutsi.
Wakimbizi hao wa Rwanda walihitaji msaada kwa kuwa waliacha vitu vyao vyote. Mashahidi wa Yehova kutoka Kenya, Kongo, Ubelgiji, Ufaransa, na Uswisi walisaidia kwa pesa, dawa, chakula, mavazi na pia madaktari na wauguzi. Mojawapo ya ndege za kwanza za msaada, ilibeba mahema mengi madogo kutoka ofisi ya tawi ya Ufaransa. Baadaye, ofisi ya tawi ya Ubelgiji ilituma mahema makubwa, ambayo yangetoshea familia nzima-nzima. Pia, vitanda vinavyoweza kubebwa kwa urahisi na vile vya kutiwa hewa ndani vilitumwa. Ofisi ya tawi ya Kenya nayo ilituma zaidi ya tani mbili za nguo na blanketi zaidi ya 2,000.
MLIPUKO WA KIPINDUPINDU
Baada ya kukimbia Rwanda, zaidi ya Mashahidi 1,000 na watu wenye kupendezwa waliishi katika Jumba la Ufalme la Goma na katika sehemu ya ardhi iliyopakana na Jumba hilo. Inasikitisha kwamba kwa sababu ya idadi kubwa ya wakimbizi kulitokea mlipuko wa maradhi ya kipindupindu mjini Goma. Upesi, ofisi ya tawi ya Kongo (Kinshasa) ilituma dawa, na Ndugu Van Bussel akapeleka makatoni 60 ya dawa kutoka Nairobi hadi Goma. Kwa muda, Jumba la Ufalme lilitumiwa kama hospitali, na jitihada zilifanywa ili kuwatenga wagonjwa. Loic Domalain na ndugu mwingine, wote wawili madaktari, pamoja na Aimable Habimana, daktari msaidizi kutoka Rwanda, walifanya kazi mfululizo. Pia, Ndugu Hamel kutoka Ufaransa alisaidia sana na vilevile ndugu na dada wengi wenye ujuzi wa kimatibabu walijitolea kuwatunza wagonjwa.
Licha ya jitihada kubwa za kuzuia ugonjwa huo, zaidi ya ndugu na watu wenye kupendezwa 150 waliathirika, na 40 hivi wakafa kabla ya ugonjwa huo wenye kufisha kukomeshwa. Baadaye, ndugu walikodi sehemu kubwa ya ardhi ambayo ingetumiwa kama kambi ya Mashahidi wa Yehova. Mamia ya mahema madogo-madogo yalisimamishwa, na hema moja kubwa kutoka Kenya lilitumiwa kama hospitali. Wafanyakazi wa afya kutoka Marekani walivutiwa na usafi na mpangilio walioona katika kambi hiyo.
Kufikia mapema Agosti 1994, halmashauri ya kutoa misaada mjini Goma ilikuwa ikiwatunza wakimbizi 2,274—Mashahidi, watoto, na watu wenye kupendezwa. Wakati huohuo, kulikuwa na ndugu wengine wakimbizi katika miji ya Bukavu na Uvira, iliyo mashariki mwa Kongo, na pia nchini Burundi. Wengine 230 walikuwa katika kambi moja ya wakimbizi nchini Tanzania.
Ndugu katika ofisi ya kutafsiri mjini Kigali walipolazimika kukimbilia Goma, walikodi nyumba ili kuendelea na kazi ya kutafsiri. Wakati wa vita akina ndugu walifaulu kuficha kompyuta na jenereta moja na wakazihamisha kutoka Kigali hadi Goma.
Mjini Goma, hamkuwa na huduma za simu wala za kutuma au kupokea barua. Hata hivyo, kwa msaada wa Mashahidi waliofanya kazi katika uwanja wa ndege, ndugu walituma makala walizotafsiri na pia barua nyingine kwa ndege kila juma kutoka Goma hadi Nairobi. Nayo ofisi ya tawi ya Kenya iliwatumia barua kupitia njia hiyohiyo.
Emmanuel Ngirente na watafsiri wengine wawili waliendea kufanya yote waliyoweza ijapokuwa hali zilikuwa ngumu. Hawakutafsiri makala zote za Mnara wa Mlinzi kwa sababu ya vita, lakini makala hizo zilitafsiriwa baadaye na kuchapishwa katika broshua za pekee ambazo ndugu walijifunza katika Funzo la Kitabu la Kutaniko.
MAISHA KATIKA KAMBI ZA WAKIMBIZI
Huku watu wengi wakikimbia kutoka Kigali, Francine, ambaye alikuwa amekimbia na kwenda Goma baada ya mume wake Ananie kuuawa, alihamishwa na kupelekwa katika kambi moja ya Mashahidi. Anasema hivi kuhusu maisha katika kambi: “Kila siku, akina ndugu na dada fulani walipewa mgawo wa kutayarisha chakula. Tulitayarisha uji wa mtama au mahindi kwa ajili ya kiamsha kinywa. Pia, tulipika chakula cha mchana. Baada ya kumaliza kazi, tulienda kuhubiri. Tuliwahubiria hasa watu wa familia zetu ambao si Mashahidi na pia watu walioishi nje ya kambi. Hata hivyo, baada ya muda, wapiganaji wa Interahamwe ambao walikuwa katika kambi nyingine, walikasirika kuona kwamba Mashahidi walikuwa katika kambi tofauti na wakimbizi wengine, na hilo likafanya hali ziwe hatari sana.”
Kufikia Novemba 1994, ilidhihirika wazi kwamba ni salama kwa ndugu kurudi Rwanda. Kwa kweli, ingefaa sana kurudi kwa sababu ya ukosefu wa usalama katika kambi za watu wasio Mashahidi zilizokuwa Kongo. Lakini ingekuwa vigumu kurudi. Interahamwe walinuia kujipanga tena na kuivamia Rwanda, na hivyo, mtu yeyote aliyerudi Rwanda kutoka Kongo alionwa kuwa msaliti.
Ndugu waliijulisha serikali ya Rwanda kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuunga mkono vita wala kushiriki katika mauaji ya Watutsi, na walitaka kurudishwa Rwanda. Serikali iliwashauri wazungumze na Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi (UNHCR), kwa kuwa ilikuwa na magari yanayoweza kutumiwa kuwarudisha nyumbani. Hata hivyo, kwa sababu Interahamwe wangewazuia kurudi Rwanda, ilibidi ndugu watumie maarifa.
Ndugu walitangaza kwamba kutakuwa na kusanyiko la pekee mjini Goma, na wakatayarisha mabango ya kusanyiko. Kisha wakawajulisha Mashahidi kisiri kuhusu mipango ya kurudishwa Rwanda. Ili kuepuka kutokeza shaka, ndugu waliagizwa kuacha vitu vyao vyote na kubeba tu Biblia zao na vitabu vya nyimbo kana kwamba wanaenda kusanyikoni.
Francine anakumbuka kwamba walitembea kwa saa kadhaa kisha wakapata malori yaliyowabeba hadi mpakani.
-
-
Rwanda2012 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Mauaji ya jamii nzima-nzima yalipoanza, nililazimika kuondoka Rwanda. Lakini punde tu baada ya hapo, niliombwa niwasaidie wakimbizi waliokuwa mashariki mwa Kongo. Nilisafiri kutoka Nairobi hadi Goma, mji ulio karibu na mpaka wa Rwanda. Sikuwa na habari zozote ila jina la mzee mmoja tu, na kwa sababu ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika huko, sikujua ningempata jinsi gani. Hata hivyo, nilipofika, nilimuuliza dereva wa teksi iliyonibeba ikiwa anamfahamu. Alizungumza na madereva wengine na hata kabla ya dakika thelathini kuisha, nilikuwa nimesimama mlangoni mwa mzee huyo. Ndugu wawili wa Halmashauri ya Nchi ya Rwanda walifaulu kuvuka mpaka na kuingia Goma, na nikawapa pesa nilizopokea kutoka kwa ofisi ya tawi ya Kenya ili wawasaidie ndugu nchini Rwanda.
Mara ya pili nilipoenda Goma kutoka Nairobi, nakumbuka nikitembea hadi kwenye mpaka wa Rwanda. Ingawa haikuwa mbali, nilitumia muda mrefu kwa sababu ya wakimbizi wengi niliopishana nao wakitoka Rwanda.
Bila kutarajia, mtu fulani aliniita: “Ndugu Henk! Ndugu Henk!” Nilipotazama upande ambao sauti hiyo ilitoka, nilimwona Alphonsine, msichana mwenye umri wa miaka 14 hivi, kutoka kutaniko nililokuwa nikishirikiana nalo mjini Kigali. Alphonsine alikuwa ametenganishwa na mama yake. Tulikaa pamoja katika umati huo mkubwa, na kisha nikampeleka kwenye Jumba la Ufalme ambapo ndugu na dada wengi wakimbizi walikusanyika. Familia moja kutoka Kongo walimtunza, na baada ya hapo dada mmoja mkimbizi kutoka kutaniko la kwao alimwandalia mahitaji yake. Mwishowe, Alphonsine aliungana na mama yake mjini Kigali.
-