-
“Si Kosa Langu”Amkeni!—1996 | Septemba 22
-
-
“Si Kosa Langu”
NI MARA nyingi kadiri gani leo usikiapo mtu akisema, ‘Nasikitika. Lilikuwa kosa langu. Napaswa kulaumika kabisa!’? Ni nadra sana ufuatiaji wa haki ulio sahili hivyo kusikiwa tena. Kwa hakika, katika visa vingi, hata wakati kosa lakiriwa, kila jitihada inafanywa ili kumwekea mtu fulani lawama au kulaumu hali zenye kupunguza ukubwa wa kosa ambazo mkosaji adai hakuweza kuzidhibiti.
Wengine hata hulaumu jeni zao! Lakini je, hili laweza kuaminika? Kitabu Exploding the Gene Myth hutilia shaka malengo na matokeo ya sehemu fulani za utafiti wa jeni. Mwandikaji wa habari wa Australia aitwaye Bill Deane, katika pitio lake la kitabu hicho, afikia mkataa huu wa kusababu kiakili: “Watu waaminio kwamba kila kitu kinaamuliwa na hali zilizopo yaonekana hivi karibuni wameanza kuamini kwamba wamepata uthibitisho unaoelekea kutokuwa na kasoro ili kutegemeza falsafa yao kwamba hakuna mtu apaswaye kutozwa hesabu kwa matendo yake: ‘Hakuweza kujizuia asikate koo la mhasiriwa wake, Mheshimiwa—aliongozwa na maumbile yake ya kijeni.’”
Kwa Kweli Si Mwelekeo Mpya
Kizazi hiki kinapositawi na kuwa kile ambacho mwandikaji mmoja akiita kizazi cha “si-mimi,” mwelekeo huu huenda ukaonekana kuwa unaongezeka. Hata hivyo, historia iliyorekodiwa hufunua kwamba kulaumu wengine, kwa kutoa udhuru kwamba “kwa kweli si mimi nipaswaye kulaumika,” kumekuwapo tangu mwanzo wa mwanadamu. Itikio la Adamu na Hawa baada ya dhambi yao ya kwanza, kula tunda lililokatazwa na Mungu, lilikuwa kielelezo halisi cha kulaumu wengine. Simulizi la Mwanzo huripoti mazungumzo yaliyokuwapo, Mungu akisema kwanza: “Je! umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.”—Mwanzo 3:11-13.
Tangu wakati huo, wanadamu wamevumbua njia tofauti-tofauti za itikadi na wametafuta udhuru usio wa kawaida ambao utawaondolea wajibu wowote wa kweli wa kutozwa hesabu kwa matendo yao. Wenye kutokeza kati ya udhuru huo ni ile itikadi ya kale katika ajali. Mwanamke Mbuddha ambaye aliamini kwa unyoofu katika Karma alisema: “Nilifikiri kwamba lilikuwa jambo lisiloeleweka kuteseka kwa kitu nilichozaliwa nacho na ambacho sikujua chochote kukihusu. Nililazimika kukikubali kuwa kitu nilichopangiwa kimbele.” Ikisitawishwa na fundisho la kuamuliwa kimbele yatakayokupata lililofundishwa na John Calvin, itikadi katika ajali pia ni jambo la kawaida katika Jumuiya ya Wakristo. Mara nyingi makasisi huambia watu wa ukoo wenye kuomboleza kwamba aksidenti fulani ilikuwa mapenzi ya Mungu. Kisha, pia, Wakristo fulani wenye nia nzuri humlaumu Shetani kwa kila kitu kinachokwenda vibaya maishani mwao.
Sasa, twaanza kushuhudia mwenendo usiotozwa hesabu ambao unakubaliwa kisheria na kijamii. Twaishi katika muhula wa haki zenye kuongezeka na madaraka yenye kupungua ya watu mmoja-mmoja.
Utafiti kuhusu mwenendo wa kibinadamu umetokeza eti uthibitisho wa kisayansi ambao watu wengine wanahisi waweza kuruhusu kabisa mwenendo kuanzia ukosefu wa adili hadi uuaji-kimakusudi. Hilo laonyesha hamu ya jamii kulaumu chochote kile, au yeyote yule, isipokuwa mtu anayehusika.
Twahitaji majibu kwa maswali kama haya: Sayansi imegundua nini hasa? Je, mwenendo wa binadamu unaamuliwa na jeni hasa? Au kani za ndani na za nje hudhibiti mwenendo wetu? Uthibitisho waonyesha nini kikweli?
-
-
Je, Ni Jeni Zetu Ziamuazo Tutakayotenda?Amkeni!—1996 | Septemba 22
-
-
Je, Ni Jeni Zetu Ziamuazo Tutakayotenda?
“TULIZOEA kufikiri kwamba ajali yetu huamuliwa na unajimu. Sasa twajua, kwa kiwango kikubwa, ajali yetu inaamuliwa na jeni zetu.” Hivyo ndivyo alivyosema James Watson, aliyenukuliwa mwanzoni mwa kitabu Exploding the Gene Myth, kilichoandikwa na Ruth Hubbard na Elijah Wald. Hata hivyo, chini tu ya mnukuo wa Watson, R. C. Lewontin, Steven Rose, na Leon J. Kamin wananukuliwa wakisema: “Hatuwezi kuwazia juu ya mwenendo wowote wa kijamii wenye maana ulioko kiasili katika jeni zetu katika njia ya kwamba hauwezi kurekebishwa na hali za kijamii.”
Karatasi yenye kufunika kitabu hicho hufupisha baadhi ya yaliyomo ndani yacho na kuanza kwa swali la maana, “Je, mwenendo wa binadamu unaongozwa na jeni?” Yaani, je, mwenendo wa binadamu unaamuliwa kabisa na jeni ambazo hupitisha hulka zenye kurithiwa na vitabia vya kibiolojia vya kiumbe-hai? Je, mwenendo fulani usio wa adili ukubaliwe kwa msingi wa kwamba unaongozwa na jeni? Je, wahalifu washughulikiwe wakiwa wahasiriwa wa msimbo jeni, wakiwa hawawezi kulaumika kwa sababu ya kuelekezwa na jeni?
Hatuwezi kukataa kwamba wanasayansi wamefanya ugunduzi wenye manufaa katika karne hii. Miongoni mwa ugunduzi huu ni DNA yenye kushangaza, iitwayo eti ramani ya mfanyizo wetu wa kijeni. Habari iliyo katika msimbo jeni imeshangaza wanasayansi na watu wa kawaida vilevile. Utafiti katika upande wa jeni umegundua nini hasa? Yaliyopatikana yanatumiwaje kutegemeza fundisho la kisasa la upangaji-kimbele wa kibiolojia au kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu?
Vipi Juu ya Ukosefu wa Uaminifu na Ugoni-Jinsia-Moja?
Kulingana na makala iliyotangazwa katika The Australian, utafiti fulani wa kijeni huthibitisha kwamba “yaelekea ukosefu wa uaminifu uko katika jeni zetu. . . . Yaonekana kwamba utu wetu wa kukosa uaminifu wa kingono uliamuliwa kimbele kuwa hivyo.” Fikiria tu jinsi mtazamo huu uwezavyo kuleta uharibifu katika ndoa na familia kwa kufanyiza fursa kwa yeyote asiyetaka kulaumika kwa mtindo-maisha wake wa ngono za ovyo-ovyo!
Kuhusu ugoni-jinsia-moja, gazeti Newsweek lilikuwa na kichwa kikuu “Ni wa Kuzaliwa Nao au wa Kusitawishwa?” Makala hiyo ilitaarifu: “Sayansi na tiba ya kiakili zang’ang’ana kufahamu utafiti mpya unaodokeza kwamba huenda ugoni-jinsia-moja ukawa jambo la tabia za urithi, si wa kukuzwa. . . . Katika jumuiya yenyewe ya wagoni-jinsia-moja, wengi hukubali dokezo kwamba ugoni-jinsia-moja huanza katika chembeuzi.”
Kisha makala hiyo yamnukuu Dakt. Richard Pillard, ambaye alisema: “Ikiwa mapendezi ya mtu kuelekea ngono yanaamuliwa na jeni, basi hilo lamaanisha ‘Hii si kasoro, wala si kosa lako.’” Akiimarisha tetezi hili la “kutokuwa na kosa,” Frederick Whitam, mtafiti wa ugoni-jinsia-moja, aonelea kwamba “kuna mwelekeo wa watu kutweta kwa kuhisi kitulizo, wanapoambiwa kwamba ugoni-jinsia-moja ni wa kiasili. Huondolea familia na wagoni-jinsia-moja hatia. Humaanisha pia kwamba jamii haihitaji kuwa na wasiwasi kuhusu mambo kama vile walimu walio wagoni-jinsia-moja.”
Nyakati fulani, ule uitwao eti uthibitisho kwamba mielekeo ya ugoni-jinsia-moja huamuliwa na jeni huonyeshwa na vyombo vya habari kuwa wa uhakika na wa mkataa badala ya kuwa jambo liwezekanalo na lisilo la mkataa.
Gazeti New Statesman & Society hukashifu ustadi wenye kuvutia katika kuripoti ugunduzi huo: “Msomaji aliyeduwaa huenda hakuona kwamba huo uthibitisho halisi wa hakika ulikuwa wa kijuu-juu—au, kwa kweli, kutowepo kabisa kwa msingi wa dai lililo wazi la kisayansi kwamba uovyoovyo wa kingono “umepangwa katika ubongo wa mtu wa kiume.’” Katika kitabu chao Cracking the Code, David Suzuki na Joseph Levine huongeza hangaiko lao kuhusu utafiti wa wakati huu wa jeni: “Ingawa yawezekana kutetea kwamba jeni huathiri mwenendo katika maana ya ujumla, ni jambo jingine kabisa kuonyesha kwamba jeni hususa—au jeni 2, au hata jeni 20—kwa hakika hudhibiti mambo hususa ya jinsi mnyama anavyoitikia mazingira yake. Kufikia hapa, ni jambo la haki kuuliza ikiwa kuna mtu yeyote ambaye amepata, katika maana halisi ya kimolekuli ya kutafuta na kubadili, nyuzi zozote za DNA ambazo huathiri mienendo hususa.”
Jeni za Uraibu wa Alkoholi na Uhalifu
Uchunguzi wa uraibu wa alkoholi umeshangaza watafiti wengi wa jeni kwa miaka mingi ambayo imepita. Wengine hudai kwamba uchunguzi umeonyesha kwamba kuwepo au kutowepo kwa jeni fulani ndiko husababisha uraibu wa alkoholi. Kwa kielelezo, jarida The New England Journal of Medicine liliripoti katika 1988 kwamba “katika mwongo uliopita, chunguzi tatu tofauti zimetokeza uthibitisho wenye mkataa kwamba uraibu wa alkoholi ni kitabia cha kurithiwa.”
Hata hivyo, wataalamu fulani katika uwanja wa uraibu sasa wanapinga maoni ya kwamba uraibu wa alkoholi unachochewa kwa sehemu kubwa na visababu vya kiasili. Ripoti moja katika The Boston Globe la Aprili 9, 1996, ilitaarifu: “Haielekei kwamba jeni ya uraibu wa alkoholi itapatikana katika wakati ujao ulio karibu, na baadhi ya watafiti hukubali kwamba kile ambacho huenda wakapata ni kukosa uthabiti kunakofanya watu fulani wanywe kupita kiasi bila kulewa—kitabia kiwezacho kuwafanya wapatwe na uraibu wa alkoholi.”
Gazeti The New York Times liliripoti kuhusu mkutano uliofanywa kwenye Chuo Kikuu cha Maryland uliokuwa na kichwa “Maana na Umuhimu wa Utafiti wa Tabia za Urithi na Mwenendo wa Uhalifu.” Wazo la kwamba kuna jeni yenye kuchochea uhalifu ni sahili sana. Watangazaji wengi wana hamu ya kuunga mkono mwelekeo huo. Mwandikaji wa kisayansi katika The New York Times Magazine alisema kwamba uovu waweza “kuwapo katika mitatio ya chembeuzi ambazo wazazi wetu hutupitishia wakati wa kutungwa mimba.” Makala moja katika The New York Times iliripoti kwamba mazungumzo yenye kuendelea juu ya jeni ya uhalifu hutokeza wazo la kwamba uhalifu una “chanzo kimoja—kasoro ya ubongo.”
Jerome Kagan, mwanasaikolojia wa Harvard, atabiri kwamba wakati utakuja ambapo majaribio ya kijeni yatatambulisha watoto walio na mwelekeo wa kuwa na mwenendo wenye jeuri. Watu fulani hudokeza kwamba huenda kukawa na tumaini la kudhibiti uhalifu kupitia urekebishaji wa kibiolojia badala ya kupitia urekebishaji wa kijamii.
Lugha iliyotumiwa katika ripoti za makisio haya kuhusu msingi wa kijeni kwa mwenendo, mara nyingi si wazi na haina uhakika. Kitabu Exploding the Gene Myth chaeleza juu ya uchunguzi uliofanywa na Lincoln Eaves, mtaalamu wa uvutano wa jeni kwa mwenendo, ambaye alisema kwamba alipata uthibitisho wa kisababishi cha kijeni kwa mshuko-moyo. Baada ya kuchunguza wanawake walioonwa kwamba huelekea kupatwa na mshuko-moyo, Eaves “alidokeza kwamba mtazamo na namna ya kushuka moyo [wa wanawake hao] huenda ulifanya matatizo aina nyingi yaelekee kutokea.” Ni nini hayo “matatizo aina nyingi”? Wanawake waliochunguzwa walikuwa “wamebakwa, kutendwa vibaya, au kufutwa kazi.” Kwa hiyo ni mshuko-moyo uliosababisha matukio haya yenye kufadhaisha? “Huko ni kufikiri kwa aina gani?” chaendelea kitabu hicho. “Wanawake hao walikuwa wamebakwa, kutendwa vibaya, au kufutwa kazi, nao walishuka moyo. Kadiri walivyopatwa na matukio yenye kufadhaisha, ndivyo mshuko-moyo ulivyokuwa mbaya zaidi. . . . Ingestahili kutafuta kiunganishi cha kijeni ikiwa yeye [Eaves] alipata kwamba mshuko-moyo haukuhusiana na ono lolote la maisha.”
Kichapo hicho-hicho chasema kwamba hadithi hizi “zafanana sana na ripoti za wakati huu kuhusu jeni [za kimwenendo], katika vyombo vya habari na vilevile katika majarida ya kisayansi. Yana mchanganyiko wa mambo ya hakika yenye kupendeza, makisio yasiyo na utegemezo, na kuongeza chumvi kusiko na msingi kwa umaana wa jeni katika maisha yetu. Jambo lenye kutokeza kuhusu mwingi wa uandikaji huu ni ukosefu wao wa udhahiri.” Chaendelea hivi: “Kuna tofauti kubwa kati ya kushirikisha jeni na hali zinazofuata kigezo cha urithi cha Mendel na kutumia ‘mielekeo’ ya kijeni ya kinadhariatete kuelezea hali zilizo tata kama vile kansa na msongo wa juu wa damu. Wanasayansi wanafikia mkataa mwingine haraka wanapodokeza kwamba utafiti wa kijeni waweza kusaidia kueleza mienendo ya kibinadamu.”
Hata hivyo, kulingana na yaliyo juu, maswali yatokezwayo mara nyingi bado yabaki: Kwa nini nyakati fulani sisi huona mabadiliko ya vigezo vya kimwenendo maishani mwetu? Na tuna udhibiti gani katika hali kama hizo? Twaweza kupataje na kudumisha udhibiti wa maisha yetu? Makala ifuatayo yaweza kusaidia katika kuandaa baadhi ya majibu ya maswali haya.
-
-
Dhibiti Maisha Yako Sasa!Amkeni!—1996 | Septemba 22
-
-
Dhibiti Maisha Yako Sasa!
UTAFITI wa kisayansi kuhusu mwenendo na msukumo wa kibinadamu umetunufaisha kwa njia nyingi. Labda tumesaidiwa kukabiliana na ugonjwa kwa kuwa na ufahamu wa kina kuuhusu. Kwa wakati uo huo, ni jambo la busara kutahadhari kuhusu nadharia zenye kuchochea hisia, hasa zile ambazo yaonekana zapingana na kanuni zilizowekwa.
Kuhusu suala la jeni na mwenendo, maswali yazuka: Je, twaweza kuondosha lawama na kutokubali kulaumika kwa matendo yetu? Je, twaweza kutoa udhuru au hata kumlaumu mtu fulani au kitu kingine kwa ukosefu wowote wa busara au kosa tulilofanya, hivyo tukijiunga na idadi yenye kuongezeka katika kizazi hiki cha “si-mimi”? Sivyo hata kidogo. Watu walio wengi hukubali kwa utayari sifa kwa mafanikio yoyote maishani, kwa hiyo kwa nini wasikubali kwa utayari vilevile lawama kwa makosa yao?
Kwa hiyo, twaweza kuuliza, Neno la Mungu Biblia Takatifu, husema nini kuhusu ni nani au ni nini kiongozacho maisha yetu leo?
Maoni ya Biblia Ni Nini?
Jambo la kwanza tupaswalo kutambua ni kwamba sisi sote huzaliwa katika dhambi iliyorithiwa kutoka kwa wazazi wetu wa awali, Adamu na Hawa. (Zaburi 51:5) Kwa kuongezea, twaishi katika wakati wa kipekee, uitwao “siku za mwisho,” wakati ambapo watu wanajionea “nyakati zilizo ngumu kushughulika nazo.” (2 Timotheo 3:1, NW) Hilo laonyesha kwamba, kwa ujumla, twakumbana na matatizo katika kudhibiti maisha yetu ifaavyo kuliko waliotutangulia walivyofanya.
Hata hivyo, wanadamu wote ni viumbe hai walio huru kuchagua mwendo watakaofuatia, wawezao kufanya machaguo yao ya kibinafsi. Kwa kadiri hiyo wanadhibiti maisha yao. Imekuwa hivyo tangu nyakati za mapema na inaweza kuonwa kwa maneno ya Yoshua kwa taifa la Israeli: “Chagueni hivi leo mtakayemtumikia.”—Yoshua 24:15.
Biblia hukubali kwamba Shetani Ibilisi ametupwa kutoka mbinguni na sasa, zaidi ya wakati mwingineo wote, ana uvutano wenye nguvu wa kuifanyia mabaya jamii yote ya kibinadamu. Hiyo pia hutuambia kwamba hata katika siku za mtume Yohana, ulimwengu wote ulikuwa chini ya uwezo wa yule mwovu. (1 Yohana 5:19; Ufunuo 12:9, 12) Hata hivyo, kama vile Mungu Mweza Yote hadhibiti kila kitendo chetu au kupanga kimbele mwisho anaoujua yeye pekee, hatupaswi kumwekea Shetani lawama moja kwa moja kwa kila kosa au ukosefu wetu wa mafanikio. Kweli ya Kimaandiko yenye kusawazisha ni kwamba “kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi.” (Yakobo 1:14, 15) Mtume Paulo aliandika maneno haya yaliyopuliziwa: “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.”—Wagalatia 6:7.
Kwa hiyo Yehova Mungu anatutoza hesabu mtu mmoja-mmoja kwa matendo yetu. Twapaswa kuwa waangalifu tusijaribu kujiondolea lawama kwa sababu ya mfanyizo wetu wa kijeni na kutokamilika tulikorithi. Mungu aliitaka jumuiya yenye jeuri, ya ugoni-jinsia-moja ya Sodoma na Gomora ya kale itoe hesabu kwa matendo yayo yenye ufisadi. Kwa wazi, yeye hakuona wakazi hao kuwa viumbe maskini, wa kuhurumiwa ambao hawakuweza kujizuia eti kwa sababu ya kasoro fulani ya kijeni. Sawa na hivyo; watu walioishi katika siku za Noa walikuwa na uvutano mwingi mwovu kuwazunguka; hata hivyo iliwabidi wafanye chaguo, uamuzi wa kibinafsi, ikiwa wangalisalimika Gharika iliyokuwa karibu kutokea. Ni wachache waliofanya chaguo lifaalo. Wengi hawakufanya hivyo.
Nabii Mwebrania Ezekieli athibitisha udhibiti wa kibinafsi wahitajiwa ikiwa tutapata upendeleo wa Mungu: “Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.”—Ezekieli 3:19.
Msaada Bora Zaidi Wapatikana
Bila shaka, sote twahitaji msaada ili kujidhibiti kibinafsi katika maisha yetu ya kila siku, na kwa wengi wetu, hili ni tatizo gumu sana. Lakini hatuhitaji kukata tumaini. Ingawa mielekeo yetu iliyorithiwa ya kutenda dhambi haikubaliwi na Mungu, ikiwa tunataka kurekebisha mwenendo wetu, yeye atatuandalia msaada bora zaidi upatikanao—roho yake takatifu na kweli yake iliyopuliziwa. Licha ya mwelekeo wa kijeni ambao huenda tukawa nao na uvutano wowote wa nje ambao huenda ukatuathiri, twaweza ‘kuuvua utu wa zamani pamoja na mazoea ya huo, na kujivika wenyewe utu mpya, ambao kupitia ujuzi sahihi unafanywa kuwa mpya kulingana na mfano wa Yule aliyeuumba.’—Wakolosai 3:9, 10, NW.
Wakristo wengi katika kutaniko la Korintho walifanya mabadiliko yenye kutazamisha katika mwenendo wao. Rekodi iliyopuliziwa hutuambia: “Waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.”—1 Wakorintho 6:9-11.
Kwa hiyo ikiwa twang’ang’ana na kutokamilika, tusijiache tushindwe, Wakristo wengi wa siku ya kisasa wamethibitisha kwamba kwa msaada wa Yehova, waliweza ‘kugeuzwa kwa kufanya upya nia zao, wapate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.’ Wao hulisha akili zao na mambo yoyote yaliyo ya kweli, ya uadilifu, safi, yenye kupendeka, yenye sifa njema, na yenye kusifika; nao huendelea ‘kuyatafakari hayo.’ Wao hula chakula kigumu cha kiroho na kwa kukitumia wanazoeza uwezo wao wa kufahamu ili kutofautisha lililo jema na baya.—Warumi 12:2; Wafilipi 4:8; Waebrania 5:14.
Inachangamsha moyo kujua juu ya ming’ang’ano yao, kutofaulu kwao kwa muda, na mafanikio yao ya hatimaye kwa msaada wa roho takatifu ya Mungu. Mungu atuhakikishia kwamba kubadili mwenendo wetu mara nyingi huhusisha moyo na tamaa zao: “Hekima itaingia moyoni mwako, na maarifa yatakupendeza nafsi yako, busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi. Ili kukuokoa na njia ya uovu.”—Mithali 2:10-12.
Kwa hivyo, ikiwa wataka kufanya uhai udumuo milele uwe mradi wako—maisha yasiyo na taabu za ulimwengu huu mwovu na yasiyo na kutokamilika kwenye kudhoofisha—‘jitahidi’ kudhibiti maisha yako sasa na kuongozwa na hekima ya kimbingu. (Luka 13:24) Jiache usaidiwe na roho takatifu ya Yehova ili uweze kutokeza matunda ya kujidhibiti. Fanya kupatanisha maisha yako na sheria za Mungu kuwe tamaa ya moyo wako, na utii shauri hili: “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.” (Mithali 4:23) Kupata “uzima ulio kweli kweli” katika ulimwengu mpya wa Mungu—ambao katika huo Yehova Mungu atarekebisha mapungukio yoyote ya kijeni kwa msingi wa imani katika dhabihu ya fidia ya Yesu Kristo—kwastahili jitihada zote unazofanya za kudhibiti maisha yako katika ulimwengu huu!—1 Timotheo 6:19; Yohana 3:16.
-