Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • 2000—Je, Ni Mwaka wa Pekee?
    Mnara wa Mlinzi—1999 | Novemba 1
    • 2000—Je, Ni Mwaka wa Pekee?

      JE, MWAKA wa 2000 ni wa pekee kwa njia fulani? Kwa ujumla watu wanaoishi katika nchi za magharibi huuona kuwa mwaka wa kwanza wa milenia ya tatu. Matayarisho makubwa ya kuusherehekea yameanza. Saa kubwa sana za elektroni zinawekwa ili kuhesabu sekunde zinazobaki kabla ya milenia mpya kufika. Sherehe za dansi za Mkesha wa Mwaka Mpya zinapangwa. T-shati zenye misemo juu ya mwisho wa milenia zinauzwa kwenye maduka ya vijijini na vilevile kwenye maduka makubwa ya majijini.

      Makanisa, makubwa kwa madogo, yatajiunga na sherehe hizo za mwaka mzima. Mapema mwaka ujao, Papa John Paul wa Pili anatarajiwa kusafiri kwenda Israeli ili kuwaongoza Wakatoliki katika ile ambayo imeitwa “Sherehe ya yubile ya milenia ya Kanisa Katoliki.” Inakadiriwa kwamba kati ya watalii milioni mbili u nusu hadi milioni sita, wakitia ndani wanadini na wadadisi, wanapanga kuzuru Israeli mwaka ujao.

      Kwa nini watu wengi hivyo wanapanga kuzuru Israeli? Akizungumza kwa niaba ya papa, Kadinali Roger Etchegaray, ofisa wa Vatikani, alisema: “Mwaka wa 2000 ni sherehe ya Kristo na maisha yake katika nchi hii. Hivyo, inafaa kwa Papa kuja hapa.” Mwaka wa 2000 unahusianaje na Kristo? Mwaka wa 2000 hufikiriwa kwa kawaida kuwa miaka 2,000 kamili tangu Kristo azaliwe. Lakini je, ndivyo ilivyo? Tutaona.

      Mwaka wa 2000 ni wa maana hata zaidi kwa wafuasi wa dini fulani-fulani. Wanasadiki kwamba katika mwaka ujao au baadaye kidogo, Yesu atarudi kwenye Mlima wa Mzeituni nayo vita ya Har–Magedoni, ambayo imetajwa katika kitabu cha Ufunuo, itapiganwa katika bonde la Megido. (Ufunuo 16:14-16) Kwa kutarajia matukio hayo, mamia ya wakazi wa Marekani wanauza makao yao na karibu mali zao zote na kuhamia Israeli. Kwa manufaa ya wowote wale wasioweza kuacha makao yao, inasemekana kwamba Mweneza-evanjeli mmoja mashuhuri wa Marekani ameahidi kutangaza kurudi kwa Yesu kupitia televisheni ya rangi!

      Katika nchi za Magharibi, mipango ya kuikaribisha milenia ya tatu inaongezeka. Hata hivyo, watu katika nchi nyinginezo wanaendelea na shughuli zao za kawaida. Watu hao—ambao ndio wengi zaidi ulimwenguni—hawaamini kwamba Yesu wa Nazareti alikuwa ndiye Mesiya. Hata si lazima wakubali utaratibu wa kuweka tarehe wa K.K. na A.D.a Kwa mfano, Waislamu wengi hutumia kalenda yao wenyewe, na kulingana na kalenda yao mwaka ujao utakuwa 1420—wala si 2000. Waislamu huhesabu miaka kuanzia tarehe ambayo Muhammad alikimbia kutoka Mecca kwenda Medina. Kwa ujumla, watu ulimwenguni kote hutumia kalenda tofauti-tofauti zipatazo 40.

      Je, mwaka wa 2000 wapaswa kuwa muhimu kwa Wakristo? Je, kweli Januari 1, 2000, ni siku yenye maana ya pekee? Maswali hayo yatajibiwa katika makala ifuatayo.

      [Maelezo ya chinis]

      a Katika utaratibu wa kuweka tarehe wa K.K. na A.D., matukio yaliyotokea kabla ya wakati wa kimapokeo wa kuzaliwa kwa Yesu huitwa miaka ya “K.K.” (kabla ya Kristo); nayo yale yaliyotokea baadaye huitwa miaka ya “A.D.”(Anno Domini—“katika mwaka wa Bwana wetu.”) Hata hivyo, wasomi fulani wenye ujuzi hupendelea kutumia usemi usio wa kidini “K.W.K.” (kabla ya Wakati wetu wa Kawaida) na “W.K.” (-a Wakati wetu wa Kawaida.)

  • Milenia ya Tatu Inaanza Lini?
    Mnara wa Mlinzi—1999 | Novemba 1
    • Milenia ya Tatu Inaanza Lini?

      JE, UMESIKIA dai la kwamba milenia ya tatu itaanza mwaka wa 2001 bali si mwaka wa 2000? Dai hilo ni kweli—kwa kadiri fulani. Tukisema kwamba Yesu Kristo alizaliwa katika ule uitwao sasa mwaka wa 1 K.W.K., kama wengine walivyodhania, basi Desemba 31, 2000 (wala si 1999), kwa kweli ndiyo tarehe itakayokuwa mwisho wa milenia ya pili, na Januari 1, 2001, iwe mwanzo wa milenia ya tatu.a Hata hivyo, leo karibu wasomi wote hukubali kwamba Yesu Kristo hakuzaliwa mwaka wa 1 K.W.K. Hivyo basi, yeye alizaliwa lini?

      Yesu Alizaliwa Lini?

      Biblia haifunui tarehe kamili ya kuzaliwa kwa Yesu. Hata hivyo, hiyo husema kwamba alizaliwa “siku za Herode mfalme.” (Mathayo 2:1) Wasomi wengi wa Biblia wanaamini kwamba Herode alikufa mwaka wa 4 K.W.K. na kwamba Yesu alizaliwa kabla ya mwaka huo—labda mapema kama mwaka wa 5 au 6 K.W.K. Wao hutegemeza mikataa yao kuhusu kifo cha Herode juu ya taarifa zilizotolewa na mwanahistoria wa karne ya kwanza Flavius Josephus.b

      Kwa mujibu wa Josephus, punde tu kabla ya Mfalme Herode kufa, mwezi ulipatwa. Wasomi wa Biblia husema juu ya mwezi kupatwa kwa kiasi kidogo katika Machi 11, 4 K.W.K., kuwa uthibitisho kwamba lazima Herode alikufa mwaka huo. Hata hivyo, katika mwaka wa 1 K.W.K., mwezi ulipatwa kikamili katika Januari 8 na kupatwa kwa kiasi kidogo katika Desemba 27. Hakuna awezaye kusema kama Josephus alikuwa akirejezea kupatwa kulikotokea mwaka wa 1 K.W.K. au kule kulikotokea mwaka wa 4 K.W.K. Kwa hiyo, hatuwezi kutumia maneno ya Josephus kubainisha mwaka hususa wa kifo cha Herode. Hata kama tunaweza, bado hatuwezi kubainisha wakati Yesu alipozaliwa bila kuwa na habari za ziada.

      Uthibitisho wenye nguvu zaidi tulio nao kuhusu tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu unatoka katika Biblia. Rekodi iliyopuliziwa yasema kwamba binamuye Yesu, Yohana Mbatizaji, alianza kazi yake akiwa nabii mwaka wa 15 wa Maliki Mroma Tiberio Kaisari. (Luka 3:1, 2) Historia ya kilimwengu huthibitisha kwamba Tiberio alitawazwa kuwa maliki katika Septemba 15, 14 W.K., hivyo mwaka wake wa 15 ungeanza mwishoni mwa mwaka wa 28 W.K. na kumalizika mwishoni mwa mwaka wa 29 W.K. Yohana alianza huduma yake wakati huo, na ni wazi kwamba Yesu alianza huduma yake miezi sita baadaye. (Luka 1:24-31) Jambo hilo, kutia ndani uthibitisho mwingine, laonyesha kwamba Yesu alianza huduma yake katika vuli ya mwaka wa 29 W.K.c Biblia husema kwamba Yesu alikuwa “na umri wa karibu miaka thelathini” alipoanza huduma yake. (Luka 3:23) Ikiwa alikuwa na umri wa miaka 30 katika vuli ya 29 W.K., ni lazima awe alizaliwa katika vuli ya 2 K.W.K. Sasa, tukihesabu miaka elfu mbili kwenda mbele kuanzia vuli ya 2 K.W.K. (tukikumbuka kwamba hakukuwa na mwaka wa sifuri; hivyo, kuanzia 2 K.W.K. hadi 1 W.K. ni miaka miwili), tunang’amua kwamba milenia ya pili iliisha na ya tatu ikaanza katika vuli ya 1999!

      Je, jambo hilo ni la maana? Kwa mfano, je, kuanza kwa milenia ya tatu kungekuwa mwanzo wa Utawala wa Miaka Elfu wa Yesu Kristo, unaotajwa katika kitabu cha Ufunuo? La. Biblia haionyeshi popote uhusiano wowote kati ya milenia ya tatu na Utawala wa Miaka Elfu wa Kristo.

      Yesu aliwaonya wafuasi wake dhidi ya kukisia tarehe. Aliwaambia wanafunzi wake: “Si juu yenu kupata ujuzi wa nyakati au majira ambayo Baba ameweka katika mamlaka yake mwenyewe.” (Matendo 1:7) Mapema kidogo, Yesu alifunua kwamba wakati huo hata yeye hakujua wakati ambapo Mungu angetekeleza hukumu juu ya mfumo huu mwovu, akiuandalia nafasi Utawala wa Milenia wa Kristo. Yeye alisema: “Kuhusu siku hiyo na saa hiyo hakuna mtu ajuaye, wala hao malaika wa mbingu wala Mwana, ila Baba tu.”—Mathayo 24:36.

      Je, ni jambo linalopatana na akili kutarajia kwamba Kristo atarudi miaka 2,000 kamili tangu azaliwe akiwa mwanadamu? La, sivyo. Ni lazima Yesu awe alijua tarehe yake ya kuzaliwa. Naye bila shaka alijua jinsi ya kuhesabu miaka 2,000 tangu tarehe hiyo. Hata hivyo, hakujua siku wala saa ya kuja kwake. Ni wazi kwamba haingekuwa rahisi hivyo kubainisha tarehe ya kurudi kwake! Baba ndiye aliyekuwa na mamlaka juu ya ‘nyakati na majira’—yeye pekee ndiye ajuaye ratiba.

      Isitoshe, Yesu hakuwaamuru wafuasi wake wamngojee mahali fulani hususa. Hakuwaambia wakusanyike na kungoja, bali watawanyike hadi “sehemu ya mbali zaidi sana ya dunia” na kufanya wanafunzi kutoka kwa watu wa mataifa yote. Hajawahi kubatilisha amri hiyo.—Matendo 1:8; Mathayo 28:19, 20.

      Je, Matumaini Yao ya Milenia Yataambulia Patupu?

      Hata hivyo, baadhi ya watu wenye itikadi kali za kidini wana matumaini makubwa kuhusu mwaka wa 2000. Wanaamini kwamba katika miezi kadhaa ijayo, sehemu fulani za kitabu cha Ufunuo zitatimizwa kihalisi. Kwa kweli, wanaona kuwa wao binafsi watahusika katika utimizo huo. Kwa mfano, wao hutaja unabii uliorekodiwa kwenye Ufunuo 11:3, 7, 8, unaosimulia juu ya mashahidi wawili ambao wanatoa unabii katika “jiji kubwa ambalo katika maana ya kiroho laitwa Sodoma na Misri, ambako pia Bwana wao alitundikwa mtini.” Wanapomaliza kutoa ushahidi, mashahidi hao wawili wanauawa na hayawani-mwitu mkali atokaye katika abiso.

      Kwa mujibu wa ripoti moja katika gazeti la The New York Times Magazine la Desemba 27, 1998, kiongozi wa dini moja “amewaambia wafuasi wake kwamba yeye ni mmojawapo wa hao mashahidi wawili ambao wamejaliwa kutangaza kuharibiwa kwa dunia na kuja kwa Bwana—kisha Shetani awaue katika barabara za Yerusalemu.” Wenye mamlaka katika Israeli wana sababu ya kuwa na wasiwasi. Wanahofu kwamba watu fulani wenye itikadi kali za kidini wanaweza kujaribu “kutimiza” unabii huo kwa njia yao wenyewe—hata ikiwa hiyo yamaanisha kuchochea mapambano ya kutumia silaha! Hata hivyo, Mungu hahitaji “msaada” wa mwanadamu ili kutimiza kusudi lake. Unabii wote wa Biblia utatimizwa katika wakati wa Mungu na katika njia yake mwenyewe.

      Kitabu cha Ufunuo kiliandikwa “kwa njia ya ishara.” Kwa mujibu wa Ufunuo 1:1, Yesu alitaka kuwafunulia “watumwa wake” (wala si ulimwengu kwa ujumla) mambo ambayo lazima yatukie upesi. Ili kukielewa kitabu cha Ufunuo, watumwa, au wafuasi wa Yesu wangehitaji roho takatifu ya Mungu, ambayo Yehova huwapa wale wampendezao. Kama kitabu cha Ufunuo chapaswa kueleweka kihalisi, hata watu wasio na imani wangeweza kukisoma na kukielewa. Nao Wakristo hawangehitaji kusali kupata roho takatifu ili kukielewa.—Mathayo 13:10-15.

      Tumeona kwamba kulingana na uthibitisho wa Biblia, milenia ya tatu tangu Yesu azaliwe inaanza katika vuli ya 1999 na kwamba tarehe hiyo wala Januari 1, 2000, wala Januari 1, 2001, haina maana yoyote ya pekee. Hata hivyo, kuna milenia ambayo huwapendeza sana Wakristo. Ikiwa si milenia ya tatu, basi ni milenia gani? Makala ya mwisho katika mfululizo huu itajibu swali hilo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ona sanduku lenye kichwa “mwaka wa 2000 au wa 2001” kwenye ukurasa wa 5.

      b Kwa mujibu wa kronolojia ya wasomi hao, milenia ya tatu ingalifika mwaka wa 1995 au wa 1996.

      c Kwa habari zaidi, tafadhali ona Buku la Kwanza la Insight on the Scriptures, ukurasa wa 1094 hadi 1095, lililochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

      [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      Mwaka wa 2000 au wa 2001?

      Fikiria kielezi hiki ili upate kuelewa ni kwa nini watu fulani hudai kwamba milenia ya tatu tangu Yesu azaliwe itaanza Januari 1, 2001. Tuseme unasoma kitabu chenye kurasa 200. Unapofikia mwanzo wa ukurasa wa 200, tayari umemaliza kusoma kurasa 199, kukiwa na ukurasa mmoja zaidi wa kusoma. Hutakuwa umemaliza kusoma kitabu hicho hadi ufikie mwisho wa ukurasa wa 200. Vivyo hivyo, miaka 999 ya milenia ya sasa, kama inavyohesabiwa kwa ukawaida, itakuwa imeisha Desemba 31, 1999, kukiwa kumebaki mwaka mmoja kabla ya milenia kuisha. Tukihesabu hivyo, milenia ya tatu inaanza Januari 1, 2001. Hata hivyo, jambo hilo halimaanishi kwamba siku hiyo miaka 2,000 kamili itakuwa imeisha tangu Yesu azaliwe, kama vile makala hii ionyeshavyo.

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      Jinsi Utaratibu wa Kuweka Tarehe wa K.K. na A.D. Ulivyobuniwa

      Mapema katika karne ya sita W.K., Papa John wa Kwanza alimpa mtawa aitwaye Dionysius Exiguus utume wa kubuni utaratibu wa kupiga hesabu ambao ungeyawezesha makanisa kuweka tarehe rasmi kwa ajili ya Ista.

      Dionysius akaanza kazi. Akapiga hesabu kurudi nyuma, akapita wakati wa kifo cha Yesu, hadi mwaka ambao alifikiri Yesu alizaliwa; kisha akahesabu kila mwaka kuanzia wakati huo na kwenda mbele. Dionysius alikiita kipindi cha tangu Yesu azaliwe “A.D.” (yaani, Anno Domini—“katika mwaka wa Bwana wetu.”) Huku akinuia kubuni tu njia yenye kutegemeka ya kupiga hesabu ili kujua tarehe ya Ista kila mwaka, Dionysius alianzisha bila kukusudia dhana ya kuhesabu miaka kuanzia kuzaliwa kwa Kristo na kwenda mbele.

      Ingawa wasomi wengi hukubali kwamba Yesu hakuzaliwa mwaka ambao Dionysius alitumia kuwa msingi wa kupigia hesabu zake, utaratibu wake wa kronolojia hutuwezesha kujua matukio katika mkondo wa wakati na kuelewa jinsi yanavyohusiana.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki