-
Warusi Wathamini Sana Uhuru wa KuabuduAmkeni!—2000 | Februari 22
-
-
Wa Kwanza Nchini Marekani
Agosti uliopita tarehe 20 hadi 22, kilele cha wahudhuriaji 670 kutoka Marekani kote na Kanada walisisimuka kuhudhuria mkusanyiko wa wilaya wa kwanza katika Kirusi uliofanywa New York City. Hotuba zote zilitolewa kwa lugha ya Kirusi, na drama ya mavazi kamili, iliyokazia simulizi la Biblia la Yakobo na Esau, ilifanywa na washiriki wa Kutaniko la lugha ya Kirusi la Los Angeles, California. Kwa kweli ilikuwa tukio kuu katika mkusanyiko huo.
Tukio jingine kuu lilikuwa ubatizo wa watu 14, wote wanaonekana kwenye picha iliyo katika makala haya. Baadhi yao walisafiri kilometa zipatazo 4,000 kutoka Portland, Oregon, na kutoka Los Angeles na San Francisco, California, ili kubatizwa kwenye mkusanyiko katika New York City. Hapo awali, hawa 14 walikuwa wameishi katika zile zilizokuwa jamhuri za Sovieti za Armenia, Azerbaijan, Belarus, Moldova, Ukrainia, na Urusi. Mambo yaliyowapata huonyesha jinsi wanavyothamini sana ujuzi wa Mungu na uhuru wa kumwabudu.
Svetlana (safu ya kwanza, wa tatu kutoka kushoto) alilelewa Moscow. Akiwa na umri wa miaka 17 aliolewa na mwimbaji mashuhuri aliyekuwa na umri mkubwa kumshinda, na wakahamia Marekani mwaka wa 1989 pamoja na mwana wao mchanga. Mume wake alisafiri kwa mapana na marefu, na wakatalikiana miaka mitano baada ya hapo.
Svetlana alipokutana na mfanyakazi mwenzi aliye Shahidi, rafiki zake walimwonya asijihusishe na “madhehebu ambayo yangedhibiti maisha [yake] na kuchukua pesa [zake] zote.” Hata hivyo, alitaka kujifunza Biblia. Alipoonyeshwa jina la Mungu katika Biblia, alisema hivi: “Nilivutiwa sana kuona kwamba ni Mashahidi peke yao waliokuwa wakilijulisha.”
Akiwa kijana, Andrei (safu ya nyuma, wa tatu kutoka kushoto) alitoka nyumbani kwao Siberia ili kupata mazoezi zaidi ya kuwa mwanariadha ile ambayo leo ni St. Petersburg. Punde baada ya hapo, Muungano wa Sovieti uliporomoka, na katika mwaka wa 1993, Andrei, akiwa na umri wa miaka 22 alihamia Marekani. Aeleza hivi: “Nilianza kufikiri juu ya Mungu na kuanza kwenda kwenye Kanisa Othodoksi la Urusi. Wakati mmoja, kwenye sherehe ya Ista ya Urusi, nilikaa kanisani usiku kucha nikitafuta kumkaribia Mungu.”
Karibu na wakati huo, Svetlana alikutana na Andrei, na akamweleza yale aliyokuwa akijifunza kwenye funzo lake la Biblia. Alikubali kuandamana naye kwenye mkutano wa Mashahidi wa Yehova, na baada ya hapo akakubali funzo la Biblia. Walifunga ndoa Januari 1999. Baada ya kubatizwa kwenye mkusanyiko walikuwa na shangwe kwelikweli.
Pavel (safu ya nyuma, wa nne kutoka kushoto) alizaliwa karibu na Qaraghandy, Kazakhstan, lakini baadaye akahamia Nal’chik, Urusi. Jiji hilo kubwa liko karibu na Chechnya na Dagestan, ambako kumekuwa na mapigano makali sana. Pavel alikutana na Mashahidi huko mara ya kwanza Agosti 1996, lakini akahamia San Francisco mwezi uliofuata. Alikuwa amejihusisha na dawa za kulevya na kuzaa binti, aliyebaki Urusi pamoja na mama yake.
Mara tu baada ya kuwasili Marekani, Pavel aliwafikia Mashahidi wa Yehova na kukubali funzo la Biblia. Alirekebisha maisha yake na kumwandikia mkewe barua kuhusu itikadi zake mpya. Sasa anajifunza na Mashahidi, na mipango inafanywa aende Marekani ili waweze kufunga ndoa na Pavel na kumtumikia Yehova pamoja huko California wakiwa na binti yao.
George (safu ya mwisho, wa pili kutoka kushoto) alizaliwa na kulelewa Moscow. Alihamia Marekani mwaka wa 1996, na mwaka uliofuata akafunga ndoa na Flora, aliyekuwa mwenyeji wa Azerbaijan. George alihudhuria ibada katika Kanisa Othodoksi la Urusi, lakini baada ya kusoma nakala ya gazeti Mnara wa Mlinzi, alikuwa na maswali kuhusu fundisho la Utatu. Barua aliyoandikia Watch Tower Society ilipojibiwa, alipokea broshua Je! Uamini Utatu? Mnamo mwaka wa 1998 yeye na Flora walianza kujifunza Biblia. Sasa yeye pia anapanga kubatizwa.
Tukio jingine kuu la mkusanyiko lilikuwa kupokea salamu kutoka Moscow, ambapo watu 15,108 walikusanyika kwa ajili ya mkusanyiko wao kwenye mwisho-juma huohuo. Wajumbe katika New York City walisisimuka kama nini kusikia tangazo kwamba watu 600 walikuwa wamebatizwa huko! Hiyo ilikuwa kweli hasa kwa sababu ya ripoti zenye kuogofya za magazeti na televisheni zilizokuwa zimeanza kutokea Marekani na kwingineko katika juma lililotangulia tarehe ya mkusanyiko.
-
-
Warusi Wathamini Sana Uhuru wa KuabuduAmkeni!—2000 | Februari 22
-
-
[Picha katika ukurasa wa 23]
Mkusanyiko wa kwanza wa wilaya wa lugha ya Kirusi nchini Marekani
[Picha katika ukurasa wa 24]
Drama ya Biblia yafanywa New York na Kutaniko la lugha ya Kirusi la Los Angeles
[Picha katika ukurasa wa 25]
Hawa 14 waliobatizwa New York wanatoka kwenye jamhuri sita za uliokuwa Muungano wa Sovieti
-