-
Mwanadamu Dhidi ya MazingiraAmkeni!—2001 | Novemba 22
-
-
Mwanadamu Dhidi ya Mazingira
“Siku hizi wanadamu ndio wanaopaswa kulaumiwa kwa kuangamia sana kwa aina za viumbe.”—Jane Goodall, Mhifadhi Wa Mazingira.
VIUMBE duniani huendelea kutimiza shughuli nyingi muhimu na hutegemeana. Sisi wanadamu ni sehemu muhimu ya viumbe hivyo. Sisi hutegemea mimea na wanyama kwa ajili ya chakula chetu na dawa, hewa tunayopumua, na madini yanayofanyiza miili yetu. Kwa siku moja tu, wanadamu hutegemea zaidi ya aina 40,000 za viumbe vingine. Viumbe vyote hufanyiza mfumo tata sana wenye kustaajabisha.
Hata hivyo, wataalamu wengi wanaochunguza mfumo huo tata wanahisi kwamba unashambuliwa! Huenda umesikia kwamba vifaru, simba-milia, panda, na nyangumi wamo hatarini. Wanasayansi fulani hudai kwamba huenda asilimia 50 ya aina zote za mimea na wanyama zitatoweka duniani katika miaka 75 ijayo. Watafiti wanahofu kwamba huenda kiwango cha kuangamia kwa aina fulani za viumbe kitaongezeka mara 10,000, kuliko kile cha kawaida. Mtaalamu mmoja anakadiria kwamba kwa wastani, aina moja huangamizwa kila dakika 10 hadi 20.
Wanasayansi huamini kuwa zamani sana, aina za viumbe ziliangamia hasa kutokana na visababishi vya asili. Lakini wanasema kwamba kisababishi kikuu cha tatizo la sasa ni tofauti. Ni wazi kwamba siku hizi aina za viumbe huangamia kwa sababu ya shughuli za wanadamu. Mwanasayansi mmoja aliwataja wanadamu kuwa “viumbe wanaoangamiza.”
Je, shughuli za wanadamu ndizo zinazoangamiza aina nyingi za viumbe? Ikiwa ndivyo, jinsi gani? Je, twaweza kuendelea kuishi bila kuwa na unamna-namna wa viumbe vinavyovutia? Je, kuna lolote linalofanywa ili kusuluhisha tatizo kubwa la kuangamia kwa aina za viumbe?
-
-
Mfumo Tata wa ViumbeAmkeni!—2001 | Novemba 22
-
-
Unamna-namna Unaotoweka
Kwa kusikitisha, ijapokuwa kuna viumbe vingi vyenye kuvutia na vya aina mbalimbali, watafiti fulani wanasema kwamba wanadamu wanaangamiza aina za viumbe haraka sana. Kwa njia zipi?
◼ Uharibifu wa makao. Hiki ndicho kisababishi kikuu cha kuangamia kwa viumbe. Uharibifu wa makao huhusisha ukataji wa miti ili kupata mbao na kupata maeneo ya malisho, kuchimba migodi, na ujenzi wa mabwawa na barabara mahala palipokuwa na misitu zamani. Maeneo yanapopungua, viumbe hupoteza vitu vinavyohitaji ili kuendelea kuwepo. Mazingira ya asili yanaangamizwa na kutenganishwa. Wanyama hukosa njia ya kuhamia maeneo mengine. Chembe mbalimbali za urithi hupungua. Viumbe haviwezi kupona vinapokabili magonjwa na hali nyingine ngumu. Hivyo, pole kwa pole aina moja baada ya nyingine hufa.
Aina fulani za viumbe zinapoangamia, aina nyingine pia zaweza kuangamia kwani sehemu moja ya mfumo wa viumbe inapoangamizwa sehemu nyingine zaweza kuathiriwa. Aina zinazotegemewa zinapoangamia—kama vile zile zinazochavusha—jambo hilo laweza kuathiri aina nyingine nyingi za viumbe.
◼ Aina ngeni za viumbe. Wanadamu wanapoingiza aina ngeni katika mazingira, aina hiyo yaweza kuchukua makao ya aina nyingine zilizokuwepo awali. Aina hizo ngeni zaweza pia kubadili mazingira kiasi cha kwamba aina zilizokuwepo hulazimika kuhama, au zaweza kuleta magonjwa yasiyoweza kukingwa na aina zilizokuwepo. Hasa kwenye visiwa, mahala ambapo aina za viumbe zimeishi zikiwa peke yake kwa muda mrefu na hazijapata kushirikiana na aina mpya, huenda aina zilizokuwepo zikashindwa kubadilika kulingana na hali hiyo mpya na hivyo kuangamia.
Mfano mzuri wa jambo hilo ni mwani “mharibifu” unaoitwa Caulerpa taxifolia. Mmea huo unaangamiza aina nyingine zinazopatikana katika Bahari ya Mediterania. Baada ya kuletwa kimakosa kwenye pwani ya Monaco, mmea huo sasa umeanza kuenea chini ya bahari. Mmea huo una sumu, na haijulikani iwapo kuna mmea mwingine unaoweza kuuangamiza. “Huu waweza kuwa mwanzo wa msiba mkubwa wa mazingira,” asema Alexandre Meinesz, profesa wa mambo ya bahari kwenye Chuo Kikuu cha Nice, Ufaransa.
◼ Uwindaji unaopita kiasi. Jambo hili limeangamiza aina kadhaa za viumbe. Mfano mmoja ni wa njiwa anayeitwa passenger. Mapema katika karne ya 19, huyo ndiye ndege aliyepatikana sana huko Amerika Kaskazini. Njiwa hao walipohamia eneo jingine—wakiwa katika makundi-makundi ya njiwa bilioni moja au zaidi—walifanya anga liwe jeusi kwa siku nyingi. Hata hivyo, kufikia mwisho wa karne ya 19, njiwa huyo alikuwa amewindwa sana hivi kwamba alikuwa karibu kuangamia. Kisha, mnamo Septemba 1914, njiwa wa mwisho kabisa wa aina ya passenger alikufa katika bustani moja ya wanyama huko Cincinnati. Vivyo hivyo, nyati wa Marekani wa zile Nyanda Kubwa aliwindwa sana hivi kwamba alikuwa karibu kuangamia.
◼ Ongezeko la idadi ya watu. Katikati ya karne ya 19, idadi ya watu duniani ilikuwa bilioni moja. Baada ya karne moja na nusu, watu bilioni tano waliongezeka. Hivyo wanadamu wameanza kujiuliza iwapo wanakabili hatari ya kumaliza mali asili. Kila mwaka, idadi ya watu inapoongezeka, aina mbalimbali za viumbe huzidi kuangamia haraka.
◼ Hatari ya kuongezeka kwa joto la dunia. Kwa mujibu wa Kamati ya Serikali Mbalimbali kuhusu Badiliko la Tabia ya Nchi, yamkini halijoto itaongezeka kwa nyuzi 3.5 Selsiasi katika karne hii. Huenda hilo ni ongezeko la haraka sana hivi kwamba aina fulani za viumbe zitaangamia. Kulingana na watafiti, yamkini kisababishi kimoja cha kuangamia kwa miamba ya matumbawe (ambayo hutegemeza sana aina mbalimbali za viumbe baharini) ni kuongezeka kwa joto la maji.
Wanasayansi husema kwamba usawa wa maji baharini ukiongezeka kwa meta moja, huenda sehemu kubwa ya maeneo ya pwani yenye umajimaji, ambayo ni makao ya aina mbalimbali za viumbe, yataharibiwa. Wanasayansi wengine huamini kwamba huenda ongezeko la joto la dunia linaathiri mabamba ya barafu ya Greenland na Antaktiki. Barafu hiyo ikiyeyuka, huenda msiba ukatokea katika mazingira.
Kuangamia Haraka
Aina za viumbe zinaangamia haraka kadiri gani? Majibu kwa swali hilo si sahihi kabisa. Wanasayansi wangali hawajui aina nyingi zinazoangamia. Kwanza, ni lazima wajue idadi ya aina zilizopo. Kulingana na John Harte, mwanasayansi wa ekolojia kwenye Chuo Kikuu cha California, Berkeley, “kuna aina milioni moja na nusu hivi za viumbe duniani zinazojulikana, lakini twajua kwamba kuna aina nyingi ambazo hazijatambuliwa, na huenda jumla ya idadi hiyo ni kati ya milioni 5 na milioni 15.” Wengine hukadiria kwamba kuna aina milioni 50 au zaidi. Kulingana na mwanasayansi Anthony C. Janetos, haiwezekani kujua idadi kamili kwani “aina nyingi za viumbe zitaangamia hata kabla hazijatambuliwa na kuainishwa.”
Bado wanasayansi wa kisasa hawajaelewa utaratibu tata unaowezesha viumbe vipatane vizuri na mazingira. Iwapo wanadamu hawajui idadi ya aina zilizopo, wataelewaje ule mfumo tata wa viumbe na jinsi unavyoathiriwa wakati aina mbalimbali zinapoangamia? Watajuaje jinsi kuangamia kwa aina za viumbe kunavyoathiri mfumo unaotegemeza uhai duniani?
Wanasayansi wanapojaribu kukadiria kiwango cha kuangamia kwa aina za viumbe, japo makadirio yao hutofautiana, kwa kawaida yanavunja moyo sana. Mwandishi mmoja alisema hivi: “Asilimia 50 hivi ya mimea na wanyama ulimwenguni watakabili hatari ya kuangamia katika miaka mia moja ijayo.” Utabiri huu wa Harte unahuzunisha hata zaidi: “Wanabiolojia wanakadiria kwamba ukataji wa miti katika maeneo ya tropiki utaangamiza nusu au zaidi ya nusu ya aina za viumbe zilizopo duniani katika miaka 75 ijayo.”
Kwa kutegemea makadirio ya mwanasayansi Stuart Pimm wa Chuo Kikuu cha Tennessee, gazeti la National Geographic lilisema kwamba “asilimia 11 ya ndege, au aina 1,100 kati ya aina zipatazo 10,000 zilizopo ulimwenguni, ziko karibu kuangamia; kuna wasiwasi kwamba aina nyingi kati ya hizo 1,100 hazitakuwapo mwishoni mwa [karne ya 21].” Gazeti hilohilo lilisema hivi: “Hivi majuzi, wataalamu maarufu wa elimu ya mimea waliripoti kwamba mmea mmoja kati ya kila mimea minane uko karibu kuangamia. Pimm asema hivi: ‘Si aina zinazopatikana visiwani au katika misitu ya mvua tu, wala si ndege wala wanyama wakubwa wenye kuvutia tu. Kila kitu kimo hatarini na jambo hilo linatukia kila mahala. . . . Aina za viumbe zinaangamia haraka kotekote ulimwenguni.’”
Je, Twahitaji Aina Zote Hizo?
Je, kuna haja ya kuhangaikia kuangamia kwa aina mbalimbali za viumbe? Je, kweli twahitaji aina tofauti-tofauti za viumbe? Wataalamu wengi wanaoheshimiwa husisitiza kwamba twahitaji aina hizo. Aina za viumbe duniani huwaandalia wanadamu chakula, kemikali muhimu, na bidhaa na huduma nyinginezo. Pia, fikiria kuhusu faida zinazoweza kutokana na aina ambazo hazijagunduliwa. Kwa mfano, imekadiriwa kwamba dawa 120 kati ya dawa 150 kuu ambazo madaktari huwapendekezea watu nchini Marekani, hutengenezwa kwa mali asili. Hivyo, aina za mimea zinapoangamia, wanadamu hupoteza njia ya kuvumbua dawa na kemikali mpya. Bwana Ghillean Prance, mkurugenzi wa Bustani za Kew huko London, alisema hivi: ‘Kila mara aina moja ya kiumbe inapoangamia, tunapoteza kitu ambacho tungetumia siku za baadaye. Tunapoteza dawa inayoweza kutibu UKIMWI, au zao linaloweza kukinza virusi. Hivyo, ni lazima tukomeshe uharibifu wa viumbe, si kwa faida ya dunia tu bali kwa ajili ya . . . mahitaji na matumizi yetu.’
Pia, twahitaji mazingira yanayoweza kudumisha uhai wa viumbe vyote. Mazingira yasiyo na kasoro hutimiza kazi muhimu kama vile kutengeneza oksijeni, kusafisha maji, kuondoa vichafuzi, na kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Wadudu huchavusha mimea. Vyura, samaki, na ndege huangamiza wadudu waharibifu; kome na viumbe vingine vinavyoishi majini husafisha maji; mimea na vijidudu hutengeneza udongo. Huduma hizo hutokeza faida kubwa sana za kiuchumi. Kulingana na kadirio la kiwango cha chini lililofanywa kupatana na bei za 1995, aina mbalimbali za viumbe ulimwenguni pote huleta faida ya dola bilioni 3,000 za Marekani kila mwaka.
Hata hivyo, japo tunategemea sana aina mbalimbali za viumbe, yaonekana kwamba wanadamu wanakabili tatizo kubwa linalohatarisha ule mfumo tata wa viumbe. Sasa, wakati ambapo twaanza kuelewa umuhimu wa aina mbalimbali za viumbe, wanadamu wanaangamiza aina nyingi kuliko wakati mwingine wowote! Hata hivyo, je, wanadamu wanaweza kutatua tatizo hilo? Unamna-namna wa viumbe duniani utapatwa na nini wakati ujao?
-