Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Maajabu na Mafumbo Katika Bahari
    Amkeni!—2000 | Novemba 22
    • Baada ya kushuka kwa muda wa dakika 90, chombo cha Alvin kilianza kwenda sambamba na sakafu ya bahari, kisha wanasayansi waliokuwamo wakawasha taa. Inaeleweka ni kwa nini walidhani kwamba walikuwa katika sayari nyingine. Taa zao zilimulika matundu kadhaa yenye maji moto yanayomeremeta kwenye sakafu ya bahari, ambako kwa kawaida maji hukaribia kuwa barafu. Karibu na matundu hayo, jambo lenye kustaajabisha hata zaidi lilitokea—jamii nzimanzima za viumbe ambao hawakuwa wamejulikana awali waliibuka. Miaka miwili baadaye, watafiti waliokuwa katika Alvin waligundua matundu yenye maji moto kupindukia yanayoitwa smokers katika Safu ya Milima ya Pasifiki Mashariki karibu na pwani ya Mexico. Baadhi ya matundu hayo hufanyiza mabomba ya ajabu, mengine hufikia kimo cha meta sita. Baadhi ya wanyama wengi walioonekana katika Bonde la Ufa la Galápagos waligunduliwa mahali hapo. Katika makala ifuatayo, tutachunguza kwa makini zaidi viumbe hawa wenye kustaajabisha na mazingira yenye hali zinazopita kiasi wanamoishi viumbe hao.

  • Sakafu ya Bahari—Siri Zake Zafunuliwa
    Amkeni!—2000 | Novemba 22
    • Chemchemi—Yenye Sumu!

      Kwa sababu ya hali yake ya kubadilika-badilika na milipuko ya volkano, safu ya milima ya katikati ya bahari ina vijito tele vya volkano na matundu mengi ya maji moto. Mchanganyiko moto sana wenye sumu wa maji na madini ya ardhini hububujika kutoka kwenye matundu hayo. Lakini, jambo la kushangaza ni kwamba mazingira hayo yasiyokalika, yanayokumbwa na kanieneo zinazozidi kwa mbali sana zile zilizo katika usawa wa bahari, huvutia viumbe chungu nzima—badala ya kuvifukuza! Mamia ya jamii za viumbe wanaoishi humo zatia ndani bakteria, chaza wakubwa—wenye urefu wa thuluthi ya meta hivi—na, la kuduwaza zaidi, choo aina ya tube worm wenye minyiri-minyiri ya rangi nyekundu iliyoiva wanaojishikilia kwa nguvu kwenye sakafu ya bahari na kufikia kimo cha meta 1.8.

      Viumbe wanaoishi katika matundu ya baharini huvunda kama mayai yaliyooza wanapoletwa ufuoni! Uvundo huo hausababishwi na kuoza, bali na hidrojeni salfaidi—kemikali yenye sumu kali inayotoa uvundo wenye kuchukiza ambayo imejaa kote katika matundu ya maji moto. Maji yanayotoka katika matundu hayo yana asidi kali na metali nyingi, kutia ndani shaba, magnesi, chuma, na zinki. Badala tu ya kustahimili katika mazingira hayo—ambayo yamelinganishwa na mahali pa kutupa takataka zenye sumu—tube worm na viumbe wengine husitawi humo! Jinsi gani? Ili kuelewa, acheni tumchunguze tube worm kinaganaga.

      Kiumbe Asiyeeleweka

      Wanabiolojia walipowachunguza tube worm, waligundua kwamba ni viumbe wasioeleweka. Hawakuwa na kinywa wala mfumo wa umeng’enyaji. Swali likazuka, Wao hulaje na kufyonza chakula chao? Kisha wakagundua jambo lenye kuduwaza: Choo hao walikuwa na damu nyekundu—si umajimaji tu bali damu halisi, yenye himoglobini nyingi—inayozunguka katika mwili wao na katika minyiri-minyiri yao inayoshabihi manyoya.

      Mafumbo hayo yalizidi kuwa tata wakati wanabiolojia walipopasua kifuko cha ute katika mwili wa tube worm. Tishu zake zilikuwa na mchanganyiko wa bakteria zipatazo bilioni 10 kwa kila gramu ya tishu! Mnamo mwaka wa 1980 mwanafunzi mmoja wa biolojia alibuni nadharia ya kwamba tube worm huishi kwa utegemeano—utegemeano huwawezesha viumbe wawili kupata manufaa kwa kushirikiana. Utafiti ulithibitisha nadharia yake kwa kuonyesha kwamba tube worm, akiwa kimelewa, hulisha bakteria hizo, na bakteria humlisha.

      Kama mashavu ya samaki, minyiri-minyiri ya tube worm hukusanya oksijeni na kaboni, vitu vinavyotumiwa na bakteria kutengenezea chakula. Minyiri-minyiri hiyo haipeperuki moja kwa moja kwenye maji moto yanayomiminwa na matundu—kufanya hivyo kungekuwa kuhatarisha uhai—bali hupeperuka katika sehemu ambako maji moto ya matundu huchanganyika na maji baridi sana ya baharini. Bila shaka, utengenezaji huo wa chakula huhitaji nishati. Katika uso wa dunia—na juu-juu ya bahari—nuru ya jua huandaa nishati muhimu kwa utengenezaji wa chakula kwa kusababisha ukuzi wa mimea. Lakini nuru ya jua haifiki hata kidogo katika lindi kuu anamoishi tube worm.

      Nishati Kutoka Katika Kiini cha Dunia

      Kwa akili nyingi, Muumba ameandaa nishati inayohitajiwa kutoka kwa kiini cha dunia kupitia kwa matundu ya maji moto na ile kemikali yenye uvundo ya hidrojeni salfaidi. Hidrojeni salfaidi ambayo ni “nuru ya jua” ya jamii zinazoishi katika matundu ya baharini, huandaa nishati inayohitajiwa na bakteria katika utengenezaji wa chakula. Wakati huohuo, bakteria hizo ni kama “mimea” katika jamii zinazoishi kwenye matundu kwa sababu ndizo za kwanza katika mlishano wa viumbe wanaoishi katika matundu ya baharini.a

      Ili kuweza kuchanganya kemikali zote zinazohitajiwa na bakteria, damu ya tube worm ina molekuli za himoglobini ambazo ni kubwa mara 30 zaidi ya molekuli za himoglobini katika mwili wa mwanadamu. Damu husafirisha kemikali hizo kwa bakteria zenye njaa, kisha bakteria humtengenezea tube worm chakula.

      Uhai Katika Matundu—Viumbe Mbalimbali!

      Kwa kweli, hakuna kiumbe yeyote anayeishi katika matundu hayo anayepasa kufa njaa, kwa kuwa bakteria zimezagaa kotekote—nyakati nyingine hufanyiza rundo kubwa! Hata katika maji vuguvugu yanayobubujika kwa nguvu juu ya matundu, nyakati nyingine bakteria hukusanyika kwa wingi, mfano wa dhoruba ya theluji, na kufanyiza mfano wa supu iliyo hai. Wanyama wengine hufurahia pia utegemeano pamoja na bakteria hao sawa na tube worm, ilhali wengine hula vijiumbe hao moja kwa moja. Kwa kweli, viumbe wanaoishi karibu na matundu ya baharini wanasitawi na kunawiri sana hivi kwamba wamelinganishwa na vinamasi vya maji ya chumvi, misitu ya kitropiki ya mvua, na matumbawe katika maji yasiyo na kina.

      Kwa kweli, jamii mpya 300 tayari zimegunduliwa karibu na matundu hayo. Hizo zatia ndani chaza weupe wakubwa na kome (rangi si lazima katika mazingira yenye giza totoro), pweza, na kaa weupe walafi wanaopenda mno kula minyiri-minyiri mitepetevu ya tube worm. Ili kujilinda, tube worm huwa na tendo-hiari la haraka ambalo huficha mara moja minyiri-minyiri hiyo ndani ya mwili wake.

      Viumbe wengine wanaoishi katika matundu hayo watia ndani buibui wa baharini, konokono, uduvi wenye kucheza-cheza, koanata, na wanyama wenye magamba, samaki wanaofanana na mkunga ambao hunyiririka kwenye miamba iliyofunikwa na bakteria na salfa, tube worm wadogo na choo wengine. Hao choo wengine hutia ndani choo wa tambi na choo wa chwago. Choo wa tambi wana jina linalofaa kwa sababu wanashabihi tambi nyeupe nyingi zinazoning’inia kwenye miamba. Choo wa chwago ni wa pekee kwa sababu wanaweza kustahimili joto kali kufikia nyuzi Selsiasi 80! Bila shaka, bakteria wa matunduni, ambao huishi kwenye choo wa chwago, wanaweza pia kustahimili joto kali.b

      Nuru ya Ajabu!

      Mnamo mwaka wa 1985, wanasayansi walishangaa kuona uduvi wenye sehemu mbili zinazoshabihi macho wakiwa karibu na matundu ya baharini, sehemu hizo zisizo na lenzi zina kemikali zinazotambua nuru kwa wepesi. Bila shaka, swali walilofikiria kwanza ni, Wanyama hao wanaweza kuona nini katika giza totoro? Ili kupata jawabu, watafiti walitumia kamera ya tarakimu yenye nguvu sana, kama ile inayotumiwa kupiga picha nyota hafifu sana. Waliielekeza kamera hiyo penye tundu, wakazima taa zote, kisha wakapiga picha.

      Matokeo yalishangaza. Picha kwenye kompyuta ilifunua “nuru maridadi, dhahiri na yenye kung’aa” ukingoni mwa bomba yalimotokea maji moto, asema mwanasayansi Cindy Lee Van Dover. Je, uduvi hutumia nuru hii ya ajabu, isiyoweza kuonwa kwa macho ya mwanadamu? Vyovyote iwavyo, ugunduzi wa kwamba matundu ya maji moto hutoa nuru “waanzisha fani mpya kabisa ya utafiti,” aongezea Van Dover.

      Mkubwa Zaidi na Mdogo Zaidi

      Hivi majuzi, sehemu ya sakafu ya bahari iliyojaa methani, iligunduliwa kuwa makao ya bakteria mkubwa zaidi aliyewahi kugunduliwa katika sayansi. Majitu hayo yaliyogunduliwa mwaka wa 1997, yanashabihi ushanga yakiwa na urefu unaozidi ule wa bakteria za kawaida kwa mara 100 hadi 200. Wao pia hula kupindukia, hula karibu salfaidi yote yenye sumu iliyo kwenye tope, na hivyo hufanya eneo hilo kuwa salama kwa viumbe wengine wa baharini.

      Kiumbe anayedhaniwa kuwa mdogo zaidi duniani aligunduliwa hivi karibuni pia chini ya bahari, lakini umbali wa kilometa tano ndani ya sakafu ya bahari! Ripoti moja katika gazeti la The New York Times yaeleza ugunduzi huo, uliotukia karibu na ufuo ulio Magharibi mwa Australia, kuwa “wa ajabu sana kiasi cha kuzusha mjadala mkali ulimwenguni pote.” Swala linalobishaniwa ni kama nanobe—zinaitwa hivyo kwa sababu hupimwa ukubwa kwa nanometa, au kipimo cha sehemu moja kwa bilioni ya meta—ni viumbe au la. Hufanana na kuvu, hutoshana na virusi, vina DNA, na yaonekana huzaana upesi na kufanyiza makundi makubwa.

      Viumbe wengi wanagunduliwa sasa, hivi kwamba wanasayansi wanaamini kuwa idadi ya vijiumbe vilivyo ndani ya tabaka la juu la dunia yaweza kuzidi idadi ya vijiumbe vilivyo kwenye uso wa dunia! Ugunduzi huo unaleta mabadiliko katika dhana za kisayansi. Mwanasayansi mmoja alisema: “Tumetupilia mbali ushikiliaji wa kauli katika elimu ya vijiumbe katika miaka kadhaa iliyopita. Fani hiyo imepiga hatua madhubuti. Kwa kweli ni sayansi mpya.”

      Isitoshe, ugunduzi huo wenye kina watufundisha somo fulani linalozidi sayansi. Biblia yaeleza waziwazi somo hilo: “Sifa zake [Mungu] zisizoonekana zaonwa waziwazi tangu uumbaji wa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zafahamiwa kwa vitu vilivyofanywa.” (Waroma 1:20) Mathalani, Mungu anahangaikia sana usafi. Hilo lathibitishwa na bakteria na viumbe wengine wa baharini wanaoondoa sumu hatari zinazotoka ndani ya dunia na kutoka kwa vitu vingine vinavyozama na kuoza kutoka sehemu ya juu ya bahari. Kwa wazi, Mungu anahangaikia hali-njema ya sayari yetu na viumbe wote waliomo. Kama tutakavyoona katika makala ifuatayo, sifa hiyo ya Muumba yahakikisha kuwapo kwa wakati ujao mtukufu kwa ajili ya viumbe wote duniani.

      [Maelezo ya Chini]

      a Bakteria zinazoishi katika matundu ya baharini hutumia utaratibu unaoitwa usanidi-kemia. Neno hilo latofautiana na usanidi-nuru, utaratibu unaotegemea nishati ya jua unaotumiwa na mimea iliyo ardhini na fitoplankitoni. Fitoplankitoni yatia ndani mimea au viumbe vinavyofanana na mimea vinavyoelea katika sehemu ya juu ya bahari, inayopata nuru ya jua.

      b Katika miaka ya 1960, wanasayansi walianza kuchunguza bakteria wanaopenda joto waliopatikana katika chemchemi za maji moto katika Mbuga ya Taifa ya Yellowstone huko Marekani. Kwa sababu ya “mazingira yenye hali ngumu sana ya jamii hizo za viumbe” ambayo yanastaajabisha, chasema kitabu cha The Deep Hot Biosphere, “wanasayansi walifahamu kwa mara ya kwanza sifa za kipekee za viumbe walioko duniani wanaoonekana kuwa sahili zaidi.”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki