Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Dunia Je, ‘Misingi Yake Iliwekwa’ kwa Nasibu?
    Amkeni!—2000 | Oktoba 8
    • Dunia Je, ‘Misingi Yake Iliwekwa’ kwa Nasibu?

      NI SHARTI dunia izunguke umbali unaofaa kabisa kutoka kwa jua ili isiwe na halijoto inayopita kiasi. Sayari zinazozunguka nyota zinazoshabihi jua zimegunduliwa katika mifumo mingine ya jua, nazo huonwa kuwa ‘sayari zinazoweza kukalika’—yaani, maji yaweza kudumu huko. Lakini hata zile zinazoitwa eti sayari zinazoweza kukalika huenda zisifae uhai wa mwanadamu. Lazima pia zizunguke kwa mwendo unaofaa na ziwe na ukubwa unaofaa.

      Kama dunia ingekuwa ndogo na nyepesi kuliko ilivyo, nguvu za uvutano zingekuwa dhaifu zaidi na sehemu kubwa ya angahewa yake muhimu ingetokomea angani. Ndivyo ilivyo kwa mwezi na sayari mbili za Zebaki na Mihiri. Hazina angahewa kwa sababu ni ndogo zaidi na zina uzito mdogo kuliko dunia. Vipi ikiwa dunia ingekuwa kubwa kidogo na nzito kuliko ilivyo?

      Basi nguvu za uvutano za dunia zingeongezeka zaidi, na gesi nyepesi, kama vile hidrojeni na heli, zingedumu katika angahewa kwa muda mrefu zaidi. “Na jambo kubwa hata zaidi ni kwamba,” chaeleza kichapo cha sayansi cha Environment of Life, “usawaziko nyeti wa gesi za angahewa ungevurugika.”

      Au fikiria tu oksijeni, ambayo inachochea moto. Kama kiwango chake kingeongezeka kwa asilimia moja, mioto ya msitu ingetukia mara nyingi zaidi. Kwa upande mwingine, endapo gesi ya kaboni inayozidisha joto duniani ingezidi kuongezeka, basi tungechomwa na joto kali zaidi duniani.

      Mzunguko wa Dunia

      Umbo la mzunguko wa dunia linafaa sana pia. Ikiwa dunia ingezuka kwa duaradufu zaidi, halijoto ya dunia ingepita kiasi sana tusivyoweza kustahimili. Badala yake, dunia inazunguka kwa umbo linalokaribia kuwa duara. Bila shaka, hali ingebadilika endapo sayari kubwa sana kama Jupita ingepita karibu na dunia. Katika miaka ya majuzi wanasayansi wamepata uthibitisho wa kwamba sayari kubwa sana zinazofanana na Jupita huzunguka karibu sana na nyota nyingine. Idadi kubwa ya sayari hizo zinazofanana na Jupita huzunguka kwa umbo la yai. Kama kungekuwapo sayari nyingine kama dunia katika mifumo hiyo basi zingekabili matatizo.

      Mtaalamu wa nyota Geoffrey Marcy alilinganisha mifumo hiyo ya mbali ya sayari na zile sayari nne Zebaki, Zuhura, Dunia, na Mihiri, ambazo hufanyiza sehemu iliyo karibu ya mfumo wetu wa jua. Katika mahoji, Marcy alisema hivi kwa mshangao: “Tazama jinsi [utaratibu] huu ulivyo kamili. Ni kama kito. Kuna mizunguko ya duara. Yote iko katika usawa uleule. Yote inazunguka kuelekea upande mmoja. . . . Ni jambo la pekee sana.” Je, kweli yaweza kuwa ilitokea kwa nasibu?

      Mfumo wetu wa jua una jambo jingine la kustaajabisha. Zile sayari kubwa sana za Jupita, Zohali, Uranusi, na Kausi huzunguka jua mbali sana na dunia yetu. Badala ya kuwa tisho, sayari hizo hutimiza fungu muhimu. Wataalamu wa nyota huzilinganisha na ‘vifyonza-vumbi vya kimbingu’ kwa sababu nguvu zake za uvutano hufyonza mawe makubwa yanayotoka katika nyota, ambayo yanaweza kuhatarisha uhai duniani. Kwa kweli, dunia ‘imewekwa kwa misingi’ imara. (Ayubu 38:4) Ina ukubwa unaofaa na iko mahali barabara katika mfumo wetu wa jua. Kuna mengi zaidi. Dunia ina mambo mengi ya pekee ambayo ni muhimu kwa uhai wa wanadamu.

  • Dunia Je, ‘Misingi Yake Iliwekwa’ kwa Nasibu?
    Amkeni!—2000 | Oktoba 8
    • [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      SAYARI YA PEKEE

      “Maji yaliweza kukusanyika kwenye dunia kwa sababu ya hali za pekee zilizo duniani zinazosababishwa na ukubwa wake unaofaa, elementi zilizomo, na mzunguko wake ulio nusura ya duara, umbali barabara kutoka kwa nyota iliyodumu muda mrefu, yaani jua. Ni vigumu sana kuwazia mwanzo wa uhai bila maji.”—Integrated Principles of Zoology, Toleo la Sita.

      [Hisani]

      NASA photo

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki