Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kuunganisha Ulimwengu-Mazuri na Mabaya Yanayotarajiwa
    Amkeni!—2002 | Mei 22
    • Kuunganisha Ulimwengu-Mazuri na Mabaya Yanayotarajiwa

      ‘Kuunganisha ulimwengu ndilo tukio la maana zaidi katika wakati wetu. . . . Linawawezesha mabilioni ya watu kotekote ulimwenguni kupata nafasi za kipekee za kufanya maendeleo.’—MARTIN WOLF, MWANDISHI WA MAMBO YA FEDHA.

      “Sisi, watu wa Dunia, ni watu wa familia moja kubwa. Enzi mpya inatokeza magumu na matatizo mapya ulimwenguni, kama vile uharibifu mkubwa wa mazingira, kupunguka kwa mali-asili, vita vya umwagaji-damu na umaskini.”—EDUARD SHEVARDNADZE, RAIS WA GEORGIA.

      MNAMO Desemba 1999, mkutano wa Shirika la Biashara Ulimwenguni huko Seattle, Marekani, ulikatizwa na ghasia. Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi, risasi za mpira, na gesi kali ili kumaliza ghasia hizo. Kisha wakakamata mamia ya waandamanaji.

      Ni nini kilichosababisha ghasia hizo huko Seattle? Ni mahangaiko mengi juu ya kupoteza kazi, mazingira, na ukosefu wa haki katika jamii. Hata hivyo, kwa ufupi, waandamanaji hao waliogopa jinsi ambavyo dunia na watu wangeathiriwa na wazo la kuunganisha ulimwengu.

      Watu hawajaacha kuhangaikia jambo hilo. Tangu mwaka wa 1999, maandamano ya kupinga wazo la kuunganisha ulimwengu yameongezeka na kuwa yenye ujeuri hata zaidi. Sasa nyakati nyingine, viongozi wa ulimwengu wanajitahidi kufanya mikutano yao katika maeneo yaliyojitenga na ambako itakuwa vigumu kwa waandamanaji kuvuruga mazungumzo.

      Kwa wazi, si kila mtu anaogopa wazo la kuunganisha ulimwengu. Ijapokuwa watu fulani husema kwamba kuunganisha ulimwengu ndicho kisababishi cha matatizo yaliyopo ulimwenguni, wengine wanasema kwamba hilo ndilo suluhisho la matatizo mengi ulimwenguni. Ni kweli kwamba huenda watu wengi wakaona kuwa mjadala huo hauwahusu, kwani wengi hawajafahamu sana maana ya kuunganisha ulimwengu. Lakini hata maoni yako yawe nini, tayari wazo la kuunganisha ulimwengu linakuathiri, na huenda likakuathiri hata zaidi katika siku zijazo.

      Ni Nini Maana ya Kuunganisha Ulimwengu?

      Usemi “kuunganisha ulimwengu” au “utandaridhi” unafafanua jinsi watu na nchi mbalimbali ulimwenguni zinavyozidi kutegemeana. Jambo hilo limeongezeka sana katika miaka kumi hivi iliyopita, hasa kwa sababu ya maendeleo makubwa ya tekinolojia. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 5.) Sasa, yaonekana kwamba mataifa yameacha kuhusika katika Vita ya Maneno, vizuizi vya biashara vimepungua au kuondolewa, masoko makubwa ya hisa ulimwenguni yamekuwa yakiungana, na usafiri umekuwa rahisi zaidi na wa bei nafuu.

      Muungano huo wa ulimwengu ambao unaendelea kuimarika umeleta mabadiliko mengi ya kiuchumi, kisiasa, kitamaduni, na ya kimazingira. Kwa kuhuzunisha, baadhi ya mabadiliko hayo ni mabaya. Kichapo cha Umoja wa Mataifa kinachoitwa Human Development Report 1999 kinasema hivi: ‘Maisha ya watu ulimwenguni pote yameunganishwa zaidi na kwa njia ya moja kwa moja kuliko ilivyokuwa hapo awali. Jambo hilo hutokeza njia nyingi za kufanya mambo mapya ambayo yanaweza kuleta faida au hasara.’ Sawa na mafanikio mengi ya wanadamu, utandaridhi una mazuri na mabaya yake.

      Mataraja ya Ulimwengu Wenye Ufanisi Zaidi

      Amartya Sen, mshindi wa Tuzo ya Nobeli ya Uchumi alisema kwamba utandaridhi “umetokeza maendeleo ya kisayansi na ya kitamaduni ulimwenguni na pia kuwafaidi watu wengi kiuchumi.” Pia, kichapo cha Human Development Report 1999 kinasema kwamba utandaridhi “unatokeza njia nyingi zinazoweza kutumiwa kumaliza umaskini katika karne ya 21.” Matarajio hayo mazuri yametokana na jinsi ambavyo utandaridhi umetokeza ufanisi mwingi sana. Leo mapato ya familia ya kawaida ulimwenguni yameongezeka mara tatu kuliko yalivyokuwa miaka 50 iliyopita.a

      Wachanganuzi fulani wanaona faida nyingine ya kuunganisha uchumi wa ulimwengu: Wanaonelea kwamba jambo hilo litazuia mataifa kushiriki katika vita. Katika kitabu chake kinachoitwa The Lexus and the Olive Tree, Thomas L. Friedman anasema kwamba utandaridhi ‘unawachochea watu sana wasipigane na kuongeza gharama za vita sana kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya kisasa.’

      Watu wanaposhirikiana mara nyingi, umoja unaweza kuongezeka ulimwenguni pote. Mashirika fulani ya haki za binadamu yametumia Internet ili kufanikisha harakati zao. Kwa mfano, mkataba wa kimataifa wa kupiga marufuku mabomu ya ardhini ambao ulifanywa mwaka wa 1997 ulifaulu kwa kadiri fulani kwa sababu kompyuta zilitumiwa kuunganisha na kuwasiliana na mashirika mbalimbali ulimwenguni pote yaliyounga mkono harakati hiyo. Njia hiyo ya kuwahusisha watu wa kawaida ilitajwa kuwa “njia mpya ya kufanya mashauriano ya kimataifa, huku serikali na raia wakiungana kupambana na tatizo linalowahusu wanadamu ulimwenguni pote.”

      Licha ya matokeo hayo mazuri, bado watu wengi wanahofu kwamba madhara ya utandaridhi ni mengi kuliko faida zake.

      Kuhofu Kwamba Ulimwengu Utagawanyika Zaidi

      Huenda hangaiko kuu kuhusu utandaridhi ni jinsi ambavyo umezidisha ile tofauti kati ya matajiri na maskini. Ijapokuwa ni wazi kwamba utajiri wa ulimwengu umeongezeka, ni watu wachache zaidi na nchi chache zaidi zilizo na utajiri huo. Sasa mali halisi za watu 200 matajiri zaidi ulimwenguni ni nyingi kuliko jumla ya mapato ya watu bilioni 2.4 hivi wanaoishi duniani—asilimia 40 ya watu wote duniani. Na ijapokuwa mapato yanaendelea kuongezeka katika nchi tajiri, mapato ya wastani katika nchi 80 zenye umaskini yamepungua katika muda wa miaka kumi iliyopita.

      Hangaiko jingine la maana linahusu mazingira. Utandaridhi wa kiuchumi umechochewa na shughuli za biashara zinazokazia faida za kiuchumi kuliko kuhifadhi mazingira. Agus Purnomo, msimamizi wa Hazina ya Mazingira ya Ulimwenguni Pote huko Indonesia, anaeleza tatizo hilo hivi: ‘Tunataka maendeleo daima. Nina wasiwasi kwamba baada ya miaka kumi, tutakuwa tumefahamu umuhimu wa kutunza mazingira, lakini hakutakuwa na viumbe wa kuhifadhi.’

      Watu pia wanahangaikia kazi zao. Imekuwa rahisi zaidi kupoteza kazi na mapato kwa sababu mashirika yanayoungana ulimwenguni pote na mashindano makali katika biashara yanalazimu makampuni kuboresha huduma zao. Makampuni yanayohangaikia kupata faida kubwa huona kwamba ni jambo la busara kuwaajiri na kuwafuta wafanyakazi kwa kutegemea faida inayopatikana, lakini jambo hilo huwaletea watu matatizo makubwa.

      Kuongezeka kwa mikopo na fedha za kigeni ulimwenguni pote kumetokeza tatizo jingine. Watega-uchumi wa kimataifa wanaweza kukopesha nchi zinazoendelea fedha nyingi sana lakini baadaye kuondoa fedha zao kwa ghafula wakati hali ya uchumi inapozorota. Wakati fedha hizo zinapoondolewa nchi zinazohusika zinaweza kukumbwa na matatizo ya kiuchumi. Mnamo mwaka wa 1998, watu milioni 13 walifutwa kazi huko Asia Mashariki kwa sababu ya hali mbaya za kiuchumi. Huko Indonesia, mapato halisi ya wale wafanyakazi ambao hawakufutwa kazi yalipungua kwa asilimia 50.

      Kwa sababu nzuri basi, watu wanatarajia mambo mabaya na vilevile mazuri kutokana na utandaridhi. Je, unapaswa kuogopa utandaridhi? Au, je, unaweza kutarajia kwamba utandaridhi utakuwezesha kufanikiwa maishani? Je, matokeo ya utandaridhi yametufanya tutarajie mazuri wakati ujao? Makala yetu inayofuata itajibu maswali hayo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Hata hivyo, makadirio ya wastani, hasa yale ya ulimwenguni pote, yanaweza kupotosha. Katika sehemu nyingi, mapato ya familia hayajaongezeka hata kidogo katika miaka 50 iliyopita, na katika sehemu nyingine mapato ya familia yameongezeka sana.

      [Blabu katika ukurasa wa 3]

      Mali halisi za watu 200 matajiri zaidi ulimwenguni ni nyingi kuliko jumla ya mapato ya asilimia 40 ya watu wote duniani

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

      VYOMBO VYA TEKINOLOJIA VINAVYOUNGANISHA ULIMWENGU

      Maendeleo ya tekinolojia yamebadili mawasiliano kabisa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Sasa ni rahisi zaidi kupata habari na kuwasiliana na watu haraka na kwa bei nafuu karibu katika sehemu zote ulimwenguni.

      TELEVISHENI Siku hizi watu wengi ulimwenguni wanaweza kutazama televisheni, hata kama hawana televisheni zao. Kufikia mwaka wa 1995, kulikuwa na televisheni 235 kati ya kila watu 1,000 ulimwenguni. Idadi hiyo ilikuwa karibu mara mbili ya ilivyokuwa mwaka wa 1980. Watu walio katika maeneo ya mbali sana wanaweza kupata habari kutoka sehemu zote za ulimwengu kwa kutumia kifaa kidogo chenye umbo la sahani kinachopokea ishara za televisheni kutoka kwenye setilaiti. Francis Fukuyama, ambaye ni profesa wa uchumi wa kisiasa, anasema hivi: “Siku hizi, hakuna nchi ambayo haiwezi kupata habari za ulimwengu.”

      INTERNET Kila juma watu wapatao 300,000 huanza kutumia Internet. Mnamo mwaka wa 1999, ilikadiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2001 watu milioni 700 wangekuwa wameunganishwa kwenye Internet. Mwandishi Thomas L. Friedman anasema hivi: “Tokeo ni kwamba watu wengi sana wanajifunza kuhusu maisha ya watu wengine wengi, bidhaa zao, na dhana zao kuliko katika kipindi kingine cha historia.”

      SIMU Gharama za simu zimeshuka sana kwa sababu ya mifumo ya setilaiti na kebo zilizotengenezwa kwa nyuzinyuzi za kioo. Mnamo mwaka wa 1930, bei ya kupiga simu kwa dakika tatu kutoka New York hadi London ilikuwa dola 245 za Marekani, lakini ilishuka hadi senti 35 za Marekani mnamo mwaka wa 1999. Mitandao ya kurusha ishara za redio imewawezesha watu wengi kuwa na simu za mkononi sawa na vile kompyuta zilivyo nyingi leo. Inakadiriwa kwamba kufikia mwisho wa mwaka wa 2002, watu bilioni moja watakuwa na simu za mkononi, na simu hizo zitawawezesha wengi wao kutumia Internet.

      KIDUDE KIDOGO CHA KUPITISHA UMEME Vifaa vyote hivyo vilivyotajwa hapo juu, ambavyo vinaendelea kuboreshwa, vinategemea vidude vidogo vya kupitisha umeme. Katika muda wa miaka 30 iliyopita, uwezo wa vidude hivyo wa kupokea na kuhifadhi habari umeongezeka mara mbili baada ya kila miezi 18. Sasa habari nyingi zaidi zinahifadhiwa katika vidude hivyo vidogo sana kuliko wakati mwingine wowote.

  • Je, Kuunganisha Ulimwengu Kutatatua Matatizo Yetu Kweli?
    Amkeni!—2002 | Mei 22
    • Je, Kuunganisha Ulimwengu Kutatatua Matatizo Yetu Kweli?

      ‘Ulimwengu wetu ulio kama mtaa, una matatizo chungu nzima. Wakazi wake wengine hutendewa vibaya; wengine hawapati njia za kufanikiwa maishani. Mamilioni ya watu hawapati mahitaji yao hivi kwamba hawawezi kuamini kuwa wao ni sehemu ya jamii fulani.’—“OUR GLOBAL NEIGHBOURHOOD.”

      FATIMA, anayeishi katika jiji moja kubwa la Afrika, anajiona kwamba amebarikiwa. Angalau ana friji. Lakini familia yake huishi katika banda la mabati lililo karibu na makaburi matatu yaliyotengenezwa kwa marumaru. Sawa na wakazi wengine nusu milioni, yeye huishi katika eneo kubwa la makaburi. Na hata eneo hilo la makaburi linaendelea kujaa. Fatima anasema hivi: “Watu wengi sana wanahamia katika eneo hili, hasa huku kwenye makaburi.”

      Kilometa 15 hivi kutoka kwenye nyumba ya Fatima, kuna nyumba mpya za anasa zilizo na mikahawa ya fahari na uwanja mkubwa wa kuchezea gofu. Bei ya kucheza gofu mara moja inazidi mshahara wa wastani kwa kila mtu mmoja katika nchi hiyo ya Afrika. Jiji hilo limekumbwa na umaskini sikuzote, lakini viwanja vya gofu—ambavyo hutumiwa na watu wa hali ya juu—vinaanza kutokea na vinawaudhi watu. Kuna ufanisi na umaskini ulimwenguni na mambo hayo hayapatani.

      Bonde la Hadhramaut ni njia ambayo ilitumiwa na wasafiri hapo kale na ina majiji ya kale hapa na pale. Bonde hilo hupita kwenye ardhi kame ya Yemeni katika Mashariki ya Kati. Mtu asipotazama eneo hilo kwa makini atafikiri kwamba hakuna mabadiliko ambayo yamefanywa huko. Lakini hiyo si kweli. Katika jiji la Saywūn lililoko karibu, jumba la makumbusho limemwomba msichana mmoja aliyehitimu chuo kikuu kutayarisha habari kwenye kompyuta zinazoorodhesha vitu vyote vyenye thamani katika jumba hilo. Ijapokuwa msichana huyo alizaliwa katika eneo hilo, alisomea huko Ohio, Marekani. Siku hizi, watu wanaweza kusafiri kokote ulimwenguni na kujifunza mambo kuliko hapo zamani.

      Maelfu ya kilometa upande wa magharibi, katika jangwa la Sahara, malori matatu yanasonga polepole kwenye barabara katika eneo lililojitenga huku yakielekea kusini. Dereva mmoja, anayeitwa Mashala, anasema kwamba anasafirisha televisheni, vifaa vya kurekodi video, na vifaa vya kupokea ishara za televisheni kutoka kwenye setilaiti. Yeye hufahamu matukio ya karibuni ya ulimwengu kwa kutazama vituo vya habari vya Marekani. Anasema kwamba katika mji wa kwao “kila mtu ana vifaa vya kupokea ishara za televisheni kutoka kwenye setilaiti.” Ni sehemu chache tu duniani ambazo haziwezi kupokea habari za ulimwengu.

      Kuenea daima kwa watu, mawazo, habari, fedha, na tekinolojia kotekote ulimwenguni, kumetokeza jamii mpya ya ulimwenguni pote ambayo inaweza kuleta faida. Utandaridhi unawasaidia watu kusambaza utamaduni wa kienyeji huko Yemeni na unamsaidia Mashala kuchuma dola 3,000 za Marekani kila anapoenda safari ya majuma matatu. Lakini sio watu wote wanaopata fedha nyingi. Fatima na majirani zake huwaona watu wachache wakifurahia faida za utandaridhi, huku wakibaki katika umaskini.

      Ijapokuwa ulimwengu wetu haujawa mahali pazuri, yaelekea kwamba matokeo ya utandaridhi hayawezi kufutika. Je, watu wanaweza kuacha kutumia televisheni zao, kutupa simu zao za mkononi, kuharibu kompyuta zao, na kuacha kusafiri katika nchi nyingine? Je, mataifa yatajaribu kujitenga na mataifa mengine ya ulimwengu, kisiasa na kiuchumi? Yaonekana mambo hayo hayawezi kutukia. Hakuna mtu ambaye angependa kutupilia mbali faida za utandaridhi. Lakini vipi juu ya matatizo ambayo yametokea? Yanasababisha wasiwasi mwingi, na yanaathiri kila mtu. Hebu tuchunguze kwa ufupi baadhi ya matokeo mabaya zaidi ya utandaridhi.

      Tofauti Inayozidi Kuongezeka

      Sikuzote kumekuwa na matajiri na maskini ulimwenguni pote, lakini utandaridhi wa kiuchumi umeongeza ile tofauti kati ya matajiri na maskini. Ni kweli kwamba inaonekana nchi fulani zinazoendelea zimefaidika tangu zilipoingia katika biashara ya ulimwenguni pote. Wataalamu wanasema kwamba katika miaka kumi iliyopita, idadi ya watu maskini huko India ilipungua toka asilimia 39 hadi asilimia 26 na kwamba maendeleo kama hayo pia yamekuwako katika bara lote la Asia. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba kufikia mwaka wa 1998, asilimia 15 tu ya watu huko Asia Mashariki ndio walioishi kwa dola 1 kwa siku, ikilinganishwa na asilimia 27 miaka kumi mapema. Hata hivyo, hali ulimwenguni pote si nzuri hivyo.

      Katika eneo lililoko kusini mwa jangwa la Sahara huko Afrika na katika maeneo fulani mengine yanayoendelea, mapato yameshuka katika muda wa miaka 30 iliyopita. Kofi Annan, katibu-mkuu wa UM, anasema hivi: “Jumuiya ya kimataifa . . . inakubali watu wapatao bilioni 3—karibu nusu ya wanadamu wote—kuishi kila siku kwa dola 2 za Marekani au chini ya hapo katika ulimwengu wenye utajiri mwingi sana.” Ubinafsi katika biashara ni jambo moja kuu linalosababisha tofauti hiyo kubwa ya kijamii. Larry Summers, aliyekuwa waziri wa fedha wa Marekani anasema hivi: ‘Ulimwenguni pote, taasisi za watu binafsi zinazoshughulika na mikopo na fedha za kigeni huwapuuza maskini hohehahe. Benki kubwakubwa hazianzishwi katika sehemu zenye umaskini—kwa sababu hazitapata faida.’

      Tofauti hiyo kubwa katika mapato ya matajiri na maskini huwafanya watu na nchi mbalimbali kugawanyika. Muda mfupi uliopita, mali za yule mtu tajiri zaidi huko Marekani zilizidi jumla ya mali halisi za Wamarekani wengine zaidi ya milioni 100. Utandaridhi pia umesaidia makampuni tajiri ya kimataifa kuimarika na kudhibiti kwa kadiri kubwa biashara ya bidhaa fulani ulimwenguni. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1998, makampuni kumi tu ndiyo yaliyodhibiti asilimia 86 ya biashara ya mawasiliano ya simu ambayo ina thamani ya dola bilioni 262 za Marekani. Mara nyingi, makampuni hayo ya kimataifa huwa na uwezo mkubwa kuliko serikali mbalimbali na, kama vile shirika la Amnesty International linavyosema, makampuni hayo “hayatilii maanani haki za binadamu na za wafanyakazi.”

      Mashirika ya haki za binadamu yanahangaikia jinsi watu wachache wanavyomiliki mali nyingi, na hilo linaeleweka. Je, ungependa kuishi mahali ambapo matajiri, ambao wanafanyiza asilimia 20 ya idadi ya watu, wanachuma mapato yanayozidi yale ya maskini kwa mara 74? Na kupitia televisheni, watu hao maskini, ambao wanafanyiza asilimia 20 ya idadi ya watu, wanafahamu vyema jinsi matajiri wanavyoishi, ijapokuwa hawana njia ya kuboresha maisha yao. Ukosefu huo mwingi wa haki katika ulimwengu wetu huchochea sana fujo na mfadhaiko.

      Utamaduni Unaenea

      Hangaiko jingine pia linahusu mgongano wa utamaduni na kuenea kwa tamaa ya mali. Utandaridhi unaeneza sana dhana mbalimbali, na Internet ni mfano bora wa jambo hilo. Kwa kusikitisha, Internet haitumiwi tu kueneza habari zinazofaa, utamaduni, na biashara. Vituo fulani vya Internet huonyesha picha chafu na kuendeleza ubaguzi wa rangi, au kamari. Vingine hata hueleza waziwazi jinsi mtu anavyoweza kujitengenezea mabomu. Kama vile Thomas L. Friedman anavyosema, ‘ni rahisi sana kupata habari hatari kwenye Internet. Unaweza kujikuta mahali ambapo watu wanapanga njama au kuona picha chafu na hakuna mtu wa kukuzuia wala kukuelekeza.’

      Televisheni na filamu huathiri sana maoni ya watu. Mara nyingi filamu hutayarishwa huko Hollywood, ambayo ndiyo biashara kuu ya kutengeneza filamu ulimwenguni. Mara nyingi, biashara hiyo kubwa ya filamu huonyesha mambo yanayoendeleza tamaa ya mali, ujeuri, au ukosefu wa adili. Huenda mambo hayo yasipatane kabisa na utamaduni wa nchi nyingi ulimwenguni. Hata hivyo, mara nyingi serikali, walimu, na wazazi hushindwa kuzuia filamu hizo.

      Mkazi mmoja wa Havana, huko Kuba, alimwambia hivi mgeni mmoja kutoka Amerika Kaskazini: ‘Tunapenda utamaduni wa Marekani. Tunajua mabingwa wenu wote wa Hollywood.’ Utamaduni wa Magharibi pia huwafanya watu wapende vitafunio na soda zao. Mfanyabiashara mmoja huko Malasia alisema hivi: “Hapa watu wanapenda kitu chochote ambacho kimetoka katika nchi za Magharibi, hasa Marekani. . . . Wanataka kula vyakula vyao na kuwa kama wao.” Mkuu wa chuo kimoja cha Havana alisema hivi kwa huzuni: “Kuba si kisiwa tena. Visiwa vimetokomea. Kuna ulimwengu mmoja tu.”

      Utamaduni wa Magharibi ambao unaenea sana unaathiri matazamio na matamanio ya watu. Kichapo cha Human Development Report 1998 kilisema hivi: ‘Watu wameacha kushindana na majirani zao na wanataka kuishi kama matajiri na watu mashuhuri ambao wanaonyeshwa kwenye filamu na kwenye vipindi vya televisheni.’ Kwa wazi, wanadamu wengi hawataweza kamwe kuwa na maisha kama hayo.

      Je, Suluhisho Ni Kuunganisha Ulimwengu?

      Sawa na miradi mingi ya wanadamu, utandaridhi umeleta faida na hasara. Umewawezesha watu fulani kufaidika kiuchumi, na kuleta maendeleo katika mawasiliano ya ulimwenguni pote. Hata hivyo, unawafaidi matajiri na watu wenye uwezo kuliko maskini. Wahalifu wametumia faida za utandaridhi vizuri kuliko serikali mbalimbali. Na virusi vinavyosababisha magonjwa vimeenea kwa sababu ya utandaridhi.—Ona masanduku kwenye ukurasa wa 8 na 9.

      Utandaridhi umeongeza sana matatizo ulimwenguni. Badala ya kusuluhisha matatizo hayo, utandaridhi umechangia matatizo. Migawanyiko na mfadhaiko umeongezeka katika jamii. Serikali ulimwenguni pote zinajaribu kutumia faida za utandaridhi huku zikiwazuia raia wasiathiriwe na athari zake mbaya. Je, serikali hizo zitafanikiwa? Je, inawezekana kwamba suluhisho ni kuunganisha ulimwengu kwa njia ya kuwajali wanadamu wengine? Makala inayofuata itajibu maswali hayo.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      KUENEA KWA UHALIFU NA UGAIDI

      Kwa kuhuzunisha, mbinu za kuendeleza biashara zaweza kutumiwa kwa urahisi na wahalifu. Kichapo cha Human Development Report 1999 kinasema hivi: ‘Mashirika ya kimataifa yamejitahidi kubuni mbinu za kusitawisha biashara ulimwenguni pote na magenge ya wahalifu ya kimataifa yanatumia mbinu hizo.’ Magenge ya wahalifu yamefaidikaje kutokana na utandaridhi?

      Magenge ya kuuza dawa za kulevya yamegundua njia nyingi za kufanya biashara yao ya mabilioni ya dola kuonekana kuwa halali. Kwa kuwa vizuizi vingi vya forodha vimeondolewa na wasafiri wameongezeka, ni rahisi magenge hayo kusafirisha dawa za kulevya kutoka nchi moja hadi nyingine au kutoka bara moja hadi jingine. Katika miaka ya 1990, utengenezaji wa kokeini uliongezeka mara mbili na wa kasumba uliongezeka mara tatu. Magenge ya wahalifu ya kimataifa pia yamesitawisha biashara ya ukahaba inayotokeza faida kubwa. Kila mwaka, wanawake na wasichana wapatao 500,000 husafirishwa kwa meli hadi Ulaya Magharibi kwa kusudi hilo—wengi wao wakipelekwa huko kwa lazima.

      Sawa na mashirika ya kimataifa, magenge ya wahalifu yameungana pia katika miaka ya hivi majuzi. Magenge mengi yanafanya kazi ulimwenguni pote, na kwa jumla magenge hayo hupata dola trilioni 1.5 za Marekani kwa mwaka—fedha nyingi kuliko jumla ya pato la taifa la Ufaransa.a

      Internet pia imetumiwa vibaya na wataalamu wakora wa kompyuta. Mnamo mwaka wa 1995, mtaalamu mmoja mlaghai wa kompyuta aliiba habari zilizokadiriwa kuwa zina thamani ya dola milioni 1 za Marekani pamoja na nambari 20,000 za kibinafsi za kadi za mikopo. José Antonio Soler, Mhispania ambaye ni mkurugenzi wa benki, alisema hivi: “Kuiba kwa kutumia tekinolojia mpya si hatari sana na kunatokeza faida kubwa.”

      Magaidi pia hutumia faida za utandaridhi. Kwa kuwa vyombo vya habari husambaza habari ulimwenguni, magaidi wanaweza kuwateka nyara watalii kadhaa wa nchi za Magharibi katika nchi ya mbali ili kutangaza haraka malalamiko yao ya kisiasa.

      VITU VIBAYA VINAVYOENEA

      Watu na vilevile magonjwa yanaweza kuenea ulimwenguni pote, na baadhi ya magonjwa hayo ni hatari. Profesa Jonathan M. Mann, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, anasema hivi: ‘Magonjwa yameenea hasa kwa sababu kuna ongezeko kubwa la wasafiri, bidhaa zinazosafirishwa, na mawazo yanayoenea ulimwenguni pote. Sasa, magonjwa mapya ya kuambukiza na yale ya zamani yanatokea na kuenea kwa urahisi ulimwenguni.’

      Jambo hilo linaonyeshwa wazi na ugonjwa wa UKIMWI ambao sasa unasababisha vifo vya watu milioni tatu hivi kila mwaka. Katika nchi fulani za Afrika, wafanyakazi wanaotoa huduma za afya wanahofu kwamba hatimaye ugonjwa huo utaua theluthi mbili ya vijana. Ripoti moja ya Mradi wa Umoja wa Mataifa Kuhusu UKIMWI inasema hivi: “Ijapokuwa kwa karne na miaka kumekuwa na magonjwa ya kuambukiza, vita na njaa, hakuna wakati mwingine wowote ambapo vijana wengi hivyo wamekufa.”

      Mbali na viini na virusi, kuna vitu vingine vinavyoenea ulimwenguni. Wanyama, mimea, na wadudu wametoroka mazingira yao ya asili na kuingia katika mabara mengine. Aina fulani ya nyoka wenye sumu kutoka Australia wamevamia Visiwa vya Pasifiki. Yaonekana waliingia huko kwa kujificha ndani ya ndege. Nyoka hao wamewamaliza karibu ndege wote wa msituni huko Guam. Gugu-maji kutoka Amerika Kusini limeenea katika nchi 50 za kitropiki, ambako linaziba mifereji na kuharibu vidimbwi vya samaki. Gazeti la International Herald Tribune linasema hivi: “Viumbe wanaovamia sehemu nyingine za ulimwengu wanasababisha hasara ulimwenguni pote kila mwaka ambayo huenda ina thamani ya mamia ya mabilioni ya dola na kueneza magonjwa na kuharibu sana mazingira.”

      [Maelezo ya Chini]

      a “Jumla ya pato la taifa” ni thamani ya bidhaa na huduma zote ambazo nchi hutoa kwa mwaka.

      [Picha]

      PESA ZINAZOSAFIRISHWA KIHARAMU

      Zikiwa zimefichwa ndani ya shehena ya wanasesere

      KUSAFIRISHA KOKEINI KIHARAMU

      Kokeini yenye thamani ya dola 4,000,000 za Marekani ilipatikana mpakani ndani ya gari moja la kwenda safari

      UGAIDI WA KIBIOLOJIA

      Maaskari watafuta virusi vya kimeta huko Capitol Hill, Washington, D.C.

      MASHAMBULIZI YA MABOMU

      Bomu lililotegwa kwenye gari lalipuka huko Israel

      KUENEA KWA UKIMWI ULIMWENGUNI POTE

      Ugonjwa wa UKIMWI umeenea sana huko Afrika Kusini hivi kwamba hospitali fulani za umma hazikubali wagonjwa zaidi

      VIUMBE WANAOVAMIA MAZINGIRA MAPYA

      Nyoka-mti wenye rangi ya kahawia wako karibu kuwamaliza ndege wote wa msituni huko Guam

      GUGU-MAJI

      Mmea huu huziba mifereji na kingo za mito katika nchi 50 hivi

      [Hisani]

      Kusafirisha pesa na kokeini kiharamu: James R. Tourtellotte and Todd Reeves/U.S. Customs Service; ugaidi wa kibiolojia: AP Photo/Kenneth Lambert; basi linaloungua: AP Photo/HO/Israeli Defense Forces; mtoto: AP Photo/Themba Hadebe; nyoka: Photo by T. H. Fritts, USGS; gugu-maji: Staff CDFA, California Dept. of Food & Agriculture, Integrated Pest Control Branch

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Utandaridhi wa kiuchumi umeongeza tofauti kati ya matajiri na maskini

      [Hisani]

      UN PHOTO 148048/ J. P. Laffont - SYGMA

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Internet inatumiwa kuendeleza ugaidi

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki