Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Namba Huathiri Maisha Yako?
    Amkeni!—2002 | Septemba 8
    • Je, Namba Huathiri Maisha Yako?

      JE, NAMBA zina ujumbe wa siri? “Bila shaka!” ndivyo wanavyojibu watu fulani, huku wakitaja mfano mmoja wenye kustaajabisha—shambulizi la magaidi lililotukia Septemba 11, 2001.

      Mbashiri mmoja anayetumia namba asema hivi: “Punde tu niliposikia habari hizo, niliangalia tarehe: tarehe 11, mwezi wa 9, mwaka wa 2001.” Kwa kawaida 11 huonwa na wabashiri wanaotumia namba kuwa moja ya “namba kuu” za ubashiri. Kwa hiyo, baadhi ya watu wanaopenda ubashiri huo wameorodhesha mambo mbalimbali kuhusu shambulizi hilo la magaidi, ambayo yanahusiana na namba 11 ambayo wanaiona kuwa “namba kuu.” Yafuatayo ni baadhi ya mambo waliyogundua:

      ■ Msiba huo ulitukia tarehe 11, mwezi wa 9. . . . 9 + 1 + 1 = 11.

      ■ Septemba 11 ilikuwa siku ya 254 ya mwaka. . . . 2 + 5 + 4 = 11.

      ■ Namba ya ndege iliyogonga jengo la kaskazini ilikuwa 11.

      ■ Ndege hiyo ilikuwa na abiria 92. . . . 9 + 2 = 11.

      ■ Ndege iliyogonga jengo la kusini ilikuwa na abiria 65. . . . 6 + 5 = 11.

      ■ Majengo Mawili yaliyogongwa yalikuwa na umbo la namba 11.

      ■ Jina la Kiingereza “New York City” lina herufi 11.

      Kubashiri kwa kutumia namba kumeenea sana Afrika, Asia, na Amerika. Katika ubashiri huo, tarakimu na jumla ya namba mbalimbali huonwa kuwa na ujumbe wa pekee. Kwa nini watu huvutiwa na ubashiri huo? Kituo kimoja kwenye Internet kinasema kwamba kufumbua mafumbo ya herufi za alfabeti zilizotumiwa katika majina—aina maarufu ya ubashiri unaotumia namba—“hufunua habari sahihi kuhusu utu wa mtu, mwelekeo wake, sifa zake na udhaifu wake.” Kituo hicho kinasema kwamba kuchunguza “tarehe yetu ya kuzaliwa huonyesha jinsi maisha yetu yatakavyokuwa, shangwe na magumu tutakayopata.”

      Je, madai hayo ni ya kweli? Au je, kuna hatari zisizoonekana katika kuchunguza ujumbe wa siri katika namba?

  • Kwa Nini Namba Zinavutia?
    Amkeni!—2002 | Septemba 8
    • Kwa Nini Namba Zinavutia?

      HEBU wazia ulimwengu ungekuwaje bila namba. Hakungekuwa na pesa. Watu wangebadilishana mali kwa mali. Vipi michezo? Bila namba hatungeweza kujua mshindi au hata idadi ya wachezaji katika kila timu!

      Hata hivyo, mbali na matumizi hayo muhimu ya namba, watu fulani huziona kuwa na ujumbe wa siri. Hiyo ni kwa sababu namba si halisi. Huwezi kuhisi au kushika namba. Kwa mfano: Tofaa lina rangi fulani hususa, ulaini, ukubwa, umbo, harufu, na ladha hususa. Unaweza kutofautisha tofaa, limau, mpira, au kitu kingine kwa kuchunguza kila moja ya sifa hizo. Hata hivyo, huwezi kutofautisha namba kwa njia hiyo. Huenda vitu saba vilivyowekwa pamoja visiwe vinafanana na vitu vingine saba—isipokuwa kwa idadi yake. Kwa hiyo, kujua maana ya namba—kwa mfano, kujua tofauti kati ya sita na saba—ni jambo linalowaziwa tu. Na ndiyo sababu watu huona namba kuwa na ujumbe wa siri.

      Sayansi ya Uwongo Badala ya Fundisho la Pythagoras

      Kwa kawaida, watu wa kale waliamini kwamba namba zina ujumbe wa pekee. Mwanafalsafa na mwanahisabati Mgiriki anayeitwa Pythagoras, aliyeishi katika karne ya sita K.W.K., alifundisha kwamba vitu vyote vinaweza kufafanuliwa kwa kutumia namba. Yeye na wafuasi wake walifundisha kwamba ulimwengu wote umepangwa kwa utaratibu na usawaziko. Basi je, kuna uwezekano wa kwamba vitu vyote vinategemea hesabu?

      Tangu siku za Pythagoras, namba zimetumiwa kubashiri na kufasiri ndoto na kukumbuka mambo. Zimetumiwa na Wagiriki, Waislamu, na waumini wa Jumuiya ya Wakristo. Wayahudi waliofumbua mafumbo walitumia ubashiri wa namba unaoitwa gematria. Waliambatanisha kila moja ya zile herufi 22 za alfabeti ya Kiebrania na namba fulani kisha wakadai kwamba wamepata ujumbe wa siri kwenye Maandiko ya Kiebrania.

      Wabashiri wanaotumia namba siku hizi wanatumia mbinu hiyohiyo. Mara nyingi, wao huanza na jina lako na tarehe uliyozaliwa. Namba fulani huambatanishwa na kila herufi ya jina lako. Mbashiri huongeza namba hizo na namba za mwezi na za tarehe uliyozaliwa ili kupata namba zako kuu. Kisha anatoa fasiri ya pekee ya namba hizo ambazo anadhani zinaeleza kila jambo kukuhusu—kutia ndani utu wako, mambo unayotamani, na mambo yatakayokupata wakati ujao.

      Labda wengi huvutiwa sana na ubashiri huo kwa sababu unaonekana kuwa sahihi. Edward Albertson asema hivi katika kitabu chake Prophecy for the Millions: “Watu wengi wameamini ubashiri wa namba baada ya kuona kwamba ujumbe wa namba fulani unawafaa kabisa watu fulani ambao wamechunguzwa.” Hata hivyo, ubashiri huo wa kutumia namba umeitwa pia sayansi ya uwongo. Kwa nini? Je, kuna sababu zinazoweza kukufanya utilie shaka ubashiri huo?

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

      JE, BIBLIA INA UJUMBE WA SIRI?

      Katika kitabu chake The Bible Code, mwandishi wa habari Michael Drosnin adai kwamba alipata ujumbe wa siri katika Maandiko ya Kiebrania kwa kutumia kompyuta. Drosnin alidai kwamba “ujumbe huo wa siri” ulikuwa na maneno haya, “mwuaji atakayeua” kisha akaona jina Yitzhak Rabin—na alipata ujumbe huo mwaka uliotangulia kuuawa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Yitzhak Rabin.

      Kitabu The Bible Code kilizusha ubishi fulani. Mwanahisabati na mwanafizikia anayeitwa Dave Thomas alionyesha kwamba habari yoyote inayochunguzwa na kompyuta inaweza kuwa na ujumbe unaoonekana kuwa wa kifumbo. Thomas alipochunguza Maandishi yaliyochunguzwa na Drosnin alipata maneno haya, “ujumbe wa siri,” “mpumbavu,” na “uwongo.” Thomas asema kwamba “ujumbe wa siri waweza kupatikana popote, maadamu uko tayari kutumia wakati wako na nguvu zako kuchunguza kila jambo linaloweza kutukia.”

      Kompyuta inaweza kutumiwa kupata mchanganyo wa herufi fulani ambazo zinaweza kutumiwa kutabiri mambo fulani kwa sababu ina uwezo wa kupiga hesabu nyingi sana. Lakini hilo hutukia tu bila kutarajiwa na halithibitishi kwamba Biblia ina ujumbe wa siri.a

      [Maelezo ya Chini]

      a Unaweza kupata habari zaidi katika Mnara wa Mlinzi, Aprili 1, 2000, ukurasa wa 29-31.

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      Pythagoras alifundisha kwamba vitu vyote vinaweza kufafanuliwa kwa kutumia namba

      [Hisani]

      Courtesy National Library of Medicine

  • Je, Inafaa Kutafuta Mwongozo Katika Namba?
    Amkeni!—2002 | Septemba 8
    • Je, Inafaa Kutafuta Mwongozo Katika Namba?

      JE, KUBASHIRI kwa kutumia namba kunapatana na akili na sayansi? Je, namba zinaweza kufunua wakati wetu ujao? Je, inafaa kupanga maisha yako ya baadaye kwa kutegemea mafumbo na ubashiri wa namba?

      Wabashiri wengi wanaotumia namba wametatizwa na kipingamizi kimoja. Kipingamizi hicho ni kwamba tamaduni mbalimbali zinatumia kalenda tofauti. Kwa mfano, vipi ikiwa mtu anaishi nchi inayotumia kalenda ya Kichina? Fikiria tarehe ile iliyotajwa kwenye makala ya kwanza—Septemba 11, 2001. Kulingana na kalenda ya Kichina, tarehe hiyo ilikuwa siku ya 24 ya mwezi wa saba, mwaka wa 18 wa mzunguko wa 78. Kalenda ya Julian inaonyesha tarehe hiyo ni Agosti 29, 2001. Kulingana na kalenda ya Waislamu, ilikuwa tarehe 22 Jumada II 1422, na kwenye kalenda ya Waebrania ilikuwa 23 Eluli 5761. Tarehe inayoandikwa kwa njia nyingi hivyo inawezaje kuwa na ujumbe muhimu? Jambo jingine ni hili: Mara nyingi majina huandikwa kwa njia maalumu katika lugha mbalimbali. Kwa mfano, herufi zilizo katika jina la Kiingereza John zinawakilishwa na namba 2, lakini herufi za jina hilohilo katika Kihispania—Juan—zinawakilishwa na namba 1.

      Ingawa vitu vingi katika ulimwengu vinategemea fomyula za hesabu, fomyula hizo zinaweza kujaribiwa na kuthibitishwa. Lakini kudai kwamba jina lako lilichaguliwa kimbele lifaane na tarehe yako ya kuzaliwa na kwamba lingeweza kuambatanishwa na namba fulani ili ujue wakati wako ujao ni jambo tofauti kabisa.

      Mkataa ni wazi: Si jambo la kiakili kuamini kwamba kubashiri kwa kutumia namba ni sahihi kwa kuwa kunategemea mambo mbalimbali yanayotofautiana sana kama vile kalenda na lugha.

      “Wakati na Tukio Lisilotazamiwa”

      Baadhi ya watu huvutiwa na ubashiri huo kwa sababu wana hamu ya kujua mambo yao ya wakati ujao. Hata hivyo, Biblia inasema waziwazi kwamba maisha ya mwanadamu hayawezi kupangwa kimbele. Tunasoma hivi: “Si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati [“tukio lisilotazamiwa,” “NW”] huwapata wote.” (Mhubiri 9:11, italiki ni zetu.) Naam, mambo mengi hutukia ghafula. Hatuwezi kamwe kubashiri mambo kulingana na tarehe ya kuzaliwa au namba zinazowakilisha jina kwa sababu ya matukio hayo ya ghafula.

      Fikiria mfano mwingine: Biblia inatutia moyo tuwe wakarimu inaposema hivi: “Tupa chakula chako usoni pa maji; maana utakiona baada ya siku nyingi. Uwagawie sehemu watu saba, hata wanane; maana hujui baa gani litakalokuwa juu ya nchi.” (Mhubiri 11:1, 2, italiki ni zetu.) Mara nyingi, misiba hutukia ghafula na watu hawawezi kujua ni lini itakapotokea. Kwa hiyo, profesa wa hesabu Underwood Dudley anaandika hivi kuhusu wabashiri wanaotumia namba: “Wanapuuza kabisa uwezekano wa mambo kutukia ghafula. Mambo yenye kustaajabisha yanaweza kutukia ghafula tu bila mpango wowote.”

      Ni kweli kwamba huenda wabashiri hao wakatabiri mambo fulani na yakatokea. Kwa nini? Nyakati nyingine, mambo hayo yanaweza kutukia kwa usahihi bila kutarajiwa. Nyakati nyingine, wabashiri hao wanaweza kutabiri mambo mengi ambayo yanaweza kuhusiana na matukio kadhaa. Lakini kuna jambo jingine zito sana ambalo linahitaji kufikiriwa.

      Je, Ni Namna Fulani ya Uaguzi?

      Biblia haitaji moja kwa moja ubashiri wa kutumia namba. Lakini inamtaja Hamani, Mwamaleki ambaye alipanga njama ya kuwaangamiza Wayahudi walioishi Uajemi katika karne ya tano K.W.K. Biblia yasema hivi: “Hamani aliagiza kura (yaani Purimu) ifanywe kupata siku na mwezi ambapo angetekeleza njama zake. Basi, kura ikaangukia siku ya kumi na nne ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari.”—Esta 3:7, Biblia Habari Njema, italiki ni zetu.

      Katika nyakati za kale, kupiga kura kulikuwa njia halali ya kukomesha ubishi.a (Mithali 18:18) Lakini Hamani alitumia kura kufanya uaguzi—zoea ambalo linashutumiwa na Biblia. Andiko la Kumbukumbu la Torati 18:10-12, BHN, lasema kwamba Mungu anamchukia kabisa ‘mtu apigaye ramli, mwaguzi, mpiga bao, mchawi, mlozi, mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo. Yeyote atendaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu.’

      Biblia inaonyesha kwamba uaguzi na nguvu za kiajabu zinahusiana na kuwasiliana na roho waovu. Roho waovu wanaweza kutumia matukio fulani ili kutimiza makusudi yao. Lolote liwalo, jambo moja ni hakika: Mungu anashutumu zoea la kuwasiliana na roho waovu, na kufanya hivyo kunaweza kumfanya mtu awe mtumwa wa roho waovu.—1 Samweli 15:23; Waefeso 6:12.

      Kubashiri kwa kutumia namba hakupatani kabisa na sayansi, wala si jambo la kiakili. Na jambo baya zaidi ni kwamba ubashiri huo ni namna fulani ya uaguzi na hivyo ni kinyume cha mafundisho ya Biblia. Kwa hiyo, kubashiri kwa kutumia namba si njia inayofaa ya kupangia maisha yako au miradi yako.

      [Maelezo ya Chini]

      a Kura zilipigwa kwa kutia vitu vidogo-vidogo—kama vile vijiwe au vipande vidogo vya mbao—katika mapindo ya nguo au katika chombo fulani na kuvitikisa. Mtu ambaye kura yake ilitwaliwa kwanza ndiye aliyechaguliwa.

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      KALENDA MBALIMBALI ZINAZUSHA KIPINGAMIZI KUHUSU KUBASHIRI KWA KUTUMIA NAMBA

      GREGORY Septemba 11, 2001

      KICHINA siku ya 24 ya mwezi wa 7, mwaka wa 18 wa mzunguko wa 78

      JULIAN Agosti 29, 2001

      WAISLAMU 22 Jumada II 1422

      WAEBRANIA 23 Eluli 5761

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      JE, NYOTA ZA UNAJIMU ZINATEGEMEKA?

      “Nyakati nyingine wewe ni mwenye urafiki, lakini nyakati nyingine u kimya tu. Unaona haifai kuwaambia watu usiowajua mambo yako ya kibinafsi. Wewe hufuati tu maoni ya watu, unahitaji kuthibitishiwa jambo lolote kabla ya kulikubali. Unapenda mabadiliko, na unahuzunika unapowekewa sheria nyingi. Una uwezo mbalimbali ambao bado hujautumia kikamili. Una mwelekeo wa kujichambua-chambua.”

      Je, maelezo hayo yanakufaa? Ikiwa wafikiri hivyo, basi huenda unayachukua maelezo hayo kwa uzito mno, kwa sababu watu wengi wana sifa hizo. Wasomaji huelekea kukubali maelezo ambayo wanaona ni sahihi na kupuuza yale ambayo si sahihi. Kitabu Why Do Buses Come in Threes—The Hidden Mathematics of Everyday Life (Kwa Nini Mabasi Huja Matatu-Matatu—Hesabu ya Siri Katika Maisha ya Kila Siku) kinasema kwamba “watafiti wamegundua kuwa watu wengi hushindwa kutambua maelezo ya nyota yao wakati alama za nyota zinapoondolewa, lakini wao huamini kuwa maelezo ya nyota yao ni sahihi wanapoona alama hizo.”

      [Sanduku katika ukurasa wa 8]

      Namba za Mfano Katika Biblia

      Biblia hutaja namba fulani za mfano kulingana na muktadha wa Maandiko. Kwa mfano, namba nne hutumiwa kuonyesha ujumla au jambo linalohusu kila mtu. Hoja hiyo inaelezwa na misemo kama vile “ncha nne za dunia” na “pepo nne za mbinguni.” (Isaya 11:12; Danieli 8:8) Nyakati nyingine, namba sita huwakilisha kutokamilika. Kitabu cha Ufunuo kinasema kwamba tengenezo la kisiasa la Shetani hapa duniani lina “nambari ya binadamu”—666. (Ufunuo 13:18) Namba sita imetajwa mara tatu, na hilo linakazia kutokamilika kwa tengenezo hilo ambalo linafananishwa na hayawani. Wakati ambapo namba saba hutumiwa kwa njia ya mfano, hiyo huwakilisha ukamilifu. (Mambo ya Walawi 4:6; Waebrania 9:24-26) Namba hizo na nyinginezo zinazotumiwa kwa njia ya mfano katika Maandiko hueleweka kulingana na unabii unaozungumziwa.

      Ingawa Maandiko hukazia umuhimu wa namba fulani, Biblia haituhimizi tupatanishe herufi za maneno fulani na namba ili kujua mambo fulani hakika ya kifumbo.

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Hamani alitumia uaguzi ili kuchagua tarehe ya kutekeleza njama yake ya kuwaangamiza Wayahudi wote

  • Mwongozo Unaotegemeka kwa Ajili ya Wakati Ujao
    Amkeni!—2002 | Septemba 8
    • Mwongozo Unaotegemeka kwa Ajili ya Wakati Ujao

      JE, KUTOTEGEMEKA kwa ubashiri wa kutumia namba na aina nyinginezo za uaguzi kunamaanisha kwamba hatuwezi kamwe kujua mambo ya wakati ujao? La hasha!

      Wanadamu hawawezi kujua mambo ya wakati ujao kupitia namba. Lakini “Mungu aliye hai,” ambaye anatangaza “mwisho tangu mwanzo” amewajulisha mambo ya wakati ujao. Naye huwajulisha kupitia Neno lake, Biblia. (1 Timotheo 4:10; Isaya 46:10) Isitoshe, neno la Mungu aliye hai ‘linaweza kufahamu fikira na makusudio ya moyo’ na hivyo kukusaidia kujua nia yako na mambo yanayoweza kukufanya ufanikiwe, lakini neno la wabashiri wanaotumia namba haliwezi kufanya hivyo.—Waebrania 4:12.

      Muumba wetu, ambaye ni Mtungaji wa Biblia, ndiye tu anayeweza kutabiri kwa usahihi mambo ya wakati ujao. Mungu ana nguvu zisizo na kifani, naye hutumainika sikuzote. Yehova Mungu alisema hivi: “Nimenena, nami nitafanya.” (Isaya 46:11) Baada ya kuwaongoza Waisraeli kuingia Nchi ya Ahadi, Yoshua alisema hivi kwa uhakika: “Halikuanguka neno lo lote katika jambo lo lote lililokuwa ni jema ambalo BWANA alikuwa amelinena katika habari ya nyumba ya Israeli; yalitimia mambo yote.”—Yoshua 21:45; 23:14.

      Biblia ina unabii mwingi ambao haujatimizwa. Baadhi ya unabii huo unatabiri kwamba uovu utaondolewa kabisa ili dunia iwe paradiso. (Zaburi 37:10, 11; Mithali 2:21, 22) Je, unavutiwa na wakati ujao wa aina hiyo? Je, unaamini kwamba Muumba wetu ana hekima na nguvu za kuboresha hali duniani? Ikiwa ndivyo, utafurahia kujua yale ambayo Biblia inasema kuhusu hali ya wakati ujao ya dunia.a

      Kwa hiyo, badala ya kutafuta habari zako za wakati ujao katika namba, tumia wakati wako kwa hekima sasa kwa kujitahidi kupata ujuzi sahihi wa Biblia na unabii uliomo. Mashahidi wa Yehova wako tayari kukusaidia kupata ujuzi zaidi kuhusu wakati ujao unaotajwa na Neno la Mungu, Biblia.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki