-
Katika Nyakati Zetu Zenye Hofu Ni Nani Unayeweza Kuitibari Kikweli?Mnara wa Mlinzi—1988 | Aprili 15
-
-
“Msitie itibari yenu katika washarifu, wala katika mwana wa mwanadamu wa dunia, ambaye kwake hakuna wokovu.”—ZABURI 146:3, NW.
-
-
Katika Nyakati Zetu Zenye Hofu Ni Nani Unayeweza Kuitibari Kikweli?Mnara wa Mlinzi—1988 | Aprili 15
-
-
Itibari Inayopungua
3. Kuna ithibati gani kwamba itibari inakosekana katika wakati wetu?
3 Katika nyakati hizi zenye hofu, tunahitaji sana wengine ambao tunaweza kuitibari, watu ambao watakuwa washikamanifu, wenye msaada katika wakati wa uhitaji. Lakini wengi wanahisi kuwa wanakatishwa tumaini na wale ambao waliwaitibari. Karatasi-habari katika bara moja ilitangaza hivi: “Watu Hawaitibari Mengi Ya Mashirika ya Serikali.” Wenye kuitibariwa kwa kadiri ndogo sana walikuwa ni viongozi wa kisiasa na kibiashara. Kutoitibariana kumeongezeka katika jamaa pia, kama inavyothibitiwa na talaka nyingi. Katika mataifa fulani, kuna talaka moja kwa kila ndoa tatu au hata moja kwa kila ndoa mbili. Katika nchi moja, asilimia 70 ya ndoa mpya zote zinapata talaka katika muda wa miaka kumi! Kwa hiyo kuitibariana kunaendelea kukosekana. Kutoitibariana kunachukua mahali pa kuitibariana. Limeacha kuwa lisilo la kikawaida lile elezo la mtu aliyesema: “Mimi siitibari tena mtu yeyote.”
4. Vijana wengi wanaathiriwa na hofu jinsi gani?
4 Kuna ukosefu mwingi sana wa kuitibariana kwa sababu huu ndio wakati wenye hofu kupita nyakati nyinginezo zote katika historia ya kibinadamu. Karne hii imeona vita vya ulimwengu viwili na vingine vingi ambavyo vimepoteza uhai wa watu zaidi ya milioni mia moja. Sasa, silaha za nyukilia zinatisha kufuta kabisa uhai wote duniani. Na jambo hilo linaathiri itibari ya hata walio wachanga sana. Jarida moja la kitiba liliripoti hivi: “Watoto zaidi na zaidi, hata watoto wadogo sana, wanaogofywa na tisho la maangamizi makuu ya kinyukilia.” Karatasi moja ya habari ya Kanada ilisema kwamba sasa kuna “hali ya kupuuza mambo, huzuni, uchungu na hisia ya kutojiweza” katika vijana wengi. Kijana mmoja alisema: “Sisi hatuhisi kamwe kuwa tuna himaya ya watu wazima. Huenda sisi tukakua na kupata kuwa kizazi chenye kupuuza mambo zaidi ya vizazi vyote ambavyo vimepata kuwako.”
5. Huenda ikawa kikundi cha wasio na hatia na wasiojiweza kingehisi jinsi gani, kama kingeweza kusema?
5 Na kikundi kingine cha vijana kingesema nini—kama wangeweza kunena—juu ya kutohisi wanapata himaya ya watu wazima? Tunamaanisha wale ambao wanauawa kwa kutolewa mimba kabla hawajazaliwa. Kadirio moja linaonyesha kwamba hesabu ya mimba zinazotolewa ulimwenguni pote ni kama milioni 55 kila mwaka. Huo ni ubaini ulioje kuelekea sehemu ya wanadamu wasio na hatia na wasiojiweza hata kidogo!
6. Uhalifu umeongezeaje kutoitibariana katika wakati wetu?
6 Kutoitibariana kumeongezeka kwa sababu ya hofu nyingine inayozidi katika siku yetu: hofu ya kuwa jeruhi wa uhalifu. Wengi sasa wanafanya kama mwanamke yule aliyesema kwamba yeye hulala akiwa na bastola chini ya mto wake. Mwanamke mwingine mwenye hofu alisema: “Mimi nachukizwa na jambo hili. . . . Nyanya yangu hakufunga kamwe milango yake kwa kufuli.” Hivyo, tahariri moja ya karatasi-habari katika Puerto Rico ilitangaza hivi: “Wanaofungwa gerezani ni sisi,” ndiyo, katika maskani zetu wenyewe zenye makomeo na zilizofungwa kwa kufuli.” Hofu hizi zina msingi mzuri. Inaelekea kwamba, katika United States, mathalani, mwanamke mmoja katika watatu ataingiliwa kwa nguvu wakati wa maisha yake. Mpasuaji mkuu huko alisema kwamba “Waamerika wapatao milioni nne wanapatwa na jeuri kubwa kila mwaka—kuuawa, kunajisiwa, kupigwa kwa wake, kutendwa vibaya kwa watoto, kuviziwa.” Uhalifu huo ni wa kikawaida katika bara nyingi, hiyo ikizidi kuharibu itibari ambayo watu wanayo katika wengine.
7. Kwa sababu gani hali mbaya za kiuchumi zinachangia kutoitibariana?
7 Katika mataifa yasiyositawi, watu walio wengi wanaishi katika umaskini. Ni wachache wanaoitibari kwamba kuna mtu ye yote atawaondoa katika huo. Rais wa bara moja kama hilo alisema kwamba katika mkoa mmoja, kati ya kila vitoto 1,000 vinavyozaliwa, 270 vinakufa kabla havijawa na umri wa mwaka mmoja. Ni nyumba moja tu kati ya kila 100 iliyo na maji. Serikali ya nchi nyingine inasema kwamba asilimia 60 ya watoto wayo ni wahitaji, na watoto milioni saba walioachwa “wanakua wakiwa wahuni wasioweza kusoma wala kuandika, walioachwa na wasioweza kuajiriwa.” Katika United States, hesabu ya vijana wasio na maskani inakadiriwa kuwa 500,000, lakini watu fulani wanasema tarakimu iliyo halisi ni ya juu zaidi. Ni itibari ya kadiri gani ambayo vijana hao wanaweza kuwa nayo katika wazazi wao, katika jamii, katika sheria na utengemano, au katika ahadi za viongozi?
8. (a) Uthibitifu wa mataifa yaliyo matajiri na uchumi wa duniani pote unatishwa jinsi gani? (b) Wastadi wanaweza kuitibariwa kwa kadiri gani ili watatue matatizo ya kiuchumi?
8 Matatizo ya kiuchumi yanakumba hata mataifa yaliyo matajiri. Hivi majuzi, United States ndiyo ilikuwa na visa vingi zaidi vya kufilisika kwa benki tangu ule Mshuko Mkubwa wa Thamani ya Pesa katika miaka ya 1930. Mtaalamu mmoja wa uchumi aliandika hivi: “Matokeo halisi ni mfumo wa kutunzia fedha ambao ni wenye kuharibika upesi leo kama ulivyokuwa katika miaka ya 1920,” kabla tu haujavunjika-vunjika. Mtazamaji mmoja alinena juu ya “dhoruba yenye uharibifu mkubwa inayoweza kuwa inakaribia” katika uchumi wa ulimwengu. Mwingine alisema: “Hisia ya kuona uharaka inatokea kwa sababu sasa mikazo hiyo katika mfumo wa kimataifa haikaribii tu; imekwisha kuwasili.” Je! wataalamu wa uchumi wanaweza kuitibariwa waongoze mataifa kutoka kwenye matata haya? Mmoja wao alisema kwamba maandishi ya matabiri yao “ni yenye kuogofya sana hivi kwamba hapana shaka kwamba wao sana-sana wanaeneza mvurugo.”
Matazamio Mema Yaliyowekwa Pasipofaa
9. (a) Ni jambo gani limepata matazamio mema yaliyokuwako mwanzoni mwa karne hii? (b) Kwa sababu gani Mashahidi wa Yehova wasingalitaka kutia sahihi katika hati ya Umoja wa Mataifa katika 1945?
9 Yote hayo yanatofautiana kama nini na matazamio mema yaliyokuwako wakati ulimwengu ulipoingia karne ya 20. Kulikuwa kumekuwa na miongo ya amani ya kadiri fulani, na ilihisiwa kwamba amani na ufanisi ungefikia vilele vipya. Lakini katika 1914 Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ilivunja-vunja tazamio hilo. Katika 1945, baada ya vita ya ulimwengu ya pili yenye kuogofya zaidi, Mkataba wa Umoja wa Mataifa ulitiwa sahihi. Mataifa yaliandika njozi yao ya kuona ulimwengu wenye amani, ufanisi, na haki, baada ya vita. Ripoti ya hivi majuzi ilisema: “Hati ya mwisho ilitiwa sahihi na nchi 51, zikiwakilisha kila kontinenti, jamii ya watu na dini.” Hata hivyo kulikuwa na dini moja ambayo haikuwakilishwa, wala haikutaka kuwakilishwa, Mashahidi wa Yehova. Wao walijua kwamba ahadi hizo za amani, ufanisi, na haki hazingetimizwa na taifa lo lote la ulimwengu huu wala na shirika lo lote la mataifa hayo, kama vile Umoja wa Mataifa.
10. Uhakika wa mambo ni nini leo kwa kulinganishwa na ile ndoto ya Umoja wa Mataifa kule nyuma katika 1945?
10 Ripoti iyo hiyo inasema: ‘Miaka 40 baadaye linaonekana kuwa jambo linalofaa kuyapitia mambo ya hakika kwa kuyalinganisha dhidi ya yale ya kuwazika tu. Ushuhuda unahuzunisha. Mambo yaliyopo ni ulimwengu uliopungukiwa na haki, uliopungukiwa na usalama, na jeuri yenye kuongezeka. Idadi ya watu inayokosa chakula, maji, nyumba, utunzaji wa afya, na elimu, inaendelea kuwa kubwa bila kubadilika. Jambo hilo halikuwa ndoto katika 1945.’ Inaongeza hivi: ‘Miaka 40 baada ya mataifa kujiunga pamoja kuhakikisha kwamba watu wote wangeweza kuishi bila hofu na upungufu wa vitu, ulimwengu halisi wa miaka ya 1980 ni wenye umaskini unaolemea sana angalau robo moja ya wanadamu. Vifo vinavyohusianishwa na njaa ni vya wastani wa 50,000 kwa siku,’ Hata hivyo, mataifa yanatumia dola zaidi ya milioni mia moja kila saa kwa vita!
11. Ahadi za kibinadamu za ulimwengu bora zinastahili itibari kwa kadiri gani?
11 Kwa sababu ya hali hiyo yenye kuhuzunisha baada ya wanadamu kupata nafasi ya karne nyingi za kutatua matatizo hayo, je! sisi tunaweza kuitibari ahadi za kibinadamu kwamba watatatua matatizo haya? Ustahili wa kuitibariwa kwa ahadi hizo unakaribia kuwa kama yale maneno ya kapteni wa meli kubwa aliyesema hivi: “Mimi siwezi kuwazia hali yo yote ambayo ingesababisha meli [kubwa] izame. . . . Ufundi wa kisasa wa kuunda meli umefanya maendeleo yanayopita kiwango cha kuweza kuzama.” Mshiriki mmoja wa wafanya kazi katika chombo hicho alimwambia hivi baharia mmoja: “Mungu mwenyewe hawezi kuifanya meli hii izame.” Hata hivyo, meli hiyo, ile Titanic, ilizama katika 1912 ikipoteza uhai wa watu 1,500. Katika 1931 Shirika la Kitaifa la Elimu katika United States lilisema kwamba kupitia elimu “uhalifu utakaribia kumalizwa kabisa kabla ya 1950.” Katika 1936 mwanajarida Mwingereza aliandika kwamba “chakula, mavazi, na nyumba vitagharimu kiasi kidogo sana” kufikia 1960. Je! wewe hukubali kwamba magumu ya leo yanaonyesha ahadi hizo zilikuwa uwongo?
-