Kuutazama Ulimwengu
MNYANYASO WASHINDWA
Hata ingawa makala ya Mnara wa Mlinzi wa Agosti 15, 1989 ilifunua mnyanyaso wa Mashahidi wa Yehova katika Burundi, mashambulizi na uonevu umeendelea bila kukoma. Hata hivyo, ripoti za karibuni zaidi kutoka Burundi zaonyesha ongezeko la asilimia 8.9 katika hesabu ya Mashahidi wanaotenda katika mzunguko mmoja wa makundi. Katika mzunguko mwingine, ambako mnyanyaso umekuwa wenye jeuri zaidi, kumekuwako ongezeko la asilimia 4.2. Mashahidi hao wanatumia wastani wa saa 17 hadi 18 kila mwezi katika kazi yao ya kuhubiri peupe. Waamini wenzi wao kuuzunguka ulimwengu wameendelea kuandikia serikali ya Burundi ili kupinga kutendewa vibaya kwa Mashahidi.
KUPUNGUZA DHORUBA
Wakati pepo za Chamchela Hugo zilipopita mbiombio dhidi ya pwani ya Amerika Kaskazini mnamo Septemba 21 na 22 mwaka jana, pepo zacho zenye kasi ya kilometa 216 kwa saa zilipiga majengo na kutupa-tupa mashua kama kwamba zilikuwa vitu vidogo tu. Mashahidi wa Yehova kutoka maeneo ya ujirani walijipanga upesi ili kuletea ndugu zao msaada katika Charleston, Karolina Kusini, ambako dhoruba hiyo iliathiri zaidi. Kufikia asubuhi ya tarehe 23, wenye kujitolea 125 walikuwa tayari wanafanya kazi, wakiondoa mabomoko na miti iliyoanguka kutoka kwenye makao ya Mashahidi wenzao na kutoka kwenye Majumba ya Ufalme. Ugavi wa maji, jenereta, na petroli uliletwa. Kesho yake, malori 14 yalifika Charleston na kujaza Majumba ya Ufalme yake matano na chakula, barafu, maji, na ugavi mwingine kwa ajili ya Mashahidi wa mahali hapo. Baada ya siku kadhaa, kikundi kimoja cha Mashahidi kilikuwa kimechanga dola 10,000 za kushughulikia mahitaji hayo ya haraka.
WEVI WA MIFUKONI WA KIMATAIFA
Kiangazi kijapo London, na wevi wa mifukoni pia huja. Dazeni nne zao, wanaojulikana kimataifa kuwa ndio stadi zaidi ulimwenguni, huja kwa ndege kwenye mji huo na kuiba zinazokadiriwa kuwa pauni milioni 10 za pesa taslimu na bidhaa kwa muda unaopungua miezi miwili, laripoti The Sunday Times. Wakiwa wanaitwa Los Chileanos, kufuatia Chile, nchi watokayo, wanasafiri hadi Madrid, Spania, au Milan, Italia, ambako wanaiba pasipoti ili waingie kiharamu katika Uingereza. Malengo makuu ni maduka makubwa ya Oxford Street, vituo vya reli vya chini ya ardhi, na sebule za hoteli za West End. Pia wanachangamana na misongamano ya watu kwenye matukio ya kijamii na pamoja na watalii kwenye vivuta-macho vinavyojulikana sana kama Mnara wa London na Makaburi ya Westminster. Kwa kuwa wao ni stadi sana na werevu na kwa urahisi wanaweza kuvuta kando fikira za wanayeshambulia, polisi wanashauri kutochukua pesa nyingi katika sehemu zenye msongamano wa watu. “Kanuni rahisi ndiyo hii,” akasema ofisa mmoja, “sikuzote vitu vyako vya thamani viwe mbele ya macho yako.”
JE! WANA HAKI YA KUJUA?
Maliki wa Japani alikufa “bila kujua hali ya ugonjwa wake wala hata kuuliza juu yao,” ikasema The Daily Yomiuri. Alikufa kwa kansa bila kujua, kama ndugu yake mchanga zaidi aliyekufa miezi 11 mapema. Ingawa hesabu inayoongezeka ya Wajapani husema wangetaka kujua kama wana kansa, theluthi tatu husema hawangeambia mtu wa ukoo mwenye kusumbuliwa na ugonjwa huo. Fikira hii ilionyeshwa na vyombo vya habari vya Kijapani, ambavyo, ingawa vilijua maliki alikuwa na kansa muda mrefu kabla hajafa, kwa ujumla waliepuka habari hiyo. Gazeti fulani kuu lililotaja jina la ugonjwa wa maliki lililazimishwa na madai makali ya umma kwamba lisitoe elezo jingine lolote maadamu maliki alikuwa angali hai.
KUKABILIANA NA UZEE
Uchunguzi wa hivi majuzi uliofanywa katika Jamhuri ya Muungano ya Ujeremani waonyesha jinsi mwelekeo na mtazamio chanya ulivyo wa maana ili watu waendelee kuwa na ziha (nguvu za mwili) waendeleapo kuongezeka umri. Uchunguzi mmoja ulipima mtazamio wa wakaaji wa kao moja la watu wazee. Kwa kutegemea majibu yaliyotolewa kwa karatasi moja ya maswali, wanasayansi waliweza kutabiri kwa usahihi wa asilimia 92 ni nani kati ya wenye kujibu wangebaki hai kwa kipindi cha miaka mitatu. Ripoti moja katika gazeti la Kijeremani Rheinischer Merkur/Christ und Welt yakata shauri kwamba wale wasiojipatia tazamio la kuwako wakati ujao, au wasiojitunza sana na kujifanyia maamuzi yao wenyewe, huenda wakawa na uwezekano haba zaidi wa kubaki hai. Hata hivyo, mara nyingi wazee hukadiriwa ubora wa chini kuliko ipasavyo. Gazeti hilo latoa maoni ya kwamba ingawa ubongo wa kibinadamu huenda ukapoteza kadiri fulani ya mwendo na uwezo wao uzee uingiapo, “huu mpunguo wa mwendo hufanywa uwe si kitu” na pande nyingine za uelewevu wa akili ambazo hunolewa na uzoevu wa mambo na ‘kufanya kazi vizuri zaidi baadaye maishani.’