Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa
—Ujeremani (Inaendelea)
“THE HARP OF GOD”
ILI kutayarisha njia ya kugawa kwa haraka kitabu The Harp of God (Kinubi cha Mungu), ambacho sasa kilikuwa kimepatikana kwa Kijeremani, Sosaiti ilitayarisha na ikachapa nakala milioni tano za kikaratasi kiitwacho “Why?” (Kwa Sababu Gani). Ilitokea kwamba viwanda vilivyopewa kazi ya kuchapa The Harp of God vilikuwa nyuma sikuzote katika uchapaji, hii ikichelewesha uchapaji mara nyingi. Bei ya kitabu iliyotajwa katika kikaratasi cha Sosaiti haikuweza kudumishwa, kwa sababu ya pesa kuzidi kupoteza thamani; na mwanzoni mwa Januari wa 1923 bei ya marks 100 ililazimika kupandishwa iwe marks 250, kiasi ambacho kilikuwa sawa na bei ya robo ratli ya siagi, ingawa wakati huu gharama ya kuchapa Harp ilikuwa imekwisha fikia marks 350. Yaliyokuwamo katika kitabu hicho yaliamsha shauku nyingi sana, si kati ya akina ndugu tu, bali pia kati ya rafiki za kweli.
SOSAITI YAHAMA
Akina ndugu waliokuwa wakisimamia kazi karibuni wakajua kwamba vifaa vya kiwanda vilivyopatikana katika Barmen vilikuwa havitoshi. Kwa wazi wakiongozwa na roho ya Yehova, walikaza fikira zao Magdeburg ambako jumba lilipatikana linunuliwe mara moja. Ingawa iliwalazimu kuamua haraka, Sosaiti ilinunua jumba huko katika Leipziger Street. Walihama rasmi kutoka Barmen kwenda Magdeburg Juni 19, 1923. Kwa ghafula vikosi vya Ufaransa vikaja na kukaa katika maeneo ya Rhine na Ruhr, pamoja na Barmen na Elberfeld. Bila shaka, hii ilimaanisha kwamba afisi ya posta, kituo kikubwa cha magari-moshi na benki ya Ujeremani vilichukuliwa pia, jambo ambalo lingalifanya iwe vigumu sana kuangalia faida za makundi kutoka Barmen. Ripoti ya kila mwaka ya 1923 ilisema hivi juu ya tukio hili: “Makao makuu ya Brooklyn yalipata taarifa asubuhi moja kwamba tawi la Ujeremani lilikuwa limehamia Magdeburg salama. Asubuhi iliyofuata magazeti yaliripoti kwamba Wafaransa walikuwa, wameanza kukaa Barmen. Twamshukuru Bwana wetu aliye mwema sana kwa ulinzi na baraka yake.”
Sasa iliwezekana kuchapa The Watch Tower katika kiwanda chetu wenyewe. Toleo la kwanza lililochapwa lilikuwa lile la Julai 15, 1923. Karibu juma tatu au nne hivi baadaye mashine kubwa yenye kujijaza karatasi yenyewe ilitayarishwa na kazi ikaanza kufanywa ya kitabu cha kwanza cha Studies in the Scriptures. Mara baada ya hapo kitabu The Harp of God kilichapwa katika mashine iyo hiyo.
KUPUNGUA KWA THAMANI YA PESA
Wahubiri walikuwa wamekwisha shauriwa katika mwezi wa Agosti wa 1921 wawe wawekevu katika ugawaji wa trakiti Bible Students Monthly kwa sababu ya gharama kubwa iliyohusika katika uchapaji. Nakala hazikupaswa zigawe bila uteuzi, bali zilipaswa zitolewe kwa wale tu walioonyesha kupendezwa kwa kweli.
Mwanzoni mwa 1922 Sosaiti ililazimika kutangaza kwamba bei ya uandikishaji wa mwaka wa The Watch Tower, ambalo wakati huo lilikuwa likichapwa kwa mwezi tu, ingekuwa marks 16. Mwezi mmoja baadaye ikawa lazima kuipandisha iwe marks 20, na Julai wa mwaka uo huo ikawa marks 30. Walakini, miezi iliyofuata thamani ya pesa ilipungua hata katika Oktoba ikawa lazima Sosaiti itangaze kwamba wakati ujao maandikisho yangekubaliwa ya kipindi cha miezi mitatu tu. Kwa sasa bei ya miezi mitatu ilikuwa imepanda kuwa marks 70. Miezi mitatu ya kwanza ya mwaka wa 1923 ikawa lazima akina ndugu walipe marks 200, na kwa kipindi cha pili cha miezi mitatu marks 750. Kufikia Juni 15 uandikishaji wa mwaka mmoja ukawa marks 3,000, na mwezi mmoja baadaye ukawa marks 40,000. Agosti 1 ikawa lazima Sosaiti iache utumishi wote wa maandikisho, nakala moja moja zikipatikana kwa malipo ya pale pale. Lakini kufikia Septemba 1 nakala moja ilikuwa marks 40,000 tayari. Mwezi mmoja baadaye nakala moja ikawa marks 1,660,000, na kufikia Oktoba 25 pesa zilipungukiwa thamani sana hata nakala moja ikawa marks mamilioni milioni mbili u nusu. Pesa hazikuwa na thamani hata kidogo. (Mark moja ni kama shilingi 2.80)
Kuangalia huku kufupi miaka yenye hatari ya kupungua kwa thamani ya pesa kwaweza kuonyesha kazi ya Bwana ililazimika kuendeshwa chini ya hali zenye magumu namna gani wakati huo. Kwa kweli, miezi mitatu ya mwisho ya mwaka wa 1923 ugawaji wa vitabu vya Sosaiti ulikaribia kukoma kabisa. Kuendelea kuliwezekana kwa msaada wa Yehova tu.
‘WAZEE WA KUCHAGULIWA’
Mpango wa kidemokrasi wa kuchagua wazee ulikuwa jambo ambalo lingaliweza kuwa la kutosha kupunguza mwendo wa kazi wakati wa miaka ya 1920. Kulikuwa na maoni mbalimbali juu ya namna uchaguzi huo upaswavyo kuwa. Wengine walitaka wenye kutaka kuchaguliwa waweze kujibu walau 85 kwa mia ya maulizo ya V.D.M. kwa usahihi. (V.D.M. maana yake ni Verbi Dei Minister, au Mhudumu wa Neno la Mungu.) Kwa mfano, katika Dresden ndivyo mambo yalivyokuwa. Lakini yaliyowapata akina ndugu katika Halle yatuonyesha matakwa hayo ya kuchukuliwa na fikira yalileta magumu ya namna gani. Walikuwako ndugu kundini ambao nia yao juu ya kazi haikuwa njema, lakini, kwa upande mwingine, waliotaka wawe viongozi kundini. Mwishowe walipoambiwa kwamba hata hawakuwa wamejibu maulizo ya V.D.M., na hivyo hawakustahili kupata vyeo vya uongozi kundini, mara hiyo walijitayarisha wapate ulioelekea kuwa uangalizi kwao. Waliposhindwa tena kupata cheo hicho baadaye ambacho walikuwa wamejitahidi wakipate, uasi ulitokea ukafanya kundi ligawanyike, karibu wahubiri 200 kufikia 250 tu wakabaki kati ya 400 waliokuwako kwanza.
Katika makundi fulani mara nyingi kulikuwa na mabishano makali wakati wa uchaguzi. Kwa mfano, katika Barmen uchaguzi wa kuinua mikono ulipaswa ufanywe kuchagua watu fulani mwaka wa 1927. Mtu aliyeona yaliyotukia kwa macho asema kwamba haukupita muda mrefu kabla kila mtu hajaanza kupaza sauti, wote kwa pamoja, na akina ndugu wakalazimika kubadili uchaguzi uwe wa kutumia karatasi za uchaguzi wa siri, ambao ndio uliokuwa ukitumiwa na makundi mengi. Katika Kiel hata ilikuwa lazima kufanya uchaguzi wa wazee chini ya ulinzi wa polisi.
Mambo haya yalitokea kwa sababu wengine wa waliotaka kuchaguliwa hawakuwa Wakristo waliokomaa. Kwa kweli, wengine kati yao waliipinga kazi ya Ufalme ama waziwazi ama kwa njia isiyo wazi.
Kwa mfano, Sosaiti ilipotia moyo kuwe na funzo la kawaida la kitabu la kundi juu ya The Watch Tower, hesabu fulani ya ‘wazee wa kuchaguliwa’ hasa ndio waliopinga shauri hili na kuleta migawanyiko katika makundi mengi. Msimamizi katika Remscheid alisema kwamba wakati ujao wale ambao wangetumiwa kuongoza funzo la Watch Tower ni wale waliokuwa wakienda katika utumishi wa shambani Jumapili asubuhi peke yao, halafu mmojawapo wa ‘wazee wa kuchaguliwa’ akanyanyua kiti na, baada ya kumtisha msimamizi nacho, akatoka kundini, akichukua watu 40 waambatane naye. Jambo kama hilo lilitokea katika Kiel ambako ndugu na dada 50 kati ya 200 kundini waliondoka, zijapokuwa jitihada za Bible House.
Tukitazama nyuma, bila shaka twaweza kusema kwamba sehemu ya pili ya miaka ya 1920 ilikuwa wakati wa kupepeta hapa Ujeremani. Wengine waliokuwa wamefuatana nasi mpaka wakati huo wakawa adui wa wazi wa Ufalme. Bila shaka kuondoka kwao hakukuwa hasara kwa tengenezo la Mungu kwa sababu miaka ya 1930 ilipata kuwa wakati wa kujaribiwa kweli kweli kwa wale waliobaki waaminifu!
KUFILISIKA KWA BENKI
Katikati ya kukosa kazi kulikokuwa kunaongezeka na hali ya uchumi isiyo na imara, benki, ambamo hazina nyingi za kuendeshea kazi katika Ujeremani na Ulaya ya kati ziliwekwa, ilifilisika. Tawi la Ujeremani peke yake likapata hasara ya marks 375,000.
Ikawa lazima Sosaiti ipashe makundi habari kwamba kusanyiko lililopangwa kuwa wakati wa kiangazi mwaka wa 1930 katika Berlin lingefutwa. Katika barua yao, walitaja pia uwezekano wa ‘kukatizwa kwa uchapaji wa vitabu.’ Lakini tangazo hili lilishtua sana. Ingawa ndugu walikuwa na pesa chache sana, kwa maana wengi wao hawakuwa wameajiriwa, ili kuhakikisha vitabu vingechapwa bila kukatizwa walikuwa wenye nia mara hiyo kuchanga pesa walizokuwa wameweka kwa ajili ya kusanyiko la Berlin, na pia cho chote kingine walichoweza kuchanga kutokana na mali zao chache. Kwa kweli, wengi walitoa pete zao za arusi na vito vingine.
Kwa sababu hiyo, mipango iliyofanywa ya kupanua kazi kabla tatizo la benki halijatokea haikuzuiwa, sivyo, wala haikuahirishwa. Katika masika ya mwaka wa 1930 sehemu zaidi ya jumba lililopakana na jumba letu la kwanza ilinunuliwa. Majengo ya zamani yaliyokuwa katika sehemu iliyonunuliwa karibuni yalibomolewa na, kwa kadiri ilivyowezekana, vifaa hivyo vikatumiwa na akina ndugu kujenga jengo kubwa jipya la Betheli lenye vyumba 72, kila chumba kikiwa na nafasi ya watu wawili, na chumba kikubwa cha kulia.
MAKUSANYIKO KATIKA PARIS NA BERLIN
Mwaka wa 1931 Ndugu Rutherford alipanga tena safari ya Ulaya. Kusanyiko lilipaswa lifanyiwe Paris kutoka Mei 23 mpaka 26, na moja katika Berlin kutoka Mei 30 mpaka Juni 1. Kwa sababu ya hali mbaya ya uchumi katika Ujeremani, Ndugu Rutherford alishauri kwamba mipango ifanywe ya kukaribisha ndugu kutoka Ujeremani ya kusini na Rhineland waje Paris, kwa maana ingewagharimu kiasi kidogo zaidi kwenda huko kuliko kwenda Berlin. Magari-moshi ya pekee yalitayarishwa yaanze safari kutoka Cologne, Basel na Strassburg. Akina ndugu walishukuru sana na, ikawa kwamba, kati ya watu 3,000 waliokusanyika Paris, 1,450 walitoka Ujeremani.
Ndugu Rutherford hakuwa amekosa kuona mambo mengine mengi miaka hiyo. Si yeye peke yake, bali pia idadi kubwa ya wale waliokuwa Betheli walikuwa wameiona hatari alimokuwa Ndugu Balzereit. Ni kweli kabisa kwamba yeye alikuwa msimamizi mwema na kwamba kazi katika Ujeremani ilipata maendeleo mema chini ya uongozi wake. Walakini, kosa lake kubwa lilikuwa kujipa sifa kubwa juu ya uwezo wake mwenyewe kwa ukuzi mkubwa sana uliokuwako badala ya roho ya Yehova. Wakati wa chakula fulani penye meza ya Betheli Balzereit aliiomba jamaa ya Betheli isimwite tena “ndugu” wakiwapo walimwengu. Nyakati hizo walipaswa wamwite “Bw. Msimamizi,” na hata akaweka kibao katika mlango wa afisi yake chenye kusema “msimamizi.”
Wakati huu ukamilifu wa Balzereit kwa Yehova ulitishwa kutoka upande mwingine. Kwa wazi yeye alikuwa ameogopa mateso sikuzote. Akiwa kiongozi mwenye daraka la afisi ya Ujeremani alikuwa ameshtakiwa juu ya ugawaji wa azimio “Viongozi wa Dini Washtakiwa.” Ni kweli kwamba aliachwa huru, lakini hakimu alipomsihi aache kutoa maneno makali kama hayo katika vitabu vyetu wakati ujao, kwa wazi yeye alikuwa na nia ya kufuata shauri hili, kwa maana semi na maneno katika The Watch Tower au katika vitabu vingine vilivyotoka Brooklyn zilipoelekea kwake kuwa kali sana, yeye alikuwa akipunguza uzito wake.
Tamaa za vitu vya kimwili zilianza kukua pia. Balzereit alikuwa amefurahia kuandika mashairi na kuyachapisha katika gazeti The Golden Age akijiita kwa uongo Paul Gerhard, na sasa alikuwa ameandika kitabu na kukichapisha katika Leipzig. Halafu kitabu hiki kiliongezwa katika orodha ya vitabu vya kugawa na makundi ambao, bila ya kujua hali zilivyokuwa, walikiagiza, kwa njia hiyo wakamletea Ndugu Balzereit faida kubwa ya pesa. Yeye alikuwa na kiwanja cha mchezo wa tennis kilichojengwa katika Betheli wakati mmoja, si kwa sababu ya faida ya jamaa nzima hasa bali kwa matumizi yake mwenyewe.
Katika jaribio la kumaliza jengo jipya liwe tayari kwa sherehe za kuliweka wakf wakati wa ziara ya Ndugu Rutherford, Ndugu Balzereit alikuwa ameongeza wafanya kazi wa Betheli kutoka 165 mwishoni mwa Desemba 1930 wakawa watu 230, lakini yeye hakuwa mwaminifu juu ya jambo hili. Akihofu kwamba Ndugu Rutherford asingeikubali hesabu ya wafanya kazi, Balzereit alipanga ndugu 50 watumwe katika “safari ya kuhubiri” ili wasionekane. Waliporudi waliulizwa kama wangependelea kurudi makwao au kuchukua utumishi wa upainia. Wakitambua kwamba kazi ya Yehova ndiyo iliyohusika wala si nyutu za kibinadamu, ndugu kadha walijitwalia nafasi hii ya kuanza kufanya upainia, ijapokuwa wengine waliondoka wakiona uchungu mwingi sana.
Januari 30, 1933, Hitler alichukua cheo cha mkuu wa Reich (Serikali). Februari 4 alitoa amri ya kuruhusu polisi wachukue vitabu ‘vyenye kuhatirisha utengemano na usalama wa watu wote.’ Amri hii iliweka vizuizi kwa uhuru wa kukusanyika na kuchapa vitabu.
Katika Magdeburg, maafisa wa polisi walikuwa wameipasha afisi habari kwamba picha iliyokuwa katika ukurasa wenye kichwa cha kitabu (shujaa wa vita aliyeshika upanga unaodondoka damu) ilikuwa haikubaliki nao wakadai iondolewe. Ndugu Balzereit, ambaye mara nyingi alikuwa ameonyesha nia ya kuridhiana, alitoa maagizo mara moja jalada zenye rangi ziondolewe katika vijitabu.
Ilikuwa juma ya ushuhuda yenye kujawa na mashaka juu ya yatakayotokea. Adui alionyesha wazi kila siku nia yake ya kupiga kwa nguvu nyingi sana. Kwa hiyo ilitia moyo sana wakati ripoti ilipounganishwa ikaonekana kwamba watu 24,843 walikuwa wamehudhuria mwadhimisho wa Ukumbusho, wakilinganishwa na 14,453 waliohudhuria mwaka uliotangulia. Hesabu ya wahubiri waliokuwa wakitenda wakati wa kipindi cha ushuhuda ilifurahisha pia: walikuwa 19,268, wakilinganishwa na 12,484 wakati wa shughuli ya kijitabu Kingdom mwaka mmoja uliotangulia. Wakati wa siku nane za shughuli vijitabu 2,259,983 vya Crisis vilikuwa vimegawa.
KUSANYIKO LA BERLIN JUNI 25, 1933
Kufikia kiangazi cha mwaka wa 1933 kazi ya mashahidi wa Yehova ilikuwa imepigwa marufuku katika sehemu nyingi za Ujeremani. Nyumba za akina ndugu zilikuwa zikipekuliwa kwa kawaida na ndugu wengi walikuwa wamekamatwa. Kumiminika kwa chakula cha kiroho kulizuiliwa kidogo, ingawa kwa kitambo tu; hata hivyo ndugu wengi walikuwa wanauliza ingewezekana kazi iendeshwe muda mrefu namna gani. Hali ikiwa hivyo makundi yalikaribishwa kwa kupashwa habari muda mfupi sana wafike kwenye kusanyiko ambalo lingefanyiwa Berlin Juni 25. Kwa kuwa ilitazamiwa kwamba wengi wasingeweza kuhudhuria kwa sababu ya marufuku mbalimbali, makundi yalitiwa moyo yatume angaa mjumbe mmoja au wengi. Lakini, kama ilivyotokea, ndugu 7,000 walifika. Wengi wao iliwachukua siku tatu, wengine wakiendesha baiskeli mwendo wote, ijapokuwa wengine walikwenda kwa lori, kwa maana mashirika ya bas yalikataa kukodisha bas kwa tengenezo lililopigwa marufuku.
Ndugu Rutherford, ambaye, pamoja na Ndugu Knorr, alikuwa amekuja siku chache tu kabla ili aone yawezayo kufanywa kuhakikisha usalama wa mali ya Sosaiti, alikuwa ametayarisha tangazo na Ndugu Balzereit litolewe kwa wajumbe wa kusanyiko lipate kupitishwa. Lilikuwa likipinga kujitia kwa serikali ya Hitler katika kazi ya kuhubiri tuliyokuwa tunafanya. Maafisa wakubwa wote wa serikali, kutoka rais wa Reich (Serikali) kufika chini, walipaswa wapokee nakala ya tangazo hilo, ikiwezekana, zitumwe salama kwa kuhakikishwa na stakabadhi. Siku kadha kabla ya kusanyiko kuanza Ndugu Rutherford alirudi Amerika.
Wengi waliohudhuria walikatishwa tamaa na “tangazo,” kwa maana lilikosa kuwa lenye nguvu katika mambo mengi kama akina ndugu walivyokuwa wametumainia. Ndugu Mutze wa Dresden, aliyekuwa amefanya kazi na Ndugu Balzereit karibu karibu mpaka wakati huo, baadaye alimshitaki juu ya kudhoofisha yaliyokuwa yameandikwa kwanza. Haikuwa mara ya kwanza kwa Ndugu Balzereit kupunguza uzito wa usemi ulio wazi wa vitabu vya Sosaiti ili kuepuka matata na mawakili wa serikali.
Hesabu kubwa ya akina ndugu walikataa kulipitisha kwa sababu hiyo tu. Kwa kweli, ndugu mmoja aliyekuwa mhaji aitwaye Kipper alikataa kulitoa lipitishwe na ndugu mwingine akafanya hivyo badala yake. Haikuweza kusemwa kwa haki kwamba tangazo lilikuwa limepitishwa na wote, ingawa baadaye Ndugu Balzereit alimwarifu Ndugu Rutherford kwamba lilikuwa limepitishwa na watu wote.
Wakusanyikaji wakarudi makwao wamechoka na wengi walikuwa wamekata tamaa. Walakini, walipeleka nyumbani nakala 2,100,000 za “tangazo” na kuzigawa kwa haraka wakizituma kwa watu wengi wenye vyeo vya madaraka. Nakala iliyotumwa kwa Hitler ilifuatana na barua ambayo sehemu yake ilisema hivi:
“Afisi ya rais ya Brooklyn ya Watch Tower Society ni yenye urafiki sana sana kwa Ujeremani na imekuwa hivyo sikuzote. Mwaka wa 1918 rais wa Sosaiti na washiriki saba wa Baraza ya Wasimamizi katika Amerika walihukumiwa kifungo cha miaka 80 kwa sababu rais alikataa kuacha magazeti mawili aliyoyatengeneza katika Amerika yatumiwe katika maenezi ya vita kwa kuipinga Ujeremani.”
Hata ingawa tangazo hilo lilikuwa limedhoofishwa na ndugu wengi hawakuweza kukubali kwa moyo wote lipitishwe, serikali ilighadhibika na kuanza kuwatesa wale waliokuwa wameligawa.
Inaendelea katika toleo lifuatalo.
—Kutoka 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses.