Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa
—UJEREMANI (Inaendelea)
“MARA nyingi nimejiuliza nilifaya nini hata nikastahili kubarikiwa hivyo na Yehova wakati uliopita. Leo naamini kwamba sala za baba yangu na mama yangu zimesaidia kuleta baraka hizo. Wao waliweka mfano bora katika mwenendo wa Kikristo katika yote waliyotenda.”
Viko visa 860 ambapo watoto walitolewa kwa wazazi wao, ingawa hesabu barabara inaweza kuwa kubwa kidogo. Kwa sababu ya ukatili huo si ajabu kwamba baadaye wakuu walifikia hatua ya kufanya isiwezekane kuzaa watoto kwa kusema tu kwamba mmoja wa wazazi alikuwa na “ugonjwa wa kurithi.” Kisha mume angeweza kuondolewa uwezo wa kuzaa chini ya mipango ya sheria.
UTARATIBU WA KESI
Mojawapo ya njia za ukatili zilizotumiwa ilikuwa kuacha mwenzi wa ndoa na washiriki wengine wa jamaa wapate mateso ambayo wapendwa wao walipaswa kupata wakati wa kuhojiwa. Emil Wilde anaeleza ukatili wa jambo hili, kwa maana yeye alilazimishwa kusikiliza akiwa katika kijumba chake cha jela mkewe alipokuwa anateswa vilivyo mpaka kufa.
“Septemba 15, 1937,” anaanza kueleza, ”asubuhi na mapema karibu saa 11:00, maafisa wawili wa Gestapo walikuja wakapekua nyumba yetu, baada ya kuhoji watoto wangu kwanza. Baadaye mke wangu na mimi tulipelekwa kwenye makao makuu ya polisi na mara hiyo tukafungiwa katika vijumba vya gereza. Kesi yetu ya kwanza ilifanywa karibu siku kumi baadaye. Niliambiwa mke wangu pia alipaswa awe na kesi yake ya kwanza siku iyo hiyo, na ndivyo ilivyokuwa.
“Kuanza adhuhuri na kuendelea, karibu saa 7:00 alasiri, nikasikia makelele ya mwanamke. Alikuwa anapigwa nayo makelele yalipozidi kuwa makubwa nikayasikia waziwazi zaidi, niliyatambua kuwa yanatoka kwa mke wangu. Nikapiga kengele nikauliza sababu gani mwanamke huyo, mke wangu, alikuwa anapigwa; nikaambiwa kwamba si mke wangu, bali ni mwingine, aliyestahili mapigo kwa sababu ya kukosa adabu. Baadaye sana alasiri hiyo makelele yakaanza tena yakawa makubwa sana hata nikapiga kengele tena nilalame juu ya mke wangu alivyokuwa anatendwa. Gestapo (polisi) waliendelea kukataa hakuwa mke wangu. Karibu saa 7:00 usiku huo sikuweza kuvumilia tena nami nikapiga kengele tena, mara hii afisa wa polisi nisiyemjua jina akasema hivi: ‘Ukipiga kengele mara moja tu zaidi, tutakutenda lile lile ambalo tumemtenda mkeo!’ Kimya kikafuata katika gereza nzima, kwa maana wakati huu walikuwa wamempeleka mke wangu kwenye hospitali ndogo ya kupimia neva. Mapema katika asubuhi ya Oktoba 3, mlinzi mkuu wa Gestapo, Classin, akaja kwenye kijumba changu akaniambia mke wangu amekufa katika hospitali ya kupimia neva. Nikamwambia pale pale bila kumwogopa kwamba wao ndio waliokuwa wa kulaumiwa kwa kifo cha mke wangu, na siku ya mazishi yake nikaandikisha mashtaka ya uuaji juu ya Gestapo. Hii ilifanya Gestapo wanishtaki kuwa nawasingizia.
“Hii ilimaanisha kungekuwa na kesi nyingine zaidi ya ile yangu ya kwanza. Ilipofanywa, dada wawili wakasimama wakati wa kesi ya pekee kortini wakashuhudia hivi: ‘Tulimsikia Bi. Wilde akilia, “Maibilisi nyie, mnanipiga hata kufa.” ‘ Hakimu akaitikia: ‘Lakini wao hawakuona, walisikia tu. Nakuhukumia kifungo cha mwezi mmoja.’ Dada kadha, waliomwona mke wangu baada ya kufa kwake, walihakiksha kwamba aliumbuliwa vibaya sana akiwa na mikwaruzo ya mapigo makubwa kuzunguka koo lake na katika uso wake wote. Nilinyimwa ruhusa ya kuhudhuria mazishi.”
Nyakati nyingine majaribio yalifanywa ya kutia ndugu katika hali ya usingizi kwa kunuiza uchawi. Wengine wao walipewa chakula kilichokuwa imetiwa dawa za kulevya, hata kwa muda fulani wakakosa kujizuia wasijue wanayosema. Katika jaribio la kulazimisha wengine waungame, mikono yao na miguu ilifungwa nyuma yao usiku kucha. Kwa kuwa wengine hawakuweza kuvumilia wakiwa chini ya namna hizo za kuogofya za rnateso, Gestapo (polisi) waliweza kupata habari juu ya namna kazi ya mashahidi wa Yehova ilivyosimamiwa na kuendeshwa.
MAAFISA NA MATAJIRI WENYE URAFIKI
Ingawa maafisa walitumia ‘usemi mpya wenye nguvu na wa sauti kubwa,’ ambao hasa ulitumiwa na viongozi wote katika serikali mpya, msingi wake ukiwa iliyoitwa ‘kanuni ya Fuhrer,’ lilikuwa jambo la kupendeza kwamba hapa na pale maafisa fulani wa polisi walikuwa wangali wanaweza kuwa wenye huruma kwa mwanadamu mwenzao walipokuwa wakishughulika na mashahidi wa Yehova ndani na nje pia ya gereza.
Carl Gohring alifukuzwa kazini na kampuni ya reli ya faragha ya Leuna Works katika Merseburg kwa sababu alikataa kutoa “salamu ya Kijeremani” na kujiunga na Tengenezo Mashuhuri la Kazi. Afisi ya kazi ilikataa kumtafutia kazi na afisi ya afya ikakataa kumpa msaada wo wote. Lakini Yehova, anayeyajua mahitaji ya watu wake, aliongoza shauri hili hata Ndugu Gohring karibuni akapata kazi katika kiwanda cha kutengeneza karatasi katika Weissenfels. Msimamizi wake, Bw. Kornelius, aliajiri ndugu wote katika ujirani huo ambao walikuwa wamefukuzwa katika kazi zao naye hakuwadai lo lote ambalo lingalipingana na dhamiri zao.
Kama ilivyotokea baadaye, walikuwako matajiri wa namna hii pia, ingawa si wengi. Kwa njia hiyo ndugu wengi kidogo waliokolewa katika mikono ya Gestapo. Kulikuwako pia mahakimu mmoja mmoja ambao kwa ndani hawakukubaliana na njia za jeuri zilizotumiwa na serikali ya Hitler. Hasa mwanzoni, hesabu kadha ya mahakimu waliwapa zawadi akina ndugu ya karatasi ya kutiwa sahihi isiyo na madhara, ambayo ilisema tu kwamba wangeepuka kuingia katika utendaji wo wote wa kisiasa. Kwa kuwa akina ndugu wangeweza kuitia sahihi bila masharti yo yote, iliokoa wengi wao wasipoteze uhuru wao.
Wenye kupekua nyumba mara nyingi walionyesha kwamba si maafisa wote waliokuwa na chuki juu ya mashahidi wa Yehova kama ambavyo huenda ilionekana kwa nje. Ndugu na Dada Poddig waliona hili nyumba yao ilipopekuliwa. Walikuwa ndio wakati huo wamepokea barua, kutia na nakala za The Watchtower pamoja na vitabu vingine, kutoka kwa dada wa kimwili wa Dada Poddig aliyeishi Uholandi. Walakini, kabla hawajapata nafasi ya kusoma lo lote, kengele ya mlangoni ikaanza kulia kwa ghafula.
“Upesi,” Dada Poddig akapaza sauti, “wekeni kila kitu katika kabati la jikoni na mfunge mlango.” Walakini, kwa sababu hili lingaliweza kuvuta fikira, akaamua mwishowe kuacha mlango wazi. Kwa sasa wakili wa Gestapo alikuwa amekwisha ingia nyumbani akifuatana na mtu wa SA. “Kwa hiyo,” akaanza kusema, “acha tuanzie papa hapa.” Kwa kusema hivyo alikuwa na maana ya kabati lenye mlango wazi. Kivulana kidogo cha Ndugu Poddig kikasema kwa ghafula: “Mtatafuta sana kabla hamjaona cho chote kabatini,” kisha wakili huyu akacheka akajibu: “Haya, basi, acha tuingie katika chumba kingine kile.” Upekuzi wote haukuwa na matokeo mazuri. Kwa kweli, Ndugu Poddig na jamaa yake walipata maoni ya kwamba—angaa wakili wa Gestapo (polisi)—hakutaka kutafuta cho chote. Ilikuwa wazi kwamba mtu yule wa SA hakudhani upekuzi ulikuwa unaendeshwa vya kutosha naye alitaka kuendelea kupekua. Lakini wakili wa Gestapo akamkemea akamkataza asiendelee kutafuta. Walipoondoka alirudi kwa ghafula akiwa peke yake akamnong’onezea Dada Poddig: “Bi. Poddig, sikiliza nikuambie. Watachukua watoto wako kwa sababu hawamo katika chama cha Vijana wa Hitler. Tafadhali wapeleke watoto wako, hata ikiwa watakwenda huko wakaonekane tu.” “Kisha wote wawili wakaondoka nasi tukaweza kusoma barua yetu kutoka Uholandi kwa amani,” Ndugu Poddig anaandika. “Tukamshukuru Yehova kwa ajili ya mambo mengi mapya na kwa ajili ya The Watchtower lililotiwa ndani tena.”
KADANGANYWA
Bila shaka, viko visa vingi ambapo maaflsa wa Gestapo walipofushwa walipoendesha upekuzi wao na ambapo mara kwa mara walidanganywa na matendo ya upesi kama umeme ya akina ndugu, ikionyesha wazi ulinzi wa Yehova na msaada wa kimalaika.
Dada Kornelius wa Marktredwitx anaeleza jambo lililotokea: “Siku moja polisi mwingine alikuja kupekua. Sisi tulikuwa na vitabu kadha nyumbani, kutia na Watchtower kadha yaliyonakiliwa. Wakati huo, sikuona uwezekano mwingine wo wote kuliko kuvitumbukiza vyote ndani ya birika tupu la kahawa, ambalo lilipata kuwa mezani. Walipokwisha kuchunguza kila kitu, ilibaki kidogo sana maficho haya yapatikane. Wakati uo huo dada yangu wa kimwili akatokea kwa ghafula chumbani. Ndiyo kwanza nikamwambia, ‘Haya, chukua upeleke kahawa yako.’ Alionekana kushangaa kidogo kwanza, walakini akaelewa nilivyomaanisha akaondoka mara moja, akipeleka birika la kahawa. Vitabu vikatoka hatarini na maafisa hawakufahamu kwamba walikuwa wamedanganywa.”
Yenye kupendeza ni hadithi ambayo Ndugu na Dada Kornelius wanaeleza juu ya mwana wao mwenye umri wa miaka mitano Segfried, ambaye wakati huo hakupata magumu ya “salamu ya Kijeremani” na mambo kama hayo kwa sababu hakuwa amepata umri wa shule. Lakini kwa kuwa wazazi wake walikuwa wanamlea katika kweli, yeye alijua kwamba vitabu vya wazazi wake, ambavyo sikuzote walificha baada ya kuvisoma, vilikuwa vya maana sana na kwamba Gestapo hawakupaswa waruhusiwe kuviona. Siku moja alipoona maafisa wawili wanakuja kupita ua kuelekea nyumba ya wazazi wake, mara moja alijua wangetafuta vitabu vilivyofichwa naye akajua mara moja atafanya nini kuwazuia wasipate cho chote. Ajapokuwa asiyepata umri wa shule, alichukua mfuko wa shule wa ndugu yake mkubwa, akatoa vyote vilivyokuwamo akajaza vitabu vyote humo. Akaangika mfuko mgongoni akatoka nje akaenda barabarani nao. Huko akangoja mpaka maafisa wakaondoka, baada ya kupekua wasipate cho chote. Baadaye akarudi nyumbani akaficha tena vitabu alipokuwa amevipata.
“KONDOO” WAPATIKANA GEREZANI
Akina ndugu walikutana na watu wa namna zote walipokuwa gerezani nao wakawaeleza tumaini lao kwa vyepesi kama ilivyowezekana. Furaha yao ilikuwa kuu kama nini wakati mmoja wa wafungwa wenzao alipoikubali kweli! Willi Lehmbecker anatueleza jambo hilo. Yeye alifungwa pamoja na wafungwa wengine katika chumba ambamo kuvuta sigara kuliruhusiwa:
“Kitanda changu kilikuwa juu, lakini mfungwa aliyelala chini yangu alivuta sigara sana hata niliweza kupumua kwa ugumu. Wale wengine wote walipokuwa wamelala niliweza kumpa ushuhuda kutoka katika Biblia juu ya kusudi la Mungu kwa wanadamu. Nilimwona kuwa msikilizaji mwenye makini. Kijana huyu alikuwa mwenye kupenda siasa sana naye alikuwa ametiwa chini ya ulinzi kwa sababu ya kugawa magazeti haramu. Tukaahidiana kwamba, tukiwa huru tena, tukiwa tungali hai, tungejaribu kutembeleana. Lakini ikawa vingine. Mwaka wa 1948 nilikutana naye tena katika mojawapo la makusanyiko yetu ya mzunguko. Akanitambua mara moja, akanisalimu kwa furaha akanieleza hadithi yake. Baada ya kutumikia wakati wake na kufunguliwa, alikuwa ameandikwa kazi ya jeshi akatumikia katika kikosi cha mbele katika Urusi. Huko alikuwa na nafasi ya kufikiri tena juu ya mambo yote niliyokuwa nimemwambia. . . . Mwishowe akaniambia: ‘Leo nikawa ndugu yako.’ Unaweza kuwazia nilivyopendezwa na namna nilivyofurahi?”
Hermann Schlomer aliona jambo kama hilo. Hii pia ilikuwa katika kusanyiko la mzunguko ambako ndugu alimfikia akauliza: “Unanitambua?” Ndugu Schlomer akajibu: “Nakumbuka sura yako, lakini sikujui.” Kisha ndugu huyo akajijulisha kuwa alikuwa ndiye mlinzi aliyekuwa akisimamia Ndugu Schlomer katika gereza ya Frankfurt-Preungesheim wakati wa kifungo chake cha miaka mitano huko. Ndugu schlomer alikuwa amemweleza mlinzi huyu mambo mengi sana juu ya kweli. Alikuwa pia amemwomba Biblia, ambayo kiongozi wa dini wa gereza alikataa kumtafutia. Mlinzi wa gereza alikuwa mwenye huruma akampatia Ndugu Schlomer Biblia. Ili awe na kazi ya kufanya katika kizuizi akiwa amefungwa peke yake na kutengwa na watu wote alimletea pia stokingi (soksi ndefu) za jamaa azishone. Ndiyo, kwa kweli Ndugu Schlomer alikuwa na sababu ya kufurahi, akijua kwamba katika habari hii neno la Yehova lilikuwa limeanguka juu ya udongo wenye rutuba.
CHAKULA CHA KIROHO KINAKUWA KICHACHE
Chakula cha kiroho katika Ujeremani kiliendelea kupungua. Namna ilivyokuwa hatari kwa watu mmoja mmoja, na pia vikundi, kupashana habari kwao na tengenezo kulipokatika wakawa hawana nafasi tena ya kupata chakula cha kiroho, inaendelea kuelezwa na Heinrich Vieker:
“Wanazi walipopata uwezo, tulikuwa kati ya wahubiri 30 na 40 katika kundi letu. Hali yenye kutatiza iliyofuatwa na jamii hii karibuni ilifanya ndugu wengi walegee, hivyo wakawa wasiotenda, karibu nusu ya wahubiri hawakuonekana tena. Hii ilikuwa na maana ya kwamba ilitupasa tuwe waangalifu sana tunaposhughulika na wale waliokuwa wameacha, tukiwasalimu tunapokutana, lakini tusiwape magazeti yanapopatikana. Wakati wa mazungumzo fulani, tuligundua kwamba ndugu wote, isipokuwa karibu kumi na wanne, walikuwa wamepiga kura katika uchaguzi uliofanywa.”
Bila shaka ilikuwako hatari ya kwamba ndugu wengine wangenyimwa chakula cha kiroho kwa sababu tu ya hali yenye huzuni iliyoleta mashaka kwamba walikuwa wamejitenga na tengenezo la Yehova. Hili ndilo lililompata Grete Klein na mama yake katika Stettin. Na tumsikie anavyosema:
“Sisi tulikuwa tunakutana vikundi vikundi katika nyumba za ndugu mbalimbali. Mwangalizi wetu wa kundi alinipa The Watchtower nichape stencil za kutokezea nakala nyingi. Lakini hii ilikuwa kwa muda mfupi tu, kisha pendeleo hili nililolithamini sana likamalizika. Akina ndugu waliogopa sana kwamba wanaweza kugunduliwa baada ya wao kujua kwamba baba yangu alikuwa akipinga kweli. Sisi, mama yangu na mimi, hata hatukupata nakala moja ya The Watchtower. Kwa kweli, woga wa akina ndugu ulikuwa mwingi sana hata hawakutusalimu walipokuwa wanakutana nasi barabarani. Wote wawili tulitengwa kabisa na tengenezo. Katika Stettin kundi la Wanafunzi wa Biblia lilikoma kwa sababu hatukuwa na uongozi na chakula cha kiroho, ingawa tulikuwa tungali huru. . . .
“Kusimama mahali pamoja tu kwa kweli kuna maana ya kurudi nyuma; tuliona hili karibuni kutokana na nia yetu ya kiroho. Baada ya vita kuanza, niliendelea kuombea ndugu zetu wa kiroho waliokuwa katika kambi za mateso; walakini, karibuni nilikuwa ninaombea ndugu zangu wa kimwili pia waliokuwa wanaendesha vita kwa silaha halisi katika Urusi na Ugiriki. Wakati huo hata sikushtuka kwamba nilikuwa ninafanya kosa. Mara nyingi wazo liliingia akilini mwangu kama iliwezekana, kweli kusimamisha taratibu mpya chini ya ufalme wa Mungu.
“Zaidi yangu, walikuwako vijana wengine wengi katika kundi la Stettin wasiojua walisimama wapi. Vijana wengi, kama vile Gunter Braun, Kurt na Artur Wiessmann, walikuwa katika utumishi wa jeshi wakipiga vita kwa silaha za kimwili. Hata Kurt Wiessmann aliuawa alipokuwa akiendelea kupiga vita. Sababu kubwa ya hali yetu isiyofaa bila shaka ilikuwa uhakika wa kwamba wenye kutuongoza walikuwa wakiogopa wanadamu. . . .
“Kwa upande mwingine, ndugu hawa waliolegea wakati huo ni mfano wa saburi, upendo na msamaha wa Yehova, kwa kuwa, kama nilivyopata kujua baadaye, wengine wao walitubu kwa unyofu wa moyo juu ya matendo yao baada ya kazi kuanza tena nao wakarudishwa kwenye upendeleo wa Yehova. Wengine wao wangali katika utumishi wa wakati wote leo, kama, kwa mfano, aliyekuwa mwangalizi wa kundi katika Stettin, ambaye kwa sababu ya kuogopa wanadamu aliacha kupashana habari na mimi na mama yangu akahamia mahali wasipojulikana kabisa akiwa na mkewe. Lakini mimi nilifurahi kama nini nilipokutana nao tena katika Wiesbaden nilipoanza kutumikia katika Betheli nami nimeweza kuwaona wote wawili wakiendelea katika utumishi wa wakati wote mpaka wakawa wazee. Kwa sababu ya mwendo wa tendo wa mwangalizi huyu wengine wa akina ndugu walitaabika sana katika kambi za mateso na gerezani, na wengi waliona ugumu wa kumsamehe. Lakini rehema ya Yehova iliwasaidia kufanya hivyo ikawa mfano mzuri sana kwao.”
WASIWASI KATIKA MAGDEBURG NA KWINGINEKO
Tukirudi nyuma katika masimulizi kwenye mwaka wa 1933 wakati Hitler alipopata kuwa mkuu wa korti, twaona kwamba Ndugu Rutherford karibuni alifahamu kwamba serikali ya Ujeremani ilikuwa ikichunguza jengo letu katika Magdeburg na viwanda vya kuchapia vyenye thamani kubwa huko. Jitihada kubwa zilifanywa kuhakikishia maafisa wenye madaraka kwamba Wachtturm Bibel-und Traktat-Gesellschaft ilikuwa msaidizi wa Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania na kwamba ilikuwa mali ya Amerika kwa kuwa jengo la Magdeburg kwa kadiri kubwa lilifanyizwa na zawadi zilizotoka Amerika. Chini ya hali hizi Ndugu Baizereit akiwa raia wa Ujeremani alikuwa akishiriki kidogo tu kupigania kukombolewa kwa mali ya Amerika. Kwa hiyo, Ndugu Rutherford akamwomba Ndugu Harbeck, mwangalizi wa tawi katika Switzerland, ajiingize katika ubishi huu, akitumia uraia wake wa Amerika.
Sasa Ndugu Balzereit, aliyekuwa amechagua kuhamia Czechoslovakia akapate usalama, akaona kwamba mamlaka yake ilikuwa ikizuiwa, naye akaona uchungu kupoteza fahari yake. Hata hivyo yeye mwenyewe hakuonyesha kutaka sana kurudi Ujeremani akaongoze mwenyewe mashauri yaliyokuwa yanaendelea ya kudumisha mali ya Sosaiti na kusaidIa ndugu zake katika pigano lao la imani. Wakati ule ule, Ndugu Balzereit na ndugu wengine kadha waliokuwa wamemwunga mkono katika ubishi huo walimshtaki Ndugu Harbeck juu ya kuwa asiyejali katika kuangalia faida za Ujeremani, hata wengine wakampelekea Ndugu Rutherford simu ya kuruka kwa niaba ya Balzereit.
Ndugu Rutherford alimjibu Balzereit ifuatavyo: “Rudi Magdeburg ukakae huko na usimamie mambo ufanye uwezayo, lakini umpashe Ndugu Harbeck mambo yote. . . . Kwa kweli si lazima uombe ruhusa ya kurudi Ujeremani, kwa kuwa, kwa kadiri mimi ninavyohusika, nawe wajua hili, ungaliweza kukaa huko pale pale mwanzoni. Wewe hata hivyo ulijaribu kunifanya niamini kwamba usalama wako mwenyewe ulitegemea kupata kwako usalama nje ya nchi.”
Mwaka wa 1933 ulikaribia mwisho bila umoja wo wote kupatikana kwa habari ya kufanya mikutano ya kawaida na kuendesha kazi ya kuhubiri. Ndugu Poddig aeleza hali ilivyokuwa: “Vikundi viwili vilitokea. Wenye kuogopa walishikilia shauri la kwamba sisi tulikuwa waasi na tulikuwa tukiwaletea wao hatari na kazi ya Yehova pia.” Barua iliyoandikwa na Ndugu Harbeck katika Agosti 1933 ilienezwa sana kati ya ndugu wa Ujeremani nayo ikatumiwa na wenye kuogopa katika mazungumzo yao kama uhakikisho wa kufaa kwa msimamo wao. Kwa sasa Sosaiti ilichapa makala ya Watchtower yenye kichwa “Msiwaogope,” iliyounga mkono hatua ya wale ambao walikuwa wamefuata sauti ya dhamiri yao wakaendelea kukutana pamoja vikundi vikundi na kuendesha kazi ya kuhubiri kwa siri, yajapokuwa mateso yenye kuongezeka na kutendwa vibaya. Iliwaonyesha kwamba hatua yao ilikuwa imepatana na mapenzi ya kimungu.
Mashauri ya kukombolewa kwa jengo la Magdeburg yalikuwa yamekoma, hata Ndugu Rutherford akamwandikia Ndugu Harbeck Januari 5, 1934: “Mimi sina tumaini sana kama tutapata cho chote kwa serikali ya Ujeremani. Nadhani bawa hili la tengenezo la Shetani litaendelea kuonea watu wetu mpaka Bwana atakapojitia ndani.”
Kwa sasa, barua zaidi kutoka kwa akina ndugu katika Ujeremani zilikuwa zimemfikia Ndugu Rutherford, zikimpa wazo sahihi zaidi juu ya hali ya kazi katika Ujeremani na pia juu ya nia ya kiroho ya akina ndugu. Moja ya hizi, iliyotoka kwa Ndugu Poddig, ilizungumza juu ya makala ya Watchtower “Msiwaogope.” Ilieleza kwamba ndugu wengine walikuwa wanakataa Watchtower hili halikuwa “chakula katika majira yake.” Wengine hata walikuwa wanajaribu kuwazuia ndugu wasiendeshe kuhubiri kwa siri. Jibu la Ndugu Rutherford lilipitishwa kwa akina ndugu kila mahali. Sehemu yake ilisema hivi: “Makala ‘Msiwaogope’ iliyotokea katika Watchtower la Desemba 1 iliandikwa hasa kwa faida ya ndugu zetu katika Ujeremani. Inashangaza kwamba wengine wa akina ndugu wanapinga wale wanaopendezwa na kutafuta nafasi za kumtolea ushuhuda Bwana. . . . Makala iliyotajwa juu inahusu Ujeremani sawa na inavyohusu sehemu nyingine yo yote ya dunia. Hasa inahusu mabaki ko kote washiriki mmoja mmoja waliko. . . . Hii ina maana ya kwamba wala mtumishi wa vitabu, msimamizi wa utumishi, kiongozi wa kazi ya mavuno wala mtu mwingine ye yote hana haki ya kuwaambieni la kufanya wala kukataa kuwapeni vitabu hivyo vinavyopatikana. Utendaji wenu katika utumishi wa Bwana si haramu, kwa maana mnaufanya kwa kutii amri ya Bwana . . . ”
MIPANGO YA TENDO LENYE UMOJA YAFANYWA KATIKA BASEL
Kusanyiko lilipangwa lifanyiwe Basel, Switzerland katika wanja za maonyesho, kuanzia Septemba 7 mpaka 9, 1934. Ndugu Rutherford alitumaini kukutana na ndugu kadha wa Ujeremani huko, apate habari zao wenyewe juu ya hali halisi nchini. Chini ya hali mbaya sana karibu ndugu elfu moja wa Ujeremani waliweza kuhudhuria. Baadaye walieleza namna Ndugu Rutherford alivyohuzunika yeye mwenyewe aliposikia habari za mambo akina ndugu waliyokuwa wamelazimika kupatwa nayo.
Kwa upande mwingine, yeye alilazimika kujua kwamba hata waangalizi wenye kusafiri waliohudhuria hawakuwa na mapatano kwa habari ya kazi ya kuhubiri. Alizungumza nao juu ya hatua zilizopaswa kuchukuliwa baada ya kusanyiko. Mipango ikafanywa ya tendo lenye umoja. (Inaendelea)—Kutoka 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses.