Mlango Ulio Wazi wa Kwenda Kwenye Visiwa vya San Blas
ILE ndege yenye enjini mbili ilipiga duara juu ya ule ukanda mdogo sana wa kutulia kandokando ya ufuo wa bahari. Rubani akatangaza kwamba njia ya ndege kukimbilia chini ilikuwa imefurika na haingekuwa salama kutua. Lakini alipopakaribia tena mahali hapo, akaamua kuishusha ndege. Ndege ilipokuwa ikigusa chini, iliruka-ruka katika ukanda ule wa changarawe, ikirusha maji hewani. Iliposimama hatimaye, sisi tulitusha moyo kwa kutokwa na woga. Wasiwasi wetu ukawa shangwe tulipotupa macho tukaona rafiki zetu wakitungojea.
Walikuwa wamekuja kutoka kile kisiwa cha Ustupu, yapata kilometa moja na kitu mbali na pwani. Hicho ni kimoja cha Visiwa vya San Blas, ambao ni msururu wa vijisiwa vipatavyo 350 vinavyofuatana-fuatana kama matone katika mwambao wa kaskazini-mashariki mwa Panama mpaka kule mbali kwenye eneo la mpaka wa Kolombia. Visiwa hivi vinakaliwa na Wahindi wenyeji wapatao 50,000 wa kabila la Kuna. Sisi tulikuwa tumekuja tukiwa na utume fulani.
Kikao cha Kuzungumza na Sahilas
San Blas ni comarca, au tarafa ya usimamizi wa serikali, ya Jamhuri ya Panama. Kila kisiwa kinasimamiwa na Sahilas yacho chenyewe, ambayo ni halmashauri ya kienyeji yenye wazee-wazee wa kiume. Wawakilishi wa kutoka katika ile Sahilas ndio wanaojumlika kuwa baraza linaloitwa Caciques, ambalo linatawala juu ya comarca nzima.
Tangu 1969, Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakizihubiri habari njema za Ufalme katika San Blas, na watu wapatao 50 sasa wanahudhuria mikutano yetu. (Mathayo 24:14) Hata hivyo, wenye mamlaka wa hapo wametunyima ruhusa ya kuhubiri katika baadhi ya visiwa. Hivi majuzi, Sahilas ya Ustupu, ambacho ndicho kisiwa cha pili kwa wingi wa watu katika kile kikundi cha visiwa, ilipeleka ombi la kuwa na mahoji pamoja na Mashahidi wa Yehova ili ifanye uamuzi wa kutoa au kutotoa utambuzi rasmi. Inaonekana kwamba Yehova ‘anafungua mlango’ kwa ajili yetu.—1 Wakorintho 16:9.
Kwenye mkutano mmoja wa mwanzo-mwanzo, hangaikio kubwa la wenye mamlaka wa hapa lilikuja kuwa wazi. Wao walionyesha kwamba kulikuwa tayari na dini nne mtaani—ya Kikatoliki, Kibaptisti, “Church of God,” na Mormoni. Kila moja yazo ina jengo kubwa la kikanisa, na baadhi ya majengo hayo yamo katika hali ya kuachiwa ukiwa. Kwa kuwa nchi-bara ni haba sana katika kisiwa, ingekuwa lazima maafisa wawe na nadhari juu ya kuruhusu humo kikundi kingine cha kidini.
Kwa kutumia mkalimani, sisi tulieleza kwamba katika mabara zaidi ya 200 kuzunguka ulimwengu, Mashahidi wa Yehova wamechangia hali njema ya mitaa kupitia viwango bora vya kiadili ambavyo wao wanadumisha. Sisi tulihakikishia maafisa kwamba sasa mikutano hiyo ingefanywa katika maskani za Mashahidi wa hapa, na ikihitajiwa kabisa kujenga mahali pa pekee pa mikutano, mahali hapo pasingeacha kutumiwa kwa kuwa mikutano yetu inahudhuriwa sana.
Baada ya mazungumzo ya muda upatao saa moja, maafisa waliamua kutokeza jambo hilo kwenye mkutano ufuatao wa Sahilas, uliofanywa baadaye katika juma hilo. Sisi tungelazimika kungojea jibu.
Ziara ya Kwenda Kisiwa cha Mbwa
Badala ya kungojea tu, sisi tuliamua kuzuru Achutupu, au Kisiwa cha Mbwa, tukiwa na ujumbe wa Ufalme. Mashua yetu, iliyopewa jina La Torre del Vigia (Mnara wa Mlinzi), imepakwa rangi nyangavu za wekundu na ubuluu, nayo ina mota ya nje-nje karibu na tezi. Mashua hii inaonekana wazi sana kwa kutofautiana na cayucos, au mitumbwi mingine mingi ambayo imefungiliwa gatini. Tulifika Achutupu kwa kuiendesha mwendo wa dakika 45 kupitia maji yenye kuyumba-yumba.
Achutupu ni kisiwa kidogo chenye hali halisi za kitropiki, nacho kina mitende yenye kuwaya-waya na fuo za mchanga-mchanga. Lakini kilionekana kama kilichosongamana watu kidogo, kwa kuwa na wakaaji wapatao 2,000. Misafa ya vijumba vya kuezekwa ilikuwa kila mahali, ikiwa imetenganishwa na vichochoro vyembamba tu, visivyotandazwa vizuri. Vijumba vyote vilifanana. Kuta, ambazo zimejengwa kwa mikongojo ya mitende myembamba iliyofungiliwa kwenye matawi membamba ya miti, zilikuwa na kimo kipatacho meta 1.5 tu na juu yazo palikuwa na paa zito iliyoinuka sana, ya vitawi vya mitende. Ndani, mlikuwamo nafasi-wazi moja tu kwa ajili ya jamaa nzima. Hamkuwa na madirisha, lakini nafasi zilizo kati ya ile mikongojo ziliruhusu nuru na hewa ya kutosha ipenyeze humo.
Kabla ya kuzuru maskani zile tukiwa na ujumbe wetu wa Biblia, tuliamua kufuata ile desturi ya huko ya kutembelea machifu wa kijiji ili tupate ruhusa yao. Kwa hiyo tukaelekea kwenye jumba la mtaa, ambalo ni jengo kubwa katikati ya mji.
Mlikuwa na giza ndani ya jumba, lakini macho yetu yalipojirekebisha, tuliweza kuona misafa ya mbao za kukalia zilizopangwa kuzunguka nafasi-wazi pale katikati. Picha za Sahilas mashuhuri wa nyakati zilizopita zilikuwa kila mahali. Kwa sababu ya giza, picha zile, na kimya kile, mahali hapo palikuwa kama ndani ya kanisa. Katikati ya vyote hivyo walikuwako wanaume watano, baadhi yao wakiwa wamejilaza kwa kuegemea vitanda vilivyoshonwa kwa kitambaa, wengine wakiwa wamekalia mbao za kukalia. Ilionekana walikuwa ndio machifu wa kijiji.
Akinena kwa lugha ya hapo, Bolivar, mmoja wa Mashahidi waliokuwa wamekuja nasi kutoka Ustupu, alieleza kusudi la ziara yetu. Papo hapo, tukapewa mapokezi ya kirafiki na ruhusa ikatolewa ili tutembelee wanakijiji.
Kwenda Kijumba kwa Kijumba Katika Achutupu
Wahindi Wakuna ni watu wenye furaha na urafiki. Tulipokuwa tukitembea katika barabara za huko, watoto walitukimbilia, wakiita kwa sauti “Mergui! Mergui!” maana yake “watu wageni.” Walitaka kutusuka-suka mikono kwa salamu. Ni wanaume wachache waliokuwako, nasi tuliambiwa kwamba walio wengi walikuwa wameenda zao kupalilia vishamba vyao katika nchi-bara.
Kwenye kila maskani tulialikwa tuingie ndani. Mke mwenye nyumba akawa akituketisha katika viti vizito vya miti iliyokunjwa kwa mikono, na washiriki wale wengine wa jamaa wakawa wakikusanyika kutuzunguka ili wasikilize kwa makini. Kabla ya kuondoka, tukawa tukitolewa kinywaji cha koko, kahawa, au matunda ya huko. Halafu ikafuata bilauri ya maji ya kusukutua kinywa. Kulingana na desturi ya huko, ilifaa sana kutema maji hayo sakafuni. Baada ya muda mfupi tukajifunza kukonga maji kidogo tu kila wakati, kwa kukumbuka kwamba zilikuwako maskani nyingi za kutembelea.
Kwenye kijumba kimoja, tuliona mifano-michonge ya mbao, ipatayo 50, yenye ukubwa tofauti-tofauti ikiwa imepangwa kandokando ya mwingilio. Bolivar alitueleza kwamba ilikuwa ya kuzuia roho waovu wasije hapo. Wakati mwanamke wa pale alipokuja mlangoni na kutuambia kwamba mume wake hakuwa mzima, sisi tulielewa sababu ya mifano ile kuwa pale, kwa maana mara nyingi ugonjwa unahesabiwa kuwa unaletwa na roho wabaya.
Baada ya sisi kualikwa ndani, tuliona mume huyo akiwa amelala katika kitanda kilichoshonwa kwa kitambaa. Juu yake zilikuwako nyuta (pinde) nyingi ndogo-ndogo zilizoning’inizwa kwenye kamba fulani, huku mishale yenye ncha nyekundu ikiwa imelengwa kuelekea mwanamume huyo mgonjwa. Zilisemekana kuwa zinaogopesha roho waovu wasije pale. Kwenye sakafu vilikuwako vibuyu kadha vya mviringo vyenye mifano midogo-midogo, viko vya kuvutia tumbako, na maharagwe ya koko yakitoa-toa moshi. Vitu hivyo vilisemekana kuwa vinawatuliza roho. Bolivar alijaribu kufariji jamaa ile kwa kuwaambia juu ya ahadi ya Mungu ya kufutilia mbali ugonjwa wote, nao wakakubali vitabu fulani vya Biblia. Kwa mara nyingine tena, ndiyo hayo tukaletewa kile kinywaji cha kidesturi na bilauri ya maji.
Mavazi ya Kikuna Yenye Rangi za Kupendeza
Yanayoonwa kwa kawaida katika visiwa hivi ni yale mavazi yenye rangi za kupendeza ya Wahindi Wakuna. Ingawa kwa kawaida wanaume leo huvaa nguo za mitindo ya Uzunguni, bado wanawake wanapendelea vazi lao la kimapokeo la shali nyekundu, blauzi ya mikono mifupi, na rinda lenye kufika magotini. Kwa kawaida sehemu ya juu ya blauzi ile inakuwa yenye rangi nyangavu. Sehemu ya katikati inajulikana kuwa mola, na mara nyingi watalii wanainunua na kuitumia kama pambo la ukutani. Huo ni muunganisho-unganisho wa vitambaa vya rangi za kupendeza vyenye maumbo ya kimapokeo ya ndege, samaki, na wanyama. Lile rinda ni kijitambaa cheusi tu cha umbo-mstatili chenye michoro-choro miangavu, ambacho kinazungushwa-zungushwa mwilini kisha mkia wacho unafutikwa kiunoni. Walio wengi wa wanawake Wakuna huacha nywele zao zibaki zikiwa fupi, ingawa baadhi ya wasichana wachanga zaidi wasioolewa wanaacha nywele zao ziwe ndefu zaidi.
Wanawake wanaonekana wanashangilia kuvaa madoido mengi. Pete za masikioni, mikufu vikuku, na pete za puani za dhahabu zinapendwa sana. Mara nyingi machumo yote ya jamaa, ambayo huenda yakawa ni maelfu ya dola yanavaliwa na wanawake kwa njia hiyo. Pia zenye kuonekana wazi sana ni zile kanda za kufungia miguu na mikono yao. Hizo zinafanyizwa kwa shanga ndogo sana za nyekundu-manjano, za manjano, na rangi nyinginezo na upana wazo unaanzia sentimeta 5 mpaka 15 hivi. Wanawake wanaingiza shanga hizi katika uzi mwembamba halafu wanakazilia uzi huo katika miguu na mikono yao. Violezo vya ustadi wa kupamba vinafanywa kwa kubadili-badili rangi ya shanga zilizo katika uzi. Zile kanda za kufungiliwa miguuni na mikononi zinakaziliwa ili ziweze kuvaliwa kwa mfululizo wa miezi mingi, bila kuondolewa hata wakati wa kuoga. Ili kukamilisha vazi lao maridadi, mstari mweusi uliosimama wima-wima unapakwa au kuchanjwa-chanjwa ukiteremka katikati ya kipaji cha uso na pua, na kumalizikia kwenye mdomo wa juu.
Tulilazimika kukatiza ziara yetu yenye kupendeza ya Achutupu, kwa kuwa ilikuwa lazima turudi Ustupu tusichelewe ule mkutano pamoja na Sahilas. Kule gatini, watu wengi walikuwa wakingojea kupata vitabu fulani vya Biblia kutoka kwetu. Sisi tulifurahi kuwaachia tulivyokuwa navyo.
Utume Katimizwa!
Tuliporudi Ustupu, tulipata lile jumba la mtaani likiwa limesongamana mamia ya watu wenye hamu nyingi ya kujua kama Mashahidi wa Yehova wangetambuliwa au hawangetambuliwa rasmi. Sisi pia tulikuwa na hamu nyingi. Mazungumzo ya kukadiria-kadiria mambo yalipokuwa yakiendelea, mwenyekiti alitokeza ule mnuio wa kuwapa Mashahidi wa Yehova mamlaka ya kuendesha dini katika kisiwa hicho. Alipoalika wasikilizaji watoe maoni yao, mdundo wa moyo wetu uliongezeka. Ni watu wawili tu waliopinga; walio wengi walipendelea jambo hilo.
Hatimaye, lile baraza kuu likapiga kura kutoa ruhusa rasmi ili sisi tufanye mikutano na kuhubiri mlango kwa mlango na kuandikisha uamuzi huo katika kumbukumbu zao. Hivyo, mashahidi wa Yehova wakawa ndiyo dini ya kwanza katika kisiwa kile kupewa na mamlaka maandishi yenye kuwaruhusu kuendesha shughuli. Dini zile nyingine zote zimepewa miafaka ya mdomo tu. Sisi tulifurahi na kushukuru kama nini kwa ushindi huu!
Inatumainiwa kwamba uamuzi huu utafungua mlango wazi ili habari njema za Ufalme zihubiriwe katika visiwa vyote vya San Blas. Kuna kila sababu ya kuhisi kama mtunga zaburi wakati aliposema: “Yehova mwenyewe amekuwa mfalme! Acheni dunia ijae shangwe. Acheni vile visiwa vingi vishangilie.”—Zaburi 97:1, NW.
[Ramani katika ukurasa wa 28]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
PANAMA
Jiji la Panama
Visiwa vya San Blas
Ghuba ya Panama
Bahari ya Karibbea
KOLOMBIA