Kupainia Kandokando ya Mto Amazon
MWITU wa Amazon! Karibu kila mmoja amesikia habari zao. Lakini ni wachache wamekuwa na fursa ya kwenda kuuona. Hata hivyo, wakati wa mwongo uliopita, hesabu fulani ya mapainia, au wahudumu wa wakati wote, wamefanya jambo hilo hasa. La maana hata zaidi, wao wamepeleka habari njema za Ufalme wa Mungu huko. Kwa kutumia mashua El Refugio (Kimbilio) ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, wao wamevuka mwitu wa Amazon kwa kutumia mfumano wa mito inayokingamana kaskazini-mashariki mwa Peru.
Huo umekuwa mgawo wa kupendeza kama nini! Makabila mengi ya Wahindi yametapakaa katika sehemu zote za eneo kubwa hilo. Chacra ndogo-ndogo, au mashamba, zinapatikana upande wa juu na chini wa mito ile, kandokando ya kingo zayo, na kule mbali upande wa nyuma wa mwitu. Ingawa wako peke yao, ni lazima watu hao pia wapewe nafasi ya kupata ujumbe wa Biblia wa uhai.—Mathayo 24:14; 28:19, 20.
Karibu na jiji la mwituni la Iquitos, mito miwili iliyo mikubwa—mto Ucayali wenye kupita kasi kwa mwendo wenye kudanganya macho, na mto Marañón—hukutana pamoja na kufanyiza mto Amazon ulio mkubwa. Kwa kuwa inaendelea kupita kwa kishindo kingi, ikijipinda-pinda, na kutukutisha maji, mito hiyo inabomoa-bomoa kingo zayo na kuangusha majiti makubwa ndani ya mikondo yayo yenye nguvu nyingi sana. Kingo zenye mchanga-mchanga zinafanyizwa kwa usiku mmoja, hivyo zikibadili mwendo wa mkondo wa maji.
Wakati El Refugio ilipokuwa ikijongea kuteremka chini katika mto Ucayali, iligonga kwa ghafula ukingo wa mchanga uliojazana chini ya maji. Kikumbo hicho kisichotarajiwa kiliwarusha wanamashua wakakosa usawaziko, lakini kushika haraka viguzo na fito za mashua ile kuliwazuia kutumbukia majini. Nahodha alirudisha mashua nyuma, lakini wapi. Ilikuwa imekwama. Kwa hiyo ndugu sita waliokuwa mashuani wakavua nguo zikafikia urefu wa kaputura, wakaruka juu ya ukingo ule wenye mchanga, na kuanza kuondoa masanduku 40 ya fasihi ili kupunguza uzito. Kwa ghafula, mwanamashua mmoja akapaaza sauti hivi: “Chungeni! Chatu wa mtoni anapanda juu mashuani.” Kweli kabisa, nyoka mwangavu wa kijani mwenye urefu wa meta 2 alikuwa akinyinyirika kwenye ubavu wa mashua. Lakini kwa kutumia kasia kumgonga-gonga kidogo, alirudi mtoni. Baada ya muda mfupi, mashua iliondoka mahali ilipokwama ikiwa imepungua uzito na kuanza tena safari.
Njia za Kuhubiri Zenye Kupangwa Kitengenezo
El Refugio si mashua kubwa, na kwa uhakika haina mwendo wa haraka. Kwa kweli, hiyo hujikokota polepole sana inapojisukumiza dhidi ya mkondo wa maji yanayopita kasi sana. Kwa hiyo, mapainia wameanzisha mpango fulani kuongezea mwendo wa kumaliza eneo la ndanindani. Kabla ya kuondoka kwenye kituo cha maskani yao katika jiji la Iquitos, wao hujaribu kujua ni nini kilichoko mbele yao katika eneo lile hasa wanalotaka kumaliza. Kwa kuuliza-uliza wenyeji wa sehemu hiyo, wanaweza kufanyiza ramani ya kihivi-hivi tu ya vijiji na chacras zilizo katika eneo hilo. Mito midogo au vipitio vya maji vinachorwa ili vitumiwe kwa visafari vya kandokando. Hivyo, ikiwa eneo lililochaguliwa lina vijiji vingi, mashua inaweza kubaki mahali pamoja kwa juma moja au mawili. Kwa kawaida, wanne kati ya wale mapainia sita humaliza kufanya kazi katika mashamba yale yaliyotapakaa, huku nahodha na painia aliyebaki wakisafiri kuingia mwituni, ambamo mashua haiwezi kwenda. Hilo linafanywa kwa kupanga wapewe nafasi ya kusafiri katika ndege ya kampuni ya kuchimbua mafuta inayokuwa ikienda nje kwenye kambi fulani.
Kambi hizo ni sehemu zilizofyekwa miti humo ndanindani ambamo ardhi huwa ikitobolewa kwa drili ili kutafuta mafuta. Wanaume mia moja au zaidi huenda wakapatikana kwenye kambi ya namna hiyo. Mashahidi hao hufanya mipango ili waongee na wanaume hao wakati wa chakula cha jioni, baada ya saa za kazi. Katika kambi moja, kijumba kilichoezekwa majani kilithibitika kuwa jumba bora la kuhutubia. Wanaume hao walisikiliza, na idadi fulani wakauliza maswali baadaye kuhusu matatizo ya kiadili waliyokabili walipokuwa wakiishi mbali sana kutoka kwenye jamaa zao. Ilikuwa fursa bora kama nini ya kutoa rai ya Biblia juu ya usafi wa kiadili! Baada ya kipindi hicho cha maswali na majibu, wanaume wengi waliomba Biblia na misaada ya kujifunzia Biblia. Majina yalichukuliwa, na baadaye mafunzo yakaanzwa pamoja na baadhi ya wanaume hao na jamaa zao katika Iquitos. Kambi nne za kuchimbua mafuta zilifanyiwa kazi kwa njia hiyo—tatu kwa kusafiri angani na moja kwa ziara ya El Refugio.
Wakati wowote caserío, au kijiji kidogo, ilipoonwa kando ya ukingo wa mto, mapainia wangefungilia mashua kwenye kidude chochote thabiti kilichoweza kuishika imara. Ingawa hivyo, mwanamashua yeyote mwenye hekima angeutahini ukingo kabla ya kuruka chini. Kigongo cha ardhi ya ufuoni ambayo mto hurundika pamoja huonekana kuwa salama lakini kumbe kinaweza kuwa kimejaa mishangazo. Mrukaji asiyeshuku neno huenda akajikuta amezama matopeni mpaka kiunoni!
Wakiisha kufika salama ufuoni, akina ndugu hujisukuma mbele kwa kupita kikundi cha watoto walio na kawaida ya kuuliza-uliza maswali na kusema-sema vijineno na hutafuta mkuu wa kijiji. Wao humweleza kwa ufupi kusudi la ziara yao na kuomba watumie kwa hotuba ya Biblia kijumba cha shule ya hapo au kituo cha mikutano ya kijiji. Kwa kawaida, ruhusa hutolewa. Matangazo hufanywa kwa kinywa kwa kuwa watoto hutawanyika pande zote wakiueneza mwaliko. Kabla ya hotuba, siku inatumiwa kuhubiri kijumba kwa kijumba. Watu ni wenye urafiki na wakaribishaji na hukubali fasihi yetu ya Biblia kwa hamu nyingi. Mahali ambapo pesa ni kidogo, vitabu hubadilishwa kwa kasa, nyani, kuku, kasuku, matunda, au hata mmea-orkidi wa kupendeza.
Wakati unaporuhusu, ziara za kurudia hufanywa alasiri. Wenye kuonyesha upendezi usio wa kikawaida huombwa walete mecheros zao, au karoboi, zikiwa na mafuta-taa na utambi ili kuangazia. Kwa ujumla, kufikia saa moja, wote huwa wameketi, wakiwa wameshika taa kwa mkono mmoja na Biblia kwa mkono ule mwingine. Baada ya hotuba, maswali huanza. Je! Mashahidi wa Yehova huamini kuna moto wa mateso? Itikadi za Mashahidi zinatofautianaje na za dini ya Katoliki? Walio wengi hufurahia kupata majibu katika Biblia zao wenyewe.
Maono ya Kuchangamsha Moyo
Baada ya hotuba moja ya jinsi hiyo, mwanamume mmoja na mkeye walimjia painia wakiwa na machozi machoni. “Akina ndugu, sisi tumengojea muda mrefu kusikia maneno ambayo tumesikia usiku huu,” akasema mwanamume huyo. “Tunapenda bara letu na lile wazo la paradiso ya kidunia ambapo tunaweza kukaa karibu nalo. Sasa je, ni nani huyu mnayesema ataenda mbinguni?” Inachangamsha moyo kweli kweli kuwa nje kule mbali katika mwitu wa Amazon, kilometa nyingi sana kutoka kwenye “utamaduni ulioerevuka,” na kupata watu hao mfano wa kondoo.
Mapainia hujaribu kuangusha vitabu vikiwa miunganisho, kwa kuwa huenda kitambo fulani kikapita kabla hawajaweza kurudia vijiji hivyo. Siku moja, mwanamume aliye na mashua ya mtoni alisimamisha mmoja wa akina ndugu na kuomba muunganisho mwingine wa vitabu vinane. Ilikuwa imekuwaje kwa muunganisho wake wa kwanza? Watu wa ukoo wake walikuwa wameazima vitabu hivyo kimoja baada ya kingine walipomfanyia ziara. Vitu vya kusoma ni haba kule mbali mwituni. Kwa njia hiyo, fasihi imefikia mahali ambako mapainia wenyewe hawafiki kamwe. Kwa roho yake, Yehova huhakikisha hivyo kwamba vichapo vyetu vya Kikristo vinaingia katika mikono inayofaa.
Kwenye kijiji kidogo kimoja, wawili wa akina ndugu walibaki pamoja na mashua wakati wale wengine walipofuata kichochoro cha kupita mwituni. Miti mikubwa sana ilifungamana juu yao, ikizuia kadiri kubwa ya mwanga wa jua, huku ndege wa rangi nyingi wakiita-ita katikati ya majani yale mabichi. Baada ya kutembea kwa dakika 15, Mashahidi hao wakatokea mahali pakubwa kiasi palipofyekwa. Ilichukua karibu saa moja kutembelea vijumba vyote hapo. Akina ndugu walipokuwa tayari kuondoka, mwanamume mmoja akawajia na kuwasihi sana wakae mahali usiku kucha, kwa maana alikuwa na maswali mengi. Kwa hiyo mmoja wa mapainia wale akabaki hapo huku wale wengine wakirudi kwenye mashua.
Painia huyo alidokeza kwamba hotuba ya Biblia itolewe jioni. Basi watoto wakatumwa, wakifuata vichochoro ambavyo akina ndugu hawakuwa wameviona, ili wakalete jirani zao. Kwa sasa, funzo la Biblia liliendeshwa katika kijiji hicho, kwa kutumia sura za kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele zilizohusisha maswali ya mwanamume huyo mkaribishaji. Ubaridi wa jioni ulipokuwa ukitandaa juu ya joto lililokuwapo, mianzi ilianza ghafula kuvuma-vuma hobelahobela. Mamia ya kasuku wenye mikia mirefu wakaanza kupayuka-payuka kama kwamba kwa wakati mmoja, kama kwamba wanakaribisha ubaridi huo wa jioni.
Kufikia mwanzo wa jioni, watu wazima 20 na watoto wengi walikuwa wamekusanyika kumzunguka msemaji. Taa nyangavu ya gesi iliangazia vizuri usomaji, lakini pia ilivutia mamia ya wadudu wa mwituni. Alipofikia karibu nusu ya hotuba yake, msemaji alimeza mmoja! Baada ya kugongwa-gongwa mgongoni, kuchekwa-chekwa, na kuhurumiwa, yeye akaendelea, akimaliza hotuba kwa mafanikio. Kufikia hapo, hali ya kuona haya ilikuwa imekwisha na mazungumzo machangamfu yakafuata.
Baada ya jirani wa mwisho kuondoka, mwanamume yule mwenye kupendezwa aliweka neti (chandarua) ya kuzuia mbu katika pembe moja ya sehemu hiyo ya jukwaa la nje la maskani yake, iliyokuwa imejengwa juu ya viguzo, meta 1.5 kutoka ardhini. Akimwacha painia huyo alale chini ya neti hiyo, mwanamume huyo akakusanya wanyama wake na kuwafungasha kwenye viguzo chini ya jukwaa hilo ili wapate himaya dhidi ya maharamia-mwitu. Ndugu yule alipokuwa amelala pale akimtolea Yehova asante kwa ulinzi wake, mivumo ya mwitu ikamlaza usingizi baada ya muda mfupi.
Muda si muda ndugu yule akajikuta akiketi wima. Jogoo alikuwa amewika, na ilisikika kama kwamba ndege huyo alikuwa pale pale chini ya godoro lake. Na kweli alikuwapo. Kwanza jogoo huyo aliwika, kisha mbwa akabweka, halafu bata-mzinga akagugumiza, na mwisho mbuzi akaliliza sauti yake. Kufuatia hilo, ndege wa aina zote wakaanza mpayuko wao wa asubuhi. Siku mpya ilikuwa imeanza.
Baada ya kupata kiamsha-kinywa cha kumtosheleza, ndugu aliondoka mbio kuteremkia kijia kile akajiunge na waandamani wake. Pale mbele tu akaona kilichoonekana kama mti mkubwa ukiwa umekingama kijia. Mtazamo wa karibu zaidi ulionyesha kwamba alikuwa chatu-maji mkubwa ambaye hubana vitu, ambaye angeweza kwa urahisi kuwa na urefu wa meta 8. Painia yule akatumia hadhari kutembea nyuma yake na kufika salama mashuani.
Upinzani wa Makasisi Waepushwa
Kijiji kilichofuata hakikuonyesha upokezi wa kadiri ile. Mashua ilipokuwa ikisogelea kituo cha nchi kavu, akina ndugu walishangaa kuona kikundi kikubwa kimekusanyika ufuoni. Kwa kuongozwa na padri Mkatoliki, watu hao walipunga-punga mikono kuambia mashua hiyo iende zake, wakipaaza sauti kwamba wao hawakuhitaji fasihi yoyote ya Biblia. Kwa hiyo akina ndugu wakasonga mbele na kufungasha mashua mahali fulani mwendo mfupi tu chini ya kijiji kile.
Punde si punde chelezo kimoja chenye kuchukua ndizi kikaja kutoka kijijini. Kilipokuwa kikielea, akina ndugu waliwapaazia sauti wanaume watatu wenye kupiga makasia ya chelezo hicho ili waje kando ya El Refugio. Walipokuja, mapainia watatu walishuka juu ya chelezo na kuanza kutoa ushuhuda. Mwenye chelezo alitaka kujua kwa nini padri yule hakutaka Mashahidi watushe mashua kijijini, na mapainia wakajibu kwamba wao hawangeweza kuelewa kwa nini padri hangetaka watu waelewe Biblia. Mathalani, ni ubaya gani ungeweza kutokana na kusoma Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia? Wanaume hao walipoanza kuchunguza kitabu kile, hawakuweza kukiweka chini.
Siku iliyofuata, mitumbwi kadhaa ilisafiri kuielekea El Refugio. Kichapo Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia kilikuwa kimesisimua sana kijiji kile. Akina ndugu waliambiwa kwamba wakitembea mwendo mfupi humo ndani-ndani wangefika kwenye kichochoro cha kuwapeleka kijijini kwa upande wa nyuma. Walipokwisha kufika na wakawa wakienda mlango kwa mlango, mapainia waliona shangwe kupewa upokezi mzuri hata zaidi. Wengi wa wanakijiji walichukua miunganisho mizima-mizima ya vitabu, ikawa ng’oo kwa padri yule wa hapo.
Jumba la Ufalme la Mbali Lajengwa
Ndipo wale mapainia wasioogopa wakaja kufika mahali fulani katika mto Amazon ambapo mipaka ya nchi tatu hukutania. Vijiji vitatu, vyote vikiwa vimeachana kwa mwendo mfupi tu, hufanyiza kitovu chenye pirikapirika nyingi za kibiashara. Hivyo ni Caballococha katika Peru, Leticia katika Kolombia, na Tabatinga upande wa Brazili. Mwingio ndani ya miji hiyo hupatikana kwa urahisi, kwa kuwa humo ndani sana mwituni hamna sheria nyingi kuhusu paspoti.
Kule Tabatinga, habari zilipatikana kwamba dada wawili mapainia Wabrazili walikuwa wakieneza kazi katika mji huo. Walikuwa na kikundi kidogo chenye kupendezwa kukutana pamoja lakini hawakuwa na mahali pa kukutania. Dada wawili hao waliwasihi sana akina ndugu wabaki hapo na kutoa hotuba katika eneo hilo, nao wakaterema kufanya hivyo. Mazungumzo yaliyofuata yalionyesha kwamba kulikuwa na michango ya kutosha miongoni mwa kikundi hicho kununua miti ya kuunda kijengo katika ardhi iliyokuwa imechangwa. Akina dada walikuwa tayari wameona mahali pa kupasulia mbao upande wa juu wa mto, ambako mwanamume mwenye kupendezwa alikuwa ameahidi kuwauzia miti kwa bei nzuri. Ilichukua visafari viwili kuiteremsha pale miti hiyo kwa kutumia El Refugio. Kwa siku 15, mikono yenye nia ikajenga Jumba la Ufalme lenye nafasi ya kuketi kwa watu 80. Wanamashua hao walichanga atril yao wenyewe, au kinara cha msemaji, na mbao kadhaa za kukalia ili kikundi kile chenye msisimuko kipate nafasi ya kuketi. Walifurahi kama nini kuwa hatimaye na mahali pao wenyewe pa kukutania!
Kungali kuna eneo kubwa la kumalizwa kandokando ya mto Amazon na mito yenye kukamatana nao. Wale wanaotii mwito wa Makedonia ‘kutangaza habari njema’ katika maeneo haya ya mbali wanabarikiwa sana. (Matendo 16:9, 10, NW) Sasa El Refugio ina kikundi kipya cha mapainia. Wao pia wana uhakika kamili kwamba Yehova atawaongoza na kuwahami katika utumishi wao mtakatifu.
[Ramani katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
KOLOMBIA
Leticia
PERU
Iquitos
Mto Amazon
Marañón
Mto Ucayali
BRAZILI
Tabatinga
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mapainia wakiwa katika “El Refugio” wanaletea watu ukweli kandokando ya mto Amazon