Fimbo ya Enzi Yenye Umbo la Komamanga Kutoka kwa Nyumba ya Yehova?
WAAKIOLOJIA katika Israeli wamefukua fimbo nyingi za enzi, fito zenye kubebwa na watu wenye mamlaka. (Mwanzo 49:10; Esta 8:4; Ezekieli 19:14) Baadhi ya fimbo za enzi zilizopatikana katika Lakishi zilikuwa na kichwa chenye umbo la komamanga. Watu wa Mungu walijua tunda hilo vema.—Kumbukumbu la Torati 8:8; Wimbo Ulio Bora 4:13.
Komamanga la pembe katika hali ya kuchanuka, lililo kushoto, lilivumbuliwa muda mfupi uliopita. Lina kimo cha milimeta 43, na shimo lililomo upande walo wa chini ladokeza kwamba lilikuwa sehemu ya fimbo ya enzi. Angalia hizo herufi zilizoandikwa katika mtindo wa Kiebrania cha mapema zilizopewa tarehe ya karne ya nane K.W.K.
Sehemu ya pembe ilivunjwa katika nyakati za kale, kwa hiyo herufi chache zinakosekana au ziko kwa sehemu-sehemu tu. Hata hivyo, wastadi katika maandishi ya kale wanapendekeza maneno yaliyorudishwa ambayo yamechorwa chini. (Yakitegemea Biblical Archaelogist) Nafasi tofauti-tofauti kati ya herufi imeongoza kwenye njia mbili kuu za kuyasoma. Mwanachuo Mfaransa André Lemaire aliyasoma hivi “Mali ya Hek[alu la Bwa]na [Yahweh], takatifu kwa makuhani.” Nahman Avigad alipendekeza “Upaji mtakatifu kwa makuhani wa (katika) Nyumba ya Yahweh.”
Wao pamoja na wanachuo wengine walikata maneno kwamba hapo awali fimbo hiyo ya enzi ilikuwa na zile herufi nne za Kiebrania za jina la Mungu la kibinafsi—Yehova. Kwa hiyo ingalitaja “nyumba ya BWANA [Yehova, NW],” fungu la maneno lililo kawaida katika Biblia.—Kutoka 23:19; 1 Wafalme 8:10, 11.
Wengi bado huhisi kwamba kichwa hiki cha fimbo ya enzi huenda kikawa kilikuwa mali ya kuhani mmoja kwenye hekalu ambalo Sulemani alijenga au kwamba kilitolewa kikiwa upaji kwa hekalu hilo. Kwa kupendeza, umbo hilo la komamanga lilionekana mara nyingi kwenye hekalu la Mungu.—Kutoka 28:31-35; 1 Wafalme 7:15-20.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Israel Museum, Yerusalemu