Matendo
24 Siku tano baadaye kuhani wa cheo cha juu Anania akateremka pamoja na wanaume fulani wazee na msemaji wa hadharani, Tertulo fulani, nao wakampa gavana habari dhidi ya Paulo. 2 Alipoitwa, Tertulo akaanza kumshtaki, akisema:
“Kwa kuwa twaonea shangwe amani kubwa kupitia wewe na kwamba marekebisho yanatokea katika taifa hili kupitia ufikirio wako wa kimbele, 3 nyakati zote na pia mahali pote twaipokea, Ewe Mtukuzwa Feliksi, kwa shukrani zilizo kubwa zaidi sana. 4 Lakini ili nisikuzuie zaidi, nakuomba sana utusikie kwa ufupi katika hali yako ya fadhili. 5 Kwa maana tumemwona mwanamume huyu kuwa jamaa msumbufu na mwenye kufanya uchochezi wa uasi miongoni mwa Wayahudi wote katika dunia yote inayokaliwa na kuwa kiongozi mkuu wa farakano la Wanazareti, 6 ambaye pia alijaribu kulichafua hekalu na ambaye tulimkamata. 7 —— 8 Kutoka kwake wewe mwenyewe waweza kwa uchunguzi kugundua juu ya mambo haya yote ambayo sisi tunamshtaki.”
9 Ndipo Wayahudi pia wakajiunga katika hilo shambulio, wakisisitiza kwamba mambo haya yalikuwa hivyo. 10 Na Paulo, wakati gavana alipomtolea ishara ya kichwa aseme, akajibu:
“Kwa kujua vema kwamba taifa hili limekuwa na wewe ukiwa hakimu kwa miaka mingi, mimi nasema kwa utayari katika kujitetea juu ya mambo yanihusuyo mimi mwenyewe, 11 kwa kuwa wewe uko katika hali ya kugundua kwamba kwangu mimi haijawa zaidi ya siku kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda kuabudu katika Yerusalemu; 12 nao hawakuniona katika hekalu nikibishana na yeyote wala nikisababisha kikundi chenye ghasia kitimke pamoja, ama katika masinagogi ama kotekote katika jiji. 13 Wala hawawezi kukuthibitishia mambo wanayonishtaki sasa hivi. 14 Lakini mimi nakiri hili kwako, kwamba, kulingana na ile njia waiitayo ‘farakano,’ kwa namna hii mimi ninatoa utumishi mtakatifu kwa Mungu wa baba zangu wa zamani, kwa kuwa naamini mambo yote yaliyoelezwa katika Sheria na kuandikwa katika Manabii; 15 nami nina tumaini kuelekea Mungu, tumaini ambalo watu hawa wenyewe hulishikilia, kwamba kutakuwa na ufufuo wa waadilifu na wasio waadilifu pia. 16 Katika habari hii, kwa kweli, mimi ninajizoeza mwenyewe kwa kuendelea kuwa na dhamira ya kutofanya kosa dhidi ya Mungu na wanadamu. 17 Kwa hiyo baada ya miaka kadhaa niliwasili kuleta zawadi za rehema kwa taifa langu, na matoleo. 18 Nilipokuwa nikishughulikia mambo haya wakanikuta nikiwa nimesafishwa kisherehe katika hekalu, lakini nikiwa bila umati wala fujo. Lakini kulikuwa na Wayahudi fulani kutoka wilaya ya Asia, 19 ambao wapaswa kuwapo mbele yako na kunishtaki ikiwa wao waweza kuwa na jambo lolote dhidi yangu. 20 Au, acha watu walio hapa wajisemee wenyewe ni kosa gani walilopata nilipokuwa nimesimama mbele ya Sanhedrini, 21 ila kwa habari ya tamko moja hili nililopaaza kilio nikiwa nimesimama miongoni mwao, ‘Juu ya ufufuo wa wafu mimi nahukumiwa leo mbele yenu!’”
22 Hata hivyo, Feliksi, akijua kwa usahihi kabisa mambo yahusuyo Njia hii, akaanza kuwaahirisha hao watu na kusema: “Wakati wowote Lisiasi kamanda wa kijeshi ateremkapo, mimi nitaamua mambo haya yanayowahusu nyinyi.” 23 Naye akamwagiza ofisa-jeshi kwamba huyo mtu atunzwe na awe na starehe fulani ya kizuizini, na kwamba asikataze yeyote kati ya watu wake kumhudumia.
24 Siku kadhaa baadaye Feliksi akawasili pamoja na Drusila mke wake, aliyekuwa Myahudi wa kike, naye akatuma watu kumwita Paulo na kumsikiliza juu ya itikadi katika Kristo Yesu. 25 Lakini alipokuwa akiongea juu ya uadilifu na kujidhibiti na hukumu itakayokuja, Feliksi akawa mwenye kuogopa na kujibu: “Kwa wakati huu wa sasa shika njia yako uende, lakini nipatapo wakati ufaao nitakuita tena.” 26 Ingawa hivyo, wakati huohuo, alikuwa akitumaini apewe fedha na Paulo. Kwa ajili ya hilo akamwita mara nyingi hata zaidi na akawa akiongea naye. 27 Lakini, miaka miwili ilipokuwa imepita, nafasi ya Feliksi ilichukuliwa na Porkio Festo; na kwa sababu Feliksi alitamani kujipendekeza kwa Wayahudi, akamwacha Paulo akiwa amefungwa.