Matendo
25 Kwa hiyo Festo, baada ya kuingia katika cheo cha serikali ya jimbo, siku tatu baadaye alipanda kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria; 2 na makuhani wakuu na watu walio wakubwa wa Wayahudi wakampa habari dhidi ya Paulo. Basi wakaanza kumsihi sana, 3 wakijiombea wenyewe upendeleo dhidi ya huyo mtu ili amwite aje hadi Yerusalemu, kwa kuwa walikuwa wakivizia ili kummaliza barabarani. 4 Hata hivyo, Festo akajibu kwamba Paulo alipasa kutunzwa katika Kaisaria na kwamba yeye mwenyewe alikuwa karibu kuondoka upesi kwenda huko. 5 “Kwa sababu hiyo acheni wale walio na mamlaka miongoni mwenu,” akasema, “wateremke pamoja nami na kumshtaki, ikiwa kuna jambo lolote lisilofaa juu ya huyu mwanamume.”
6 Kwa hiyo alipokuwa amekaa siku zisizozidi nane au kumi miongoni mwao, akateremka kwenda Kaisaria, na siku iliyofuata akaketi juu ya kiti cha hukumu na kuamuru Paulo aletwe ndani. 7 Alipowasili, Wayahudi waliokuwa wameteremka kutoka Yerusalemu wakasimama kumzunguka huku na huku, wakileta dhidi yake mashtaka mengi na mazito ambayo hawakuweza kuonyesha uthibitisho.
8 Lakini Paulo akasema katika kujitetea: “Wala dhidi ya Sheria ya Wayahudi wala dhidi ya hekalu wala dhidi ya Kaisari sijafanya dhambi yoyote.” 9 Festo, akitamani kujipendekeza kwa Wayahudi, akasema kwa kumjibu Paulo: “Je, wewe ungetaka kupanda kwenda Yerusalemu uhukumiwe huko mbele yangu kuhusu mambo haya?” 10 Lakini Paulo akasema: “Mimi nimesimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ambako napaswa kuhukumiwa. Sijawatendea Wayahudi kosa, kama vile wewe pia unavyogundua vema kabisa. 11 Ikiwa, kwa upande mmoja, mimi ni mkosaji kwa kweli na nimefanya jambo lolote linalostahili kifo, sitoi udhuru nisife; ikiwa, kwa upande mwingine, hakuna hata moja la mambo hayo lililoko ambalo watu hawa wanishtakia, hakuna mtu awezaye kunikabidhi kwao ili kujipendekeza. Mimi nakata rufani kwa Kaisari!” 12 Ndipo Festo, baada ya kusema na kusanyiko la washauri, akajibu: “Kwa Kaisari umekata rufani; kwa Kaisari hakika wewe utaenda.”
13 Basi siku kadhaa zilipokuwa zimepita, Agripa mfalme na Bernike wakawasili katika Kaisaria kwa ziara ya kumwamkua Festo. 14 Kwa kuwa, walikuwa wakitumia siku kadhaa huko, Festo akaweka mbele ya mfalme mambo yenye kuhusu Paulo, akisema:
“Kuna mwanamume fulani aliyeachwa mfungwa na Feliksi, 15 na wakati nilipokuwa Yerusalemu makuhani wakuu na wanaume wazee wa Wayahudi walileta habari juu yake, wakiomba hukumu ya adhabu dhidi yake. 16 Lakini nikawajibu kwamba si utaratibu wa Kiroma kukabidhi mtu yeyote ili kujipendekeza kabla ya huyo mtu aliyeshtakiwa kukutana uso kwa uso na washtaki wake na kupata nafasi ya kusema katika kujitetea kuhusu lalamiko. 17 Kwa hiyo walipokuja pamoja hapa, sikukawia, bali siku iliyofuata niliketi juu ya kiti cha hukumu na kuamuru huyo mwanamume aletwe ndani. 18 Wakisimama, washtaki hawakutokeza shtaka juu ya mambo maovu niliyokuwa nimedhani kumhusu. 19 Walikuwa tu na mabishano fulani pamoja naye kuhusu ibada yao wenyewe ya mungu na kuhusu mtu fulani Yesu aliyekuwa mfu lakini ambaye Paulo alifuliza kusisitiza kwamba alikuwa hai. 20 Kwa hiyo, nikiwa nimefadhaishwa na bishano juu ya mambo haya, niliendelea kuuliza kama angependezwa na kwenda hadi Yerusalemu na huko akahukumiwe kuhusu mambo haya. 21 Lakini Paulo alipokata rufani atunzwe kwa ajili ya uamuzi wa Aliye Mwadhamu, nikaamuru atunzwe mpaka nimtume kwa Kaisari.”
22 Hapo Agripa akamwambia Festo: “Mimi mwenyewe ningependezwa pia na kumsikia huyo mtu.” “Kesho,” akasema, “hakika wewe utamsikia.” 23 Kwa hiyo, siku iliyofuata, Agripa na Bernike wakaja kwa wonyesho mwingi wenye fahari za madaha na kuingia ndani ya chumba cha baraza pamoja na makamanda wa kijeshi na vilevile wanaume waheshimiwa katika jiji, na Festo alipotoa amri, Paulo akaletwa ndani. 24 Naye Festo akasema: “Mfalme Agripa na nyinyi wanaume wote mliopo pamoja nasi, nyinyi mnaona mtu huyu ambaye kuhusu yeye umati wote wa Wayahudi ukiwa pamoja umepeleka ombi kwangu katika Yerusalemu na hapa pia, ukipaaza sauti kwamba hapaswi kuishi tena kamwe. 25 Lakini mimi nikahisi hakuwa amefanya jambo lolote linalostahili kifo. Kwa hiyo mwanamume huyu mwenyewe alipokata rufani kwa Aliye Mwadhamu, niliamua kumtuma. 26 Lakini kuhusu yeye sina jambo hakika la kumwandikia Bwana wangu. Kwa hiyo nikamleta mbele yenu, na hasa mbele yako wewe, Mfalme Agripa, ili, baada ya uchunguzi wa kihukumu kutukia, nipate jambo fulani la kuandika. 27 Kwa maana laonekana kuwa jambo lisilo la akili kwangu kutuma mfungwa na kutoonyesha pia mashtaka dhidi yake.”