Yohana
14 “Msiache mioyo yenu itaabishwe. Dhihirisheni imani katika Mungu, dhihirisheni imani pia katika mimi. 2 Katika nyumba ya Baba yangu mna makao mengi. Kama sivyo, ningaliwaambia nyinyi, kwa sababu nashika njia yangu kwenda kuwatayarishia nyinyi mahali. 3 Pia, nikishika njia yangu kwenda na kuwatayarishia nyinyi mahali, mimi ninakuja tena na hakika nitawapokea nyinyi nyumbani kwangu mwenyewe, ili mahali nilipo nyinyi pia mpate kuwa. 4 Na ninakoenda nyinyi mwaijua njia.”
5 Tomasi akamwambia: “Bwana, sisi hatujui unakoenda. Twaijuaje njia?”
6 Yesu akamwambia: “Mimi ndiyo njia na kweli na uhai. Hakuna ajaye kwa Baba ila kupitia mimi. 7 Kama nyinyi watu mngalikuwa mwanijua, mngalikuwa mwamjua Baba yangu pia; tangu dakika hii na kuendelea nyinyi mwamjua na mmemwona.”
8 Filipo akamwambia: “Bwana, tuonyeshe Baba, na hiyo yatosha kwetu.”
9 Yesu akamwambia: “Je, mimi nimekuwa pamoja nanyi watu kwa muda mrefu sana hivyo, na bado, Filipo, hujaja kunijua mimi? Yeye ambaye ameniona mimi amemwona Baba pia. Ni jinsi gani wewe wasema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, wewe huamini kwamba mimi nimo katika muungano na Baba na Baba yumo katika muungano nami? Mambo niwaambiayo nyinyi watu sisemi kwa ubuni wangu mwenyewe; bali Baba ambaye hukaa katika muungano nami anafanya kazi zake. 11 Niaminini mimi kwamba nimo katika muungano na Baba na Baba yumo katika muungano nami; kama sivyo, aminini kwa sababu ya zile kazi zenyewe. 12 Kwa kweli kabisa mimi nawaambia nyinyi, Yeye ambaye hudhihirisha imani katika mimi, huyo pia atafanya kazi ambazo mimi hufanya; naye atafanya kazi kubwa zaidi ya hizi, kwa sababu nashika njia yangu kwenda kwa Baba. 13 Pia, lolote lile mwombalo katika jina langu, hakika nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa kuhusiana na Mwana. 14 Mkiomba jambo lolote katika jina langu, hakika nitalifanya.
15 “Ikiwa mwanipenda, mtashika amri zangu; 16 nami hakika nitamwomba Baba naye atawapa nyinyi msaidiaji mwingine awe pamoja nanyi milele, 17 roho ya ile kweli, ambayo ulimwengu hauwezi kupokea, kwa sababu hauitazami wala kuijua. Nyinyi mwaijua, kwa sababu hiyo hukaa pamoja nanyi na imo katika nyinyi. 18 Sitawaacha nyinyi ukiwa. Mimi ninakuja kwenu. 19 Bado muda kidogo zaidi na ulimwengu hautaniona tena, lakini nyinyi mtaniona, kwa sababu mimi naishi nanyi mtaishi. 20 Siku hiyo mtajua kwamba mimi nimo katika muungano na Baba yangu nanyi mumo katika muungano nami na mimi nimo katika muungano nanyi. 21 Yeye aliye na amri zangu na kuzishika, huyo ndiye ambaye hunipenda. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami hakika nitampenda na hakika nitajionyesha wazi kwake.”
22 Yudasi, si Iskariote, akamwambia: “Bwana, ni nini kimetukia hivi kwamba wewe wakusudia kujionyesha wazi kwetu wala si kwa ulimwengu?”
23 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Ikiwa yeyote anipenda mimi, atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi hakika tutakuja kwake na kufanya kao letu pamoja naye. 24 Yeye asiyenipenda hayashiki maneno yangu; na neno mnalolisikia si langu, bali ni la Baba aliyenituma.
25 “Nilipokuwa nikikaa pamoja nanyi nimesema mambo haya kwenu. 26 Lakini msaidiaji, roho takatifu, ambayo Baba atapeleka katika jina langu, hiyo itawafundisha nyinyi mambo yote na kuwakumbusha mambo yote niliyowaambia. 27 Mimi nawaachia nyinyi amani, nawapa amani yangu. Mimi siwapi nyinyi hiyo kwa njia ile ambayo ulimwengu huitoa. Msiache mioyo yenu itaabishwe wala msiiache ikunyatike kwa sababu ya hofu. 28 Mlisikia kwamba niliwaambia, Ninaenda zangu nami ninakuja tena kwenu. Kama mngenipenda, mngeshangilia kwamba ninashika njia yangu kwenda kwa Baba, kwa sababu Baba ni mkubwa zaidi kuliko mimi. 29 Kwa hiyo sasa nimewaambia nyinyi kabla ya hilo kutukia, ili, wakati litukiapo, mpate kuamini. 30 Sitasema mengi tena kamwe pamoja nanyi, kwa maana mtawala wa ulimwengu anakuja. Naye hana mshiko juu yangu, 31 lakini, kusudi ulimwengu ujue kwamba nampenda Baba, kama vile Baba amenipa amri kufanya, ndivyo ninavyofanya. Inukeni, twendeni kutoka hapa.